Sunday, September 15, 2013

MAMIA WAJITOKEZA KUPOKEA WALIOANDAMANA KUPINGA UJANGILI NA PEMBE ZA NDOVU NCHINI



Na Mwandishi Wetu, TANZANIASASA
MAMIA ya wakazi wa jiji la Arusha, juzi walijitokeza katika uwanja mdogo wa ndege Arusha kuwapokea watu walioandamana kwa kutembea kwa miguu kutoka Arusha hadi jijini Dar es Salaa kupinga vitendo vya ujangili na biashara ya pembe za ndovu.
Maandamano hayo yaliyozinduliwa na Mkuu wa mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo Agosti 24, mwaka huu na kupokelewa jijini Dar es Salaam Septemba 12, mwaka huu na Naibu waziri wa Utalii na Maliasili, Lazaro Nyalandu, yaliandaliwa na kuongozwa na Mtanzania mwenye asili ya Asia, Pratik Patel kupitia Taasisi ya African Wildlife Trust ya jijini Arusha.
Pamoja na Patel, muandamanaji mwingine aliyeanzia safari yake kutoka Arusha katika eneo la jengo la Mkuu wa mkoa hadi Dar es Salaam ni raia wa Marekani, Maraya Cornel.
Akizungumza mara baada ya mapokezi hayo, Patel aliwataka Watanzania wote kushiriki vita dhidi ya ujangili na biashara ya pembe za ndovu kwani jukumu la ulinzi wa marasilimali za taifa linahusu raia wote bila kujali tofauti zao kiuchumi, kisiasa na kimaeneo (kikabila).
“Taasisi kama Shirika la hifadhi za taifa (TANAPA) na Mamlaka ya bonde la Ngorongoro (NCAA) na mamlaka zingine za serikali zimepewa tu dhamana ya kusimamia na kuongoza shughuli za uhifadhi. Lakini ukweli ni kwamba sote tuna wajibu wa kulinda rasilimali zetu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Patel
Kwa upande wake, mmoja wa waongoza watalii aliyehudhuria mapokezi hayo, Engbeth Quorro aliwaomba viongozi serikalini na wale wa kisiasa kuwa na dhamira safi katika usimamizi wa maliasili na rasilimali za taifa.
“Wote wenye dhamira mbaya na rasilimali zetu wadhibitiwe mara moja bila kujali nyadhifa zao hata itakapobainika kuwa miongoni mwao wamo viongozi wa serikali au wanasiasa wenye ushawishi,” alisema Quorro
Awali akizindua maandamano hayo wiki tatu zilizopita, Mkuu wa Arusha, Mulongo alisema ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki vita dhidi ya ujangili kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwatia mbaroni wanaojihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo.
“Wahifadhi, wasimamizi na watekelezaji wa sheria za uhifadhi watimize wajibu na majukumu yao kwani wasipofanya hivyo hawatabaki salama katika msako dhidi ya majangili unaoendelea,” alisema Mulongo
Kaimu Mkuu wa Kikosi cha kupambana na ujangili Kanda ya Kaskazini, Michael Melakiti alisema kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita pekee, watuhumiwa 64 wametiwa mbaroni kwa makosa ya kujihusisha na ujangali katika kanda hiyo ambapo 51 kati yao walipigwa faini ya Sh. 10.6 milioni.
Melakiti alisema kipindi hicho kinachoanzia Juni mwaka jana hadi Juni mwaka huu, watuhumiwa 11 walifikishwa mahakamani na kesi zao ziko katika hatua mbalimbali huku mmoja akipewa onyo kwa maandishi.
Alisema katika kipindi hicho, jumla ya Tembo 29 waliuawa na nyara zake kuchukuliwa na majangili. Tembo hao waliuawa katika wilaya za Ngorongoro, Rombo, Monduli, Longido na Simanjiro.
Licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa, sekta ya utalii nchini inachangia asilimia 17 ya pato la taifa.
Mwisho.

No comments: