Tuesday, April 1, 2014

TANAPA YAKAMATA MAJANGILI 6, NA MENO 53 YA TEMBO



Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu akizungumza na waandishi wa habari jana katika hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha 
Waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu (Hayupo Pichani)

Msemaji wa Shirika la Hifadhi za Taifa Pascal Shelutete akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akimkaribisha waziri Lazaro Nyalandu jana.


NA SEIF MANGWANGI, ARUSHA

KIKOSI kazi cha shirika la hifadhi ya wanyamapori (TANAPA) kwa kushirikiana na makachero wa jeshi la Polisi wilaya ya Manyoni mkoani Singida, wamefanikiwa kukamata majangili sita pamoja na  meno 53 ya tembo yenye jumla ya kilo 169.7 na silaha moja ya kivita aina ya SMG na magazine tatu.a

waandishi wa habari wakimsikiliza waziri Nyalandu kutoka kulia
ni Shechelela Kongola(TBC), Mwanaidi Mkwizu (ITV) na
Abraham Gwandu (RAI)
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Waziri wa utalii na Maliasili Lazaro Nyalandu alisema tukio hilo lilitokea juzi katika kijiji cha kiombo Wilaya ya manyoni ambapo tembo 26 wameuwawa na majangili katika maeneo ya hifadhi za Rungwa na Kizigo

Akizungumzia mazingira ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao ambao serikali inawasaka kwa udi na uvumba, Waziri Nyalandu alisema taarifa mbalimbali za kiintelejensia ndizo zilizofanikisha kukamatwa kwa watu hao pamoja na idadi hiyo ya meno.

'Majangili 6 wameshikiliwa chini ya ulinzi mkali katika kituo cha polisi cha Manyoni ambapo walikutwa na meno ya tembo 53,silaha ya kivita moja na magazine tatu, hawa ni watu hatari sana ambao Serikali imekuwa ikiwasaka kila kukicha,"alisema Nyalandu.

 Nyalandu alisisitiza kuwa pamoja na changamoto kubwa iliyopo dhidi ya ujangili, serikali imeazimia kuwasaka na kuwakamata majangili na washirika wao popote walipo na kwamba zoezi la kuwasaka ni la usiku na mchana

 Aidha alisema kuwa msako unaendelea kuwasaka wauaji wa tembo 26, huku akiwaomba wananchi wenye taarifa kuhusu uhalifu watoe ushirikiano wao kwa askari wa wanyamapori,jeshi la polisi na vyombo vya usalama


Nyalandu alitoa pongezi zake kwa mkurugenzi wa wanyamapori na kikosi chake dhidi ya ujangili kanda ya kati Manyoni na kikosi kazi maalum(Task force)kwa weledi na kujituma kwao ambapo imefanikisha kukamatwa majangili hao na meno ya tembo

No comments: