Thursday, May 16, 2013

MKE WA WAZIRI MKUU TUNU PINDA AITAKA SERIKALI KUWAKUMBUKA KWENYE MISHAHARA MAKATIBU MUHTASI 'SEKRETARI'


Na Mwandishi wetu, Tanzaniasasa

MKE wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda Tunu Pinda ameitaka serikali kuzingatia kada za makatibu muhtasi waandamizi  ili kuendana na kiwango cha mishahara wanayolipwa ikiwa ni moja ya njia ya kuendelea kuithaminisha kazi hiyo.

Mama Pinda alitoa kauli hiyo jana jijini hapa alipokua akifungua mkutano wa makatibu muhtasi nchini(TAPSEA)unaofanyika jijini Arusha katika kituo cha mikutano cha AICC unaowakutanisha makatibu muhutasi wa ofisi za serikali na watu binafsi kote nchini.

Alisema kuwepo na kima sawa cha mishahara kwa watumishi wa kada hiyo ya makatibu muhutasi pasipo kuzingatia kada zake kunasababisha kukosekana utumishi bora kwakua hakuna manufaa yoyote watumishi hao wanayoyapata kwa kukaa muda mrefu kazini.

Aidha aliwataka watumishi hao kuzingatia maadili ya kazi yao hususani suala la mavazi yenye heshima ili kuondoa dhana kuwa mtumishi wa idara hiyo ya ukatibu muhutasi ni lazima avae nguo zinazoonyesha maungo yake.

Alisema kuendelea kuvaa mavazi yasiyo na heshima wawapo makazini hali inayosababisha kazi hiyo kudharaulika huku wao wakibaki kulalamika kunyanyasika na baadhi ya mabosi wanaowafanyia kazi.

Pia aliwataka kuacha kufanya kazi ya kuwasemea mabosi zao pindi wateja na watu mbalimbali wanapohitaji kuonana na viongozi hali ambayo inawajengea picha mbaya na hata kusababisha kuwagombanisha viongozi na watu wanaowatumikia.

“Mimi nimefanya kazi hii tangu mwaka 1984 huko wilayani Lushoto mkoani Tanga kabla sijastaafu,  kazi ilikua na maadili sana ila sasa hivi imeharibika sana badilikeni vaeni vizuri mheshimike”alisema Mama Pinda.

Nae Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu uwekezaji na uwezeshaji Dk.Mary Nagu ambae ni mlezi wa chama cha makatibu muhutasi nchini alisema ili nchi iweze kuendelea na hususani kwa upande wa wanawake ni lazima wanawake wenyewe waweze kupendana wawapo makazini.

Alisema sehemu nyingi za kazi kunapokua na bosi mwanamke akawepo katibu muhtasi mwanamke hali inakua mbaya kutokana na malumbano ya hapa na pale ambayo husababisha kuharibika kwa kazi na kukwamisha maendeleo.

Aliwataka pia watumishi hao kuitumia vyema fursa ya kukopa katika Saccos ya chama hicho kwa malengo ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuondokana na lindi la umasikini wa kipato linalowakumba zaidi kundi la wanawake.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi mwenyekiti wa chama cha makatibu muhutasi nchini Pili Mpenda alisema chama chake kimejikita katika malengo ya kutafuta fursa za mafunzo kwa wanachama wake ili kuongeza zaidi ufanisi kazini.

Alisema hadi hivi sasa chama kina wanachama wachache wapatao 600 wakati makatibu muhtasi nchini ni wengi zaidi ambao hawajataka kujiunga hali iliyosababisha mkutano huo kufurika wajumbe zaidi wapatao 2000 na kuwataka ambao hawajajiunga kujiunga na chama hicho.

Pia alirejea wito wa kuwataka wanachama wake kuzingatia maadili yao makazini ikiwa ni pamoja na kuwa wakarimu kwa wageni na kuacha kuwa miungu watu pindi watu wanapofika katika ofisi zao kwa shida mbalimbali kwakua kufanya hivyo ni kujijengea chuki na wananchi.

Mkutano huo wa siku tatu unatanguliwa na kongamano la siku mbili la wanachama wote na kisha kufuatiwa na mkutano mkuu ambao utakua na jukumu la kupitia utendaji kazi wa chama chenyewe pamoja na wanachama wake makazini.


No comments: