Sunday, June 30, 2013

HALMASHAURI SIMANJIRO YATUNISHIANA MISULI NA MAMLAKA YA MJI MDOGO MIRERANI, DIWANI NYARI AAPA MAMLAKA HIYO IKIFA ATAJIUZULU

 MANYARA
Na Mwandishi wetu, Tanzaniasasa,


MGOGORO Mkubwa umeibuka kati ya Halmashauri ya Wilaya ya  Simanjiro na uongozi wa mamlaka ya mji mdogo Mirerani wilayani humo baada ya mamlaka hiyo kutangaza msimamo mgumu wa kuzuia watendaji wa Halmashauri hiyo kukusanya mapato ndani ya mji huo na badala yake wao ndio watafanyakazi hiyo.

Adha wajumbe wa mamlaka hiyo wameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kuwataka radhi wajumbe hao kwa madai ya kuwakashifu kwa kuwaita ‘bado watoto wadogo’ kupitia barua waliomuandikia mtendaji mkuu wa mamlaka hiyo baada ya wao kuitaka Halmashauri hiyo kusitisha zoezi la kukusanya mapato ndani ya mji wao.

Uamuzi huo mgumu ulifikiwa jana katika kikao cha wajumbe wanaounda baraza la mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani chini ya mwenyekiti wake Albert Siloli ambao kwa pamoja walimtaka Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo ya mji mdogo  kuiandikia barua Halmashauri kuhusu uamuzi huo walioufikia.

Wajumbe hao walikubaliana kuanza zoezi la kukusanya mapato hayo leo (Julai mosi, 2013), ambapo watatawanyika katika maeneo mbalimbali ya mji huo mdogo wa mirerani na fedha watakazozikusanya wataziweka benki kwa ajili  ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo zinazohusu mji huo.

Diwani wa viti maalum kupitia kata ya Mirerani Rahel Kinaliki akichangia katika kikao hicho baada ya kutuhumiwa kuihujumu mamlaka hiyo, lakini hata hivyo alikanusha na kusema yuko pamoja na wajumbe wengine kuzuia mapato hayo kukusanywa na watendaji wa Halmashauri
Hata hivyo akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Brigedia Jenerali Francis Kayombo alikiri kuwepo kwa mgogoro huo lakini alisema bado Halmashauri ya Wilaya ndio yenye mamlaka ya kukusanya mapato katika eneo hilo kufuatia kuwa na watendaji wa kuweza kusimamia mapato hayo.

“ Mgogoro huu naufahamu lakini hii mamlaka bado ni ndogo sana na haina watumishi  wa kutosha, haina mwekahazina ambae atakuwa na jukumu la kusimamia mapato watakayokusanya lakini zaidi watazihifadhi wapi hizo fedha wapi?, naomba unisubiri mpaka nirudi kutoka safarini nitawapatia taarifa nzuri zaidi,”alisema.

Afisa mtendaji mkuu wa Mamlaka hiyo ya mji mdogo Mirerani, Nelson Msangi alisema mji huo wenye wakazi zaidi ya elfu54 unatakiwa kupokea ruzuku ya milioni 30 kwa mwaka kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro lakini wamekuwa hawapati fedha hizo na kushindwa kulipa madeni inayodaiwa.

Vyanzo vya mapato hayo ni pamoja na ushuru wa stendi ya mabasi mirerani, machinjio, soko, mnada, hoteli, saluni, nyumba za kulala wageni, kodi ya mabango, leseni za vileo na leseni za biashara ambavyo kwa kipindi cha miaka minne toka 2008 eneo hilo lilipopewa hadhi ya mamlaka ya mji mdogo bado halmashauri hiyo ndio imekuwa ikikusanya.

Wakati huo huo Diwani wa kata ya Mirerani na mjumbe wa baraza hilo Justine Nyari amesema endapo Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro itaifuta mamlaka hiyo atakuwa tayari kujiuzulu wadhifa wake wa udiwani kwa kile alichodaiwa itakuwa ni kuihujumu mamlaka hiyo.


Gari la kubeba uchafu ililokabidhiwa mamlaka ya mji mdogo Mirerani, hata hivyo gari hilo ni bovu

Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani Albert Siloli akifungua kikao hicho cha baraza la mamlaka ya mji mdogo Mirerani

Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya mji mdogo Mirerani Nelson Msangi akisoma moja ya barua zilizotoka Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro

Diwani wa kata ya Mirerani Justine Nyari akichangia hoja ya kuizuia Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro kuendelea kukusanya mapato katika mamlaka ya mji mdogo Mirerani leo

mmoja wa wajumbe wa baraza la mamlaka ya mji mdogo Mirerani akichangia hoja katika kikao hicho

No comments: