TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA KWA UMOJA WA WANAFUNZI WALIOFUKUZWA VYUO NA VIKUU NCHINI UTANGULIZI 14.03.013
Awali ya yote tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema na fadhia ambaye amekuwa ni tumaini la maisha yetu.
Ndugu waandishi wa habari, Mbele yenu ni umoja wa wanafunzi
tuliofukuzwa vyuo vikuu nchini. Umoja huu unaitwa UUEST na unahusisha
vyuo vikuu vifuatavyo; Chuo kikuu cha Dar es Salaam “UDSM”, Chuo kikuu
cha Dodoma “UDOM” na Chuo kikuu cha Mhimbili “MUHAS”,Chuo kikuu cha
MWALIMU NYERERE MEMORIAL, MUCCOBS, IFM na STJN. Umoja huu ulianzishwa
rasmi tarehe 26/01/2013 baada ya maazimio ya wanafunzi waliofukuzwa
kutoka vyuo husika kukubaliana kutengeneza umoja tajwa hapo juu.
Historia ya nchi yetu inaonyesha kuwa timua timua ndani ya vyuo vikuu
nchini ilianza miaka ya 1990 [1992] lakini miaka ya 2008 hadi sasa suala
hili limezidi kuwa kubwa ndani ya taifa letu,watawala wa vyuo vikuu
nchini ambao ni maprofesa na baadhi ya viongozi waliopo serikalini
wanalichukulia suala hili la kikatili kama mila na desturi na ni haki
yao kimsingi kufukuza wanafunzi wa vyuo vikuu wenye mawazo mbadala,
wenye uwezo wa kuhoji mambo, kukosoa uovu uliopo na unaoendelea
kutendeka ndani ya vyuo vyetu na ndani ya taifa letu na wenye uwezo wa
kutoa ushauri pale inapobidi kwa maslahi ya taifa lao. Ndugu waandishi
wahabari, Kimsingi timua timua vyuoni ni janga la kitaifa ndani ya vyuo
vikuu nchini na hakika tukilifumbia macho tunalizika taifa letu huku
macho yetu yanashuhudia kwa sababu tunaidadi kubwa ya wanafunzi
tuliofukuzwa vyuoni bila makosa kama takwimu hapo chini zinavyojionyesha
na hatukustahili adhabu tulizopewa, pia tunatambua kunamikakati ya
wazi iliyowekwa na baadhi ya viongozi waliopo serikalini wakishirikiana
na watawala wa vyuo vikuu kuvizika vyuo vikuu visiwe visima vya fikra
huru “think tank of our nation” na hii ni kwa sababu ya mfumo mbovu wa
kuwapata watawala wa vyuo vikuu, mfumo huu wa kuteuana unawafanya
watawala wa vyuo vikuu kutokuwa huru na kuwaabudu waliowateua, kutumika
kisiasa, kukosa utashi wa maamuzi na kushinikizwa kufanya maamuzi ambayo
hayaendani na utashi wa taaluma zao. Hii inapelekea vyuo vikuu kutokuwa
huru na kuenenda kinyume na Tamko la Ulimwengu la tarehe 29th April,
1990 linalohusu uhuru wa kitaaluma (Academic Freedom) ambalo sisi kama
taifa tuliridhia kulisaini hapa Dar Es Salaam ,Tanzania. Tamko hili
linasema wazi kuwa ni lazima Vyuo vijiendeshe kwa uhuru kamili bila
kuingiliwa na serikali .
Ndugu waandishi wa Habari, baada ya juhudi tulizozifanyandani ya mfumo
na nje ya mfumo bila mafanikio na baada ya kupata taarifa mbaya juu
yetu ambazo watawala wa vyuo vikuu walizipeleka ndani ya mfumo na nje ya
mfumo kwa lengo la kutuchafua, tukaona tunahaja ya sisi wanafunzi
tuliofukuzwa vyuo vikuu nchini kutafutana na kuungana kwa ajili ya
kupeana taarifa rasmi za ndani ya mfumo na nje ya mfumo na pia tuamue
hatima ya maisha yetu kwa kuwa na sauti moja, kupeana matumaini,
kufikiri pamoja, kupanga na kufanya juhudi za pamoja ilikuhakikisha kila
mmoja wetu anatimiza ndoto zake kielimu kwa namna yoyote ile.
TAKWIMU ZA WANAFUNZI TULIOFUKUZWA VYUONI MWAKA WA MASOMO 2011/2012
Kuanzia mwaka 2011 mpaka sasa, ni zaidi ya wanafunzi 145 wamefukuzwa
ndani ya vyuo vyetu nchini. Tukimaanisha UDSM, UDOM, MUHAS, MWALIMU
NYERERE MEMORIAL, MUCCOBS, IFM, STJN, na MZUMBE. Sababu zilizofanya
wanafunzi hawa kufunzwa vyuoni ni kama ifuatavyo; Kudai mafunzo kwa
vitendo,vifaa vya kujifunzia na mazingira bora ya kijifunzia Kudai
kurejeshwa kwa serikali ya wanafunzi iliyofutwa na watawala wa vyuo
Kudai mikopo ambayo inawasaidia kulipa ada zao na kujikimu maisha wakiwa
vyuoni Kimsingi kupoteza ndoto za wanafunzi zaidi ya 145 ambao
kiuhalisia wamesomeshwa na kodi za watanzania kwa sababu tu ya kudai
haki zao za msingi ndani ya taifa lao ni kitendo kisichokuwa na dira
njema kwa taifa.
Kwa sasa tuna msiba wa taifa katika sekta ya elimu, wanafunzi wengi
waliofeli kidato cha nne ni watoto wa masikini waliosoma shule za kata,
watoto hao hao wanaojitahidi kusoma na kufika vyuoni, wananyimwa mikopo,
wananyimwa mafunzo kwa vitendo na wanaposimama kudai haki zao ili
wamudu maisha ya kitaaluma vyuoni wanafukuzwa kikatili na kusingiziwa
vitu wasivyovitenda. Uhalisia ni kwamba Taifa hili linatengeneza Tabaka
la walionacho waendelee kuwaburuta tabaka la wasionacho.
NJIA TULIZOTUMIA KUTAFUTA SULUHU
Mara baada ya kufukuzwa vyuo vikuu nchini, tuliamua kuchukua hatua mbali
mbali za kidiplomasia ili kuhakikisha suala letu linapatiwa ufumbuzi.
Zifuatazo ni hatua tulizozifanya ndani ya taifa letu;
Tulifanya hatua za ndani ya vyuo vyetu ikiwemo kukata rufaa kwa maamuzi
yaliyofanyika zidi yetu, kuomba mabaraza ya vyuo vyetu yapitie upya
maamuzi yaliyofanyika kwa kuwaeleza ukweli halisi kinyume na taarifa
potofu walizozitoa mbele ya vyombo vya habari bila mafanikio yoyote.
Tuliamua kwenda kwa waziri wa elimu Mh. Shukuru Kawambwa na kutuma
taarifa sahihi kinyume na taarifa potofu zilizotolewa na watawala wa
vyuo vyetu bila mafanikio yoyote.
Tuliamua kutuma taarifa sahihi kwa waziri mkuu wa nchi, Mh. Peter
Kayanza Pinda na kumueleza ukweli halisi kinyume na taarifa potofu
zilizotolewa na watawala wa vyuo vyetu, bila mafanikio yoyote.
Tarehe 27/07/2012 tuliamua kutuma waraka wa wanafunzi tuliofukuzwa vyuo
vikuu nchini Bungeni kupitia kwa waziri kivuli wa Elimu Mh. Suzan. Lymo
ili Bunge nalo lituhukumu kwa uhalisia wa taarifa tuliyoipeleka,
Mh.mbunge aliwasilisha taarifa yetu wakati anasoma taarifa yake lakini
tarehe 14/08/2012, waziri wa Elimu Mh. Shukuru Kawambwa aliipuuza hoja
hii inayohusu mustakabali wa maisha yetu kielimu ndani ya taifa letu. 5.
Tuliamua kwenda kamati ya bunge ya huduma za jamii na kuwapelekea
taarifa rasmi juu ya matatizoyetu kinyume na taarifa za watawala wa vyuo
vikuu bila mafanikio yoyote
6. Tuliamua kuwafuata viongozi mbali mbali ndani ya taifa letu ambao
tulihisi watatusaidia kwa namna moja au nyigine, tulichoambulia ni
taarifa mbaya zidi yetu ambazo zimepangwa na watawala wa vyuo vikuu
wakishirikiana na baadhi ya viongozi serikalini.Ndugu waandishi wa
habari; baadhi ya taarifa hizi ni kama zifuatazo ambazo tulizitoa kwa
kiongozi nyeti ndani ya taifa hili.
Hatuta soma ndani ya nchi hii mpaka uongozi uliopo madarakani uondoke hivyo tusubiri miaka mitatu minne,
Tuliopo mahakamani tunajisumbua hatuwezi kupata haki katika mahakama,
Hatutadahiliwa chuo chochote nchini.
7. Tuliamua kupeleka taarifa katika asasi mbali mbali zisizo za
kiserikali, LHRC, TLS, FORDIA, TAMWA, TAWLA, nk. Ili kuwaambia taarifa
za ukweli na kuwaomba msaada wao wanaoweza kutupatia kutokana na tatizo
letu. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwani baadhi yetu tulipata msaada wa
kisheria toka LHRC na TLS.
8.Tuliamua kwenda katika asasi za kidini, tulituma taarifa sahihi kwa
viongozi wetu wa kidini ili kupata msaada wao wa kiroho na kuliombea
suala letu, pia wao kama viongozi wa dini kuingilia kati juu ya uonezi
uliofanyika lakini mpaka leo bado suala letu halijapata ufumbuzi.
SABABU ZA KUUNDA UMOJA HUU
Tunafahamu kuwa ndani ya taifa letu tuna mihimili mikuu mitatu,
Serikali, Bunge na Mahakama, mpaka sasa Serikali ya jamhuri ya muungano
wa Tanzania na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halijawa suluhu
ya matatizo yetu na hii ni kwa sababu ya taarifa potofu zilizotolewa na
watawala wa vyuo vikuu nchini, na kupelekea kuchafua taswira zetu na
kupoteza utu wetu mbele ya jamii. Ndugu waandishi wa habari;
Tumechukua hatua stahiki mbali mbali kama ilivyoelezwa hapo juu bila
mafanikio yoyote, na tukizingatia matamko ya watawala wa vyuo vikuu kuwa
haturuhusiwi kudahiliwa vyuo vyovyote vya umma ndani ya Taifa letu
kiuhalisia nisawa na kuwa tumehukumiwa adhabu ya kifo ndani ya Taifa
letu na sisi tunaamini hatustahili adhabu hii.
kwa sababu watawala wa vyuo vikuu wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa
kututenganisha na jamii zetu, familia zetu, ndugu na jamaa, viongozi
wetu wa kidini na kisiasa kwa taarifa za uongo kupitia vyombo vya habari
tumeona suluhu ya maisha yetu ni kuungana, muungano huu umeundwa kwa
sababu zifuatazo;
1.Hatua zote tajwa hapo juu tulizozichukua ndani ya Taifa letu zimeshindikana.
2.Wote tulikuwa tuna tatizo la aina moja la kufukuzwa vyuo vikuu kwa
sababu ya uzalendo wetu wa kutetea haki zetu na haki za wavujajasho
ndani ya taifa letu
3.Tumeungana kwa sababu nafsi nyingi za wanafunzi tuliofuzwa vyuoni
zinakufa, kwa sababu ya kukosa matumaini ya maisha, kukosa msaada kutoka
katika familia na jamii tunayotoka, hali hii ilitokana na taarifa
potofu zilizotolewa na watawala wa vyuo vikuu wakishirikiana na serikali
kupitia vyombo vya habari, kutusingizia kuwa ni vinara wa vurugu,
tumepiga wajawazito, tumebaka, tumetengeneza mabomu, tunatumiwa na vyama
vya siasa na kashfa mbali mbali ambazo jamii kwa ujumla wake
walijengeka kuwa sisi ni watu hatari na hatufai hatimaye kututenga
katika mapito yetu.
Kiujumla hizi ndizo sababu zilizotufanya tuungane.
AZIMIO LETU
Tunaiomba serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunamuomba raisi
Jakaya Mrisho Kikwete alichukulie jambo hili kwa uzito unaostahili huku
akiangalia mustakabali wetu na wa taifa letu. Lakini umefika wakati
wetu wa kuwaambia ukweli kwamba tumenyanyaswa, tumepuuzwa,tumebezwa,
tumetukanwa , tumeteswa na tumeonewa kwa mda mrefu mpaka hivi sasa kana
kwamba sisi ni watumwa kwenye nchi hii.
HITIMISHO
Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini tutambue kwamba sisi ni sehemu ya
wanajamii ya kitanzania. Hivyo kwa nafasi yetu tuna haki na ni wajibu
wetu kukemea,kurekebisha,kuhoji na kushauri pale tunapoona mambo
yanaenda ndivyo sivyo.Vyuo vikuu vimepoteza dira, macho yetu
yanashuhudia. Taifa letu limekuwa shamba la bibi, tunashuhudia hayo na
bado tupo kimya, vyuo vyetu vinazimwa visiwe visima vya fikra huru.
Maadili ya viongozi ndani ya taifa letu yamepotea. Bunge linashindwa
kulitendea haki taifa hili kwa sababu ya mvutano wa kiitikadi wasomi
tunashindwa kunyosha vidole vyetu kukemea uovu, Tunashindwa kusimama
kulisaidia taifa letu, kwa sababu ya mabomu, risasi,virungu tunayopigwa
tukisimama kutetea muafaka mwema wa taifa letu, vijana wa taifa hili
tufumbue macho. Ikumbukwe kuwa Mwl J.K.Nyerere aliwahi kufika chuo kikuu
cha Dar es Salaam wanafunzi walipogoma, alienda akawasikiliza akayapima
na akatambua kuwa wanafunzi wanahoja za msingi akaamua aanze
kujipunguzia mshahara wake mwenyewe kwanza. Huyu ni mfano kiongozi wa
kuigwa ambaye anahitajika ndani ya taifa letu. Suluhu ya matatizo vyuo
vikuu nchini sio timua timua, sio vitisho na Mabavu, sio nguvu ya vyombo
vya dola, sio mabomu, sio risasi za moto, sio virungu ila ni busara
kama aliyoitumia hayati Mwl. J. K . Nyerere kuenda kusikilizana na
kupata muafaka sahihi.
MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA 13/03/2013.
RAI YANGU KWA WATANZANIA.
MIMI KAMA MSEMAJI MKUU WA UMOJA HUU "UUEST".
HII NI TAARIFA SAHIHI KUTOKA KWETU. CHOMBO CHOCHOTE CHA HABARI, MTU
YOYOTE YULE ATAYEPOTOSHA UKWELI HUU MFAHAMU ANALENGO LAKE BINAFSI AU
AMENUNULIWA.
LAKINI PIA NACHUKUA FURSA HII KUWAOMBA WATANZANIA WOTE YANI VIONGOZI
WEMA WALIOKO SERIKALINI, VIONGOZI WEMA WA KIDINI, WABUNGE WOTE BILA
KUJALI ITIKADI ZA VYAMA VYETU, ASASI ZOTE ZOTE ZA KISERIKALI NA ZISIZO
ZA KISERIKALI, NA WADAU MBALI MBALI AMBAO WANATAMBUA KUWA TULIPOFIKA
KAMA TAIFA NI PABAYA NA NI HATARI KWA AMANI YA NCHI HII. WATUUNGE MKONO
KWA NAMNA MOJA AU NYINGINE ILI KUHAKIKISHA NDOTO ZA VIJANA ZA KIELIMU
ZILIZOPOTEZWA ZINAPATIKANA KWA NJIA YOYOTE ILE. HIVYO KUANZAIA SASA
TUNAKUJA KWENU WATANZANIA.
KWA WALE WOTE WALIOPOST KUWA TUMEOMBA MSAMAHA HAMJUI MLITENDALO, MJUE
KUWA NI UDHALIMU TU TUMETENDEWA NDANI YA TAIFA LETU . MKIKUA KIFIKRA
MTAYAACHA HAYO, HATUNA UGONVI NA NYIE ILA MTAMBUE KUWA TAIFA LETU
LINALIA NA TUNAHITAJI NGUVU YA PAMOJA ILI KULIKOMBOA TAIFA BILA KUJALI
ITIKADI ZETU ZA KIDINI, KIVYAMA, MAKABILA YETU. ILA KWA PAMOJA TUBEBE
ITIKADI YA UTANZANIA, HAKIKA TUTAFIKA.
WANAFUNZI WA VYUO VIKUU LISAIDIENI TAIFA.
MWISHO KABISA NI WAJIBU WA RAISI JAKAYA KIKWETE KULITENDEA HAKI TAIFA
HILI. MOYO WAKE UTAMBUE KUWA VYUO VIKUU NI INJINI YA NCHI YOYOTE
ILE DUNIANI, NI VISIMA VYA FIKRA HURU NA HUU NI UKWELI AMBAO UTASIMAMA
MILELE.KUVIZIMA VYUO VIKUU NI KULIZIKA TAIFA, KITU AMBACHO NAAMINI RAISI
WETU HANA LENGO HILO. TUTAITAMBUA DHAMIRA YA RAISI WETU JAKAYA MRISHO
KIKWETE KWA VITENDO NA SI VINGINEVYO.
MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA.
No comments:
Post a Comment