Dereva wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro akiwa juu ya mti baada ya gari alilokuwa anaendesha kusombwa na maji katika eneo la Melela wilayani Karatu juzi |
Na Mwandishi Wetu, Karatu
Dereva wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) mkoani Arusha, Juma Moshi, amenusurika kufa maji baada ya gari alilokuwa akiliendesha kusombwa na mafuriko katika mto Malera uliopo nje kidogo ya mji wa Karatu kwa kupanda juu ya mti.
Juma alilazimika kutoka kwenye gari hilo aina ya Toyota Land Cruizer SU 36037 lililokuwa limesombwa na mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha kwa umbali wa mita zipatazo 70 kutoka barabarani, alfajiri jana na kujiokoa kwa kupanda juu ya mti wakati akienda mjini Arusha kikazi.
Mkuu wa Idara ya Huduma ya Uhandisi wa NCAA, Isra Missana na wafanyakazi wengine wa mamlaka hiyo wakishirikiana na wakazi jirani wa eneo hilo, walimwokoa dereva huyo saa 12:30 asubuhi.
Nao mamia ya wasafiri waliokuwa wakitoka maeneo ya Karatu na watalii Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwenda mjini Arusha, Dar es Salaam na maeneo mengine nchini jana walikwama kwa muda kuvuka Mto Kirurumo uliokuwa umefurika maji hadi kupita juu ya barabara huku ukiporomosha mawe makubwa kutoka milima ya Mbulumbulu.
Mto huo upo mpakani mwa Wilaya za Monduli na Karatu. Miongoni mwa abiria ni waliokuwa wasafiri kwa mabasi ya Dar Express na Sai Baba kwenda Dar es Salaam.
Pia mamia ya magari yaliyokuwa yakiwasafirisha watalii kutoka hifadhi za taifa yalikuwa miongoni mwa magari mengine mengi yaliyokwama katika eneo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Felix Ntibenda, akizungumza katika eneo la tukio hilo alisema tatizo la mafuriko katika mto huo limekuwa likijirudia mara kwa mara na serikali inafanya utafiti wa kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
No comments:
Post a Comment