mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha Namelok Sokoine akimjulia hali mmoja wa watoto wenye ulemavu wa mtindio wa ubongo katika kituo cha kulelea walemavu kilichopo Monduli jijini Arusha
Na Seif Mangwangi, Monduli
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida,
juzi Katibu wa umoja wa wanawake wa CCM (UWT), Mkoa wa Arusha Stamili Dendegu
alijikuta akitokwa machozi baada ya kupata taarifa ya mahitaji muhimu yanayokikabili
kituo cha kulelea watoto yatima waliopasuliwa miguu na kunyooshwa kufuatia kuzaliwa
wakiwa walemavu.
Katibu huyo aliyekuwa akimribisha
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Arusha Namelok Sokoine aliyetembelea kituo hicho cha
walemavu kilichopo Monduli kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki jimbo la Arusha,
alisema watoto hao wanahitaji kupata msaada mkubwa kutoka kwa watanzania wote
na sio kuliachia kanisa pekee.
“Jamani tuwaonee huruma hawa
watoto, na wale watoto waliokuwa majumbani ni vyema wakaletwa hapa wapate
msaada, hata hivyo kituo kinakabiliwa na uhaba wa fedha za kujiendesha inatia
uchungu sana, ndugu zangu tujitokeze kusaidia hawa watoto kwa fedha na mahitaji
mengine,”alisema huku akitokwa machozi.
Akizungumza katika hafla hiyo fupi
iliyoenda sanjari na ugawaji wa misaada mbalimbali ya kibinaadam, Namelok
Sokoine alisema kituo hicho kimekuwa kikikabiliwa na upungufu wa fedha za
kujiendesha jambo ambalo limeulazimu uongozi wa kituo kuwatoza wazazi wa watoto
wanaofikishwa kituo hicho sh1500 kwa siku.
“Disemba mwaka jana nilitembelea
hiki kituo na kukuta tatizo kubwa wanalokabiliana nalo ni ukosefu wa ufadhili
na kulazimika kuwatoza wazazi wa watoto wanaoletwa kwa matibabu hapa Tsh1500,
kihalisia ni fedha ndogo lakini kwa hali duni za wazazi ni fedha nyingi sana na
ndio maana leo nimetembelea hapa kuleta msaada kidogo,”alisema.
Alisema ni wakati sasa wa kila
mtanzania kujiona ni mwenye jukumu la kusaidia yatima na wasiojiweza ili waweze
kupata mahitaji muhimu ikiwemo fedha za matibabu na kuwaondolea hali ya ulemavu
waliyokuwa nayo.
Awali akitoa taarifa ya kituo
hicho, Mratibu wa kituo Mireile Kapilima alisema kituo hicho kimekuwa
kikikabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa ufadhili na kwamba mahitaji
yamekuwa mengi kulingana na uwezo wa kituo ambapo hivi sasa kinalaza wagonjwa
52 huku uwezo wake ikiwa ni kulaza watoto 30.
Misaada mbalimbali ilitolewa jana
na mbunge Namelok ni pamoja na Blanketi kwa ajili ya kujifunika, unga, sabuni,
mafuta ya kupikia na fedha.
|
No comments:
Post a Comment