Tuesday, April 1, 2014

WADAU WA VOLLEYBALL WATAKIWA KUANZISHA CHAMA ILI KUTAMBULIKA


Mkuu wa Wilaya ya Arusha John Mongela katikati akipiga mpira kuashiria ufunguzi wa uwanja wa wavu uliopo katika bustani ya Pentagoni Suye jijini Arusha, wa kwanza kushoto ni mratibu wa klabu hiyo

Mkuu wa Wilaya ya Arusha John Mongela akirusha juu mpira kupiga ikiwa ni ishara ya ufunguzi wa uwanja wa mpira wa wavu ulioenda sanjari na bonanza la mpira huo ulioshirikisha timu kutoka kanda ya Kaskazini. wa sita mbele ni mmiliki wa bustani ya Pentagon Estomii Mallah 

wachezaji wa Mbulu wakijaribu kuzuia mashambulizi kutoka kwa wachezaji wa timu ya Hai

Wachezaji wa tiimu za Hai na Mbulu wakichuana vikali katika fainali baada ya mchezo wa wavu katika bustani ya pentagon, hata hivyo timu ya Hai iliibuka kidedea kwa seti tatu, huku mbulu ikiambulia patupu

Mmoja wa wachezaji wa timu ya Hai kutoka mkoani Kilimanjaro, katikati akiwa juu baada ya kupiga mpira kuelekeza mashambulizi upande wa timu ya Mbulu . Mashindano hayo yaliyoshirikisha timu 20, timu ya Hai iliibuka kidedea.

NA SEIF MANGWANGI

UONGOZI wa Taifa wa chama cha mpira wa wavu nchini(TAVA) umewataka wadau wa mchezo huo Mkoa wa Arusha kutafuta uongozi utakaosaidia kuwezesha uwepo wa klabu mbalimbali za mchezo huo jijini Arusha na ambao utakuwa ukiratibu shughuli mbalimbali za mchezo huo ndani na nje ya Arusha.

Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa kamati ya makocha wa mchezo huo  na Kaimu Mwenyekiti wa TAVA Taifa Emanuel Majengo mbele ya mkuu wa wilaya ya Arusha John Mongela katika fainali za mchezo huo ulioambatana na ufunguzi wa uwanja wa mchezo huo katika bustani ya Pentagoni jijini hapa.

Majengo alisema kwa muda mrefu chama chake kimekuwa kikihaha kuushirikisha mkoa wa Arusha katika michuano mbalimbali ya mchezo huo kutokana na kukosekana kwa uongozi jambo ambalo linautia aibu mkoa mkubwa kama wa Arusha.

Alimshauri Mongela kusimamia jambo hilo ili kupatikane hata uongozi wa muda mfupi utakaowezesha mkoa huo kushiriki hata katika michezo ya Muungano na mingine mingi inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Katika uzinduzi huo timu 20 zilishiriki na kufikia hatua ya nusu fainali na fainali ambapo timu ya Halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro iliibuka mshindi kwa kuifunga timu ya Mbulu mkoani Manyara kwa seti tatu kwa bila.

Katika hatua ya nusu fainali timu ya Mbulu iliitoa timu ya KCMC ya Moshi kwa kuifunga kwa seti tatu kwa bila wakati timu ya Hai iliingia fainali kwa kuibugiza timu ya Ngorongoro kwa seti nne kwa moja.

Akizungumza wakati wa shukurani mmiliki wa uwanja huo Estomii Mallah alisema lengo la kuanzisha kwa bonanza hilo haikuwa kumpaya mshindi wala vikombe bali ilikua ni kuwaunganisha wanafamili wa mchezo huo katika kanda ya kaskazini ili kukuza mchezo huo.

Alisema hata hivyo kumukuwa na mwamko mkubwa kwa wanafamilia wa mchezo huo hususani mashuleni na vyuoni hadi kufikia kujichanga na kuwezesha kujengwa kwa uwanja huo kupitia michango yao mbalimbali.

Awali mratibu wa bonanza hilo Willium Nkanga alieleza kuwa mchezo huo mkoani Arusha unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa vifaa,viwanja,vyama na viongozi wa michezo hiyo,wanamichezo,timu pamoja na wafadhili wa michezo hiyo.

Aidha alisema ujenzi wa uwanja huo mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 80 pekee hali ambayo bado inawahitaji kupata fedha kwaajili ya kukamilisha kwa kutegemea michango toka kwa wadau na wanafamilia wa mchezo huo.

Nae Mongela alipongeza hatua za mmiliki huyo kujitolea eneo la ujenzi wa uwanja huo pamoja na wanafamilia wa mchezo huo kwa kujitolea kuanzisha kwa juhudi za mchezo huo mkoani Arusha na kuahidi kwaunga mkono.

Aidha aliahidi kuundwa kwa uongozi wa muda na kuanzishwa kwa chama hicho haraka iwezekanavyo mkoani hapa kama njia ya kutafuta mwelekeo wa kuwepo kwa uongozi wa kudumu na timu za mchezo huo.

Alisema ni aibu kwa mkoa mkubwa kama Arusha kukosa chama,viongozi na hata timu zinazoweza kuuwakilisha mkoa katika michuano mbalimbali ya mchezo huo na kuagiza jiji la Arusha kwa kuanzia kuanzisha timu itakayoweza kushiriki michuano ya hivi karibuni.

Pia Mongela alikubali kuwa mlezi wa kilabu hiyo kama njia ya kukuza mchezo huo mkoani Arusha pamoja na kutoa kiasi cha shilingi 500,000 taslimu kama mchango wake katika kukamilisha ujenzi wa uwanja huo.


No comments: