Friday, May 10, 2013

WALIOFARIKI KWA BOMU KANISA KATOLIKI MT.JOSEPH MFANYAKAZI OLASITI KANISANI WAZIKWA LEO, MISA TAKATIFU ILIONGOZWA NA KADINALI PENGO

Miili ya marehemu watatu Regina, James na Patricia ikiwa kanisani huku misa ya kuwaombea ikiendelea na kuendesha na kadinali Pengo

Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni Freeman Mbowe akitoa salamu zake za mwisho
Na mwandishi wetu, TANZANIASASA

MAMIA YA Wakazi wa jiji la Arusha na Mikoa jirani jana walijitokeza katika mazishi ya waumini watatu wa kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph Parokia ya Olasiti mfanyakazi jijini hapa waliokufa katika shambulio la bomu lililotokea kanisani hapo Juni 5 mwaka huu.

Katika mazishi hayo ambayo yalianza kwa ibada takatifu ilioongozwa na Kadinali Policapi Pengo Marehemu hao Regina Loning’o mkazi wa Olasiti, Patricia Assey mkazi wa Majengo na aliyekua akisoma darasa la tatu shule ya msingi Elerai na James Kessy mkazi wa  Majengo aliyekua mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Arusha walizikwa kanisani hapo.

Vilio na simanzi kubwa ndivyo vilivyopamba mazishi hayo hasa baada ya Askofu wa kanisa katoliki mkoani Arusha Mhashamu Josephat Lebule alipotangaza kuwa Mtoto Patricia ambaye alikua ni mapacha aliyefariki katika tukio hilo mama yake mzazi hajapata nafasi ya kuhudhuria maziko ya mwanaye kwakua naye amejeruhiwa vibaya na yupo hospitali ya rufaa ya Muhimbili kwa matibabu.

Waziri Mkuu panda akitoa salamu za rambirambi za Serikali aliwataka wananchi kote nchini hususani mkoani Arusha kuiachia serikali kupitia vyombo vyake vya usalama kuwasaka wahusika wa tukio hilo na kuacha kunung’unika pindi kamatakamata itakapozidi.

Alisema tangu kutokea kwa tukio hilo vikao mbalimbali vimekaa ambapo yeye na Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Dk.Emanuel Nchimbi wamekubaliana kutumia vyombo vyote vya dola kuwasaka wahalifu hao usiku na mchana ili kufanikisha kukomesha matukio hayo.

“Naomba wananchi mtupe imani na mtuamini kwamba wote wanaofanya vitendo vya kigaidi watakamatwa na watachukuliwa hatua kali za kisheria, kikubwa tunaomba mshirikiane na sisi kuwapata wahalifu hawa kwa kuwa ni ndugu zenu na mnakaa nao mahali pamoja, hata kama ni mimi Pinda nitajwe,”aliagiza waziri Mkuu Pinda.

Waziri Pinda alisema watu wanaofanya vitendo hivyo ni wachache wasiopenda amani ya Tanzania na kwamba watambue kuwa kuua kiongozi wa dini sio suluhisho la kuteketeza dini hiyo kwa kuwa dini zote zimeanza muda mrefu na zimekuwa na historia kubwa nchini.

“ Tuwapuuze hawa wachache wenye nia ya kuvuruga amani ya nchi yetu kwakua kumuua Askofu, Padri,Mchungaji au Kadinali sio kuumaliza ukristo na wala kumuua Sheikh au Imamu siyo kuumaliza uislamu, dini hizo mbili zimekuwepo miaka mingi na zina waumini wake wengi sana,”alisema Pinda.

Awali akizungumza katika ibada ya maziko hayo kiongozi wa kanisa katoliki nchi Mwadhamu Kadinali Polikap Pengo aliwataka waumini wa kikristo na dini zingine nchini kuwaombea viongozi wenye mamlaka nchini ili waweze kuzinduka na kutekeleza majukumu yao ikiwemo usalama wa nchi.

Pengo alisema endapo Tanzania itasambaratika kutokana na matukio ya namna hii watakaopaswa kulaumiwa ni viongozi wenye mamlaka kwa kulea vitendo hivyo ambavyo vimedumu kwa muda mrefu sasa pasipo kukemewa na wale wahusika kuchukuliwa hatua kali.

Aliwataka waumini wa kikristo nchini kuendeleza ibada na maombi pasipo  kulipiza kisasi dhidi ya matukio ambayo yamekuwa yakielekezwa kanisani na kuwasisi  kuwasamehe wale wote waliohusika na matukio yote na kuviachia vyombo vya dola na serikali kuwaadhibu kwa taratibu zake.

Akitoa salamu za Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Rais wa baraza hilo  nchini ambaye pia ni askofu wa jimbo kuu Katoliki Iringa Tracisius Ngalalekuntwa aliitaka serikali kuacha kukalia kimya matukio kama hayo yanayohatarisha amani kwakua yakiendelea kuachiwa huenda yakazaa machafuko zaidi nchini.

Alisema vipo viashiria mbalimbali vya udini hapa nchini ikiwemo kundi la waislamu waliojikusanya mwaka 2011 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam na kutoa tamko kuwa nchi inaendeshwa kwa mfumo kristo ulioasisiwa na Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na serikali ilikalia kimya jambo hilo bila wahusika kuchukuliwa hatua .

“ Mbali na kauli hii kali pia waislamu hao hao walitoa kauli kuwa wakristo nchini wanapendelewa, wanapeana vyeo katika nafasi mbalimbai pamoja na kupewa fedha na serikali za kujenga shule na vyuo vyao jambo ambalo  pia serikali ilishindwa kulikemea,”alisema Askofu Ngalalekuntwa.

Alisema suala la waislamu kutamka waziwazi kuwa wakristo wana chama chao cha kisiasa na kwamba muungano pia una mfumo kristo na kuziachia kauli hizo bila kuzitolea kauli zimesababisha mahusiano baina ya waislamu na wakristo kuwa mabaya.

Askofu Ngalalekungwa aliitaka serikali kuwachukulia hatua wale wote wanaotoa kauli za kichochezi na kuacha kuwakamata wale wanaotoa taarifa za vificho zilizo na nia ya kuwakomboa wakristo dhidi ya matukio maovu yakiwemo ya vifo vya viongozi wa kikristo pamoja na uchomaji wa makanisa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa muungano wa madhehebu ya kikristo mkoani Arusha Askofu Stanley Hotay aliwataka wanahabari nchini kuacha kuandika habari za tukio hilo na mengine mengi kiushabiki kwakua hata wao hawapo salama sana.
Alisema wanahabari nchini ni sawa na wasafiri katika gari moja ambao hawapaswi kumchekea abiria mwenzao anayeng’oa magurudumu ya gari wanalosafiria kwakua ajali ikitokea hata wao watahusika pia.

Maziko hayo ambayo pia yalihudhuriwa na Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowasa pia yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini wakiwemo Masheikh, maaskofu kutoka majimbo ya Tanga, Kilimanjaro, Geita, Same, askofu mkuu wa KKKT Dk.Alex Malasusa,Waziri wa mambo ya ndani Dk.Emanuel Nchimhi,Naibu Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Goodluck Ole Medeye,Naibu waziri wa tawala za mikoa na serikali za mitaa Agrey Mwanri,mbunge wa Monduli Edward Lowasa na mkuu wa mkoa wa Arusha Magesa Mulongo.
Baadhi ya Mapadri wa kanisa Katoliki  jimbo la Arusha wakiwa wamebeba mwili wa marehemu Regina laizer wakiutoa nje ya kanisa baada ya kumalizika kwa ibada na kuupeleka kwenye makaburi kwaajili ya mazishi leo


No comments: