Thursday, April 25, 2013

KIFO CHA MWANAFUNZI CHUO CHA UHASIBU NJIRO CHASABABISHA VURUGU, MBUNGE LEMA ASAKWA KWA MADAI YA KUCHOCHEA VURUGU

MWANAFUNZI wa mwaka wa pili  katika chuo cha uhasibu  kilichopo Njiro jijini Arusha,Henry Koga anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka (25 hadi 30) ameuawa kinyama kwa kuchinjwa na kisu shingoni na kundi la watu wasiofahamika wakati wakitoka kwenye kumbi za starehe na wenzake.

Kufuatia tukio hilo ,kundi la wanafunzi walileta vurugu kubwa na kukataa kutii amri ya mkuu wa mkoa wa Arusha,Magesa Mulongo ya kuwataka warudi darasani wakati hatua zaidi za kisheria zikichukuliwa huku wakimzomea,hali iliyosababisha polisi kuingiliaka kali na kuwafyatulia mabomu zaidi ya 50 na baadhi yao kujeruhiwa.

Tukio la kuuawa kwa mwanafunzi huyo limetokea  majira ya saa 4 usiku wa kuamkia leo ambapo marehemu huyo akiwa na wenzake walivamiwa na kundi la wahuni wapatao wanne katika eneo la CDA ,umbali mchache kutoka eneo la chuo hicho na kumchoma kisu shingoni .

Hata hivyo jitihada za wenzake kutaka kuokoa maisha yake kwa kumkimbiza hospitalini, zilishindikana kwani alifariki dunia muda mfupi baada ya tukio hilo kutokana na kuvuja damu nyingi.

Aidha wanafunzi hao walijikusanya asubuhi yake na kuanza kuandamana  kushinikiza uongozi wa chuo hicho kutoa tamko juu ya vitendo vya uhalifu vinavyojirudia mara kwa mara katika chuo hicho  bila kuchukuliwa hatua zozote na kufanya maisha ya wanachuo hao kuwa hatarini.

Wanafunzi hao walisikika wakilalamikia hali  ya ukimya wa viongozi kushindwa kudhibiti matukio ya uhalifu kwani mwishoni mwa mwaka jana mwanafunzi mwingine aliuawa na vibaka kwa kuchomwa na kisu pia wanafunzi hao waliwahi kuvamiwa  chuoni wakiwa wamelala na kuporwa vitu mbalimbali ikiwemo laptop simu na fedha.

Wakati vurugu za wanafunzi zikiendelea alifika mkuu wa mkoa wa Arusha ,Magesa Mulongo na kuwasihi waache vurugu na wakubali kumsikiliza hata hivyo wanafunzi hao zaidi ya 500 walianza kumzomea huku baadhi yao wakionekana kurushia mawe

Mkuu wa mkoa alilazimika kuondoka eneo hilo ,hatua iliyowalazimu askari wa kutuliza ghasia kufyatua mabomu ya machozi kwa lengo la kuwatawanya na kujikuta baadhi yao wakijeruhiwa vibaya .

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Arusha ,Ibrahimu Kilongo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa  wanafunzi zaidi ya 7 wanashikiliwa katika vurugu hizo huku uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea .

Mkuu wa mkoa Magessa Mulongo pamoja na timu yake wakiingia katika eneo la shule ambapo aliambulia zomea zomea ,kurushiwa mawe,lugha za kejeli kutoka kwa wanafunzi hao kwa kile wanachodai kuwa serikali imekuwa siyo sikivu kutatua matatizo yao ya mara kwa mara ikiwepo kuibiwa vitu mbalimbali




ASKARI WA FFU WAKIWA TAYARI KUDHIBITI VURUGU CHUONI HAPO

UMATI WA WANAFUNZI WA CHUO CHA UHASIBU NJIRO IAA WAKIMSIKILIZA MKUU WA MKOA MAGESA MULONGO KABLA YA KUANZISHA VURUGU WAKIPINGA MWANAFUNZI MWENZAO KUUAWA

No comments: