Sunday, July 21, 2013

JIJI LA ARUSHA KUNUNUA GREDA KUDHIBITI BARABARA KOROFI



Na Mwandishi Wetu, Tanzaniasasa 

HALMASHAURI ya Jiji la Arusha inakusudia kununua magreda na vifaa mbalimbali vya ujenzi wa barabara ili kujijengea uwezo wa kujenga na kuhudumia barabara zake kwa wakati na gharama nafuu.

Akizungumza katika mahojiano maalum ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita, Meya wa Jiji la Arusha, Mstahiki Gaudance Lyimo alisema kwa kuanzia, halmashauri itanunua magreda mawili na rola mbili ifikapo Agosti mwaka huu.

“Fedha kwa ajili ya ununuzi wa Magreda haya mawili na rola tayari tumepata. Tunaendelea kufanya majadiliano na wahusika ili tuweze kupata zana na vifaa vingine kwa njia ya mkopo nafuu ili Jiji liwe na uwezo kamili wa kujenga na kuhudumia barabara zake,” alisema Mstahiki Lyimo.

Katika mpango huo wa kuboresha miundombinu ya barabara, Jiji la Arusha pia linakusudia kuanzisha ujenzi wa barabara za mawe ambazo licha ya kuwa imara lakini pia ujenzi wake hutoa fursa ya ajira kwa vijana wengi watakaohusika katika ukusanyaji na urandazaji wa mawe hayo.

“Wenzetu wa Jiji la Mwanza na Kigali nchini Rwanda tayari wamefanikiwa kujenga barabara za mawe, kwanini sisi tushindwe,” alisema na kuhoji Meya Lyimo.

Alisema mpango huo ukitelezwa kwa mafanikio, kata zote 19 za Jiji la Arusha aidha zitakuwa na barabara za lami au za mawe na hivyo kurahisisha mawasiliano na kuwaondolea adha wananchi wa barabara kutopitika nyakati za masika.

No comments: