Thursday, July 18, 2013

WAANDISHI WA HABARI WATIMULIWA ZIARA YA WAZIRI MKUU SONGEA

Na Gideon Mwakanosya,Songea

WAANDISHI wa habari wawili wawakilishi wa vyombo vya habari tofauti mkoani Ruvuma wamefukuzwa kawenye ziara ya waziri mkuu wa Jamhuri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda kwa kushutumiwa kuandika habari ya ajali iliyotokea kwenye ziara hiyo wakati msafara wa waziri mkuu ukitoka wilayani Tunduru kuelekea wilyani Namtumbo.


Habari zilizopatikana jana mjini Songea ambazo zimethibitishwa na katibu wa chama cha waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma Andrew Chatwanga zimeeleza kuwa tukio la kufukuzwa kwa waanahabari hao wawili limetokea jana majira ya saa 1.45 katika eneo la Ikulu ndogo ya mjini Songea wakati msafara huo unatarajia kuondoka kuelekea wilayani Nyasa.


Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wakiwemo waandishi wa habari wa mkoani Ruvuma ambao walionyesha kushangazwa na tukio hilo la mwandishi wa habari wa ofisi ya waziri mkuu Said Nguba kuwahoji kwa nyakati tofauti wanahabari hao wawili kuhusiana na tukio la ajali iliyotokea juzi kwenye ziara hiyo ya waziri mkuu ambayo ilisababisha magari manne kugongana na kusababisha taharuki kwenye msafara huo huku baadhi yao kujeruhiwa.


Walisema kuwa mara baada ya ajali hiyo kutokea kulitolewa maelekezo na Afisa habari wa mkoa wa Ruvuma Revokatus Ksimba mbele ya waandishi wa habari waliokuwepo kwenye eneo la tukio kuwa taaifa hiyo ya ajali isitangazwe kwenye vyombo vya habari kwa madai kuwa haina madhara makubwa kauli ambayo ilipingwa pale pale na baadhi ya waandishi wa habari .


Ajali hiyo ilihusisha magari manne yenye namba za usajili PT 1437 Mali ya jesji la polisi,STK 7929,DFP 6627 na DFP 8709 iliyokuwa imewabeba baadhi ya waandishi wa mkoa wa Ruvuma pamoja na Afisa habari wa mkoa huo ambaye anadaiwa kuwa alipewa maelekezo na baadhi ya waandishi wa habari waliotoka jijini Dar Es Salaam pamoja na mwandishi wa habari wa ofisi ya waziri mkuu ambao walitoa maelekezo kuwa ajali hiyo ni ndogo na haina haja kuandikwa na kutangazwa kwenye vyombo vya habari jambo ambalo baadhi ya waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma walilipinga kwa sababu wao ndiyo wahanga.

Katika ajali hiyo jumla ya waandishi habari nane wa mkoani Ruvuma walikuwemo kwenye magari mawili kati ya magari manne yaliyopata ajali hiyo iliyotokea kwenye kijiji cha Namingwea wilayani Namtumbo kwenye msafara huo.


Hata hivyo katibu wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Ruvuma Chatwanga alionyesha kusitikishwa na kitendo cha kuwafukuza waandishi wawili ambao ni Nathan Mtega mwakilishi wa ITV na Radio One Stereo mkoani Ruvuma na Ngaiwona Nkondola mwakilishi RFA na STAR TV Mkoani Ruvuma ambao wanadaiwa kuandika na kutangaza habari za tukio hilo la ajali iliyotokea wakati wao kama wanataaluma wa tasnia ya habari wamehabarisha jamii yaliyojiri kwenye msafara huo.


Hata hivyo jitihada za kumpata mwandishi wa habari wa ofisi ya waziri mkuu Nguba zimeshindikana kwa kuwa bado yuko kwenye msafara huo wa waziri mkuu.

No comments: