muonekano wa bwawa la Kalemawe lililopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro wakati UNCDF walipotembelea eneo hilo.
ZAIDI ya watu 10,000 wanaozunguka bwawa la Kalemawe wilayani Same mkoani Kilimanjaro watanufaika na ukarabati wa bwawa hilo na kuwekewa muundo mpya wa kiutawala na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Ukuzaji wa Mitaji (UNCDF).
Bwawa hilo ambalo lipo katika kata za Kalemawe na Ndungu lilijengwa na watawala wa Kiingereza mwaka 1952-1959 kwa ajili ya kusaidia shughuli za kilimo na ufugaji baada ya kuanzishwa kwa hifadhi ya Mkomazi na hivyo wakazi kuzuiwa kwenda katika hifadhi hiyo kwa shughuli mbalimbali.
Taarifa ya kuwepo kwa mradi huo mkubwa, imetolewa na Mkuu wa ushauri wa ufundi wa Mfuko wa Umoja wa mataifa wa Ukuzaji Mitaji (UNCDF) nchini, Bw. Peter Malika wakati akiwakaribisha madiwani wa kata hizo ambao wameitwa katika kongamano la siku moja Dar es salaam kuzungumzia ukarabati na uendeshaji wa bwawa hilo.
Malika amesema Mfuko huo wa ukuzaji wa mitaji unasaidia ukarabati wa bwawa hilo kupitia mpango wake wa uendelezaji rasilimali kwa kutumia fedha za ndani (LFI) .
Amesema baada ya ukarabati huo, mradi utaendeshwa kwa pamoja kati ya serikali na watu binafsi.
Malika alisema ukarabati huo unakidhi lengo la mfuko ambalo ni kuwezesha miundombini inayoleta maendeleo.
“Ukarabati na hatimaye uendeshaji wa bwawa hilo kutasaidia kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo ya mitaji kwa watu binafsi na umma.” alisema
|
No comments:
Post a Comment