Tuesday, April 9, 2013

A TO Z KULIFIKISHA GAZETI LA RAI KWA PILATO KWA KUANDIKA HABARI YA UONGO

Mkurugenzi msaidizi wa A TO Z Godwin George Abedi kushoto pamoja na wakili Loomu Ojare wa kampuni ya uwakili ya  Loomu Ojare and Co. Limited kulia wakizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za kiwanda hicho zilizopo kisongo nje kidogo ya mji wa Arusha, wakilalamikia habari iliyoandikwa na gazeti la RAI.
Mkurugenzi Msaidizi wa A TO Z Godwin George Abedi akizungumza na waandishi wa habari pichani jana

Waandishi wa habari wakichukua habari
A TO Z KUIFIKISHA RAI MAHAKAMANI KWA KUANDIKA HABARI YA UONGO
 
Na Seif Mangwangi

UONGOZI na Menejimenti ya kampuni ya kutengeneza chandarua chenye dawa, A TO Z umekanusha taarifa zilizoandikwa na gazeti moja la wiki (sio jamboleo), kuwa vyandarua hivyo vinatengenezwa chini ya kiwango na havizuii mbu anaeambukiza ugonjwa wa malaria kutopenya.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Mkurugenzi msaidizi wa kampuni hiyo, Godwin Abedi alisema ubora wa chandarua hicho umehakikiwa na shirika la viwango nchini (TBS), taasisi ya Malaria Ifakara, pamoja na mashirika makubwa duniani ikiwemo (WHO).

Alisema taarifa zilizochapishwa katika gazeti hilo sio za kweli na kwamba zimeandikwa kwa lengo la kuchafua kampuni hiyo na kuharibu shughuli ambazo zimekuwa zikifanywa na kampuni.

“Chandarua chetu kinatengenezwa katika hadhi ya kimataifa, taarifa za kwamba hazina ubora si kweli kwa kuwa hiki chandarua kabla ya kupakiwa na kusafirishwa kwa wateja kote duniani mashirika ya viwango nchini kama TBS, (Ifakara Health Institute) na WHO wanavikagua kuthibitisha ubora wake,”alisema.

Alisema kwa kuwa taarifa hiyo iliyoandikwa haikuwa sahihi, wamekusudia kulishtaki gazeti hilo mahakama kuu kanda ya Arusha  na kwamba kupitia kampuni ya uwakili ya Loomu Ojare and advocate ya jijini Arusha wameshamuandikia Mkurugenzi mtendaji wa kampuni inayomiliki gazeti hilo barua ya kusudio la kulishitaki gazeti lake.

“Tumeshamuandikia mkurugenzi mtendaji wa kampuni inayomiliki gazeti kusudio letu la kulishitaki gazeti  lake kwa habari waliyoiandika ambayo sio ya kweli, tumewapa siku 14 wakanushe habari waliyoiandika na kulipa hasara ambayo imetupata,”alisema Wakili Loomu Ojare.

Alisema wamelazimika kufungua kesi mahakama kuu bila kupitia baraza la habari nchini kwa kuwa kampuni hiyo imekuwa ikifanya shughuli zake kimataifa na imekuwa na wabia wengi nje ya nchi 

Kampuni hiyo imetuma barua yenye kumbukumbu namba 42/MENH/MIS/LOC/2013 ya tarehe 8 Aprili 2013 kwenda kwa mkurugenzi mtendaji  New habari (2006), Limited yenye kichwa cha habari ‘Demand letter for withdrawal and apology for defamatory libel concerning A TO Z Textile mills limited published in RAI newspaper of April 4 to April 10, 2013’.

No comments: