Friday, August 9, 2013

SINTOFAHAMU KIFO CHA MFANYABIASHARA BILIONEA WA MADINI ARUSHA

Na Mwandishi Wetu, Arusha

SINTOFAHAMU kubwa kuhusu kuuawa kwa mfanyabiashara maarufu wa madini  ya Tanzanite mjini hapa, Erasto Msuya imetawala baada ya marafiki na  watu wake wa karibu kudai kuwa mauaji hayo yamesababishwa na aidha  visasi vya kibiashara au visa vya wivu wa mapenzi.

Katika mahojiano yaliyofanywa na gazeti hili kwa kuzungumza na baadhi  ya marafiki wa karibu na marehemu ambao wameomba  majina yao kutotajwa  gazetini, walisema kipindi cha uhai wake, Msuya alijijengea uhasama  mkubwa kati yake na wafanyabiashara wenzake kutokana na kuingilia dili  za wanaoitwa ‘wakubwa’ katika biashara ya Tanzanite.

Marafiki hao walidai kuwa marehemu alikuwa mtaalam wa kupata madini  kwa kutumia nguvu kubwa hususani madini yaliyokuwa yakipatikana kutoka  kwenye migodi ya kampuni ya Tanzanite One, aidha kwa kuibiwa na  wafanyakazi wa kampuni hiyo au wachimbaji wadogo wanaojipenyeza na
kuingia ndani ya migodi hiyo ya mwekezaji.

Taarifa zaidi zilidai kuwa marehemu alikuwa akinunua madini kutoka kwa  wafanyakazi wa kampuni ya Tanzanite One baada ya kuwazidi  wafanyabiashara wenzake kwa kutoa dau kubwa na hivyo kufanikiwa  kuchukua madini yote ambayo yamekuwa yakipatikana kutoka ndani ya  mgodi huo.

Alisema tabia hiyo ya kuongeza dau kwenye madini yanayoibiwa kutoka  Tanzanite One ilifanya wafanyabiashara wengine kumchukia Msuya na  kumwekea visasi vilivyosababisha waingie kwenye ugomvi hata kutishia  maisha na wakati mwingine kutumia nguvu ya fedha kubambikiana kesi za
jinai.

 Aidha marafiki zake hao walidai kifo chake pia kinawezekana  kusababishwa na tabia yake ya kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi na  wake za watu, wakiwemo wafanyabiashara wenzake wa madini baada ya  kuwarubuni kwa fedha nyingi.

Watoa habari hao walidai kuwa mara nyingi marehemu Msuya alikuwa  akitumia fursa ya safari zake za kibiashara nje ya nchi katika nchi za  Marekani, Thailand, China, Dubai na kwingineko duniani kuchukua wake  za watu na kwenda kutanua nao.

Wakati huo huo hali ya huzuni, majonzi na ukimya jana ilitawala katika  hoteli ya kitalii ya SG Resort ambayo ni miongoni mwa vitega uchumi  kadhaa alizokuwa akimiliki marehemu Msuya ambapo licha ya kuendelea  kutoa huduma, wafanyakazi walikuwa wakimya huku nyuso zao zikionyesha  taharuki kila anapoingia mtu mgeni eneo la hoteli hiyo.

“ Tuna huzuni na mengi ya kueleza kuhusu msiba huu. Licha ya kuwa  mwajiri wetu, pia alikuwa kama rafiki na mzazi kwetu, hatukutarajia  atutoke ghafla na kwa mazingira haya. Siwezi kusema mengi kwa sababu  mimi siyo msemaji wa kampuni,”alisema mmoja wa wafanyakazi wa kampuni  hiyo.

Kwa mujibu wa kaka mkubwa wa marehemu Msuya, Israel Msuya marehemu  anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwa wazazi wake eneo la Mirerani,  wilayani Simanjiro Jumanne ijayo.

Alisema kikao cha dharura cha wanandugu kilichofanyika jana nyumbani  kwa marehemu kiliamua mazishi hayo yafanyike baada ya kufika kwa mmoja  wa watoto wa marehemu anayesoma nchini Australia anayetarajiwa  kuwasili nchini Jumatatu ijayo.

“Marehemu ameacha mjane na watoto wanne ni pigo kubwa kwa familia  kutokana na mazingira yaliyoambatana nayo, hakufariki kwa kuugua wala  ajali, ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana kwa sababu  zisizojulikana pia. Ni huzuni mkubwa kwetu kumpoteza katika mazingira
na tukio kama hilo,” alisema Msuya

Mwili wa marehemu Erasto umehifadhi katika chumba  cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya  kanisa la kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT  ) Seliani jijini hapa.


Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi zinazodaiwa kufikia ishirini na watu wasiojulikana  alipokuwa njiani akiwa eneo la Mijohoroni ambapo inadaiwa alienda kufuata biashara baada ya kupigiwa simu na watu hao kufanya biashara ambayo hata hivyo haikujulikana ni biashara gani.

No comments: