Saturday, April 27, 2013

MWANDISHI MBWAMBO ASITULETEE TENA `UMBILIKIMO` WAKE WA FIKRA KATIKA UKURASA HUU.



Na Mwandishi Wetu

Mwenyekiti General Ulimwengu,aliwahi kusema `Raia Mwema ama Raia Muungwana ni Yule anayeamka asubuhi na kujiona ni mwenye afya njema ,kisha anampigia simu daktari wake na kumuuliza hatma ya afya yake kwa miaka mitano ama kumi ijayo.(Ntafafanua).

Nimekuwa mmoja wa `waumini` wazuri wa gazeti la Raia Mwema kwa muda mrefu sasa,nemepata mengi na kujifunza mengi kupitia makala mbalimbali zinazopewa nafasi katika gazeti hili hasa kwa Makala zinazoandikwa na Waandishi waliyobobea kama Johnson Mbwambo ambaye ameanza `kuzeeka vibaya`.

Toka nipo Shule ya Msingi na Mpaka sasa nimekuwa Mwanahabari Bado namsoma Mzee Mbwambo ambaye kwangu nilimuona kama Mwalimu Wangu wa siku nyingi sana bila yeye kujijua,lakini hivi karibuni amenifundisha somo ambalo si tu sijalipenda bali pia sijapata jibu kama Mwalimu Wangu alikuwa `amelewa` wakati anaandika ama  alikuwa ametanguliza hasira za kunyimwa Ukuu wa Wilaya mbele!!!

Katika Raia Mwema Toleo na.292 la April 30,ukurasa wa 11 Kuna  Tafakuri Jadidi Iliyoandikwa na Johnson Mbwambo.Ina kichwa Kikubwa cha Habari kinasema KIKWETE KAWASIFU,SASA WANASHINDANA KUITUKANA CHADEMA! Nimesoma kilichoandikwa na Mwalimu Wangu nikapata shaka na anapoelekea `kiumri`.

Kwakawaida Binadamu kadiri unapoongezeka Umri na ndivyo Busara zinavyoongezeka na ndiyo maana kukawa na msemo usemao `Utu uzima ni dawa`.Mimi ni mmoja wa wanaoamini Mbwambo anaongezeka Umri na siyo urefu,kidogo Napata shaka kuamini kama  ongezeko lake la umri linakwenda sambamba na ongezeko la busara.

Mbwambo amekuwa mshabiki kiasi cha kupitiliza,na kwa kiwango hicho ameshindwa kuthibiti hasira zake na kujitofautisha na hao wabunge wanaotoa lugha `chafu` nayeye ametumbukia humo huku `akijifanya kutumia mgongo wa falsafa za Mwalimu Nyerere.

Katika Makala iliyotoka katika gazeti hili Mbwambo kama kawaida yake ametumia muda mwingi kuwashambulia Wabunge vijana wa chama cha Mapinduzi  kwa madai `eti` wamekuwa wakikikejeli chama chake cha Chadema Bungeni badala ya kuongea mambo ya Msingi.Akasema `eti`wamekuwa wakiwafanya hata Wabunge wa `chama chake ` cha Chadema kujibu kwa Ukali( hakuita ni matusi) eti kwasababu ya Wabunge vijana wa ccm wanaotukana.( ya CCM akaita matusi)

Akiendelea kuandika makala yake Mbwambo kila  mara amekuwa akijikingiliza katika kimvuli cha Mwalimu Nyerere `kinafiki`kujaribu kuhalalisha  maandishi yake yakukitetea chama chake kinachodaiwa kuwa na `udini na ukanda`( Mwambo anatokea Kilimanjaro)

Mbwambo katika maandishi yake akasema (namnukuu) ``Isitoshe,Chadema kiumri si chama kikongwe kama ccm na hivyo katika hali ya kawaida wabunge wa ccm ndiyo wanaopaswa kuonyesha mfano wa uungwana Bungeni kwa wabunge wa Chadema kwakuwa wao wanatoka katika chama kikongwe na kinachokamata serikali kwa miaka mingi`` ( mwisho wa kunukuu)  ``Mzee Mbwambo anamaudhi sana`.

Kwa maandishi yake anataka kutufundisha kuwa wabunge wa Chadema wakitukana tuwaunge mkono kwakuwa wapo katika chama kichanga wala wasikosolewe, na Kwakuwa Chama chao hakishiki Dola basi waachwe tu waporomoshe matusi kama wanavyofanya sasa!!

Yaani Mbwambo anataka Wabunge wa ccm wawe wavumilivu kuvumilia `upuuzi ` wa wabunge wa Chadema . Sitaki kuamini kama Kule kwao Kilimanjaro mtoto akitukana anaachwa kwakuwa bado mdogo ( labda anafanya hivyo kwake) Ndiyo maana Napata shaka na umri wa Mzee Mbwambo unapoelekea! Katika makala yake Mbwambo ameongea mengi yanayokera `kama yeye alivyokerwa na Yule mwandishi aliyemwita `mhandisi anayempigia debe Babu wa Loliondo eti Dawa zake ni tiba sahihi`.

Katika kuifanya Jamii izidi kuiamini taaluma ya Uandishi wa habari ni lazima sisi waandishi wa habari  bila kujali mkongwe ama mchanga tusiwe makatibu waenezi wa vyama vya siasa.

Katika Maandishi  yake Mbwambo anaandika kama vile siyo mwandishi wa habari bali ni `Mwajiriwa wa Chadema`.

Siku zote nimekuwa nikimsoma Mbwambo na kumwelewa na kujifunza kwa kile anachokiandika lakini kwa hili nimeshindwa kuingiza ndani ya ubongo wangu `ushawishi wake` usiyofaa mbele ya jamii kuwa eti watukane wa Chadema,lakini ccm hapana.

Binafsi siungi  mkono lugha chafu zinazotolewa na baadhi ya wabunge bila kujali vyama vyao,sipendi kuona wabunge wanakuwa kichaka cha matusi kwa sisi vijana ama watoto wadogo zaidi yangu kwa namna yeyote ile.

Mbwambo amejielekeza zaidi kuiaminisha jamii kuwa yanayotolewa na Chadema siyo matusi bali ni hoja za msingi na yanayotolewa na baadhi ya wabunge wa ccm siyo majibu ama hoja bali ni matusi.
Mzee Mbwambo amefika mbali zaidi kwa kudai kuwa baadhi ya wabunge wa CCM  wamesifiwa na Rais Jakaya Kikwete na ndiyo maana wamezidi kutukana matusi

Akasema Mwigulu Nchemba alipewa zawadi ya cheo baada ya kukitukana Chadema  na ndiyo maana basi wengine wanaiga ili wapewe zawadi ya vyeo.

Anavyoamini yeye (Mbwambo) CCM wakichaguana katika chaguzi zao kama Chadema basi ni kupeana zawadi za vyeo na siyo haki, CCM wakiteuana kulingana na katiba yao kwa mtazamo wa Mzee Mbwambo huo siyo uteuzi ila ni zawadi baada ya kutukana!

Mzee Mbwambo ameondoka katika uandishi na kuwa mtu wa Propaganda wa Chadema,sitaki kuamini kama kuna mwandishi anayefuata misingi ya taaluma anaweza kuwa na upendeleo kiasi hicho.

Inawezekana kabisa alichokiandika Mzee Mbwambo ni Mawazo yake. Lakini mawazo gani hayo yanayowaza upande mmoja pake yake,mawazo gani ambayo hubadilisha `matusi` kuwa maneno matamu?
Mawazo gani hayo nayaona matusi ya wabunge wa chadema  kuwa ni maendeleo? Huu ni umbilikimo wa fikra ambao hauendi sambamba na heshima alonayo Mzee Mbwambo.

Mzee Mwambo aliwahi kumshambulia Mwandishi mmoja mkoani Arusha akimwita `Mhandisi wa habari` kwa kuwa mwandishi huyo aliandika habari zinazomhusu Babu wa Loliondo na Mwandishi huyo hakuonyesha kuiaminisha jamii kuwa dawa za Babu hazifai.

Alimshambulia mwandishi na kumwelekeza kuwa ni afadhali angeandika habari hiyo kwa mtindo wa kukejeli  ili asionekane kushabikia ushirikina wa Babu.

Sasa Mzee Mbwambo alichokiandika yeye ni afadhali ya huyo Mwandishi aliyemwita `Mhandisi`.
Ameshabikia upuuzi wa baadhi ya wabunge hasa wa chadema,na siwezi kumwita yeye ni `mhandisi`.

Waandishi jamii ya Mzee Mbwambo huko tuendako ni hatari kwa kizazi cha taaluma ya habari.Atawaambukiza ushabiki waandishi wachanga na wanaomsoma ambao watakuwa ni wavivu wa kutafakari kama anavyomaliziaga makala zake kwakusema tafakari.

Binafsi nimetafakari nimebaini umendika kiushabiki,na kama siyo kiushabikia basi pengine unaweza kuwa na una hasira na Rais Kikwete,labda hukupata ukuu wa wilaya nk.tafakari mwenyewe.

Raia Mwema ni Yule anayeamka asubuhi na kujiona ni mwenye afya njema lakini anampigia simu daktari wake akimuuliza hatma ya afya yake miaka kumi ijayo.

Mzee Mbwambo ameamka asubuhi amejiona ni mwenye afya njema,hampigii daktari wake simu anadunda tu barabarani hajui madhara ya baadaye.

Angempigia daktari wake simu angeambiwa maradhi yako ya fikra yanaambukiza hivyo usisambaze maradhi yako ya fikra za upande mmoja kwa watu wote hasa kwa sisi vijana tunaokuwa katika maadili mazuri.

Tafakari…O752 25 01 57…// 0655 2501

No comments: