
SINTOFAHAMU kubwa kuhusu kuuawa kwa mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite mjini hapa, Erasto Msuya imetawala baada ya marafiki na watu wake wa karibu kudai kuwa mauaji hayo yamesababishwa na aidha visasi vya kibiashara au visa vya wivu wa mapenzi.
Katika mahojiano yaliyofanywa na gazeti hili kwa kuzungumza na baadhi ya marafiki wa karibu na marehemu ambao wameomba majina yao kutotajwa gazetini, walisema kipindi cha uhai wake, Msuya alijijengea uhasama mkubwa kati yake na wafanyabiashara wenzake kutokana na kuingilia dili za wanaoitwa ‘wakubwa’ katika biashara ya Tanzanite.
Marafiki hao walidai kuwa marehemu alikuwa mtaalam wa kupata madini kwa kutumia nguvu kubwa hususani madini yaliyokuwa yakipatikana kutoka kwenye migodi ya kampuni ya Tanzanite One, aidha kwa kuibiwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo au wachimbaji wadogo wanaojipenyeza na
kuingia ndani ya migodi hiyo ya mwekezaji.
Taarifa zaidi zilidai kuwa marehemu alikuwa akinunua madini kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni ya Tanzanite One baada ya kuwazidi wafanyabiashara wenzake kwa kutoa dau kubwa na hivyo kufanikiwa kuchukua madini yote ambayo yamekuwa yakipatikana kutoka ndani ya mgodi huo.
Alisema tabia hiyo ya kuongeza dau kwenye madini yanayoibiwa kutoka Tanzanite One ilifanya wafanyabiashara wengine kumchukia Msuya na kumwekea visasi vilivyosababisha waingie kwenye ugomvi hata kutishia maisha na wakati mwingine kutumia nguvu ya fedha kubambikiana kesi za
jinai.
Aidha marafiki zake hao walidai kifo chake pia kinawezekana kusababishwa na tabia yake ya kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi na wake za watu, wakiwemo wafanyabiashara wenzake wa madini baada ya kuwarubuni kwa fedha nyingi.
Watoa habari hao walidai kuwa mara nyingi marehemu Msuya alikuwa akitumia fursa ya safari zake za kibiashara nje ya nchi katika nchi za Marekani, Thailand, China, Dubai na kwingineko duniani kuchukua wake za watu na kwenda kutanua nao.
Wakati huo huo hali ya huzuni, majonzi na ukimya jana ilitawala katika hoteli ya kitalii ya SG Resort ambayo ni miongoni mwa vitega uchumi kadhaa alizokuwa akimiliki marehemu Msuya ambapo licha ya kuendelea kutoa huduma, wafanyakazi walikuwa wakimya huku nyuso zao zikionyesha taharuki kila anapoingia mtu mgeni eneo la hoteli hiyo.
“ Tuna huzuni na mengi ya kueleza kuhusu msiba huu. Licha ya kuwa mwajiri wetu, pia alikuwa kama rafiki na mzazi kwetu, hatukutarajia atutoke ghafla na kwa mazingira haya. Siwezi kusema mengi kwa sababu mimi siyo msemaji wa kampuni,”alisema mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa kaka mkubwa wa marehemu Msuya, Israel Msuya marehemu anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwa wazazi wake eneo la Mirerani, wilayani Simanjiro Jumanne ijayo.
Alisema kikao cha dharura cha wanandugu kilichofanyika jana nyumbani kwa marehemu kiliamua mazishi hayo yafanyike baada ya kufika kwa mmoja wa watoto wa marehemu anayesoma nchini Australia anayetarajiwa kuwasili nchini Jumatatu ijayo.
“Marehemu ameacha mjane na watoto wanne ni pigo kubwa kwa familia kutokana na mazingira yaliyoambatana nayo, hakufariki kwa kuugua wala ajali, ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana kwa sababu zisizojulikana pia. Ni huzuni mkubwa kwetu kumpoteza katika mazingira
na tukio kama hilo,” alisema Msuya
Mwili wa marehemu Erasto umehifadhi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya kanisa la kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT ) Seliani jijini hapa.
Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi zinazodaiwa kufikia ishirini na watu wasiojulikana alipokuwa njiani akiwa eneo la Mijohoroni ambapo inadaiwa alienda kufuata biashara baada ya kupigiwa simu na watu hao kufanya biashara ambayo hata hivyo haikujulikana ni biashara gani.
No comments:
Post a Comment