Tuesday, May 7, 2013

POLISI ARUSHA YAKAMATA DAWA ZA KULEVYA


Mkuu wa Kitengo cha kuzuia Madawa ya Kulevya Mkoa wa Arusha Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Abeny Mgode akiwaonyesha waandishi wa habari madawa ya kulevya aina ya bangi baada ya jeshi hilo mkoani hapa kukamata magunia sita ya madawa hayo. (Picha na Rashid Nchimbi wa jeshi la Polisi Arusha)

Gari aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T. 526 BWX lililokamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa arusha likionekana kutolewa viti vya nyuma hivyo kuweza kubeba magunia sita ya madawa ya kulevya aina ya bangi kwa urahisi. (Picha na Rashid Nchimbi wa jeshi la Polisi Arusha)

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Mapambano dhidi ya uzuiaji wa dawa za kulevya nchini yanazidi kupamba moto baada ya jeshi la Polisi Mkoani hapa kukamata gari lililokuwa na magunia sita ya bangi. Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa mwezi wa April muda wa saa 6:00 Mchana wilayani Longido.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Sabas alisema tukio hilo lilifanikiwa baada ya askari wa jeshi hilo kupata taarifa kutoka kwa raia wema juu ya kuwepo kwa tukio la kusafirisha madawa hayo toka Longido Mjini kuelekea Namanga.

Alisema askari walipopata taarifa hiyo walianza kulifualia gari hilo aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T. 526 BWX na mara baada ya dereva wa gari hilo kugundua anafuatiliwa aliamua kulitelekeza na kisha kukimbia.

“Mara baada ya askari kulifikia gari hilo walilipekua na kukuta gunia sita za dawa za kulevya aina ya bangi zikiwa nyuma ya siti ya gari na mpaka hivi sasa mmiliki wa gari hilo bado hajajulikana na tunafanya juhudi za kumtafuta”. Alisema Kamanda Sabas.

Kamanda Sabas aliwashukuru baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Arusha kutokana na ushirikiano mzuri juu ya utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa jeshi hilo hali ambayo inasaidia kuzuia vitendo vya uhalifu na kukamatwa kwa wahalifu wa matukio mbalimbali.

 Aliwasihi wakazi wa mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani kuendelea kushirikiana na jeshi hilo katika kupeana taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuweza kuzidi kuimarisha hali ya amani na utulivu nchini.

No comments: