Wednesday, June 19, 2013

POLISI YAKWAYA CHADEMA, YASHINDWA KUWAFIKISHA MAHAKAMANI WABUNGE ILIYOWAKAMATA, WAFUASI

Wabunge wa CHADEMA wakiwa wamepozi viwanja vya mahakama kuu mkoa wa Arusha wakisubiri wabunge wanne kufikishwa mahakamani hapo

Wabunge wa CHADEMA John Wenje na Muhonga Ruhanywa wakiwa viwanja vya mahakama kuu

Mbunge Selasini wa Rombo na wabunge wengine wakiwa viwanja vya mahakama Kuu jijini Arusha

Wabunge wa CHADEMA Mahakamani


Na Mwandishi wetu, Tanzaniasasa

SAKATA la mlipuko wa bomu jijini Arusha limechukua sura mpya baada ya  Jeshi la Polisi  jijini hapa kutangaza kumtafuta Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema wakituhumiwa kufanya mkutano bila kuwa na kibali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa Kamishana wa Polisi operesheni na mafunzo, Paul Chagonja alisema viongozi hao wa chadema wanatafutwa kwa kuwa walifanya kusanyiko kinyume cha sheria, pasipokuwa  na kibali cha Polisi.

Kamishna Chagonja alisema awali katika mkutano na viongozi wa Chadema uliofanyika katika ofisi za Polisi jijini Arusha , walikubaliana wafike uwanjani hapo kwa ajili ya kuwatawanya wafuasi wa chama hicho waliokuwa wamekusanyika katika uwanja wa Soweto kwa ajili ya taratibu za kuaga miili ya marehemu.

“Tulikubaliana waende pale uwanjani kutawanya wafuasi wao lakini  badala ya kufanya kama tulivyokua tumekubaliana wakaanza kufanya mkutano, huku wakiwatuhumu Polisi kuwa polisi ndio walihusika na shambulio la bomu lililotokea jumamosi”alisema 

Chagonja alisema kuwa baada ya askari kuvumilia matusi hayo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha aliwafuata viongozi wa Chadema na kuwaeleza kuwa hawajaruhusiwa kufanya mkutano katika eneo hilo na kuwataka waondoke katika eneo hilo la Soweto jambo ambalo walilikaidi na Polisi wakaamua kuwatawanya kwa mabomu ya machozi.

Alisema jeshi hilo linashikilia pikipiki 106,baiskeli 16 na gari 6 ikiwemo ya Mwenyekiti wa Chadema Mbowe ambapo vyote vilikamatwa baada ya madereva wa vyombo hivyo vya usafiri kuvitekeleza uwanjani hapo.

Alitoa wito kwa wakazi wa Arusha kutoa taarifa zozote za watu waliohusika na mlipuko wa bomu katika uwanja wa Soweto sanjari na kuwataka kutokaa katika makundi  katika kipindi hiki ambacho jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa mlipuko huo.

WABUNGE KUFIKISHWA MAHAKAMANI

Katika hatua nyingine jeshi la Polisi mkoa wa Arusha likiongozwa na Kamishna wa operesheni na mafunzo Paul Chagonja jana liliwaachia kimyakimya watuhumiwa iliyowakamata kwa madai ya kukusanyika katika uwanja wa Soweto kinyume cha sheria bila kuwafikisha mahakamani kama ilivyotangaza hapo awali.

Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari Kamishna Chagonja aliwatangazia waandishi wa habari kuwa wabunge na wafuasi hao wangefikishwa mahakamani saa 6.00 mchana lakini taarifa iliyotolewa baadae zilisema kuwa wataachiwa wakiwa polisi bila kufikishwa mahakamani.

Umati mkubwa wa wafuasi wa chadema na wabunge wa chama hicho walikuwa wamekusanyika katika viwanja vya mahakama kwa lengo la kuwadhamini watuhumiwa hao waliokamatwa lakini hali ilibadilika baada ya taarifa ya kuwa watuhumiwa hao watadhaminiwa kituo cha polisi na hivyo kulazimika kuondoka mahakamani hapo kuelekea polisi.

Baada ya kufika Polisi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha  Liberatus Sabas aliwaeleza waandishi wa habari  kuwa wabunge wa CHADEMA waliokuwa wamekatwa ambao ni Mbunge wa Mbulu Mustafa Akoonay, Mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani bungeni Tundu Lissu, Joyce Munkya (viti maalum), na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho  na mbunge wa Mpanda Said Arfi walikuwa wamejidhamini na kuondoka kituoni hapo.

Alisema kuwa watuhumiwa wengine 63 ambao ni wafuasi na wanachama wa CHADEMA walikuwa wamedhaminiwa na ndugu zao na  kuruhusiwa kuondoka kituoni hapo.

KAULI YA MBUNGE TUNDU LISSU

Akizungumza baada ya kuachiliwa kwa dhamana Mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni Tundu Lissu alisema jeshi la Polisi limeshindwa kuwafikisha mahakamani kutokana na maelezo ya msingi waliyotoa Polisi.

Lissu ambae pia ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema awali viongozi wa CHADEMA walifanya mazungumzo na viongozi wa Jeshi la Polisi kuhusu kufika uwanjani hapo kutawanya umati wa watu uliokuwa umekusanyika lakini jeshi hilo liliwashambulia kabla hawajawaeleza wananchi hao lengo lao la kufika uwanjani hapo.

Alisema wanashangazwa na jeshi la Polisi kulazimika kutumia nguvu za ziada badala ya kutoa wito kwa kutumia vipaza sauti kuwataka kuondoka eneo hilo kama sheria inavyowataka.

“Polisi hawakutumia taratibu kama sheria zinavyosema, walipaswa kutumia vipaza sauti kutueleza tuondoke eneo lile lakini hata hivyo sisi tulishakubaliana na kabla hatujamaliza mkutano wa kuwatawanya wananchi wakaanza kutushambulia kwa mabomu,”alisema na kuongeza:
“Tumetakiwa kurudi tena polisi Julai 22, mwaka huu ila mimi ninavyojua ukiniambia kuhusu kurudi hiyo ‘imeishatoka, hakuna kesi tena hapo’, tumelazwa sero wanawake na wanaume, tumechangia choo kimoja hiyo inatosha kabisa,”alisema.

NDUGU WA MAJERUHI
Wakati huo huo Ndugu wa majeruhi wa mlipuko wa bomu katika uwanja wa Soweto waliolazwa katika hospitali ya Seliani mkoani hapa wamelalamika kutishiwa na kutaka kutekwa na watu wa usalama pamoja na askari wa jeshi la Polisi.

Akizungumza na waandishi wa  habari katika viwanja vya mahakama kuu jijini hapa, mmoja wa ndugu hao ambae ni pacha na majeruhi Peter Mshanga  aliyelazwa katika hospitali ya Seliani aliyejitambulisha kwa jina la Paul Mshanga alisema ndugu yake huyo ametishiwa na watu wa usalama kwa madai ya kutaka kumhamisha hospitali hapo.

Alisema askari wa upelelezi walidai kutaka kumhamishia katika hospitali nyingine kwa madai ya kuwa hali yake ni mbaya jambo ambalo sio kweli kwani hali yake ni nzuri kwa mujibu wa madaktari hospitali hapo.

“ Sisi tuna wasiwasi sana na usalama wa ndugu yetu, wanataka kumhamishia hospitali nyingi kwa madai eti hali yake ni mbaya,  kwani maofisa hao wa upelelezi wamekuwa hawabanduki hospitalini hapo baada  ya yeye kuhama kwani hali yangu ni nzuri,”alisema Paul ambae ni pacha wa Peter.

KAULI YA MNYIKA
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika viwanja vya mahakama kuu jijini hapa Katibu Mwenezi wa CHADEMA John Mnyika alivitaka vyombo vya usalama nchini kuacha vitisho dhidi ya majeruhi wa mlipuko huo na kwamba vitendo wanavyofanyiwa majeruhi hao ni hatua ya vyombo vya usalama kutaka kupoteza ushahidi dhidi ya tukio hilo   

“ Hata Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari alipata taarifa ya kuwepo kwa maofisa usalama katika hospitali ya Seliani waliokuwa wakizungukia majeruhi huku wakiwa wameshikilia vifaa vya hospitali na kuwatia hofu majeruhi hao, “alisema.

Alisema mbunge huyo baada ya kuwaona watu hao alipiga kelele za kutaka msaada wa kuwakamata na wagonjwa waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo walitoka katika wodi zao na watu hao kutokomea kusikojulikana.

Akitangaza ratiba ya mazishi Mnyika alisema kufuatia jeshi la Polisi kuzuia mkusanyiko wa watu katika viwanja jijini Arusha, chama hicho kimeamua kutoa heshima za mwisho za kuaga mwili wa marehemu Judith Moshi aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Kata ya Sokoni one katika kanisa ambapo ibada itafanyika. 

Mnyika alisema kanisa ambalo ibada hiyo ya mazishi itafanyika na makaburi ambayo marehemu huyo atazikwa vitatangazwa hapo baadae baada ya taratibu zaidi kuendelea kufanyika ambapo anatarajiwa kuzikwa jijini Arusha.

No comments: