Wednesday, July 24, 2013

ALIYEFANYA MAUAJI YA MCHIMBAJI TANZANITE ONE AKAMATWA, SERIKALI YAFUNGA MIGODI MINNE KUPISHA UCHUNGUZI
Na Mwandishi Wetu, Arusha

WAKATI Mmiliki wa mgodi uliodaiwa kutobozana na mgodi wa Tanzanite One,  Joseph Mwakipasile ‘Chusa’ akishikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano kuhusu mauaji ya mfanyakazi wa Kampuni ya Tanzanite One, Willy Mushi, wizara ya Nishati na Madini imefunga migodi minne ya wachimbaji wadogo inayopakana na mgodi wa kampuni hiyo kupisha uchunguzi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa aliwaambia waandishi wa habari eneo la Mirerani jana kuwa jeshi hilo linamshikilia  Mwakalinga katika kituo cha polisi Mirerani kwa mahojiano baada ya kutajwa na wafanyakazi wa Tanzanite One kuwa mhusika wa mauaji ya mwezao.

Marehemu Mushi aliyeacha mjane na watoto wanne aliuawa kwa kupigwa risasi mbili kifuani Saa 6:00 usiku wa kuamkia Julai 20, mwaka huu alipokuwa zamu ya usiku na mfanyakazi mwenzake, Kennedy Msambaji.

“Polisi tunamshikilia Chusa kwa mahojiano baa ya kutajwa kuhusika na tukio la mauaji ya Willy Mushin a tunawaomba wote wenye taarifa za kuhusika kwake na mauaji haya kujitokeza kusadia polisi kukamilisha upelelezi ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake,” alisema Kamanda Mpwapwa.

Kwa upande wake, Kamishina wa madini Kanda ya Kaskazini, Benjamin Mchwampaka alitangaza kuyafunga migodi mine ya wachimbaji wadogo kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi wa tukio la mauaji.

Akizungumza mbele ya mamia ya wafanyakazi Tanzanite One ambao tangu juzi wamekusanyika katika eneo maalum la mikutano ya kampuni hiyo karibu na bwalo lao la chakula, Kamishina Mchwapaka alitaja miongoni mwa migodi iliyofungwa kuanzia jana kuwa ni ya Joseph Mwakalinga ‘Chusa’ anayeshikiliwa na polisi kwa mahojiano kuhusu mauaji hayo.

Wachimbaji wadogo Abdurahakim Mulla, Jackson Simon na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Maningoo ambao migodi yao yapo kitalu “D” pia wamejikuta migodi yao ikifungwa kutokana na uamuzi huo wa serikali kwa sababu inapakana na mgodi wa mwekezaji.

“Timu maalum ya wachunguzi kutoka Wizara ya Nishati na Madini inatarajiwa kuwasili Mirerani kati ya leo na kesho tayari kuanza uchunguzi wa tukio hilo na kubaini migodi yote ya wachimbaji wadogo waliovamia mgodi wa Tanzanite One,” alisema Kamishina Mchwampaka.

Alisema baada ya uchunguzi huo, serikali itaendesha oparesheni maalum kuwaondoa wachimbaji wote waliovamia eneo la mgodi wa Tanzanite One huku akiwataka wote waliovamia eneo la mwekezaji kuondoka wenyewe kwa hiari kabla ya oparesheni.

Hata hivyo, Kamishina huyo alisema mipaka ya migodi eneo la Mirerani ina utata mkubwa, hasa chini ya ardhi kutokana naugwaji uliofanyika miaka ya tisini kutozingatia mahitaji halisi na sheria kwa wachimbaji kugawiwa maeneo madogo yasiyolingana na taratibu za uchumbaji madini ya vito.

Kuhusu usalama kipindi hiki cha mpito cha uchungzi na hali tete ya mahusiano kati ya wachimbaji wadogo na mwekezaji wa Tanzanite One, Kamishina Mchwampaka aliutaka uongozi wa kampuni hiyo kuchukua tahadhari wakati wafanyakazi wake wanaingia chini ya ardhi mgodini ili kuepuka madhara zaidi wakati serikali inaendelea na taratibu zingine za kisheria.

Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi migodini (TAMICO), Raphael Ombade alisema  wafanyakazi wamekubaliana kusitisha mgomo wao uliodumu kwa siku tatu na kuahidi kurejea kazini kuanzia leo baada ya serikali kusikia kilio chao na kuchukua hatua kuhusu mauaji ya mfanyakzi mwezao.

Aidha uchunguzi wa mwili wa marehemu Mushi uliofanywa jana na madakatari na jeshi la polisi kwa kushirikiana ndugu ulibainisha kuwa kifo cha marehemu kilitokana na kupigwa risasi mbili kifuani ambazo zilipatikana mwilini mwake.

No comments: