Friday, October 4, 2013

SERIKALI YAFANYA MAAMUZI MAGUMU, YAAMURU MAJANGILI KUUWAWA WANAPOKAMATWA

NA SEIF MANGWANGI

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki amewaagiza Askari wa  wanyamapori na vikosi vyote vinavyolinda wanyama pori katika hifadhi  za Taifa na Mapori ya Akiba kuwaua majangili pindi watakapowakamata  ili kukomesha tatizo hilo nchini na duniani.

Akizungumza kwenye kilele cha matembezi ya kupinga mauaji ya tembo  duniani katika maazimisho yaliyofanyika jijini Arusha kitaifa, Kagasheki alisema kwa kauli yake hiyo anatarajia kupingwa vikali na
watetezi wa haki za binaadam lakini hiyo ndio hali halisi.
Vijana wakiwa kwenye matembezi ya kulaani kuuawa kwa wanyamapori ikiwemo Tembo, matembezi yaliyoanzia katika eneo la ofisi za TANAPA

Matembezi yakiendelea huku nyimbo mbalimbali zikiimbwa

Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi akijadiliana jambo na mmoja ya waliokuwepo kwenye maandamano hayo

Mkurugenzi wa TANAPA Allan Kijazi wa kwanza kulia akinywa maji huku akirufahi jambo wakati watoto wakionyesha shoo katika maonyesho hayo

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamisi Kagasheki akipokea zawadi kutoka kwa wanafunzi wa Upendo Academy ya jijini Arusha

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamisi Kagasheki akihutubia mamia ya wakazi wa Arusha waliojitokeza kwenye matembezi hayo
Wanafunzi wa kituo cha kulelea watoto cha Watoto Foundation wakiwa katika picha ya pamoja na waziri wa Maliasili na Utalii Khamisi Kagasheki

“Ukiniuliza mimi nini cha kuwafanya majangili wanaoteketeza  wanyamapori wetu nitakujibu kuwa wanapaswa kuuwawa huko huko wanapokamatwa na hii itasaidia kutokomeza kabisa jambo hili ambalo
linamaliza wanyamapori wetu nchini na duniani,”alisema.

Alisema kuwa jangili yoyote akikutana na askari atakachofanya ili kujinasua ni kumuua askari huyo hivyo ni wazi kutangulia kuwaua wao itakuwa ndio suluhu ya matatizo ya kumalizika kwa wanyamapori nchini
jambo ambalo linahatarisha kumalizika kwa urithi wa Taifa la Tanzania.

 Kagasheki pia aliwageukia wanasiasa na kusema kuwa wamekuwa sehemu ya  kukwamisha jitihada za Serikali za kupambana na ujangili kwa kuwatetea  baadhi ya watu ambao wamekuwa wakihusika kuteketeza wanyamapori  nchini.

Alisema hata hivyo Serikali imelitambua hilo hivyo itapambana nao ili kuhakikisha suala la mapambano dhidi ya majangili linafanikiwa huku akiwasihi kufanya kazi ya siasa kama ambavyo wamekuwa wakiomba kwa
wapiga kura wao na kuiachia Serikali kupambana na majangili.

Kagasheki alisema ili kudhibiti ujangili nchini, Jeshi la Wanachi wa Tanzania (JWTZ), limejumuishwa kwenye mchakato wa mapambano dhidi ya majangili nchini na kuwataka majangili waliokuwepo kwenye matembezi
hayo kujiandaa katika mapambano hayo na ambao hawajakuwepo wapelekewe  salamu.

“ Najua miongoni mwetu kuna majangili napenda kuwaambia kuwa siku zenu  sasa zimefika mwisho, na wale ambao hawapo wapelekeeni salamu, Serikali kupitia kwa Rais Kikwete imeamua kuliingiza jeshi kwenye
mapambano ya kuokoa rasilimali wanyamapori na nina uhakika  tutafanikiwa,”alisema Kagasheki.

Akizungumzia sheria ambazo wamekuwa wakihukumiwa majangili, Waziri  Kagasheki alisema wizara yake inatarajia kupeleka mabadiliko ya Sheria hiyo bungeni ambayo itawezakutoa adhabu kali kwa watakaokamatwa wakifanya ujangili.

“Adhabu wanayopewa mahakamani majangili ni sawa na utani kabisa, na  ndio maana kila kukicha majangili wanaongezeka hivi sasa tumeamua kupeleka mswada wa mabadiliko ya sheria hii ili kutoa hukumu kali
zaidi na kutokomeza tatizo la majangili nchini.”alisema Kagasheki.

Awali akitoa salamu katika matembezi hayo Mwenyekiti wa Chama cha  waendesha utalii nchini (TATO), Willy Chambulo aliiomba Serikali kusitisha zoezi la uwindaji wa wanyamapori kama Tembo ili kukomesha
tatizo hilo nchini.

Pia Chambulo aliiomba Serikali kuzungumza na nchi ambazo zimekuwa  kinara wa ununuzi wa meno ya tembo ikiwemo China ili kushiriki kwenye mapambano dhidi ya mauaji ya mnyama huyo nchini na duniani.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi za wanyamapori (TANAPA), Allan Kijazi aliwataka watanzania kuungana na Serikali kwenye mapambano dhidi ya ujangili na kwamba endapo hawatafanya hivyo shirika hilo litakufa kwa kuwa litakuwa hakuna itakachokuwa ikikihifadhi.

Alisema wananchi ndio ambao wamekuwa wakikaa na majangili majumbani mwao hivyo ni wajibu wao kuwataja hadharani ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa lengo la kunusuru maliasili ya Taifa.

No comments: