Friday, April 5, 2013

TAMKO LA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI TANZANIA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MGOGORO WA ARDHI WA LOLIONDO

TAMKO LA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI TANZANIA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MGOGORO WA ARDHI WA LOLIONDO
Pori tengefu la Loliondo ni eneo lililopo mashariki mwa hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Eneo hili linajumuisha vijiji ambavyo vinatambulika kisheria tangu wakati wa ukoloni na kulindwa kisheria na sheria ya ardhi ya vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 na sheria ya Serikali za Mitaa, Tawala za Wilaya namba 7 ya Mwaka 1982. Vijiji hivyo ni Ololosokwan, Soitsambu, Oloipiri, Olorien, Maaloni, Arash, Malambo na Piyaya. Eneo hili pia limekuwa likijulikana kama pori tengefu la Loliondo kulingana na sheria ya wanyama pori ya mwaka 1974 na sheria ya wanayma pori namba 5 ya mwaka 2009 ambazo zote hazija badilisha hadhi ya vijiji vilivyopo wala haki za ardhi za wenyeji wa vijiji husika wala hazihamishi haki hizo kwenda kwa mamlaka nyingine yoyote ikiwemo wizara ya malisaili na Utalii. Itambulike kwamba hadhi ya pori tengefu haingilii hadhi ya umiliki wa ardhi bali inatoa mamlaka kwa mkurugenzi wa wanyama pori kusimamia wanyama pori waliopo katika eneo hilo pamoja na kutoa mamlaka ya kugawa vitalu vya uwindaji kwa makampuni ya uwindaji bila kuingilia haki za ardhi kwa wakazi wa maeneo husika. Aina hii ya mgawanyo, usimamizi na matumizi ya ardhi na rasilimali zake imekuwa ndicho kiini kikubwa cha mgongano wa maslahi na migogoro ya mara kwa mara katika eneo hili na maeneo mengine yenye sifa ya aina yake.

Mwaka 1992 serikali ilimruhusu mwana mfalme Brigadia Mohamad Al-­‐Ali kupitia kampuni ya Otterlo Business Corporation (OBC) kuwinda ndani ya vijiji vya tarafa vya Loliondo na Sale. Ruhusa hiyo haikufuta haki na uhalali wa wananchi wa kuendelea kuwepo na kutumia ardhi yao kulingana na sheria ya Ardhi ya vijiji ya mwaka 1999 na sheria ya serikali za mitaa, tawala za wilaya.
Tangu wakati huo kumekuwepo na upotoshaji mkubwa kuhusu uhalali wa umiliki wa eneo la Loliondo ambao umefanywa na serikali kwa lengo la kuilinda kampuni ya uwindaji ya OBC. Upotoshaji huo umekuwa ukifanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii na uongozi wa Mkoa wa Arusha na wilaya ya Ngorongoro na kupelekea wananchi kutolewa kwa nguvu katika maeneo hayo kwa madai mbalimbali ikiwa ni pamoja na madai kuwa wananchi wa Loliondo ni wakenya, waharibifu wa mazingira na kuongezeka kwa watu na mifugo. Upotoshaji huu umekuwa na lengo la kuwaahadaa umma wa Watanzania na ulimwengu kwamba eneo lote la Loliondo ni eneo la hifadhi pekee na siyo ardhi ya vijiji na kwamba wananchi ni wavamizi wa eneo hilo jambo ambalo siyo sahihi wala halina uhalali wowote wa kisheria.
Kutokana na nia ya serikali kuwaondoa wananchi katika maeneo yao ya vijiji vyao kumekuwepo na harakati mbalimbali za wizara kutumia mbinu mbalimbali za kumega na kupokonya kilomita za mraba 1500 ya ardhi ya vijiji na kuikabidhi kampuni ya OBC kwa kisingizio cha kwamba wanawagawia wananchi sehemu ya pori tengefu la Loliondo. Jambo hili siyo sahihi kwani ardhi hiyo ni ardhi ya vijiji husika.
Tarehe 21 Marchi 2013 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Balozi Khamisi Khagasheki, alitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari. Taarifa hiyo ina kichwa cha habari “Wizara ya Maliasili kurekebisha mipaka na ukubwa wa eneo la Pori tengefu la Loliondo kutoka Kilometa za mraba 4,000 hadi 1500”. Katika taarifa hiyo Waziri ametangazia umma kwamba serikali imeamua kupunguza ukubwa wa eneo hilo ili kutatua migogoro iliyopo katika eneo hilo, kunusuru ikolojia ya hifadhi ya Serengeti, Ngorongoro na Pori tengefu la Loliondo.
Vilevile katika tamko lake Waziri alielezea sababu zingine kwamba ni kulinda masalia ya wanyama pori, mapito na vyazo vya maji kwa ajili ya ustawi wa hifadhi kwa manufaa ya

wananchi wenyewe na taifa kwa ujumla. Pia waziri alizungumzia kwamba wananchi wataweza kuanzisha hifadhi za wanyama pori (WMA) katika ardhi itakayobaki kuwa ardhi ya vijiji.
Kutokana na tamko hili la Mh. Waziri , SISI mashirika ya kiraia yanayojihusisha na utetezi wa Haki za Ardhi na Haki za Binandamu na ambao tumekuwa tukifuatilia suala hili kwa karibu sana tunapenda kujulisha umma wa watanzania kama ifuatavyo;
 1. Kwamba siyo kweli serikali inawaachia wananchi ardhi yenye ukubwa wa kilomita za mraba 2500 kwani ardhi hiyo ni ardhi ya vijiji iliyopo ndani ya mipaka ya vijiji na kinachofanyika ni kuwapokonya wananchi ardhi iliopo ndani ya mipaka ya vijiji vyao yenye ukubwa wa kilomita za maraba 1500 na kumpatia mwekezaji wa OBC.
 2. Hakuna eneo lolote alilopewa OBC kama waziri alivyo potosha katika ukurasa wa pili wa taarifa yake kwa umma kwamba “serikali ipo tayari kuangalia upya eneo kubwa alilopewa OBC na ikibidi litapunguzwa...” Ukweli ni kwamba OBC iko katika eneo la pori tengefu la Loliondo ndani ya vijiji husika kwa kibali cha kuwinda tu na sio umiliki wa ardhi na hawakuwahi kupewa ardhi anayodai Mh Waziri kwamba wamepewa. Vilevile waziri anatuaminisha kwamba mgeni amemilikishwa ardhi ya Loliondo jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya ardhi na sheria ya uwekezaji inyokataza wageni kumiliki ardhi isipokuwa kwa kuwekeza tu.
 3. Kwamba uamuzi wa serikali wa kugawa eneo la vijiji na kulifanya kuwa pori tengefu unachochea mgogoro uliopo. Kusema kuwa serikali inawagawia wananchi eneo watakaloikalia ni upotoshaji kwani wananchi ndio wenye haki ya kugawa eneo lolote ndani ya mipaka ya vijiji vyao kwa matumizi watakayoamua wao. Serikali kudai kuwagawia wananchi eneo ambalo tayari ni la kwao inatosha kuchochea mgogoro katika eneo hilo na ni dalili ya serikali kutaka kutumia mabavu kama ilivyotokea mwaka 2009.
 4. Kwamba siyo kweli kuwa serikali ina lengo la kuinusuru ikologia ya hifadhi ya Serengeti ila ina lengo la kumpatia mwekezaji (OBC) eneo la kuwindia bila kuzingatia sheria na matakwa ya wananchi wa vijiji husika. Hili pia halina ukweli wowote kwani serikali wasingeruhusu uwindaji ufanyike kama wangekuwa na uchungu wa kuwalinda

wanyama pamoja na ikolojia hiyo. Hili linadhihirishwa na wanyama wenyewe kukimbilia karibu na maboma ya wafugaji ili kuwakimbia wawindaji wa OBC kwani wanyama pori wanajisikia wako salama zaidi wanapokuwa karibu na mifugo kuliko kuwa karibu na wawindaji.
 1. Siyo kweli kwamba serikali inataka kulinda vyanzo vya maji kama anavyodai Mh Waziri. Hili linadhihirishwa na ujenzi wa kambi ya kudumu ya OBC kwenye chanzo cha mto wa Olasae linalotegemewa na wanyamapori pamoja na wanakijiji wa kijiji cha Soit Sambu , Arash,Ololosokwa na Kirtalo. Ujenzi huu umefanywa na kampuni ya OBC ndani ya mita 10 kutoka chanzo cha maji kinyume cha sheria.
 2. Taarifa ya Mh. Waziri haikuzingatia suala la utawala bora wala sheria ya wanyama pori ya mwaka 2009 kifungu cha 16(5) ikinachomtaka kwamba hakuna ardhi ya kijiji itakayoingizwa ndani ya pori tengefu. Kipengele hiki kinasomeka kama ifuatavyo; 16(5) “For the Purposes of subsection (4), the Minister shall ensure that no land faIling under the village land is included in the game controlled areas.” Kipengele cha 16(6) “Subject to subsection (4), the Minister shall, in consultation with the relevant authorities, make regulations prescribing the manners in which sustainable management of game controlled areas shall be achieved.”
Kutokana na maelezo yetu hapo juu sisi mashirika ya hiari tunaitaka serikali kutekeleza yafuatayo;
 1. Serikali iache mara moja mpango wake wa kugawa ardhi ya wananchi kwa manufaa ya mwekezaji kwa kisingizio cha manufaa ya umma badala yake itambuwe ardhi yote ya Loliondo kama ardhi ya vijiji na kuwaachia vijiji kujipangia matumizi yao ya ardhi kwa njia shirikishi na mujibu wa sheria za ardhi.
 2. Kuacha mara moja kupotosha umma kwamba ardhi hiyo siyo ya vijiji na izingatie sheria kwa kuvipa vijiji haki yao ya kujiamulia mambo yao wenyewe kwa kutumia sheria zilizopo za ardhi na za serikali za mitaa.
 3. Serikali iweke bayana kwa umma nia yake ya kuchukua ardhi hii kwamba ni kwa ajili ya mwekezaji wa OBC badala ya kisingizio cha uhifadhi wa mazingira na sio vinginevyo.

 1. Serikali iache mara moja vitisho kwa wananchi wa Loliondo na wawakilishi wao, wanaharakati, mashirika na waandishi wa habari wanaofuatilia mgogoro huu. Serikali kuendelea kutishia makundi haya inakiuka haki ya kikatiba ya kupata habari na kuzuia jamii kuelimishwa juu ya haki zao za kikatiba na kisheria kwa manufaa yao wenyewe na taifa kwa ujumla. Kufanya hivyo ni kuwanyima haki yao ya kupata taarifa na kutoa maoni kama inavyolindwa na katiba ya Tanzania na mikataba ya Kimataifa ambayo serikali imeridhia.
 2. Serikali iache mara moja kudharau na kuingilia utendaji wa mhimili wa mahakama kwa kuacha kuingilia suala la Loliondo kwa kuzingatia kuwa tayari kuna kesi ya kikatiba (MISC CIVIL CAUSE NO 15/2010) iliyofunguliwa katika mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha ambapo Waziri wa Maliasili na Utalii na mwekezaji wa OBC ni miongoni mwa wa walalamikiwa.
 3. Serikali iache mara moja visingizio kwamba mgogoro wa Loliondo unasababishwa na wanaharakati na mashirika ya nje kwani yenyewe inatambua uwepo wa mgogoro huo unasababishwa na maamuzi ya serikali ya kugawa ardhi ya wananchi bila kuwashirikisha kwa kuangalia upande mmoja wa manufaa kwa wawekezaji tu bila kuangalia athari kwa wananchi.
 4. Serikali iache matumizi mabaya ya vyombo vya usalama hasa jeshi la polisi ambalo hutumiwa kuwaondoa wananchi katika makazi yao kwa nguvu huku wakisababisha athari kubwa kwa wasiojiweza, wanawake na watoto.
TAMKO HILI LIMETOLEWA LEO TAREHE 4 APRILI 2013 NA MASHIRIKA AMBAYO NI;
 1. PINGOs Forum
 2. Tanzania Land Alliance- TALA
 3. Haki Ardhi
 4. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu- LHRC
 5. Tanzania Human Rights Defenders
 6. Tanzania Gender Network Program (TGNP)
 7. Tanzania Natural Resource Forum –TNRF
 8. Cords
 9. Ujamaa Community Resource Team- CRT
 10. Pastoralists Women Council –PWC
 11. Ngorongoro NGOs Network –NGONET
 12. Tanzania Pastoralists Community Forum-TPCF
 13. OSEREMI

No comments: