Thursday, September 26, 2013

KENYA YAFANIKIWA KUTEKELEZA MALENGO YA MILENIUM, YATOKOMEZA UGONJWA WA KIFUA KIKUU






 



































NA SEIF MANGWANGI, NAIROBI

SERIKALI ya Kenya imesema kuwa imefanikiwa kutekeleza malengo ya millennia katika sekta ya afya kwa kutokomeza maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu uliokuwa miongoni mwa magonjwa makuu yaliyokuwa yakiua maelfu ya wananchi wa Kenya.

Akizungumza katika hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano la chama cha waandishi wa habari za sayansi, kilimo na afya nchini Kenya (MESHA), Mkurugenzi wa idara ya Afya nchini Kenya,  Dkt Shahnaz Sharrif alisema jitihada za kutokomeza ugonjwa huo ni matokeo mazuri ya utendaji wa
watafiti nchini Kenya.

Alisema katika utekelezaji wa malengo ya dunia ya millennia namba sita, wizara ya afya imekuwa ikipambana na magonjwa sugu ambayo yamekuwa yakisababisha vifo vya wakenya wengi na kufanikiwa kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu.

Dkt.Sharrif alisema mapambano ya ugonjwa huo yamechangiwa na sekta mbalimbali ikiwemo waandishi wa habari za sayansi, afya na mazingira ambao wamekuwa wamekuwa wakiandika taarifa  tofauti kuhusu madhara na namna ambavyo ugonjwa huo umekuwa ukiambukiza.
“Pia Serikali imekuwa katika mapambano ya kutokomeza magonjwa mengine sugu kama Malaria na Ukimwi ambayo yamekuwa yakiua sehemu kubwa ya wakenya, hata hivyo mapambano haya bado yanahitaji jitihada za pamoja,”alisema.
Dkt.Sharrif alisema katika kuboresha sekta ya afya nchini Kenya, nchi hiyo imeanza utekelezaji wa matakwa ya katiba ya nchi hiyo yanayoiagiza Serikali kuteremsha majukumu ya kupanga shughuli za maendeleo katika ngazi za chini.
Aliwataka waandishi wa habari nchini Kenya kuendelea kutoa elimu sahihi kwa wananchi kuhusiana na upelekwaji wa madaraka hayo ngazi za chini ambapo wananchi watapata nafasi ya kuamua shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
Kongamano hilo la siku tatu lililoenda sanjari na mkutano mkuu wa chama cha waandishi wa habari za sayansi,kilimo na afya nchini Kenya (MESHA),  limekutanisha watafiti kutoka katika taasisi mbalimbali za sayansi, kilimo, afya na waandishi wa habari kutoka nchi za Kenya, Uganda na Tanzania.
Ends…

No comments: