Wednesday, April 24, 2013

MDUDU WA AJIRA ZA UPENDELEO AANZA KULALAMIKIWA BANDARI


Mwakyembe ampa ajira kiaina Bandari mtoto wa Mkuchika

Mdudu wa ajira za upendeleo aanza kulalamikiwa Bandari

Martin Malera,

MIONGONI mwa mambo ambayo tume aliyoiunda Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, iligundua na kupendekeza adhabu kwa wahusika ni ajira za upendeleo zilizoonekana hazikufuata taratibu zilizomo ndani ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA). Wakati huo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, Ephrem Mgawe na Mkurugenzi wa Utumishi, Maimuna Mrisha, walituhumiwa vikali kwenye ripoti hiyo ya tume ya Waziri Mwakyembe.

Watendaji hao walituhumiwa kwa kile kilichoonekana kuwa walivunja utaratibu wa kanuni za ajira kwa kuwaajiri ndugu na watoto wa wakubwa bila uwepo wa usaili wowote wala nafasi hizo kutangazwa kwa watu wa ndani ya taasisi au nje kwa nia ya kupata ushindani wenye tija.

Kinachoshangaza ni takriban miezi minane tangu uongozi wa zamani uondolewe kwa tuhuma mbalimbali na suala la ajira za upendeleo likiwamo, tayari uongozi mpya uliowekwa, nao umeshaaza kufanya kile kile kilichowaondoa wenzao.

Waziri Mwakyembe huko nyuma aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari wakati akiwa kwenye harakati zake za timuatimua huko TPA kwamba ajira zilikuwa zinauzwa kwa sh milioni mbili na kuendelea na ndiyo maana aliamua kufanya mabadiliko makubwa kuondoa uozo huo uliokuwepo kwa miaka nenda rudi.

Wiki iliyopita kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi kilichofanyika Bagamoyo na kumalizika Jumapili Aprili 21, 2013 wafanyakazi walishtushwa na kuajiriwa kwa mtoto wa waziri mmoja wa utawala Bora (wizara hiyo ina waziri na naibu wake) aliyeajiriwa kama ofisa katika kitengo cha teknohama (Computer & Information Technology) bila usaili wala nafasi kutangazwa. Hata mkuu wa idara husika hakuhusishwa ili atoe mapendekezo kama mtu wa namna hiyo anahitajika au la. Yeye ameshtukia tu analetewa mtu ambaye inasemekana ni agizo kutoka kwa waziri kuja kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu Kipande, ikimtaka kuwa aajiriwe kwa njia hiyo.

Kikao cha bodi kilichokaa hivi karibuni kiliagiza kuwa nafasi zilizo wazi, ikiwa ni pamoja na ya mkurugenzi mkuu zitangazwe mapema lakini taarifa zilizopo ni kwamba matangazo kwa nafasi husika yamepelekwa wizarani ili waziri afanye ‘vetting’ na kuhakiki sifa sinazohitajika kwenye nafasi husika kabla ya kupelekwa kwenye magazeti.

Kinachoonekana hapa ni namna fulani ya uchakachuaji wa kuwawezesha watu fulani waombe ili wakipishwa ionekane kuwa walikidhi vigezo vilivyowekwa. Kwa mfano, nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA sifa zake ziko kwenye sheria iliyounda TPA na inasema wazi kuwa nafasi hii inahitaji pamoja na sifa nyingine mtarajiwa atatakiwa awe na uzoefu na elimu kwenye sekta husika (port & shipping industry).

Kwa hali iliyopo TPA, kwa sasa panahitajika mtu makini na mwenye upeo mpana wa biashara za kimataifa na mtawala kwa ujumla na si watu waliozoea ukiritimba wa kiserikali (bureaucratic approach). Ni lazima sasa siasa ziachwe na badala yake suala la ajira katika sekta nyeti kama bandari lifanywe kwa kuzingatia taaluma husika, uadilifu na lilenge kuboresha biashara.

Source: Mdudu wa ajira za upendeleo aanza kulalamikiwa Bandari

No comments: