(Inatolewa chini ya kanuni ya 99(9) toleo la mwaka 2013)
A: UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri wa Nishati na Madini
ilianzishwa kwa mujibu wa kipengele cha 21 cha Nyongeza ya Waraka wa
Rais uliochapishwa kama Tangazo la Serikali Na. 494 la tarehe 17 Desemba
2010. Majukumu ya Ofisi hii yameainishwa katika Tangazo la Ukasimishaji
wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010 (The Ministers [Assignment of
Ministerial Functions] Notice, 2010) lililochapishwa katika Gazeti la
Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 494A la tarehe 17 Desemba 2010.
Mheshimiwa Spika, Katika kujadili Mapitio ya Utekelezaji kwa
mwaka wa fedha 2012/2013 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya
Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2013/2014 naomba tuyatafakari
maandiko ya katika muktadha wa uongozi wetu wa leo na hatma ya sekta
hizi mbili muhimu za nishati na madini.
Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE katika ukurasa wa pili tutafakari kwamba, naomba kumnukuu ‘ukweli
una tabia moja nzuri sana. Haujali mkubwa wala mdogo; haujali adui wala
rafiki. Kwake wote ni sawa. Pia ukweli unayo tabia ya kujilipiza kisasi
kama ukipuuzwa.Ukiniona nataka kulipiga teke jiwe kwa kuwa nafikiri
kuwa ni dongo au mpira, natumaini utanionya. Lakini nikilipuuza onyo
lako kwa sababu eti wewe ni mdogo au kwa sababu sikupendi, nitalipiga
teke, basi litanivunja dole japo ningekuwa nani. Ukweli haupendi
kupuuzwapuuzwa.
Mheshimiwa Spika, Tuendelee kutafakari maandiko ya Nyerere kwamba
‘Wakati mwingine, mtu tunayempinga huwa anamakosa kweli, lakini hoja
tunazozitoa ni za kinafsi na hazihusiani kabisa na hoja zake.Nikisema
mbili na tatu ni sita, nakosa. Lakini ni bora kunionyesha kwamba pengine
nilifikiri tunazidisha kumbe tunajumlisha.Ni kweli mbili mara tatu ni
sita;lakini mbili na tatu ni tano, siyo sita. Lakini ukijaribu
kuwashawishi wenzetu wakatae mawazo yangu na kukubali yako kwa kusema
kuwa meno yangu ni machafu ,au natoa kamasi daima, utakuwa unatumia hoja
ambazo hazina maana, Huu ni mfano wa upuuzi; lakini mara nyingi hoja
tunazozitumia kuwashawishi watu wakatae mawazo ya wale tusiowapenda,au
kukubali mawazo yetu, huwa hazihusiani kabisa na mambo tunayojadili’.
Mheshimiwa Spika, Tutafakari maandiko ya Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha UONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA
uk. 50, nanukuu “Rais Mwinyi ni mtu mwema na mpole, lakini ni
kiongozi dhaifu; au upole wake na udhaifu wake unatumiwa na watu ambao
wala si wema wala wapole kuhatarisha umoja na amani ya nchi yetu,
Kipindi chake cha pili kinakaribia kwisha”.
Mheshimiwa Spika, Tutafakari maandiko mengine ya Mwalimu Nyerere kwamba
“lakini hatulazimiki kuendelea na uongozi mbovu wa chama na Serikali.
Wala tukiendelea na hali hii, bila kubadili uongozi wa Chama na
Serikali, sina hakika kama tutafika huko salama. Masuala muhimu ya nchi
yetu hayatashughulikiwa.Viongozi wetu wataendelea na matendo yao ya
kuvuruga muungano. Matatizo ya kweli ya muungano hayatashughulikiwa,
maana hatuna serikali ya kuyashughulikia.Na masuala mengine muhimu ya
uchumi, huduma za umma, rushwa,chuki za uzawa na ukabila na udini
yataachwa yajitatue yenyewe. Nasema, katika hili kama hiyo sina hakika
kama tutafika salama;na tukifika “salama”, tukiwa na uongozi huu huu wa
chama na serikali, mbele yetu kutakuwa ni giza tupu. Majuto ni mjukuu,
huja baadaye. Tunaweza tukafikishwa mahali tukilinganisha uongozi wa
rais Mwinyi na wa rais wa kesho tukaona kuwa chini ya Ndugu Mwinyi,
Pamoja na udhaifu wake wote, tulikuwa peponi”!
Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere anaendelea kuandika kwamba
“Waingereza wana msemo “Nature abhors vacuum”, “hulka huchukia ombwe” .
Hata siasa huchukia ombwe. Kama uongozi ni mbovu, upo kama haupo au upo
kwa mas lahi ya wenyewe, watatokea watu waujaze uwazi uliopo;hauwezi
kuachwa wazi hivi hivi.Lakini uongozi mbovu ni kama mzoga, unatabia ya
kukaribisha mafisi na mainzi. Tusidhani kuwa hulka ya siasa yetu ni
tofauti na hulka ya siasa ya watu wengine; kwamba sisi tunaweza
kuvumilia uongozi mbovu na tusivune matunda ya hulka ya uongozi mbovu”.
Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere alikuwa akiandika wakati wa
awamu ya Rais Mwinyi kuhusu masuala yanayohusu Muungano; sisi tutafakari
maandiko haya katika muktadha wa uongozi wa sasa wa taifa letu na
mustakabali wa sekta nyeti kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi za
nishati na madini.
B: MASUALA MTAMBUKA
1.0 MAPITIO UJUMLA YA UTEKELEZAJI KWA MWAKA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2013/2014
Mheshimiwa Spika, tarehe 27 Julai, 2012 niliwasilisha Bungeni
maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu mapitio ya utekelezaji
wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya
Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kufuatia maoni hayo,
yapo masuala machache ambayo Serikali imeyazingatia kwenye utekelezaji
na mengine mengi ambayo Serikali haikuyazingatia pamoja na umuhimu wake
kwa maslahi ya nchi na maisha ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka kiwango cha
bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kuongezwa, miongoni mwa masuala
ambayo serikali imetekeleza ni pamoja na kuongeza bajeti ya wizara hii
kwa kupanga kutumia kwa mwaka 2013/2014 jumla ya shilingi 1,099,434,031,000/= ikilinganishwa na mwaka 2012/2013 ambako kiasi cha shilingi 641,269,729,000/=
kilipangwa kutumika. Aidha napenda kuikumbusha serikali kuzingatia
vipaumbele vya miradi ya maendeleo ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani
ilipendekeza katika Hotuba zake za 2011 na 2012 ili kuweza kuleta maana
ya ongezeko hili la bajeti kwa maana ya kuvipatia vipaumbele uzito
unaostahili kwa Kuwekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya umeme na Gesi
ili kumaliza kabisa tatizo la nishati ya Umeme na kupunguza gharama za
maisha kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ilishauri kuwepo kwa mfumo thabiti wa kuhakikisha maoni na maazimio
yanatekelezwa kwa wakati na kwa ukamilifu. Lakini serikali imeendelea
kupuuza mapendekezo hayo na kutoa ahadi ambazo haikuwa tayari
kuzitekeleza, mathalani ahadi ya Mhe Waziri Mkuu aliyotoa wakati
akiahirisha bunge la bajeti 2011/2012 ya kupunguza matumizi yasiyo ya
lazima ili kuongeza pesa wizara ya Nishati na Madini lakini tofauti na
ahadi yake, Serikali ikaamua kuja na mpango wa kukopa fedha katika
taasisi za fedha ili kulinusuru shirika la umeme Tanzania TANESCO, ambao
nao haujatekelezwa kwa ukamilifu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo ninatambua maoni machache
ambayo yalizingatiwa kuhusu gesi asili, ikiwemo kuendelezwa kwa mchakato
wa kuwa na sera na sheria ya gesi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inayoongozwa na CHADEMA ikaitaka Serikali ieleze hatua ilizochukua juu
ya maoni ya kambi rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo hayakuzingatiwa na
mengine yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge na michango ya Wabunge
kwa nyakati mbalimbali mwaka 2011 na 2012.
Aidha, ni Kwa bahati mbaya kabisa serikali haikupenda kufanyia kazi
maoni na ushauri iliyopewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,kamati ya
Bunge na wabunge mbalimbali kwa nyakati tofauti na ambayo kama
yangezingatiwa kikamilifu yangeweza kuliepusha taifa na matatizo
yaliyotokea katika mikoa ya Lindi na Mtwara na ambayo bado yanaendelea
mpaka sasa.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013 makadirio ya mapato na matumizi ya kawaida yanaombewa jumla ya shilingi 107,221,286,000/= kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi 11,612,542,000/= ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa wizara na taasisi zilizochini yake na kiasi cha shilingi 95,608,744,000/= ni kwa ajili ya matumizi mengine (OC). Matumizi haya yanaonekana ni pungufu ya kiasi cha shilingi 2,857,582,000/= kwenye bajeti ya mwaka jana katika fungu hili la matumizi ya kawaida.
Mheshimiwa Spika, upungufu huu, unaacha maswali, Kambi rasmi ya
upinzani Bungeni inaitaka serikali kuwaeleza watanzania sababu za
kupungua kwa bajeti ya mishahara ya wizara na taasisi zilizokochini
yake, ambayo katika mwaka wa fedha 2012/2013 Wizara ya Nishati na Madini
ilitengewa shilingi 17,292,347,000/= na kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014 serikali inaomba kiasi cha shilingi 11,612,542,000/= ikiwa ni pungufu ya shilingi 5,679,805,000/=
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka majibu kwa kuwa wakati wafanya kazi
wakitarajia kupandishwa madaraja na ongezeko la mishahara kutokana na
kupanda kwa gharama za maisha pamoja na mfumko wa bei, bajeti ya
mishahara kwa Wizara na taasisi zilizochini yake inapunguzwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka maelezo iwapo
punguzo hilo ni kutokana na kubana matumizi au ni udhaifu katika
maandalizi ya bajeti na nini athari zake kwenye ufanisi wa wizara na
taasisi zake? Au wizara imebaini mianya ya ufisadi ambayo ilikuwepo
katika bajeti zilizopita kuhusiana na fungu la mishahara?
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya CCM inaonekana kuziba masikio
katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima pamoja na Kambi rasmi ya
upinzani Bungeni, wananchi na wadau wa maendeleo kulipigia kelele swala
hili. Jambo hili limejirudia kwa upande wa matumizi ya kawaida, ambapo
serikali iliomba kiasi cha shilingi 92,786,521,000/= katika Bajeti ya mwaka 2012/2013 na mwaka huu wa fedha 2013/2014 serikali inaomba kiasi cha shilingi 95,608,744,000/= ikiwa ni ongezeko la shilingi 2,822,223,000/=.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa
wabunge na Bunge kuungana pamoja kabla ya kupitisha matumizi haya
makubwa na kuitaka Wizara ya Nishati na madini kubana matumizi kwa
kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ili tupate fedha za kuwekeza kwenye
nishati .
Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuonyesha udhaifu na uwezo
mdogo wa wizara katika kusimamia sheria za nchi, kwa mujibu wa taarifa
ya CAG ya Juni 2012 nchi imepoteza kiasi cha dola za kimarekani
12,634,354.61 sawa na shilingi bilioni 19.71. Hizi ni fedha ambazo
hazikukusanywa kutoka kwa makampuni ya madini kwa kufuata sheria mpya ya
madini ya mwaka 2010, kifungu cha 87(1) kuwa mrahaba wa 4% utozwe kabla
ya makato na badala yake mrahaba ukawa ni 3% na kutozwa baada ya
makato kama sheria ya zamani ilivyokuwa.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha utekelezaji wa bajeti ya
mwaka 2011/2012 na 2012/2013, serikali iliathiriwa kwa kiwango kikubwa
na mvutano baina ya Watendaji Waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini
na Taasisi zake kwa upande mmoja na baadhi ya wabunge kwa upande
mwingine katika mvutano ambao uliambatana na kutuhumiana hadharani
kupitia vyombo vya habari juu ya madai ya ubadhirifu na matumizi mabaya
ya madaraka. Baadhi yamejidhihirisha kufuatia chunguzi na ripoti
zilizofanyika na kubaini kasoro kubwa za kiutendaji hususan kupitia
ukaguzi maalum uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
katika Shirika la Umeme (TANESCO).
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na
CHADEMA, inataka Serikali ieleze hatua iliyofikiwa katika uchunguzi juu
ya ununuzi wa mafuta mazito kama ambavyo tulipendekeza ufanyike. Kambi
Rasmi ya Upinzani inatambua kwamba Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA)
nayo iliwahi kueleza kwenye vyombo vya habari kuwa imeanza uchunguzi
ambao ulipaswa kukamilika mwaka 2012; hivyo tunataka taarifa ya
uchunguzi iwekwe hadharani na Serikali ieleze hatua ilizochukua dhidi ya
madai ya ufisadi na matumizi ya madaraka kupitia mianya ya dharura ya
umeme.
2.0 Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge
2.1 Maazimio ya uchangishaji haramu wa fedha wizara ya nishati na madini (‘Sakata la Jairo’).
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2011/2012 Bunge lako
lilishuhudia mambo kadhaa yaliyokiuka miiko ya uongozi, ambalo
yalilazimu bunge kuunda kamati teule kuchunguza uhalali wa uchangishaji
uliofanyika katika Wizara ya Nishati na Madini (‘Sakata la Jairo’) na
baadhi ya mapendekezo yake ambayo yalipitishwa kuwa maazimio yalikuwa;
(1). Kamati Teule inapendekeza kwamba Serikali ichukue hatua za
kinidhamu kwa Ndugu David Kitundu Jairo kwa matumizi mabaya ya madaraka,
kukusanya na kutumia fedha za Serikali kinyume cha Sheria, Kanuni na
Taratibu za Fedha za Umma na kuruhusu matumizi mabaya ya fedha za Umma.
(2)Vile vile Serikali iwachukulie hatua za kinidhamu, kwa mujibu wa
Sheria, watumishi wote wa Wizara ya Nishati na Madini waliotajwa kwenye
Taarifa hii kushiriki kwa namna mbalimbali katika mchakato wa
uchangishaji na matumizi ya fedha hizi za umma. Aidha, kwa kuwa kwa
mujibu wa Mwongozo wa Baraza la Mawaziri Waziri ndiye Msimamizi Mkuu wa
Wizara, hivyo suala la uchangishaji halikupaswa kufanyika bila yeye
kufahamu,
(3). Kamati Teule inapendekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. William Ngeleja, (Mb.)
(4).,……….. Kamati Teule inapendekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa
kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa upotoshaji huo..
,
(5). …… Kamati Teule inapendekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa kwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na
CHADEMA inahoji ni kwanini hadi sasa Bunge hili limeshindwa kuhakikisha
kwamba maazimio haya yametekelezwa na Serikali? Hakika huu ni uzembe wa
wazi wa Bunge kushindwa kutimiza majukumu yake ya kuisimamia serikali
kwa mujibu wa Katiba.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hatua
za utekelezaji wa maazimio hayo ya Bunge, kwani baadhi ya wahusika bado
wapo ma-ofisini wakiendelea na kazi na wengine wakiendelea kuteuliwa
kushika nafasi zingine katika uongozi na utumishi wa umma kama vile
hakuna liliowahi kutokea.
2.2 MAAZIMIO YA RICHMOND
Mheshimiwa Spika: Itakumbukwa kwamba taarifa mbili za serikali
kuhusu utekelezwaji wa maazimio haya ziliwasilishwa Bungeni na Waziri
Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, tarehe 28 Agosti, 2008 na tarehe 11 Februari,
2009 . Taarifa moja ilikabidhiwa na kujadiliwa na Kamati, ambazo
zililitaarifu Bunge kuwa utekelezaji wa Maazimio 10 kati ya 23
yaliyotolewa na Bunge, yalifanyiwa kazi hadi mwezi Februari, 2009 na
Maazimio 13 bado yalikuwa hayajakamilika.
Mheshimiwa Spika; Bunge liliazimia kwamba taarifa za utekelezaji
wa maazimio yaliyobaki ziwasilishwe kwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi
na Usalama ambayo hata hivyo katika mwaka 2011, 2012 na mpaka mabadiliko
ya muundo wa Kamati yalipofanyika kamati hiyo haikuwasilisha taarifa
yoyote bungeni ya kueleza kukamilika kwa utekelezaji wa maazimio husika
hali ambayo inahitaji bunge kuingilia kati kuweza kuisimamia Serikali
kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Ibara ya 63 (2) na (3).
Mheshimiwa Spika, katika hali inayozua maswali kuhusu umakini wa
Bunge katika kusimamia maazimio yake mwaka 2011, Mbunge wa Monduli
Mheshimiwa Edward Lowassa; aliyekuwa Waziri Mkuu na kujiuzulu kufuatia
kashfa hiyo ya Richmond alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama iliyopewa dhamana na Bunge kufuatilia
utekelezaji wa maazimio kuhusu mkataba kati ya TANESCO na Richmond.
Katika hali hiyo, haishangazi kwamba kwa miaka miwili toka wakati huo,
mpaka mabadiliko ya Kamati za Bunge yalipofanyika; Kamati hiyo katika
Taarifa zake zote bungeni haijawahi kuisimamia Serikali kuhakikisha
maazimio husika ya Bunge yanatekelezwa. Huu ndio uwajibikaji, ndani ya
Serikali na uongozi wa Bunge; vyote vikiongozwa na CCM.
Mheshimiwa Spika, sasa inajulikana wazi kuwa Mkataba wa TANESCO
na Richmond ulirithishwa kinyemela kwenda kwa Dowans kama inavyoonekana
katika nyaraka za mahakama ambapo Dowans na Richmond zilidaiana huko
Marekani; na kuwa hilo lilifanyika bila kuitaarifu TANESCO kinyume na
kifungu cha 15:12 cha Mkataba huo.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na hukumu ya Dowans ushahidi
umepatikana na kuwa mashahidi mbalimbali walioitwa mbele ya Kamati Teule
ya Bunge na wakiwa chini ya kiapo walitoa taarifa za uongo kuwa mkataba
kati ya Richmond na Tanesco ulihamishwa kwenda Dowans Disemba 23, 2006
na hivyo wahusika hao mbalimbali – wakiwemo wamiliki wa Richmond –
walidanganya au kuficha ukweli mbele ya Kamati Teule na hivyo kuonesha
dharau dhidi ya Bunge.
Mheshimiwa Spika; Masuala haya ni muhimu yakajadiliwa sasa ili
kupata undani wa wahusika wanaopaswa kubeba mzigo wa fidia kwa kampuni
ya Dowans badala ya kubebesha mzigo huo TANESCO na umma wa watanzania.
Kushindwa kuwashughulikia kwa ukamilifu mafisadi wa Richmond na kukwepa
kutumia mianya ya sheria za kimataifa kukana mikataba iliyoingiwa kwenye
mazingira ya ufisadi kwa mara nyingine tena kunaelekea kuligharimu
taifa hivyo wakati umefika sasa wa Bunge kuingilia kati kwa niaba ya
wananchi.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara ya
Nishati na Madini na Serikali kwa ujumla kutoa majibu bungeni juu ya
hatma ya maazimio 10 yaliyobaki: Nambari 3,5,7,8,9,10,11,13,14 na 18 ili
bunge liweze kuishauri na kuisimamia serikali kuhakikisha maazimio
husika yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwa haraka.
Kambi Rasmi ya Upinzani, inataka Taarifa ya utekelezwaji wa Maazimio
tajwa yaliyotolewa na Bunge juu ya Mkataba baina ya TANESCO na Kampuni
ya Richmond Development Company LLC badala ya kuwasilishwa kwenye Kamati
ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambayo kwa sasa haipo, sasa
iwasilishwe kwenye Bunge zima ili yaweze kujadiliwa na hatima yake iweze
kujulikana.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
ieleze kwanini mpaka sasa haijatekeleza maazimio hayo na bunge liweke
muda wa ukomo wa kutekeleza Maazimio yote ya Bunge yaliyokuwa yamesalia
katika sakata hili la Richmond ili mara moja na daima sakata hili la
Richmond limalizwe na kufungwa baada ya maazimio yote kutekelezwa kwa
ukamilifu. Ikiwa maazimio ya mwaka 2008 utekelezaji wake haujakamilika
mpaka mwaka 2013 kwa miaka mitano, nini kitalihakikishia taifa kwamba
maazimio mengine mapya yaliyopitishwa 2011 na 2012 yatatekelezwa kwa
wakati na kwa ukamilifu?
Mheshimiwa Spika: Azimio Na. 3, ambalo liliagiza kwamba “Mkataba kati ya TANESCO na Richmond
Development Company LLC (uliorithiwa na Dowans Holdings S.A.) na ile
kati ya TANESCO na IPTL, SONGAS, AGGREKO na Alstom Power Rentals,
ipitiwe upya mapema iwezekanavyo kama ambavyo Mikataba ya Madini
ilivyopitiwa upya na Serikali”. Iwapo Azimio hili lingetekelezwa kwa
ukamilifu wake, gharama za uzalishaji TANESCO na serikali kwa ujumla
zinazotokana na matatizo katika mikataba zingepungua.
(1) Mheshimiwa Spika, Azimio Na. 5 Mkataba kati ya
TANESCO na Richmond Development Company LLC na sasa Dowans Holdings S.A
umesheheni makosa mengi ya kisheria yanayoashiria udhaifu mkubwa wa
kitaalamu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au ukosefu wa
umakini ama ubinafsi katika kuiwakilisha Serikali. Kwa mfano, kushindwa
kutambua ukosefu wa sifa za kikampuni za Richmond Development Company
LLC; kushindwa kuishauri Serikali kuifanyia kampuni hiyo ukaguzi wa
awali (due deligence) au ukaguzi baada ya uteuzi (post qualification);
kushindwa kutambua tofauti kati ya consortium agreement na proprietary
information agreement; kushindwa kuona dosari kisheria za proprietary
information agreement; kushindwa kuona tofauti kisheria kati ya Richmond
Development Company LLC, RDEVCO,RDVECO na RDC, majina ambayo wamiliki
wa Richmond Development Company LLC walikuwa wanayatumia kwa kubadilisha
badilisha (interchangerbly) kwa makusudi; kushindwa kuwashauri Wajumbe
wa GNT kwamba business card si mbadala wa hati mahsusi kisheria;
kushindwa kuishauri Serikali kuhakikisha kuwa muhtasari wa majadiliano
kati ya Kamati ya Serikali ya Majadiliano (GNT) na Richmond Development
Company LLC ambao ulizingatia baadhi ya maslahi ya nchi, uwe sehemu ya
Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC; kushindwa
kuishauri Serikali kutumia fursa iliyokuwepo wazi ya kuvunja Mkataba
baada ya Richmond Development Company LLC kushindwa kutekeleza sehemu
yake ya Mkataba; kushindwa kuhudhuria idadi kubwa ya vikao muhimu vya
majadiliano;n.k. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye katika majadiliano
yake na Kamati Teule alionyesha kutokuelewa kabisa kilichokuwa
kinatendeka na wasaidizi wake, na mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Wakili wa Serikali Donald Chidowu, ambaye ushiriki wake katika
GNT haukuwa na tija yeyote, wawajibishwe na Mamlaka ya juu ya nchi kwa
kuchangia kuiingiza nchi katika mkataba wa aibu.
(2) Mheshimiwa Spika, Azimio Na. 7 lilikuwa “ Kamati Teule
inapendekeza kuwa Wajumbe wote wa GNT ambao ni maafisa waandamizi wa
Serikali wawajibishwe mara moja kwa kushindwa kutumia elimu na ujuzi wao
kulinda maslahi ya Taifa”.
Aidha, Azimio namba 9 lilikuwa linataka mabadiliko ya haraka ya uongozi wa taasisi ya TAKUKURU.
Mheshimiwa Spika, Azimio Na. 13 “ Kamati Teule inatoa wito kwa
Kamati zote za Bunge zihakikishe kuwa zinapitia mikataba mikubwa na ya
muda mrefu ya kibiashara chini ya sekta zao ili kuliondolea Taifa mizigo
isiyo ya lazima. Pale ambapo upatikanaji wa mikataba hiyo unakwamishwa
kwa urasimu usio wa lazima Kamati zitumie utaratibu uliotumiwa na Kamati
ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara ya kuunda Kamati Teule yenye ufunguo
wa mikataba iliyofichika”.
Mheshimiwa Spika, Azimio Na. 14 “Kamati Teule inapendekeza
kwamba Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo Mhe. Dk. Ibrahim
Msabaha (Mb) na Katibu Mkuu Ndugu Arthur Mwakapugi wachukuliwe hatua
kali za kinidhamu kwa kuliingiza Taifa kwa makusudi kwenye mkataba na
kampuni ya mfukoni ambao umesababisha hasara kubwa kwa nchi. Aidha
Kamishna wa Nishati Ndugu Bashir Mrindoko naye achukuliwe hatua za
kinidhamu kwa kushindwa kumshauri Katibu Mkuu mpya wa Wizara kuhusu
udhaifu wa Richmond Development Company LLC ambao ulijulikana dhahiri na
Wizara toka mwaka 2004 kwenye mkataba wa Bomba la Mafuta. Ndugu
Mrindoko ndiye aliyeiandikia barua kampuni hiyo kusitisha mkataba wake
na Serikali mwezi mmoja tu kabla ya mchakato wa zabuni ya umeme wa
dharura haujaanza”.
2.3 Kamati ya wataalamu wa Ofisi ya Spika.
Mheshimiwa Spika, mbali na maazimio hayo pia kuna uchambuzi
uliofanywa na kamati ya wataalam wa Ofisi ya Spika, kuhusiana na
makampuni yanayouza umeme kwa TANESCO ambayo mikataba yake haipishani na
ule wa RICHMOND, taarifa hiyo iliwasilishwa Bungeni wakati Mhe Harrison
Mwakyembe akiwasilisha Taarifa yake ya Kamati Teule ya RICHMOND ili
Waziri atoe ufafanuzi ni kwa kiwango gani mapendekezo yake Serikali
imeyafanyia kazi;
(a) “Uhalali kisheria wa Kampuni ya Aggreko (legal status)
Kwa mujibu wa maelezo yaliyomo kwenye Mkataba, Kampuni ya Aggreko
International Projects Limited ni Kampuni iliyosajiliwa chini ya Sheria
za nchi ya Scotland. Uchambuzi na utafiti wetu haukuweza kuthibitisha
kuwa Kampuni hiyo kweli imesajiliwa kisheria huko Scotland ili kubaini
kama kulikuwa na udanganyifu kama ule uliofanywa na Kampuni ya RICHMOND,
yaani kutoa taarifa za uongo kuhusu uhalali kisheria wa Kampuni.
(b) Malipo ya Kodi
Kama ilivyo katika Mkataba wa Kampuni ya Richmond, Kifungu cha 3.4
cha Mkataba wa AGGREKO kinatamka kwamba, kodi zote na malipo mengine
yanayotokana na uingizaji nchini na utoaji nchi za nje ya nchi wa
Mitambo ya uzalishaji wa umeme, ikiwa ni pamoja na vipuri na vifaa
vingine vinavyohusika na uendeshaji wa Mtambo huo italipwa na TANESCO.
Aidha, Kifungu hicho kimeweka pia sharti kwamba, pale ambapo bodi au
malipo yoyote yatadaiwa na Mamlaka yoyote ya kodi kutoka kwa AGGREKO,
Kampuni hiyo italijulisha Shirika la TANESCO ambalo litalipa kodi au
malipo hayo kwa mamlaka husika au litairejeshea AGGREKO fedha ambazo
itakuwa imelipa kwa Mamlaka hiyo katika kipindi cha siku 14.
(c) Malipo
Kwa mujibu wa Vifungu vya 4.2 na 4.3 vya Mkataba, Shirika la TANESCO
linawajibu wa kuilipa Kampuni ya Aggreko malipo yafuatayo:-
i. ‘Capacity Charge’ – Dola za Marekani 35.928 kwa Kw kwa mwezi [Tazama Kiambatanisho C cha Mkataba].
ii. Malipo ya Umeme (energy purchase price) – Dola 4.99 kwa Kwh
[Tazama tafsiri ya interim energy purchase price katika uk. wa 3 wa
Mkataba]
(d) Fidia kwa Ucheleweshaji wa Kuzalisha Umeme.
· Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.4.2 cha Mkataba, Aggreko
inawajibika kulipa kwa TANESCO Dola ya Marekani 0.5 kwa Kw kwa siku kwa
wiki 4 za kwanza za ucheleweshaji, na baada ya hapo’ kama ucheleweshaji
wa uzalishaji umeme utaendelea, anawajibika kulipa Dola ya Kimarekani 1
kwa Kw kwa siku.
· Hata hivyo, malipo hayo ya fidia (liquidated damages)
yamewekewa ukomo chini ya Kifungu cha 10.3 (a) na (c) ambapo hayatazidi
Dola za Kimarekani 350,000 na kwamba, malipo hayo kwa ujumla wake chini
ya Mkataba huo hayatazidi Dola za Kimarekani 500,000.
· Aidha, Kifungu cha 8.8 cha Mkataba wa Richmond
kinachoiruhusu TANESCO kuendesha Mitambo ya Richmond pale ambapo Kampuni
hiyoi itaitelekeza (abandon) Mitambo hiyo, kimeondolewa kwenye mkataba
wa AGGREKO.
(c) Nyongeza ya Mkataba
· Mkataba huo una Nyongeza (Addendum) au (Amendment No.2) ya
Januari, 2007 ambayo imebadilisha formula ya kupata ‘capacity payments’,
ambapo muda uliopotezwa na TANESCO kutokana na matatizo ya upatikanaji
wa gesi na pia kutokana na TANESCO kutoomba kupewa umeme kutoka AGGREKO
umepigiwa hesabu kwa ajili ya AGGREKO kulipwa na TANESCO.
· Nyongeza hiyo pia imebadilisha bei ya Umeme unaotolewa na
AGGREKO ambapo, bei mpya sasa ni Dola za Kimarekani 0.0499 x 1000 kwa
kila Mwh.
4.1.1 Mkataba Kati ya TANESCO na ALSTOM POWER RENTALS ENERGY LLC
(b) Tarehe ya Kusainiwa kwa Mkataba
Mkataba huo ulisainiwa tarehe 27 Oktoba, 2006
(c) Madhumuni ya Mkataba (Subject Matter)
Mkataba huo ni kwa ajili ya uzalishaji na usambazji wa umeme wa
dharura kutoka kwenye Kinu cha dizeli cha kuzalisha umeme (emergency
supply of power from a diesel – based generating plant in Mwanza with a
capacity of 40 Mw).
(c) Muundo (form) wa Mkataba
Kama ilivyo kwa Mikataba iliyotangulia, Mkataba huu upo katika muundo wa ‘Standard Power Off-take Agreement’
(d) Muda wa Mkataba
Muda wa Mkataba huo ni miezi kumi na mbili (12) kwa mujibu wa Kifungu cha 2.1 cha Mkataba.
(e) Uhalali Kisheria wa Kampuni ya Alstom Power Rentals Energy LLC
Kwa mujibu wa maelezo yaliyomo kwenye Mkataba hususan kwenye Kifungu
cha 5.1 (a) na (b), Kampuni ya Alstom Power Rentals Energy LLC
imesajiliwa chini ya Sheria za Florida, Marekani.
(f) Malipo ya Kodi
Kifungu cha 3.4 cha Mkataba kinatamka kwamba, TANESCO itatumia juhudi
za kibiashara kuhakikisha kwamba Serikali ya Tanzania inatoa msamaha
kwa Alstom wa kutolipa ‘import duties’ na kodi ya ongezeko la thamani
(VAT) kuhusiana na Mtambo au utekelezaji wa majukumu ya Alstom, chini ya
Mkataba huo.
Aidha, Kifungu hicho kinatamka pia kuwa, pale ambapo kodi hizo
zitadaiwa, Alstom itaiomba TANESCO ilipe kodi hiyo au kama italipwa na
Alstom, TANESCO itarejeshea Alstom malipo hayo ya kodi.
(g) Kutii Sheria za Mazingira
Kifungu cha 3.9 cha Mkataba huu kinamtaka Alstom kuhakikisha kwamba,
hatafanya kitendo chochote ambacho kitasababisha kuwepo kwa hali ya
mazingira ambayo inakiuka Sheria za Tanzania.
(h) Malipo ya Umeme
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.3 cha Mkataba, TANESCO inawajibika kulipa
malipo ya ‘capacity charge’ kwa kiasi cha Dola za Marekani 43.8 kwa Kw
kwa mwezi.
(i) Malipo ya Fidia kwa Ucheleweshaji wa Kuzalisha Umeme
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.4 na cha 10.1(a) cha Mkataba, Alstom
anawajibika kulipa kwa TANESCO kiasi cha Dola za Kimarekani 400,000 kama
kiwango cha mwisho cha malipo ya fidia (damages) kwa ucheleweshaji wa
kuzalisha umeme na kiasi cha Dola za Kimarekani 600,000 kama kiwango cha
mwisho cha malipo yote ya fidia (damages).
(j) Dhamana ya Malipo kwa Alstom
Kifungu cha 4.6 cha Mkataba kinaitaka TANESCO kufungua ‘Letter of
Credit’ ya kiasi cha Dola za Kimarekani 3,500,000 kwa kipindi chote cha
Mkataba, kama dhamana ya malipo kwa Alstom.
Aidha, Kifungu cha 4.7 cha Mkataba kinaitaka TANESCO kufungua
‘Standby Letter of Credit’ ya kiasi cha Dola za Kimarekani 14,000,000
kwa ajili ya malipo ya miezi minane (8) ya Mkataba.
(k) Mafuta (fuel)
Kifungu cha 6 cha Mkataba kinatamka kuwa, TANESCO itawajibika kulipia
mafuta ya dizeli yatakayotumika kuendeshea Mtambo wa Alstom wa
kuzalisha Umeme.
(l) Kutolipa Malip ‘Capacity Charges’ Wakati wa Majanga
Kwa mujibu wa Kifungu cha 13.1 cha Mkataba, malipo ya ‘Capacity
Charges’ yanayotakiwa kulipwa na TANESCO yatasitishwa kwa siku 30 iwapo
litatokea janga lolote ambalo litasababisha Alstom kutelekeza majukumu
yake ya kuzalisha na kusambaza umeme.
(m) Kuhamisha (assign) Majukumu
Kwa mujibu wa Kifungu cha 15.12 cha Mkataba, Alstom au TANESCO
inaweza kuhamisha (assign) sehemu au majukumu yote yaliyomo kwenye
Mkataba kwa Kampuni Tanzu, baada ya kutoa taarifa kwa mhusika wa pili
uuzaji uhamishaji huo wa majukumu. Hata hivyo, mhusika yeyote
anayehamisha majukumu atabaki na wajibu wa kuhakikisha kuwa majukumu
hayo yanatekelezwa ipasavyo na yasipotekelezwa, atawajibika.
4.1.2 Mkataba Kati ya TANESCO na WARTSILA FINLAND OY
(a) Tarehe ya Kusainiwa kwa Mkataba
Mkataba huo ulisainiwa tarehe 20 Juni, 2006.
(b) Madhumuni ya Mkataba (Subject Matter)
Mkataba huo ni kwa ajili ya uzalishaji na usambazaji wa umeme wa
dharura kutoka kwenye Kinu cha gesi cha kuzalisha umeme (Energy Purchase
Contract for Procurement of Emergency 100 Mw Gas-based Power Generation
Plant at Ubungo, Dar es Salaam.)
(c) Muundo (form) wa Mkataba
Tofauti na Mikataba yote iliyotangulia kufanyiwa uchambuzi hapo juu,
Mkataba huo upo katika muundo uliowekwa na Kanuni ya Ununuzi wa Umma
[The Public Procurement (Goods, Works, Non-Consultant Services and
Disposal of Public Assets by Tender) Rgulations, G.N. No.97 of
15/4/2005] zilizotungwa chini ya Kifungu cha 88 cha Sheria ya Ununuzi wa
Umma Na.21 ya Mwaka 2004 [The Public Procurement Act, 2004 (No.21 of
2004)].
Kanuni ya 115(1) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2005, Taarifa
ya Serikali Namba 97 ya Mwaka 2005 inaelekeza kama ifuatavyo:-
“Kwa kadri inavyowezekana, kila jitihada itafanywa kutumia miundo ya
rasimu za mikataba iliyotayarishwa na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma.”
Tafsiri na msisitizo ni wetu.
Ili kuondoa tatizo la tafsiri, Kanuni hiyo iliyoandikwa kwa lugha ya Kingereza inasomeka kama ifuatavyo:-
“Every effort shall be made to utilize as for as possible, the sample Standard Contract documents prepared by the Authority.”
(d) Muda wa Mkataba
Muda wa Mkataba (contract period) ni miezi 21, kwa mujibu wa Kifungu
cha G.C.C 1.1 (aa) na GCC 8.1[Tazama Uk.1 na 2 wa ‘Special Conditions of
Contract]
(e) Uhalali kisheria wa Kampuni ya WARTSILA FINLAND OY
Kwa mujibu wa maelezo yaliyomo kwenye Mkataba, Kampuni hiyo
imesajiliwa chini ya Sheria za Finland. Hatukuweza kufanya utafiti wa
kina kuthibitisha kuwa maelezo hayo ni sahihi, isipokuwa tumefanya hivyo
kwa Kampuni moja tu ya RICHMOND.
(f) Malipo (Contract Price)
Kwa mujibu wa Kifungu cha 2.1 cha Mkataba, TANESCO anawajibika kulipa
kiasi cha Euro 57,550,000/= kama malipo ya huduma ya kupatiwa umeme wa
Megawatt 100 kutoka kwenye Kinu cha kuzalisha umeme cha WARTSILA.
(g) Utaratibu wa malipo
Kwa mujibu wa Kifungu cha 2.2 cha Mkataba, TANESCO anawajibika
kufanya malipo ya huduma ya umeme kwa kufungua ‘Letter of Credit’ ya
kiasi cha Euro 51,795,000/= kwa jina la WARTSILA.
(h) Dhamana ya Utekelezaji (Performance Bond)
Chini ya Kifungu cha 3.1 cha Mkataba, WARTSILA anawajibika kutoa
dhamana ya utekelezaji wa kazi (Performance security/bond) ya kiasi cha
10%ya malipo anayostahili kulipwa, kabla ya kuanza kazi.
(i) Malipo ya Kodi
§ Kwa mujibu wa Kifungu cha 14.4 (GCC), uk. wa 3 wa Special
Conditions of Contract, kodi zote ambazo WARTSILA anapaswa kulipa
zitasamehewa (be exempted) au zitalipwa na TANESCO.
§ Aidha, chini ya Kifungu hicho pia, kodi na malipo yote yanyohusu
mishahara ya watumishi wa kigeni wa Kampuni ya WARTSILA zinapaswa
kulipwa na TANESCO.
(j) Taratibu za Usuluhishi
Chini ya Kifungu cha 6.2.3 taratibu zitakazotumika wakati wa
Usuluhishi ni za Mahakama ya Kimataifa ya usuluhishi ya London, chini ya
Sheria za Uingereza.
Tunadhani kifungu hiki si kwa manufaa na maslahi ya TANESCO.
(k) Malipo ya bonus
Chini ya Kifungu cha 26.3 cha Mkataba (Taz. Uk. wa 5 wa SCC malipo ya bonus hayaruhusiwi.
(l) Kipindi cha Matengenezo (Defect liability period)
§ Kwa mujibu wa Kifungu cha 27.2 cha Mkataba (Uk. wa 5 wa SCC),
kipindi cha matengenezo ni miaka miwili (2) baada ya kukamilika kwa
ufungaji wa Mtambo.
§ Tunadhani kwamba, Kifungu hiki ni kwa manufaa na maslahi ya TANESCO.
4.1.3 Mkataba Kati ya TANESCO na SONGAS LIMITED
(a) Tarehe ya Kusainiwa kwa Mkataba
Mkataba huo umesainiwa tarehe 11 Oktoba, 2001.
(b) Madhumuni ya Mkataba (Subject Matter)
Mkataba huo ni kwa ajili ya uzalishaji na usambazji wa nishati ya
umeme kutokana na gesi ya Songosongo (Power purchase relating to the
Songosongo gas-to-electricity)
(c) Muundo (form) wa Mkataba
Mkataba huo upo katika muundo wa ‘Standard Power Purchase Agreement’.
(d) Muda wa Mkataba
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.1 cha Mkataba, muda wa Mkataba ni miaka
ishirini (20), na unaweza kuongezwa kwa makubaliano kati ya TANESCO na
SONGAS.
(e) Uhalali Kisheria wa Kampuni ya SONGAS LIMITED
Kampuni ya SONGAS LIMITED ni Kampuni ya kitanzania iliyosajiliwa
chini ya Sheria ya Makampuni, Sura 212, Toleo la 2002 [The Companies
Ordience (Cap.212) of the Laws of Tanzania, R.E, 2002] (Tazama Kifungu
cha 5.1 cha Mkataba)
(f) Malipo ya Kodi
Kwa mujibu wa Kifungu cha 15.1 cha Mkataba, SONGAS LIMITED inatakiwa
kulipa kodi kulingana na masharti yaliyomo kwenye Mkataba wa Utekelezaji
(Implementation Agreement) ulioingiwa kati yake na Serikali ya
Tanzania.
(g) Malipo ya Umeme
Kwa mujibu wa Kifungu cha 2.1(a)(i) na (ii) cha Mkataba, kikisomwa
pamoja na Vifungu 9.2 na 9.5, TANESCO anawajibika kulipa malipo
yafuatayo kwa SONGAS:- ‘Capacity Charge’ – Dola za Kimarekani 6,638,600
‘Energy Charge’ – kwa kiasi kitakachotokana na ‘formula’ iliyowekwa na
Kifungu cha 5 cha Nyongeza F ya Mkataba.
(h) Usuluhishi
§ Kifungu cha 3.10 cha Mkataba kinatamka kwamba, TANESCO na SONGAS
wamekubaliana kutotekeleza masharti na matakwa ya Kifungu cha 20(2) cha
Sheria ya Umeme, Sura 131, Toleo la 2002 [Electricity Act, (Cap.131) of
the Laws of Tanzania, R.E 2002], na badala yake kusuluhishwa migogoro
baina yao kwa kutumia utaratibu uliowekwa na Mkataba.
§ Kwa kuwa kinahusu makubaliano ambayo yanavunja sheria, Kifungu hicho hakina uhalali wowote wa kisheria.
(i) Kuvunjwa kwa TANESCO
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.3(a) cha Mkataba, kikisomwa pamoja na
Kifungu cha 17.12, TANESCO haiwezi kuvunjwa kwa Sheria au kuhamisha
majukumu yake yaliyoainishwa kwenye Mkataba, isipokuwa tu kwa kuzingatia
masharti yaliyowekwa na Kifungu cha 8.7 cha Mkataba wa Utekelezaji
(Implementation Agreement).
(j) Uuzaji Umeme wa SONGAS
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.1(b), iwapo TANESCO watakataa kuongeza
muda wa Mkataba baada ya muda wa awali wa miaka 20 kumalizika, SONGAS
wataruhusiwa kuingia Mkataba na mtu yoyote anayetaka kuuziwa umeme.
(k) Haki ya Kununua Mradi
Chini ya Kifungu cha 4.8 cha Mkataba, TANESCO na T.P.D.C wamepewa
haki ya kununua Mradi huo wa SONGAS iwapo SONGAS atakiuka masharti ya
Mkataba.
Mapendekezo Mengine
Pamoja na mapendekezo ya hapo juu, tunashauri na kupendekeza pia
kuwa, kuna ulazima kwa Mikataba mikubwa ambayo inahusu maslahi na
manufaa ya Taifa kama vile Mkataba wa IPTL kuwasilishwa Bungeni, kwa
utaratibu wa dhana ya demokrasia ya uwajibikaji (accountability in a
Parliamentary democracy) kwa ajili ya ushauri wa Bunge.
Tunapendekeza na kushauri vilevile kuwa, pale ambapo kuna ulazima wa
kutumia rasimu ya Mkataba ambayo ni tofauti na ile iliyotayarishwa na
Mamlaka ya Ununuzi wa Umma, mabadiliko muhimu yafanywe katika rasimu
hiyo ili masharti yaliyomo ambayo hayafai yaondolewe na yale ambayo ni
kwa manufaa ya Taifa letu yawekwe. Wanasheria watumike katika
kuitekeleza jambo hili.
Tunashauri na kupendekeza vilevile kuwa, Mikataba yote ya umma
ifanywe kwa kuzingatia misingi ya kibiashara na si vinginevyo, na
kwamba, Taasisi na Mashirika yote ya Umma lazima yatekeleze na kufuata
utaratibu, masharti na matakwa yaliyowekwa na Sheria ya Ununuzi wa Umma,
Namba 21 ya mwaka 2004, pamoja na Kanuni zilizotungwa chini ya Sheria
hiyo.
Aidha, tunapendekeza na kushauri kwamba utoaji Mikataba utumike kama
njia au chombo cha kutekeleza Sera za Taifa na malengo ya jamii, badala
ya kutumika kama chombo cha kuchota rasilimali za Taifa na kuongeza
umaskini wa wananchi wa nchi hii.
Aidha, tunashuri pia kwamba, pale inapotokea ukiukwaji wa masharti ya
Mkataba unaofanywa na Mwekezaji basi hatua mwafaka zichukuliwe, ikiwa
ni pamoja na kudai malipo ya fidia iwapo kuna kifungu cha Mkataba
kinachotoa haki hiyo.
Kwa kuzingatia kuwa Mikataba mibovu kati ya TANESCO na Makampuni
mbalimbali ambapo Makampuni hayo yanalipiwa kodi yote na TANESCO imekuwa
ni chanzo cha bei kubwa za umeme katika nchi yetu, na kwa kuzingatia
kuwa Mikataba hiyo inasababisha Sera muhimu za Taifa, kama vile, Sera ya
Kupiga vita Umaskini, Sera ya Huduma Bora kwa Jamii, Sera ya Taifa ya
Nishati inayolenga kusambaza nishati ya bei nafuu vijijini n.k.
kutotekelezeka, tunashauri kuwa Mikataba hiyo ipitiwe upya ili
irekebishwe, kwa maslahi na manufaa ya Taifa letu.
Mwisho, kwa kuzingatia ukweli kwamba, Mikataba hiyo mibovu, kwa kiasi
kikubwa inadidimiza uchumi wa nchi yetu, tunapendekeza Serikali
ichukuwe hatua muafaka zinazofaa ili kuondoa hali hiyo ambayo
inalipeleka Taifa letu ‘shimoni’[1].
Mheshimiwa Spika, hali hiyo ya kuachwa kutekelezwa kwa maazimio
ya Bunge la Tisa ya Mwaka 2008, hayahusu tu Richmond bali pia juu ya
Kashfa ya Mgodi wa Kiwira aliyomgusa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na
baadhi ya mawaziri kama ambavyo hotuba hii itaeleza kwa ufupi wakati wa
kutoa maoni kuhusu sekta ya madini. Serikali wakati inaendelea kuchukua
hatua kuhusu kashfa hii ni muhimu ikarejea maelezo ya ziada na vielelezo
zaidi vilivyotolewa wakati wa kusomwa kwa orodha ya mafisadi (List of
Shame) Septemba 15 mwaka 2007 katika uwanja wa Mwembe Yanga.
Mheshimiwa Spika, Aidha, matokeo ya Bunge kuzembea kuisimamia
Serikali kukamilisha utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya mwaka 2008
yamesababisha udhaifu wa Serikali katika kutekeleza maazimio ya Bunge ya
mwaka 2011 kuhusu “Sakata la Jairo” kama nilivyoeleza katika Hotuba hii
lakini pia kuhusu uchunguzi juu ya Sekta ndogo ya Gesi Asili na Mpango
wa Dharura wa Umeme kama nitakavyoeleza wakati nawasilisha maoni kuhusu
sekta ya gesi ya nishati.
C. NISHATI
3.0 SEKTA NDOGO YA GESI ASILIA TANZANIA
Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya gesi asilia ni sekta ambayo
kutokana na ukubwa wa hazina iliyokwishapatikana na inayokisiwa kuwepo
itakuwa ni kubwa sana katika shughuli za uchumi kwa nchi yetu. Lakini
Sekta ya gesi asilia imegubikwa na utata mwingi ambao kwa njia moja au
nyingine unatokana na kutokuwepo kwa sera na sheria mahususi ya gesi. Na
hivyo kusababisha utendaji wake kutokuwa na mdhibiti (regulator) wa
kuhakikisha maslahi ya taifa, mwekezaji na mlaji yanaangaliwa.
Mheshimiwa Spika, Utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi(
Upstream); shughuli zote za utafutaji wa mafuta na gesi nchini
unatawaliwa na Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji Mafuta ya mwaka 1980
(The Exploration Act,1980). Shughuli ya usafirishaji na uuzaji (down
stream) hii hutawaliwa na sheria ya EWURA sura 414 kwa kuwa kwa sasa
sheria ya gesi nchini haipo. Hivyo basi, makubaliano katika mkataba
baina ya wadau hutakiwa kuwasilishwa EWURA kwa mapitio tu, na baada ya
kujiridhisha EWURA hupanga bei za gesi.
Mheshimiwa Spika, mkataba wa ubia ndiyo mwongozo mkuu wa
mahusiano yote yanayohusu uzalishaji na ugawanaji wa mapato ya gesi
baina ya TPDC na mbia yeyote. Lakini kwa makusudi wabia na TPDC wamekuwa
hawafuati matakwa yaliyomo kwenye PSA na mfano mzuri ni Pan African
Energy
[2].
Mheshimiwa Spika, utakumbuka moja ya mapendekezo ya kamati ndogo
iliyoundwa na Bunge lako tukufu toka kwenye iliyokuwa kamati ya Kudumu
ya Nishati na Madini ilipendekeza na Bunge kukubali, kuwa nina nukuuu ‘’ipo
haja ya kudurusu Sera ya Nishati, kuandaa Muswada wa gesi asili wenye
kutoa majibu ya maswali magumu ya Watanzania wa leo na wa miaka 50
ijayo…
Majukumu kati ya asasi moja na asasi nyingine yaainishwe bayana na
kutenganishwa kwa lengo la kuleta ufanisi na kuongeza tija. Aidha,
mipango mkakati na kabambe iandaliwe ili kuibua miradi ya miundombinu na
mahitaji ya rasilimali. Taifa likichelewa kuweka nyenzo hizi muhimu,
likaruhusu majadiliano na mikataba kuchukuwa nafasi, kipindi si kirefu
yatashuhudia manun’guniko kuwa nchi imeuzwa na mivutano kati ya wananchi
na wawekezaji na ya wananchi na Serikali yao itajitokeza kwa nguvu sana
jambo ambalo ni vyema likaepukwa mapema[3]’’
Mheshimiwa Spika, mapendekezo haya yalitolewa Bungeni Novemba 17,
2011 na kupitishwa kuwa azimio la bunge. Sasa ni mwaka mzima na miezi
sita, hadi tunashuhudia maandamano na malalamiko ya wazi toka maeneo
ambapo gesi asili imegunduliwa.
Mheshimiwa Spika, Licha ya ukweli kwamba gesi asili ilianza
kutafutwa toka mwaka 1952 na iligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini
mwaka 1974 na baadae mwaka 1982, wakati wote huo hakuwahi kuwa na sera
mahususi ya gesi mpaka mwishoni mwa mwaka 2012 zaidi ya miaka 30 baadae
ndipo serikali imeanzisha mchakato wa kutunga sera ya Taifa ya gesi
asili.
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhihirisha udhaifu mkubwa wa kisera
na kiutendaji kwa kuzingatia kuwa mikataba kadhaa ya uchimbaji na
utafutaji wa gesi imeshatiwa saini kati ya serikali na wawekezaji bila
kuwa na sera wala sheria inayotoa mwongozo juu ya namna Taifa
linavyopaswa kuthibiti rasilimali hii adhimu. Uwepo wa sera na sheria ya
gesi asilia ungetoa mwelekeo juu ya namna gani serikali ingeshirikiana
na wakazi wa maeneo yaliyogunduliwa gesi, pamoja na wadau wengine katika
kutafuta,kugundua na kuvuna, kusafirisha, kununua na kutumia gesi
asilia.
Mheshimiwa Spika, Serikali bila uwepo wa sera na sheria hiyo,
tayari imefunga mkataba na kampuni ya Statoil, Ophir, British Gas,
Artumas, Shell, Texaco, Agip, PetroBras na kadhalika. Ni wazi kwamba
mikataba husika imeingiwa bila muongozo wowote wa kisera wala kisheria
mahususi. Aidha, licha ya makosa hayo na wakati mchakato wa sera uko
karibu kukamilika Serikali imefunga mkataba mwingine kwa Kampuni
nyingine kufanya utafutaji kwenye Ziwa Tanganyika. Jambo hili
linazidisha wasiwasi kama kweli Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha
sekta hii ya gesi inanufaisha Taifa na watu wake.
Kitendo cha Serikali kuendelea kuingia mikataba na makampuni ya kutafuta
gesi asilia bila ya kukamilisha kwanza sera na sheria ni sawa na kuweka
mkokoteni mbele ya punda.
Mheshimiwa Spika; Waziri Mkuu akiwa ndiye msimamizi na mdhibiti
wa shughuli za kila siku za Serikali ndani na nje ya Bunge, anapaswa
kutoa maelezo kuhusu hali inayoendelea hivi sasa katika sekta ndogo (sub
sector) muhimu kwa nchi yetu ya gesi asili kuhusu mazungumzo
yanayoendelea na makampuni mbalimbali ya kimataifa na mikataba inayozidi
kusainiwa huku kukiwa na ombwe la kisera na udhaifu wa kiuongozi katika
sekta hizo nyeti hali ambayo itakuwa na athari za muda mrefu sana kwa
taifa.
Mheshimiwa Spika, Ucheleweshwaji wa sera na sheria katika sekta
ya gesi asilia unachangiwa na wizara yenyewe kwa watendaji wake kuwa na
udhaifu katika kuweka mifumo ya kuifanya sekta hiyo kuwa endelevu na
yenye manufaa kwa nchi. Hili linathibitishwa na ukweli kwamba TPDC
imeshindwa kusimamia kwa ukamilifu sekta hii ya gesi asilia kwani hata
mikataba iliyopo inayotaka kampuni inayofanya utafiti baada ya muda
Fulani kuchimba kisima kipya; lakini hadi sasa kwa mfano tangu Kampuni
ya Songas kuchukua visima vilivyochimbwa na TPDC haijawahi kuchimba
visima vipya kwa kadiri ya mahitaji.
Mheshimiwa Spika, mfano mwingine ni kampuni ya Pan African
Energy Tanzania (PAT) kukosa sifa za uaminifu ambapo Kamati ilishauri
Mkataba wa Pan African Energy Tanzania (PAT) usitishwe. Aidha,
utekelezaji wa kuvunja mkataba huu ulipaswa kwenda sambamba na
kuhakikisha kuwa taratibu za kisheria na za kimkataba zinazingatiwa,
uwepo wa usalama wa visima na mitambo na uwepo wa uhakika wa huduma ya
upatikanaji wa gesi nchini. Hili lilikuwa ni pendekezo namba 4 la kamati
iliyochunguza uendeshwaji wa sekta ndogo ya gesi asilia hapa nchini na
baadae kuwa azimio la Bunge. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kwanini mpaka sasa Serikali
haijatekeleza azimio hilo? Aidha, ni lini Bunge litachukua hatua ili
kuepusha uzembe kwa upande wa chombo hiki muhimu? Aidha ni lini
mabilioni yote ya mapunjo yenye mwelekeo wa ufisadi yatarejeshwa?
Mheshimiwa Spika, kuhusu gesi asilia, tarehe 15 Julai, 2011 Kambi
Rasmi ya Upinzani ilieleza kuwa, nchi yetu imejaliwa utajiri wa gesi
asilia katikati ya lindi la umaskini wa wananchi na kwamba Taifa letu
lina fursa ya kuwa nchi kiongozi katika gesi Afrika na kushindana
Kimataifa ikiwa tutaweka mstari wa mbele uzalendo,upeo, umakini na
uadilifu katika sekta ya nishati kuepusha laana ya rasilimali.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mapitio ya utekelezaji kwa mwaka wa
fedha 2011/2012, yalionesha Serikali kutochukua hatua thabiti
kushughulikia ufisadi na udhaifu wa kiuongozi katika sekta ndogo ya gesi
asili.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitaka hatua
za haraka kuchukuliwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 ili kuepusha
rasilimali kuwa chanzo cha migogoro na kuhatarisha pia usalama wa nchi
lakini kwa sababu ya udhaifu wa serikali hii kutosikiliza ushauri
kitendo hicho kilisababisha vurugu na uharibifu wa mali kwa mikoa ya
Lindi na Mtwara.
Mheshimiwa Spika, ushahidi wa hili unapatikana katika ushauri
ambao serikali ilipewa kwa nyakati mbili tofauti lakini ikashindwa
kuzuia vurugu za Lindi na Mtwara. Tarehe 27 Julai 2012 nikiwasilisha
maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapitio na makadirio ya mapato
na matumizi ya wizara ya nishati na madini nilishauri “Mapitio ya
utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2011/2012, yanaonekana bado serikali
haichukui hatua thabiti kushughulikia ufisadi na udhaifu wa kiuongozi
katika sekta ndogo ya gesi asili hivyo hatua za haraka zisipochukuliwa
katika mwaka 2012/2013 na kuendelea rasilimali inaweza kuwa chanzo cha
migogoro na kuhatarisha pia usalama wa nchi”. Lakini pamoja na
angalizo hili serikali haikuchukua hatua yeyote na matokeo yake sote
tunayafahamu, kambi rasmi ya upinzani inahoji ni nani mpaka sasa
amewajibika kutokana na hali hiyo?
Mheshimiwa Spika, wakati wa mchakato wa kutoa maoni juu ya rasimu
ya gesi , pamoja na kwamba mchakato huo haukufanyikakiwa ufanisi
katika maeneo mengine muhimu kama Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM)
ambacho kina kozi mbalimbali za masuala haya na ambako tungepata ushauri
mzuri na wa kitaalamu kutokana na wadau hao kutokujua na hivyo
kutokujitokeza .
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa wananchi waliojitokeza kutoa maoni
ni pamoja na wananchi waliofunga safari kutoka Mtwara hadi Dar es
salaam kuja kutoa maoni yao juu ya rasimu ya gesi. Miongoni mwa
mapendekezo aliyotoa mwananchi huyo (jina linahifadhiwa) mbele ya
viongozi wa serikali alishauri serikali kujua matatizo yanayotokea
katika sekta ya madini ili tuhusianishe na gesi asilia.
Mheshimiwa Spika, Pamoja mwananchi huyo kuwakilisha mikoa ambayo
ndiko hasa nishati hiyo inakopatikana, mwananchi huyo alipendekeza
kutengwa kwa asilimia kumi (10%) ya mapato yatokanayo na gesi kwa ajili
ya kuboresha maeneo rasilimali hiyo inapopatikana. Akapendekeza kijengwe
Chuo Kikuu Mtwara kitakachofundisha watanzania elimu ya gesi na pia
vijengwe viwanda vitatu kwa faida ya wana mtwara. Mapendekezo ambayo
pia yamewahi kutolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA
kwa mwaka 2011 na 2012, katika hali kama hii ya kushindwa kutimiza
wajibu na kusababisha migogoro, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali ikiri kuwa imeshindwa kuiongoza sekta hii.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya kudumu ya bunge ya nishati na madini
ilitoa mapendekezo ya kukamilishwa kwa sera na sheria ya gesi kwa haraka
na umakini mkubwa. Kamati pia ilishauri serikali kuonyesha katika sera
na sheria hiyo ya gesi asilia jinsi ambavyo mapato yanayotokana na gesi
asilia yatakavyo simamiwa, mapendekezo hayo ya kamati yalizingatia wingi
wa upatikanaji wa nishati hii kwa sasa katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kushangaza serikali imeendesha
mchakato mzima wa kutengeneza rasimu ya gesi asilia bila kuwa na
ushiriki mkubwa wa wananchi kinyume na mapendekezo ya kamati ya kudumu
ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, hakukuwa na uhamasishaji wa kutosha kwa
wananchi katika kutoa maoni juu ya rasimu ya kwanza ya gesi iliyotolewa
na Wizara ya Nishati na Madini na ndio maana mahudhurio katika sehemu
ambako mijadala iliendeshwa yalikuwa madogo sana. Kwa mfano katika
ukumbi uliopo Makumbusho ya Mwalimu Nyerere waliohudhuria siku ya kwanza
hawakufika hata 25 na siku ya pili hawakuzidi watu 30. Pia katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), wanafunzi na wadau wa gesi kutoka taasisi
hiyo muhimu ya elimu ya juu hawakujitokeza kwa sababu ya uhamasishaji
hafifu na hivyo kupelekea kuahirishwa kwa zoezi hilo katika suala la
msingi linalohusu uchumi wa watanzania. Lakini pia suala hili kwa wakati
huo lilitakiwa liwe ni mjadala wa kitaifa ndani ya vyuo vikuu vingi
nchini na jamii kwa ujumla ikihusisha pia mikoa yote ambako kuna uvunaji
au utafutaji wa gesi asilia ili kupanua dhana ya kuwashirikisha
wananchi katika maswala yanayohusu rasilimali za Taifa kinyume na
uhalisia wenyewe.
Mheshimiwa Spika, Kufuatia kasoro zilizoanza kubainishwa na
wabunge na wadau mbalimbali katika toleo la tatu la rasimu ya gesi;
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo ni kwanini
haikuzingatia baadhi ya maoni muhimu ya wadau yaliyotolewa mara baada ya
kutolewa kwa rasimu ya kwanza ya Sera hiyo. Aidha, Kambi Rasmi ya
Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inataka mchakato wa kupitia rasimu ya
tatu ya sera hiyo upanue wigo wa ushirikishwaji wa wananchi katika mikoa
yote ambayo utafutaji wa gesi asilia umeanza au unatarajiwa kuanza
pamoja na mikoa yote itakayofikiwa na miradi ya uendelezaji wa gesi
asilia.
Ikumbukwe kwamba udhaifu wa Serikali katika kuwezesha ushirikishwaji wa
wananchi katika mipango na miradi ya maendeleo na matumizi mabaya ya
muda mrefu ya rasilimali za nchi ni kati ya sababu zilizochangia
migogoro katika maeneo ambayo uendelezaji wa miradi ya gesi asilia
umeanza hususani katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali
kuwashirikisha wananchi na kutoa taarifa za kutosha na kwa wakati juu ya
suala hili la gesi asilia na rasilimali nyingine za taifa ili kuondoa
mkanganyiko unaojitokeza kwa wananchi juu ya mchakato mzima wa uwekezaji
kwenye rasilimali za Taifa, rasimu ya sera haikidhi haja irudishwe upya
kwa wananchi ikiwemo kwenye mikoa yote yenye utafutaji unaoendelea na
maeneo ya matumizi yanayotarajiwa.
Mheshimiwa spika, kwa mujibu wa michango mbalimbali iliyotolewa
na wabunge wakati wa mjadala wa kuchangia bajeti ya Wizara ya Nishati na
Madini 2012/2013 waheshimiwa wabunge pia walitaka kujua kama taifa
mipango ambayo serikali imeweka kufuatia kugundulika kwa kiasi kikubwa
cha gesi, kama rasilimali watu kwa maana ya wataalamu waliobobea, idadi
ya wataalamu tunaowaandaa kwenda sambamba na uhalisia wa uhitaji wa
wataalamu wenyewe katika sekta ya gesi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inarudia kuitaka serikali kufanya maandalizi ya kutosha ya kuwekeza
katika suala la rasilimali watu ili kuondoa matatizo yanayoweza
kujitokeza hivi karibuni kutokana na uhaba wa wataalamu katika fani
hiyo.
3.1 Ugawaji wa Vitalu vipya vya utafutaji wa gesi na mafuta.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa
majukumu ya Wizara kwa mwaka 2012/13, baada ya kupokea ushauri wa Kamati
kuhusu kusitisha ugawaji wa vitalu vya utafutaji gesi, Serikali
iliahidi kwa kusema kuwa “zoezi la kugawa vitalu vipya kwa ajili ya
utafutaji wa mafuta umesitishwa mpaka hapo sera ya Gesi Asilia na
sheria ya Gesi Asilia nchini itakapokamilika na kuanza kutumika”
Mheshimiwa Spika, Jambo la kushangaza ni kwamba wakati sera ya
Gesi Asilia ipo kwenye rasimu na ndio kwanza wabunge tumeletewa kutoa
maoni, Serikali tayari imetangaza kwa mujibu wa vyombo vya habari na
tamko la TPDC tarehe 18.5.2013 kuanza mzunguko mwingine wa leseni za
utafutaji Mafuta na Gesi kwenye Bahari kuu na Ziwa Tanganyika Kaskazini.
Kutoa leseni kwenye kitalu ya utafutaji ni hatua ya kuelekea kutoa
mkataba wa uvunaji.
Zabuni hii mpya ya leseni za vitalu vya utafutaji imetolewa wakati kuna
maamuzi ya Bunge kuzuia ugawaji huu mpya mpaka sera ya Gesi Asilia na
Sheria ya Gesi vikamilike. Haraka hii ya serikali kugawa vitalu bila
sera wala Sheria inatoka wapi.
Mheshimiwa Spika, uharaka huu unaifanya Kambi Rasmi ya Upinzani
iwe na mawazo kwamba Wizara iliidanganya Kamati ya Kudumu ya Bunge, je
ilifanya hivyo kwa maslahi ya nani? Tunamtaka Mheshimiwa Waziri alieleze
Bunge sababu za kuidanganya kamati inayofanyakazi kwa niaba ya Bunge.
Wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikitoa ufafanuzi potofu kwamba
tangazo la sasa halina athari kwa kuwa maamuzi ya utoaji wa leseni
yatafanyika mwaka 2014 baada ya kuwa na sera na sheria. Hata hivyo,
ufafanuzi huu wa Wizara hauzingatii ukweli kuwa, hata zabuni ya maombi
ikiwemo vigezo, utaratibu na masuala mengine ilipaswa kutolewa kwa
kuzingatia misingi mipya inayopaswa kuwekwa kupitia mchakato wa katiba
mpya na maandalizi ya Sera na Sheria ya Gesi Asili.
Katika muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kutengua tangazo hilo mpaka baada ya kukamilika kwa mchakato wa katiba
mpya na maandalizi ya sera na sheria mpya sio tu kwenye sekta ndogo ya
gesi asilia bali katika sekta nzima ya nishati ikiwemo juu ya masuala
yanayohusu mafuta.
Vinginevyo, watanzania wataamini kwamba hatua hiyo imefuatia msukumo
uliotokea baada ya ziara ya Rais wa China nchini Tanzania; hasa kwa
kuzingatia namna ambavyo, pamoja na vitalu vilivyotangazwa kwenye
zabuni ili kutolewa kwa ushindani, vipo vitalu ambavyo vimebakishwa
mikononi kwa TPDC ambavyo mazingira ya mchakato wa utolewaji wake
yanaacha maswali.
Mheshimiwa spika, Katika hatua ya sasa Wizara ya Nishati na
Madini ijielekeze katika kusimamia mikataba ambayo tayari nchi yetu
imeingia mpaka sasa kwa maslahi ya nchi na kupitia upya mikataba mibovu.
Aidha, katika kutekeleza azma hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani
inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Wizara ya Nishati na Madini kutoa kwa
Bunge taarifa ya uchunguzi wa mikataba hiyo iliyokamilika toka mwaka
2012 lakini imeendelea kufanywa kuwa siri mpaka hivi sasa.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka pia serikali kuweka wazi
kwa watanzania wote mikataba hiyo na mingine ambayo serikali imeisaini
inayohusu rasilimali za Taifa hili. Aidha inatoa mwito kwa wananchi
kuhakikisha kwamba masuala ya uwazi katika mikataba yanapewa kipaumbele
katika katiba mpya, sera na sheria.
Mheshimiwa spika, Kitendo ambacho serikali ilikuwa inakifanya
kupitia Shirika la Maendeleo ya Petrol (TPDC) cha kugawa vitalu vipya
nane vya gesi wakati bado sera na sheria ya gesi haijakamilika ni
ushahidi tosha kuwa kuna watu wachache katika serikali wameanza
kulichukulia suala hili la gesi asilia kwa manufaa ya watu binafsi.
Mheshimiwa spika, Wizara ya Nishati na Madini katika bajeti yake
ya miaka iliyopita imekuwa ikitenga fedha nyingi kwa ajili ya mishahara
na posho kitengo cha sheria cha Wizara. Jambo hili la kugawa vitalu
vipya nane vya gesi wakati sera na sheria kuhusu gesi havijakamilika
linadhihirisha siyo tu udhaifu katika idara hii ya ushauri wa kisheria
bali pia mazingira yanayoashiria mianya ya matumizi mabaya ya raslimali
za umma katika zoezi hili. Kambi Rasimi ya Upinzani Bungeni
inalichukulia jambo hili kuwa ni udhaifu ambao hauwezi kuvumilika hata
kidogo na tunaitaka wizara ieleze sababu hasa za kuendesha zoezi hili
kinyume na maoni na mapendekezo ya kamati ya kudumu ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba chama
lege lege huzaa serikali legelege; udhaifu huu wa wizara unaweza
kutafsiriwa kwamba unachangiwa na ushiriki wa Chama cha Mapinduzi (CCM)
kupewa na kukubali hisa toka kwa moja ya makampuni yanayojihusisha na
utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini, kampuni ya Ophir energy.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi za Bunge za tarehe 08.11.2012 ni kuwa
wakati CCM ikipewa hisa wapo pia baadhi ya watanzania ambao waligawiwa
sehemu ya hisa hizo kwa ajili ya CCM
Aidha,Katibu Mkuu wa CCM Abdurahaman Kinana anatajwa na vyanzo
mbalimbali kwamba amewahaki kuwa Mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya
kampuni ya Artumas ambayo iliingia mkataba na Serikali wa kuzalisha Mega
Watt- 300 za umeme Mtwara eneo la Mnazi Bay. Mkataba huo ulikuwa wa
misingi ya mabadilishano ya gesi kwa nishati ya umeme (gas for power).
Kwamba Artumas ingechimba na kuuza gesi asilia na kuilipa serikali kwa
pamoja na mambo mengine kuizalishia umeme wa 300MW. Baadae mwaka 2010
Artumas baada ya kufaidika vya kutosha kutokana na uvunaji na uuzaji
iliacha kuendeleza mradi huo kwa kisingizio cha madai ya mdororo wa
Uchumi mwaka 2009 na kuuza hisa zake kwa kampuni ya Wentworth ya Ufaransa.
Mheshimiwa Spika, Ushiriki huu wa viongozi waandamizi wa Chama
Cha Mapinduzi na chama hicho kwenye shughuli ambazo zinaitia hasara
serikali unazua mazingira ya kwamba CCM inasababisha unyonywaji wa Taifa
na wananchi, na hivyo ni dhahiri si mwafaka kuendelea kuongoza nchi
hii. CCM na baadhi ya viongozi wake wamekuwa wakifaidika kutokana na
ombwe la kisera na kisheria katika sekta hii na nyingine muhimu. Katika
hali kama hii, maneno ya Mwalimu Nyerere yanapaswa kuongezewa nukuu mpya
kwamba “chama cha mafisadi huzaa serikali ya mafisadi”.
3.2 Haki ya Wananchi kumiliki rasilimali asilia
Mheshimiwa Spika, Wakati Katiba yetu inatambua haki ya kumiliki mali na
hifadhi ya mali hiyo na inakataza unyang'anyi wa mali kwa lengo la
kuitaifisha au kwa malengo mengine, haki za wananchi kumiliki rasilimali
zao za asilia kama ardhi, madini, mafuta, gesi asilia, misitu na
wanyama pori, uvuvi, n.k., zimekuwa haziheshimiwi na mamlaka za
kiserikali kwa hoja kwamba rasilimali asilia hizo ni mali ya umma.
Mheshimiwa Spika, Dhana ya mali ya umma ni dhana yenye asili yake
katika ukoloni. Ni dola ya kikoloni ya Kijerumani ndio ilikuwa ya
kwanza kutangaza kwamba mali asilia zote katika koloni lao la Tanganyika
ni mali ya Mfalme wa Kijerumani. Baada ya Wajerumani kushindwa Vita ya
Kwanza ya Dunia na kunyang'anywa makoloni yao ya Afrika, dola ya
kikoloni ya Waingereza iliyokabidhiwa Tanganyika, walitangaza kwamba
rasilimali asilia zote ni mali ya umma chini ya mamlaka na udhibiti wa
Gavana wa kikoloni. Dhana hii ilipokelewa bila mabadiliko yoyote ya
msingi baada ya uhuru na ndio imekuwa msingi mkuu wa sera za rasilimali
asilia za nchi yetu kwa muda wote wa uhuru wetu. Jambo hili ni hatari
kwani mali ya umma maana yake ni mali isiyokuwa na mwenyewe, na ndio
maana wenye nguvu wanatumia mwanya huo kupora wasio na nguvu.
Mheshimiwa Spika, Kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni, utekelezaji
kivitendo wa dhana ya mali ya umma wakati wote wa uhuru umekuwa ni
kuwanyang'anya wananchi rasilimali asilia zilizoko kwenye maeneo yao na
kuzimilikisha mamlaka za Serikali (wakati wa miaka ya uchumi-dola), au
kuzimilikisha kwa wawekezaji wa kigeni katika zama hizi za soko holela
kwa kisingizio cha huria.
Mheshimiwa Spika, Matokeo ya mfumo huu ni kwamba milki na mamlaka
ya maamuzi juu ya matumizi ya rasilimali asilia yameondolewa mikononi
mwa wananchi na kuhamishiwa kwenye mikono ya warasimu wa Serikali. Sio
hio tu, wananchi wamejikuta wakiondolewa kwa nguvu kutoka kwenye maeneo
yao ili kuwapisha wamiliki wapya wa rasilimali hizo, yaani wawekezaji wa
kigeni au wa ndani. Kwa sababu hiyo, uchumi wa wananchi umeanguka,
umaskini umeongezeka na matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu
yameongezeka.
Mheshimiwa Spika, Dhana ya mali ya umma katika umilikaji wa
rasilimali asilia imehakikisha kwamba maeneo yenye rasilimali asilia
hayapati faida na manufaa yanayotokana na uwepo wa rasilimali hizo
katika maeneo yao. Mrahaba, kodi na tozo nyingine zinazotokana na
matumizi au mapato ya rasilimali hizo yanapelekwa kwenye mamlaka za
Serikali Kuu. Kwa upande mwingine, madhara yanayotokana na matumizi ya
rasilimali hizo Kama vile uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya
matumizi ya rasilimali husika, yanawaangukia wananchi wa maeneo ziliko
rasilimali hizo.
Mheshimiwa Spika, naomba nieleze mtazamo na msimamo wa Kambi
Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA kuhusiana na umiliki pamoja na
uendelezaji wa Raslimali zetu asilia,ni kwamba:
i. Wananchi hawatanyang'anywa rasilimali zao asilia na mamlaka za
Serikali kwa ajili ya matumizi na watu au taasisi nyingine bila kwanza
Wananchi watakaoathiriwa na unyang'anyi au matumizi hayo kutoa ridhaa
yao baada ya kupatiwa taarifa zote na kamili zinazohusu matumizi
yanayotarajiwa ya rasilimali hizo na athari za matumizi hayo kwa
mazingira, kiuchumi na kijamii (the right of prior informed consent).
Wananchi Kama wamiliki wa msingi wa rasilimali asilia, watakuw
ii.Wananchi wana haki ya kulipwa mrahaba kwa ajili ya matumizi ya watu
au taasisi nyingine ya rasilimali asilia za Wananchi, wakati mamlaka za
Serikali za mitaa, Majimbo na Serikali Kuu zitakuwa na haki ya kutoza
kodi mapato yatakayotokana na matumizi ya rasilimali hizo.
3.4 BOMBA LA GESI TOKA MTWARA HADI DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Spika, Pamoja na ushauri wa kambi rasmi ya upinzani
bungeni wakati wa kuwasilishwa kwa bajeti ya wizara 2012/2013 kuitaka
Serikali kuwasilisha Bungeni na kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi
husika ili Bunge liweze kuishauri na kuisimamia Serikali kwa mujibu wa
katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63; kuanzia katika
hatua za awali kuhakikisha kwamba maslahi ya Taifa yanalindwa katika
hatua zote na pia wananchi wananufaika kutokana na fursa za uwekezaji
huo mkubwa lakini bado serikali haikutilia maanani ushauri huu. Matokeo
yake siyo tu kusababisha mkanganyiko kwa wakazi wa Lindi na Mtwara bali
pia kuacha maswali mengi kwa watanzania juu ya nini hasa nia ya serikali
kwa kuficha mikataba inayohusu rasilimali hizi za Taifa kwa wananchi
wake na hata kwa chombo cha kuwakilisha wananchi kama Bunge.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA
inaitaka Serikali isiendelee na ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara
mpaka Dar Es Salaam hadi kwanza; Mosi, iweke wazi kwa Bunge mikataba
yote inayohusu uendelezaji wa gesi asilia ikiwemo ya ujenzi wa Bomba
hilo. Pili, ikutane na wananchi kuwashirikisha na kuhakikisha manufaa
kwa taifa na kwao.
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA imeshangazwa na
hatua ya Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo tangu
kuibuka kwa mgogoro huo amejikita zaidi katika kutoa kauli kupitia
vyombo vya habari badala ya kwenda kukutana na wananchi hatua kwa hatua
na kuwezesha ufumbuzi kupatikana. Aidha, manufaa kwa wananchi wa Lindi
na Mtwara ambayo taarifa yake imechapwa kwenye vyombo vya habari yaletwe
kama taarifa rasmi bungeni ikiwa na ulinganisho baina ya shughuli za
kijamii zilizofanywa na makampuni tajwa pamoja na miradi iliyotekelezwa
na Serikali kufuatia mapato katika sekta hii tangu mwaka 2004 na thamani
halisi ya mapato ambayo makampuni tajwa na Serikali wamepata.
Mheshimiwa Spika, pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya
kusafishia gesi asili Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya mradi huo,
Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia kuitaka Serikali kueleza ni miradi ipi
iliyotengewa fedha inayoambatana na mradi huo ambayo imepangwa
kuwanufaisha wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara na imetengewa kiasi
gani cha fedha katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 ili kuharakisha
msukumo wa maendeleo kwa mikoa hiyo ya Kusini ambayo imesahaulika kwa
siku nyingi na hivyo siyo tu kuharakisha maendeleo kwa mikoa ya Kusini
bali pia kuhakikisha usalama wa mradi huo mkubwa kwa manufaa mapana ya
jamii ya kitanzania.
Mheshimiwa Spika, kuanza kwa ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi
asilia pamoja na bomba la kusafirisha gesi hiyo hadi Dar es salaam na
usambazaji wa umeme katika vijiji 52 vinavyopitiwa na bomba la gesi
kutoka Mtwara hadi Lindi haikidhi wala kujibu kilio cha wananchi wa
Mtwara na Lindi cha kutaka ugunduzi wa gesi asilia katika mikoa hiyo
uweze kunufaisha mikoa hiyo kimaendeleo kutokana na kuwa nyuma
kimaendeleo miaka 52 baada ya uhuru wa Taifa hili.
Mheshimiwa Spika, wakati waziri akiwasilisha hotuba ya bajeti ya
mwaka 2012/2013 ya Wizara ya Nishati na Madini tarehe 27-07-2012
aliliambia bunge hili kuwa, kusainiwa kwa mkataba wa mkopo kati ya
Tanzania na China kwa ajili ya kusafirisha Gesi asili na ujenzi wa Bomba
la kusafirishia gesi toka Mnazi BAY hadi Dar es saalam na kusainiwa kwa
mikataba mingine mitano (5) na mkataba wa uzalishaji na ugawanyaji wa
mapato ya mafuta na Gesi asili kuwa ni miongoni mwa jitihada ambazo
serikali imechukua katika jitihada za kukabiliana na tatizo sugu la
umeme hapa nchini, hata hivyo kama ulivyo utaratibu wa serikali mikataba
hii inaendelea kuwa siri.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali na
Wizara ya Nishati na Madini kuainisha miradi hiyo na kuitengea fedha ili
wananchi wa mikoa ya kusini waweze kunufaika na rasilimali hiyo kwani
kwa muda mrefu sana wamekuwa wavumilivu wakisubiria utekelezwaji wa
ahadi za kuwapelekea maendeleo kwa miaka mingi bila kuyaona wala
kuyapata.
Kambi rasmi ya Upinzani , inaitaka serikali isitishe ujenzi wa Bomba
hilo kwanza iende ikajadiliane na wananchi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na
Pwani na wakubaliane jinsi ya kuendelea na mradi huo ndipo ujenzi wa
bomba hilo uweze kuendelea , kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeamua
kumaliza tatizo la msingi kwani serikali ikiendelea bila kujali madai ya
wananchi hawa na kuamua kutumia mabavu kujenga hakuna atakayekuwa
mshindi kati ya serikali na wananchi hawa. Ni rai yetu kuwa serikali
itaweza kuiona busara hii ili gesi iweze kuwanufaisha watanzania wote
yaani wa Mtwara na wale wa maeneo mengine.
4.0 MAFUTA
4.1 MFUMO WA UAGIZIAJI MAFUTA KWA UFANISI
Mheshimiwa Spika, Marekebisho ya Sheria ya petrol (Petroleum
Supply Act 2008) kifungu cha 33(1) kinatamka kuwa uagiziaji wa bidhaa za
petroli lazima ufanyike kwa ufanisi na kwa kigezo cha unafuu mkubwa wa
gharama na kufafanuliwa zaidi na kifungu cha 33(2) ambacho kinaeleza
ufanisi wenyewe ikiwa ni pamoja na :-
a) Uagiziaji wa pamoja wa kushirikiana (Joint Procurement)
b) Uagiziaji wa ushindani (Compitative Procurement)
c) Uagiziaji wa shehena kubwa (Bulk Procurement)
d) Kwa kutumia fursa ya viwango vya kiuchumi (Taking advantage
of economic Scale). Pia Sheria imetoa fursa ya kubadili kwenye aina
nyingine za uagiziaji utakao onekana unatija zaidi.
Mheshimiwa Spika, sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji
na Nishati (EWURA) sura ya 414 pamoja na Petroleum Conservation Act
(cap 392) zimeongeza majukumu ya kudhibiti na kuratibu uagiziaji mafuta
kutoka nje. Pia mfumo wa ununuzi na usafirishaji wa mafuta kwa pamoja
umependekeza kuwa na mratibu (Petroleum Importation Co-ordinator - PIC)
wa kukusanya taarifa za mahitaji na kutayarisha zabuni.
Mheshimiwa Spika, Kampuni hii , iliratibiwa na EWURA lakini
ilisajiliwa kwa masharti ya sheria ya makampuni na hivyo kuifanya kuwa
kampuni binafsi inayomilikiwa na Umoja wa Makampuni yanayoagiza na
kusafirisha mafuta nchini (TAOMAC). Uendeshwaji wa Kampuni hiyo upo
chini ya bodi na Mwenyekiti wa bodi uteuliwa na mkutano wa wanahisa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa ikieleza jinsi
gani Wizara inavyoshindwa kusimamia mambo ya msingi kwa mujibu wa sheria
na kanuni za uwepo wake. Mfano dhahiri ni kitendo cha Mhe Waziri kuteua
Mwenyekiti wa Bodi ya PIC kwa kutumia Nafasi yake na mbaya zaidi
kumteua Ndugu James Andindile ambaye ni Kamishna msaidizi-Wizara ya
Nishati ni dhahiri kuwa Wizara itashindwa kufanyakazi yake ya usimamizi.
Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe.Waziri alieleze Bunge ni kwa
vipi ana uwezo wa kuingilia utendaji wa Kampuni Binafsi kwa kuteua
Mwenyekiti wa Bodi? Ni mfumo gani umewekwa wa kuhakikisha Wizara
inafanya usimamizi?
Mheshimiwa Spika, ili kuepusha watanzania kubebeshwa mzigo wa gharama kubwa ya mafuta katika Kikao
cha Arobaini na Mbili – Tarehe 9 Agosti, 2011,kulitolewa hoja ya
dharura kuhusu uhaba wa mafuta baada ya michango kadhaa ya waheshimiwa
wabunge na hatimae Serikali ilitoa kauli yake. Baada ya mjadala huo
Bunge lilifanya uamuzi. Hata hivyo hakukuwa na ufuatiliaji wa karibu
baada ya maazimio. Hali hii ni moja katika kasoro kubwa ambayo
kuanzia mwaka huu Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA
ilitaka irekebishwe. Katika Kamati zote zilizopo za sekta hakuna Kamati
ambayo inafuatilia maazimio yote ya Bunge ili Serikali kusimamiwa kwa
zile ahadi au maazimio tuliyoyapitisha hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Nishati na Madini ya Bunge la Tisa
iliweza kupendekeza kwa Serikali mara nyingi sana kuhusu suala la TPDC
kupitia kampuni tanzu ya COPEC kuanzisha biashara ya mafuta. Kamati ya
Nishati ya Bunge la Tisa ikazungumzia pia Bulk Procurement pia Strategic Reserve. Masuala yote haya yamehojiwa na Kambi Rasmi ya Upinzani mwaka 2011 na 2012
Mheshimiwa Spika, baada ya kushindwa kuchukua hatua hatimaye Serikali ikaleta ahadi nyingine, nanukuu “leo
hii tarehe 9 Agosti, 2011, Serikali kupitia EWURA imeipa leseni Kampuni
ya COPEC ambayo ni Kampuni Tanzu ya Serikali kupitia TPDC kuanza
kufanya biashara ya mafuta mara moja.
Naomba kurudia. Leo hii tarehe 9 Agosti, 2011 Serikali kupitia EWURA
imeipa leseni COPEC ambayo ni Kampuni Tanzu ya Serikali kupitia TPDC
kuanza kufanya biashara ya mafuta mara moja”.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2011/2012 wa fedha Wizara ya Nishati
na Madini, COPEC ilikuwa imepangiwa shilingi milioni 20 tu kwa ajili ya
kampuni hiyo kuanza kufanya biashara. Ukweli ni kwamba kampuni hiyo
haikuwa na miundombinu yoyote ya kuiwezesha kufanyabiashara kama
Serikali ilivyoagiza.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ilieleze Bunge toka ilipopatiwa leseni ya biashara hadi sasa COPEC imeongeza tija ipi katika biashara ya mafuta kwa watanzania?
Mheshimiwa Spika, Waziri aliahidi mbele ya bunge kuanza kwa mpango wa
utekelezaji uingizaji wa mafuta wa pamoja (Bulk procurement) mwezi
January 2012. Wizara ieleze kuanza kwa utaratibu huu umeokoa kiasi gani
cha pesa kilichokuwa kinapotea kabla ya kuanza kutumika kwa utaratibu
huu mpya na sababu za mpango huo kushindwa kushusha bei ya mafuta
kinyume na ahadi za Serikali.
5.0 UMEME
Mheshimiwa Spika, Bado kunaendelea kuwepo na utata kuhusu mgawo wa umeme
katika maeneo mengine ya nchi huku serikali ikikanusha kuhusu mgawo
wakati watanzania wakiendelea kupewa nishati hiyo kwa mgawo kwa nyakati
mbalimbali. Aidha Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini akiwasilisha
makadirio ya Bajeti ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka 2012/1013
aliliambia bunge lako tukufu kuwa “hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni 2012 lengo la kuondoa mgao wa umeme lilifikiwa kwa asilimia 100”.
Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inalitaka shirika la umeme Tanzania
(TANESCO) na Wizara ya Nishati na Madini kuwaambia ukweli watanzania
kuhusu mgawo wa umeme kwa kuzingatia hali mbaya ya shirika hilo kifedha
ambayo imeripotiwa na vyombo vya habari hivi karibuni kwa sehemu
ikichangiwa na wingi wa mikataba mibovu ya miaka mingi ya ukodishaji wa
mitambo ya umeme na hali ya sasa ya ununuzi wa ziada wa mafuta ya
kluendeshea mitambo ya dharura.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha kutowaambia wananchi ukweli kuhusu
mgawo wa umeme wakati wananchi wakipata nishati hiyo kwa mgawo huku
wakipewa sababu ambazo zinaonekana hazina ukweli kinazidi siyo tu
kushusha heshima na hadhi ya serikali kwa wananchi wake bali pia
kinadhihirisha udhaifu uliopo katika mfumo wa kiutendaji wa serikali
pamoja na mashirika yake likiwemo shirika la umeme Tanzania (TANESCO).
Mhesimiwa Spika, mradi wa kuboresha mifumo ya umeme katika jiji
la Dar es salaam ambayo imekuwa ndio kisingizio kikubwa cha mgawo wa
umeme hali ambayo inazua maswali mengi kwa watanzania. Hii ni kutokana
na ukweli kwamba kazi hiyo ilianza katika bajeti ya 2011/2012 na mpaka
sasa tatizo la kukatika kwa umeme bado linaendelea kitendo ambacho
kinatafsiriwa kuwa kazi hiyo bado haijakamilika miaka miwili tangu
kuanza kwa kazi hiyo iliyogharimu shilingi billion 120. Watanzania
wanapenda kujua ni lini hasa kazi hii itakamilika ili kupunguza kero ya
mgawo wa umeme kwa Dar es salaam na Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha serikali kutoa ahadi hewa zisizo
tekelezeka na kutochukua hatua stahiki dhidi ya watumishi wa serikali
wanaoihujumu TANESCO imekuwa ndio chanzo cha kuzorotesha ufanisi wa
shirika hili na kufanya liendelee kuendeshwa kwa hasara. Kambi Rasmi ya
Upinzani bungeni imekuwa ikishauri mara kadhaa juu ya kufikishwa
mahakamani kwa watumishi wote wa serikali na mafisadi wote wanaohujumu
uchumi wakiwemo wale wa TANESCO, Kiwira, Meremeta, Richmond n.k lakini
inaonekana kuwa ni utaratibu wa serikali hii au udhaifu wa serikali
katika kushughulikia watuhumiwa hao wa uhujumu uchumi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na udhaifu wa Serikali ya CCM katika
kuchukua hatua, kama ilivyokuwa katika kusamehe baadhi ya wezi wa EPA na
kuzimwa kwa sakata la Richmond lililosababisha hasara ya mabilioni ya
fedha. Hali hiyo imechangia kuzaliwa kwa sakata jipya la DOWANS
linalopelekea TANESCO kutakiwa kuilipa kampuni hii ya DOWANS ambayo
ilirithi mkataba wa kampuni hewa ya Richmond zaidi ya shilingi
97,000,000,000 kunazidi kulipatia taifa mzigo mkubwa. Hii ni kwa sababu
kodi za wananchi na malipo ya wateja zinazotumika katika kashfa zote
hizo na kuwasababishia wavuja jasho wa taifa hili kuwa na ugumu wa
maisha pamoja na kwamba waliahidiwa maisha bora kwa kila mtanzania.
Mheshimiwa spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka
serikali kutoa taarifa kwa Bunge lako tukufu ikieleza sababu
zinazowafanya wasimfikishe Mahakamani aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa
Tanesco Eng. William Mhando, siyo tu kwa matumizi mabaya ya ofisi
yaliyosababisha TANESCO hasara ya zaidi ya bilioni 6,000,000,000 kwa
kila mwezi baada ya kukatisha mkataba wa ununuzi wa mafuta kwa ajili ya
IPTL kutoka kwa BP waliokuwa wakiuza kwa bei nafuu na kuanza kununua kwa
kampuni za Oryx na Camel oil ambayo gharama yake ilikuwa juu bali pia
kwa kukiuka miiko ya maadili ya viongozi wa umma?
Mheshimiwa spika, katika mjadala wa bajeti ya mwaka 2012/2013
kulijitokeza pia wasiwasi wa namna TANESCO inavyojiendesha. Bunge
liliiomba Wizara ya Nishati na Madini ichunguze kwa kina suala la mapato
ya TANESCO na jinsi yanavyotumika. Ilionekana TANESCO kwa mwezi inapata
takribani Billion 60 au Billion 70. Mishahara ya wafanyakazi wa TANESCO
peke yake ni takribani Billion kumi na moja. TANESCO inatumia fedha
nyingi sana kununua umeme kutoka makampuni yanayotumia umeme hususani wa
dharura na kukodisha mitambo ya kufua umeme wa dharura. Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka serikali kupitia wizara ya Nishati na Madini
itoe majibu juu ya uchunguzi unaohusu uendeshaji wa shirika hili.
Mheshimiwa spika, Mnamo tarehe 18 Julai, 2011 serikali kupitia
Waziri Mkuu Mizingo Pinda iliahidi kupunguza matumizi yasiyo ya msingi
ya serikali ilikupata fedha ambazo zilitegemewa kuliongezea Shirika la
Umeme la TANESCO ili liweze kutekeleza mpango wa umeme wa dharura na
kuliongezea shirika hilo uwezo wa kujiendesha. Hata hivyo ahadi hiyo
ilichukua sura mpya baada ya serikali kushindwa kutekeleza tamko lake la
kwanza na kutoa ahadi nyingine tena ya kupata fedha kwa kukopa ambayo
mpaka sasa utekelezaji wake bado unasuasua.
Mheshimiwa spika, Mnamo 13 Agosti, 2011 serikali ilitoa ahadi ya
kuisaidia TANESCO kuweza kukopa bilioni 408 kutoka kwenye mabenki,
lakini mpaka sasa ni jumla ya dola za marekani milioni 65 ambazo ni sawa
na billion 104 tu ndizo TANESCO imeweza kukopa tena kwa kuchelewa. Hii
ni kwa mujibu wa taarifa ya serikali kama ilivyoainishwa na Wizara
katika ripoti yake ya utekelezaji kwa Kamati ya Nishati na Madini
TANESCO ilipokea fedha hiyo mwezi Januari mwaka huu (2013). Ahadi hizi
zisizotekelezeka zimekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya sekta hii
muhimu ya umeme ndiyo maana mpaka sasa ni sehemu ndogo sana ya
Watanzania wameunganishwa na huduma hii muhimu ya umeme.
Mheshimiwa spika, katika mwaka wa fedha 2012/13 kamati ya kudumu
ya bunge ya nishati na madini ilitoa mapendekezo kazaa kwa lengo la
kuboresha sekta ya umeme, mapendekezo hayo ya kamati pamoja na yale
yaliyotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni mengi hayajafanyiwa
kazi na serikali na hata yale ambayo yamefanyiwa kazi utekelezaji wake
ni kwa kiwango kidogo. Aidha mapendekezo ambayo hayajafanyiwa kazi ni
kama ifuatavyo:
(i) kuanzishwa kwa mfuko wa kuendeleza nishati ya umeme nchini kwa
lengo la kutumia mfuko huo kama mtaji (Equity) ili fedha zake zitumike
katika kuboresha huduma ya upatikanaji wa umeme nchini na pia kukopa
kutoka vyombo vingine vya fedha.
(ii). Kamati pia ilishauri wizara kutenga fedha za kutosha katika
uzalishaji, usambazaji na usafirishaji wa umeme kwani vinategemeana. Cha
kushangaza katika bajeti ya serikali ya mwaka 2013/2014 haijatengwa
fedha yoyote ile kwa ajili ya kuboresha njia za usafirishaji umeme mbali
ya kuwepo kwa asilimia 22.5 ya upotevu wa umeme unaozalishwa
inayosababishwa na miundombinu chakavu ya umeme.
(iii). Kamati baada ya kuona ugumu na gharama ambayo TANESCO itapata
katika kusafirisha mafuta toka bandarini kwenda Nyakato Mwanza ilishauri
tangu kwenye bajeti ya mwaka 2011/2012 na kurudia ushauri huo katika
bajeti 2012/2013 kwamba mradi huu uhamishiwe sehemu ambayo yatapatikana
mafuta ya uhakika na mitambo hiyo itumie mafuta ya dizeli ili kuweza
kunusuru gharama ambazo nchi itaingia baadaye na kupelekea ufanisi wa
mitambo hiyo kuwa mdogo.
(iv) Pia Kamati iliitaka serikali kuiwezesha TANESCO
kumiliki mitambo yake badala ya kutegemea mitambo ya kukodi ambayo
inaligharimu shirika hilo fedha nyingi linazolipa kwa makampuni
yanayomiliki kama capacity charge.
Mheshimiwa Spika, Katika hoja hii Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni
inaamini kwamba kamati ilifanya uchunguzi wa swala hili kabla ya kutoa
ushauri kwa serikali. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
serikali kutoa mchanganuo wa gharama ambazo TANESCO itazipata katika
kusafirisha mafuta mazito ya mitambo ya kufua umeme inayo jengwa Nyakato
Mwanza.
Mheshimiwa spika, katika hoja hii serikali imejaribu kueleza
jitihada yake ya kujenga mitambo mbalimbali ya kufua umeme wa gesi
ikiwemo ile ya Kinyerezi, Ubungo na Mwanza.
Mheshimiwa spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
serikali kueleza bayana namna mitambo hii inayojengwa itakavyokuwa
mbadala wa mitambo ya kukodi kuliko kuendelea kijisifia inajenga mitambo
wakati kuna baadhi ya mitambo imekamilika lakini bado mitambo ya kukodi
haipungui na TANESCO inazidi kulipa capacity charge.
Mheshimiwa spika, umeme vijijini, zaidi ya bilioni50 ambazo REA
imetengewa, kiasi hiki ni kikubwa, hivyo kitendo cha Wizara kutenga
fedha kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini bila kutaja idadi na majina
ya vijiji vitakavyonufaika na miradi ya fedha hizo linatoa mwanya wa
kutumia vibaya fedha za serikali. Hali hii imejitokeza pia katika
Taarifa za Serikali za mwaka wa fedha 2012/2013 ambapo hakuna vijiji vya
kutosha vilivyooneshwa kunufaika na hivyo kuleta mkanganyiko mkubwa
katika utekelezaji wa miradi hii vijijini.
Mheshimiwa Spika, pia tunamtaka Waziri aelezee juu ya mradi
uliotengewa fedha na Serikali katika bajeti mwaka wa fedha 2011/2012
mradi uliohusu taa za mwanga bora vijijini ambao ulitakiwa kutekelezwa
Bukombe, Kahama, Biharamulo na Chato. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali itoe majibu kwa nini mradi huo haukutekelezwa wakati fedha za
mradi huo zilitengwa? Pamoja na majibu hayo Kambi Rasmi Bungeni pia
inaitaka Wizara kueleza juu ya mradi mwingine ambao ulifahamika kwa jina
la “TANZANIA AFFORDABLE RURAL ELECTRIFICATION PLAN” ambao ulitakiwa
utekelezwe Bukombe na Kibondo, hasa juu ya hatua iliyofikiwa hadi sasa.
Mheshimiwa Spika, TANESCO imefika hapo ilipo sasa kutokana na
kutokuwa makini katika uingiaji wa mikataba mbalimbali na makampuni
yanayoiuzia umeme. Kamati ya wataalam wa sheria ya Bunge wakati wa
sakata la RICHMOND ilishauri yafuatayo kuhusiana na mikataba: “kuna
ulazima kwa Mikataba mikubwa ambayo inahusu maslahi na manufaa ya Taifa
kama vile Mkataba wa IPTL kuwasilishwa Bungeni, kwa utaratibu wa dhana
ya demokrasia ya uwajibikaji (accountability in a Parliamentary
democracy) kwa ajili ya ushauri wa Bunge kuwasilishwa Bungeni….. Aidha,
Kwa kuzingatia kuwa Mikataba mibovu kati ya TANESCO na Makampuni
mbalimbali ambapo Makampuni hayo yanalipiwa kodi yote na TANESCO imekuwa
ni chanzo cha bei kubwa za umeme katika nchi yetu, na kwa kuzingatia
kuwa Mikataba hiyo inasababisha Sera muhimu za Taifa, kama vile, Sera ya
Kupiga vita Umaskini, Sera ya Huduma Bora kwa Jamii, Sera ya Taifa ya
Nishati inayolenga kusambaza nishati ya bei nafuu vijijini n.k.
kutotekelezeka, tunashauri kuwa Mikataba hiyo ipitiwe upya ili
irekebishwe, kwa maslahi na manufaa ya Taifa letu”.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mheshimiwa
Waziri alieleze Bunge katika ufanyaji kazi wake ni mikataba mingapi ya
uzalishaji wa umeme na kuiuzia TANESCO, Madini au Gesi imefungwa bila ya
kuzingatia ushauri au mapendekezo yaliyokwishatolewa Bungeni? Kama
imefanyika je jukumu la Bunge kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba
Ibara ya 63 ina maana gani?
Mheshimiwa Spika, matumizi mabaya ya raslimali za umma hayako
katika mikataba ya kukodi mitambo ya umeme tu, bali katika ununuzi wa
huduma za kisheria. Hivyo, narudia kutoa mwito kwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali aeleze ni kiasi cha fedha kilichotumika kwenye kuendesha kesi
za Dowans na IPTL mpaka sasa na hatua zilizochukuliwa dhidi ya mawakili
wa TANESCO na makampuni binafsi yanayotuhumiwa kusababisha mzigo mkubwa
wa gharama za kesi ambazo serikali inashindwa kwa nyakati mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Izingatiwe kuwa kwa mwaka wa fedha 2011/2012
pekee jumla ya shilingi bilioni 10 zimetumika kwa ajili ya gharama za
kuendesha kesi hizo kwa kuilipa kampuni ya Rex Attorneys na Makampuni
mengine ambayo kwa nyakati mbalimbali yamekuwa yakiiwakilisha serikali
na TANESCO na kushindwa katika mahakama za kitaifa na kimataifa.
Mheshimiwa Spika, kufuatia mfululizo wa TANESCO kushindwa mahakamani
huku mabilioni ya walipa kodi na wateja wake yakitumika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inapendekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu
wa Hesabu za Serikali (NAO) na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma
(PPRA) wachunguze tuhuma za ufisadi na ubadhirifu kwa Shirika la Umeme
(TANESCO) kwenye matumizi ya mabilioni katika idara ya sheria na
ununuzi wa huduma za kisheria kutoka makampuni binafsi unaofanywa na
TANESCO.
Ukaguzi na uchunguzi huo ufanywe kuhusu matumizi na ufanisi wa huduma za
kisheria ambazo TANESCO imekuwa ikizipata kutoka kwenye makampuni
binafsi katika kesi kubwa za kimataifa ikiwemo ya Dowans na IPTL kwa
kurejea pia maoni niliyoyawasilisha bungeni tarehe 27 Julai 2012.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Kambi Rasmi bungeni mwaka jana
ilitaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu matumizi ya kifungu cha
1005 cha Kitengo cha Sheria ambacho kina kasma ya 229900 ambayo kwa
mwaka wa fedha 2012/2013 kimetengewa kiasi cha Shilingi Bilioni 4 kama
gharama za utetezi wa Serikali katika kesi ya IPTL ikiwemo kwa ajili ya
kuilipa kampuni ya Mkono & Co. Advocates.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani iliitaka Serikali kueleza jumla ya fedha
zilizotumiwa na Wizara kati ya mwaka 1995 mpaka 2011 kwa ajili ya kulipa
makampuni binafsi ya uwakili kwenye kesi kubwa za kitaifa na za
kimataifa pamoja na kutaja orodha ya makampuni hayo.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali ilitakiwa ieleze mkakati wa
kudhibiti ongezeko la gharama za kisheria ambazo ni mzigo mkubwa kwa
mashirika ya umma na wananchi walipa kodi kwa kuwa yamekuwepo mazingira
ya kesi kuendelezwa kwa muda mrefu na kugeuzwa kuwa vitega uchumi vya
watu wachache. Nilitaja Mifano ya kesi zilizodumu kwa muda mrefu ni ya
IPTL ambayo Serikali inawakilishwa na Mkono and Co. Advocates na ile ya
Dowans ambayo Serikali imekuwa ikiwakilishwa kwa nyakati mbalimbali na
Rex Attorneys.
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Nishati na Madini na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali wanapaswa kulieza Bunge sababu za kuacha kutoa majibu
kuhusu suala hilo mpaka hivi sasa. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua
hatua ambazo Serikali imechukua juu ya matumizi hayo.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011 Benki ya Standard Hong-Kong ambayo
ni mdeni mkuu katika sakata la IPTL ilifungua kesi ya madai katika
mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICSID case Na. ARB/10/20) inayodai
kiasi cha dola za Kimarekani milioni 225, pamoja na riba katika
kuendesha kesi hiyo. Kampuni ya uwakili ya Mkono (inayomilikiwa na
Nimrod Mkono Mbunge wa CCM) ilipewa zabuni ya kuitetea Serikali katika
shauri hilo, na kwa kujiamini iliishauri Serikali kuwa kesi hiyo
tutashinda pamoja na wanasheria wengine kuwa na maoni kinzani kuhusu
suala hilo. Kampuni ya Mkono imekuwa ikiishauri Serikali isifanye
usuluhishi nje ya mahakama ya ICSID wakati wadai kupitia kwa Mfilisi wa
Mali na Madeni za IPTL (RITA) wanakubali kusuluhishwa nje ya mahakama.
Je, mpaka lini Serikali itaendelea kuingia gharama hizo na ni kiasi gani
Serikali imelipa kwa kampuni hiyo na zingine mpaka hivi sasa?
5.1 MPANGO WA UMEME WA DHARURA
Mheshimiwa spika, itakumbukwa kuwa Bunge lako tukufu lilipitisha
mpango wa umeme katika mkutano wake wa nne. Serikali ililiambia Bunge
hili usafirishaji wa gesi kutoka Songosongo hadi, Somanga hadi Dar es
salaam ungeongezwa ndani ya miezi kumi na mbili ili majenereta
yaliyokuwa yamenunuliwa kutumika katika mfumo wa gesi yafanye kazi ndani
ya miezi kumi na mbili. Aidha ilikusudiwa pia kuwa mpango huo ulilenga
kushusha gharama za uzalishaji wa umeme hapa nchini. Ikiwa sasa ni mwaka
mmoja na zaidi umepita fedha zinazidi kutengwa kwa ajili ya kununulia
mafuta mazito ya kuendeshea majenerata, kwa sehemu kubwa ikiwa ni kwa
ajili ya mitambo ya kufua umeme.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa
kauli kuhusu sababu za ucheleweshaji katika utekelezaji wa mpango wa
dharura wa umeme na kushindwa kubadilisha mfumo wa majenereta kutumia
gesi badala ya mafuta, na kama kweli dharura iliyokuwepo bado ipo au
imekwisha?
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa miradi ya dharura iliyotakiwa kuwa
imekamilika ni pamoja na mradi wa Jacobsen awamu ya pili ambao
ulitakiwa kutekelezwa kuanzia mwezi Januari hadi disemba 2012 ambao
ungezalisha mega-watt 150 na kuendeshwa na fedha za mkopo. Tunapenda
kupata ufafanuzi kuhusu miradi hii ya umeme wa dharura miradi mingapi
imekamilika, kiasi gani cha pesa kimetumika na kama taifa tunadaiwa
kiasi gani cha fedha ambazo hadi sasa zimekopwa kwa ajili ya miradi ya
umeme kwa vile ni miongoni mwa maeneo ambayo nchi hii imekuwa ikiingia
gharama kubwa lakini ikishindwa kumaliza tatizo hili na kuchangia katika
deni la Taifa ambalo sasa linafika trilioni 22.
Aidha Mheshimiwa Spika, moja ya mambo ambayo serikali iliahidi
kuyafanyia kazi katika mpango wa umeme wa dharura ni kununua mitambo
yake, napenda kunukuu maneno ya mheshimiwa waziri mkuu “Mheshimiwa spika ushauri mlioutoa ni wa msingi sana, moja mumesema serikali nunueni mitambo,
”Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kuliambia bunge hadi
sasa tangia kupitishwa kwa mpango wa umeme wa dharura ni mitambo
mingapi ya kuzalisha umeme ambayo inenunuliwa na tayari imeshaanza
kuzalisha umeme. Pia serikali iliambie bunge lako tukufu ina mpango gani
kuhusu mitambo ambayo tumekuwa tunakodi kwa maana ya mitambo ya Symbion
miaka miwili, na mitambo ya Aggreko ambayo yote tumekuwa tunalipa
capacity charge, je serikali imeandaa njia gani mbadala zaidi ya ambayo
tumekuwa tukitumia?
Mheshimiwa Spika katika mpango wa umeme wa dharura, mashirika ya mifuko
ya jamii kama NSSF nayo yaliruhusiwa kuwekeza katika sekta hii ya
umeme, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupata ufafanuzi kuhusu mipango
inayoendelea juu ya nia hiyo ya mifuko ya jamii kuwekeza katika sekta ya
umeme hapa nchini.
5.2 SYMBION POWER AFRICA LLC, TANESCO NA KUANZISHA KAMPUNI MPYA YA UMEME KUSINI MWA TANZANIA (SECO).
Mheshimiwa Spika, kutokana na andiko la kinadharia ‘conceptual
proposal’la kujenga mtambo wa kufua umeme katika mji wa Mtwara na
usambazaji wake lililoandikwa na kuwasilishwa Wizara ya Nishati na
Madini ,TANESCO na TPDC mnamo tarehe 07 Septemba 2012 na baada ya andiko
hilo kupitiwa kwa kina na TANESCO kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 12 Februari 2013 Symbion Power
Africa LLC waliandaa /waliwasilisha MOU baina yao na Tanesco ili iweze
kusainiwa kwa ajili ya kuanzisha kampuni ya kuzalisha umeme chini ya
kinachoitwa ‘Special Purpose Company’ (SPC) ,Kampuni hiyo itajulikana kama “Southern Electric Company” (SECO)
ambayo inaanzishwa chini ya utaratibu wa PPP .Kwa mujibu wa MOU ni kuwa
Kampuni hii itakuwa ni kwa ajili ya kujenga ,kumiliki na kuendesha
mitambo inayotumia gesi kuzalisha umeme 600 MW katika miji ya Mtwara na
Dar Es Salaam.
Aidha ,kampuni hiyo ‘mpya’ ya SECO itajenga ,kumiliki na
kuendesha mtandao wa usafirishaji na usambazaji wa umeme kutoka kusini
mwa Tanzania kwenda kwenye Gridi ya Taifa , Kaskazini mwa Msumbiji na
Malawi ( ….AND to build,own and operate transimission and
distribution networks that will link power plants in the south to the
Tanzania grid, northern Mozambique and Malawi (“the project”))
Mheshimiwa Spika, MOU hii iliingiwa baada ya Symbion kufanya mazungumzo na Shirika la umeme la Msumbiji ‘Electricite de Mozambique’ (EDM) kwa ajili ya kuwauzia umeme eneo la kaskazini mwa Msumbiji katika maeneo ya Pemba na Nacala, hii ni baada ya EDM kuonyesha kuwa watakuwa tayari kununua umeme kutoka Symbion Tanzania.
Aidha kwa mujibu wa MOU hiyo ni kuwa tayari Symbion wameshasaini
makubaliano na Wizara ya Nishati ya Malawi kwa ajili ya kuanzisha
uchunguzi kuhusiana na mradi huo wa umeme kutoka nje , kipengele E cha
MOU kinasomeka hivi, nanukuu “Symbion has signed an agreement with
the Ministry of Energy in Malawi that provides for the investigation of a
cross border project”
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa MOU kipengele cha 2.1 ni kuwa
Symbion ndio watakuwa na jukumu la kufanya upembuzi yakinifu kwa gharama
zao wenyewe na kuwasilishwa TIC kupitia kampuni ya ‘Special Purpose Company’ (SPC) kwa ajili ya kupatiwa hati ya PPP. Aidha, kampuni ya Special Purpose Company (SPC) itapewa hadhi ya kuwa ‘mwekezaji wa kimkakati’ ‘strategic Investor’ .
Aidha , kwa mujibu wa kipengele cha 2.2 cha MOU ni kuwa umbembuzi
yakinifu huo utahusisha pia kuhusiana na mtaji unaohitajika kuwekezwa na
SPC kwa ajili ya mtambo wa kuzalisha 300MW kwa kutumia gesi pamoja na
mtambo wa kuzalisha 300MW Kinyerezi DSM kwa kutumia gesi.
Mheshimiwa Spika, kipengele cha 2.4 cha MOU kinasema kuwa
upembuzi yakinifu huo utahusisha pia uwezekano wa kuhamisha mara moja
baadhi ya mitambo ya kuzalisha umeme kutoka mtambo wa kuzalisha umeme wa
Symbion Ubungo na kupelekwa Mtwara,lengo likiwa ni kuongeza ufanisi kwa
muda mfupi huko Mtwara.
Kwa mujibu wa kifungu cha 2.5 ni kuwa upembuzi yakinifu huo pia
utahusisha utoaji wa mafunzo ya kina kuhusiana na uendeshaji wa mitambo
ya kisasa ya uzalishaji,usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini
Marekani kwa ajili ya utawala wa baadae wa SPC .
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani inasikitishwa sana na tabia
ya Serikali hii ya CCM kutokana na tabia yake ya kuendelea kupuuza
maazimio ya Bunge hili ,kwani itakumbukwa kuwa Moja ya maazimio ya Bunge
kuhusiana na Richmond ilikuwa ni kuhusisha Kamati za Bunge katika
kuingia mikataba na makampuni ya kuzalisha umeme , sasa hapa sio
kuzalisha tu bali ni kuanzisha kampuni nyingine .
Aidha , tunataka kujua ni kwanini serikali hii ya CCM imeamua kusaini
MOU ya aina hii bila kuishirikisha kamati ya Bunge au Bunge , tena huu
ni mkataba wa kwenda kuuza umeme nje ya nchi wakati sisi tuna shida
kubwa ya umeme.
Je? hii haiwezi kwenda kuwa Richmond nyingine?
5.3 MIRADI MIKUBWA YA UMEME NCHINI 2013/2014
5.3.1 Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Mheshimiwa Spika, wakala huyu alianzishwa kwa sheria Na 8 ya
mwaka 2005 na alianza kazi rasmi oktoba mwaka 2007, ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2003. Lengo likiwa ni
kuwapatia wananchi waishio vijijini nishati bora. Pamoja na umuhimu wa
wakala huyu bado serikali haijaonyesha kwa vitendo kuwa ina nia ya
kusaidia wakala huyu ili aweze kutimiza majukumu yake kikamilifu na hasa
linapokuja suala la kuupatia fedha kama zinavyoombwa na zinavyopitishwa
na Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, Takwimu zinaonyesha kuwa serikali imekuwa
haitimizi wajibu wake wa kuipatia REA fedha kama zinavyotengwa na
kuidhinishwa na Bunge hili , kwa mfano mwaka 2008/2009 zilipitishwa shilingi bilioni 20.00 ila zilitolewa shilingi bilioni 12.06 sawa na asilimia 60. Mwaka 2009/2010 zilipitishwa shilingi bilioni 39.55, zilizotolewa ni bilioni 22.14 sawa na asilimia 56. Mwaka 2010/2011 zilipitishwa bilioni 58.883, zilizotolewa zilikuwa bilioni 14.652 sawa na asilimia 25. Mwaka 2011/2012 zilipitishwa bilioni 71.044,zilitolewa bilioni 56.748 sawa na asilimia 80 na mwaka 2012 /2013 zilipitishwa bilioni 53.158, zilitolewa bilioni 6.757 sawa na asilimia 13.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014 wakala
unahitaji kiasi cha shilingi bilioni 366.9 kwa ajili ya kutekeleza
miradi sita ya nishati vijijini ambayo ni pamoja na awamu ya pili ya
kusambaza umeme vijijini bilioni 200, mradi wa kupunguza gharama za miundombinu na usambazaji wa umeme vijijini bilioni 10, kupeleka umeme katika makao makuu ya wilaya mpya 13 bilioni 70, mradi wa kusambaza umeme kwenye maeneo yaliyopitiwa na njia kuu bilioni 75, mradi wa Global Village Energy Partinership bilioni 10.4 na mradi wa kuhamasisha na kuongeza matumizi ya nishati jadidifu bilioni 1.5.
Kambi rasmi ya Upinzani, inaitaka serikali kutenga fedha kama
zilivyoombwa na wakala yaani bilioni 366.9 kwa mwaka huu wa fedha na sio
kutenga kiasi cha shilingi bilioni 91 za ndani na bilioni 62 za nje,
kama Kifungu 3001, kasma 3113 zinavyoonyesha, kwani wakala huyu
asipopewa fedha kulingana na mipango ilivyo atashindwa kufikia lengo la
kusambaza umeme kwa asilimia 30 Vijijini
Aidha, Kambi rasmi ya Upinzani, inataka kujua fedha zilizotengwa kwa
ajili ya REA 2012/2013 asilimia 87 zimeenda wapi ? Mbona hazikupelekewa
REA kama Bunge lilivyokuwa limeamua?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na
CHADEMA, haikubaliani na pendekezo la Waziri aliloliwasilisha mbele ya
kamati ya Bunge (randama uk 22) la kuongeza tozo ya shilingi 100 kwenye
kila lita moja ya mafuta ya petrol kwa ajili ya nishati Vijijini kwani
huku ni kumwongezea mwananchi mzigo wa gharama za maisha, badala yake
tunaendelea kusisitiza kuwa fedha zilizoongezwa kwenye kila lita moja ya
mafuta ya taa mwaka 2011/2012 kwa hoja kwamba ni kuzuia uchakachuaji
shilingi bilioni 600 kwa mwaka zipelekwe zote REA kwani watumiaji wakuu
wa mafuta ya taa wapo vijijini na nusu zipelekwe TANESCO. Aidha
makampuni ya madini yalipe kodi na tozo za mafuta wanayosafirisha na
wanayotumia.
5.3.2 Thermal Power Operation Bilioni 273.207
Mheshimiwa Spika, mradi huu ni kwa ajili ya kuhudumia vituo vya
uzalishaji umeme ambavyo vimeungwa kwenye Gridi ya Taifa na kununua
vipuri vyake wakati kina cha maji kwenye mabwawa ya kufua umeme
kitakapopungua kutokana na ukame. Kwa mwaka huu fedha zilizotengwa ni
kwa ajili ya kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya dharura ya kufua
umeme na kununua umeme kutoka kwa wazalishaji hao binafsi.
Mheshimiwa Spika, Mnamo tarehe 28.07.2012 Naibu Waziri wa Nishati
na Madini (nishati) Mhe.Simbachawene wakati akiwasilisha maoni juu ya
hotuba ya bajeti alisema kuwa tatizo la mgao wa umeme nchini ni la
kupangwa mezani, nanukuu (hansard uk.488) ‘………..lakini kila unapokaa
siku mbili unaombwa kukubaliana na mgawo wa umeme na mkizungumza mezani
mgawo unatoweka .Kumbe umeme wa Tanzania ni suala la kuzungumza mezani
halafu mnakubaliana kuwa unakuwepo mgao au haupo;hii haikubaliki’
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani inaona kuwa hata suala
la kutenga fedha nyingi kiasi hiki kwa ajili ya mafuta ya kuendeshea
mitambo binafsi ya kuzalisha umeme wa mafuta nalo ni jambo la kupangwa
mezani, kwani kama tukiamua kuwekeza kwenye vyanzo vingine vya umeme
hakika tusingekuwa tunatumia fedha nyingi namna hii kwa ajili ya umeme
wa mafuta nchini tena kutoka kwa wazalishaji binafsi.
Mwenendo wa wizara hii ni kutenga mabilioni ya fedha kila mwaka , Kwa
mfano mwaka 2011/2012 zilitengwa bilioni 204.643, mwaka jana 2012/2013
tulitenga bilioni 51.3 (lakini serikali ikatumia kiasi cha shilingi bilioni 242.96 randama uk.4) na
mwaka huu wa fedha tunatenga bilioni 273.207 kwa ajili ya kununulia
mafuta ya mitambo ya kuzalishia umeme. Yaani kwa miaka 3 tu taifa
limeunguza fedha kiasi cha shilingi bilioni 720.81.kwa ajili ya
kulipa makampuni binafsi, hivi Mchuchuma,Liganga, Stiglersgorge,
inahitaji uwekezaji wa kiasi gani?
5.3.3 MRADI WA UMEME IGUNGA
Mheshimiwa Spika, kutokana na mradi wa umeme ambao unaendelea
katika Wilaya ya Igunga kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa
wananchi wa vijiji vya Mbutu, Mwamakona, Bukama, Igunga na vijiji
vingine ambavyo mradi huu unapita kutokana na kutokuridhishwa na kiwango
cha fidia ambacho walilipwa ili kuweza kupisha na kuachia ardhi yao,
nyumba zao na mazao yao kwa manufaa ya mradi huo .Wapo waliolipwa
shilingi laki sita, milioni moja nk
Kambi rasmi ya upinzani, imepokea malalamiko ya wananchi juu ya
viwango vidogo vya fidia kwani na madai yao ya kutoona tathimini
iliyofanywa kulingana na mali zao na pia hawakulipwa kwa njia ya hundi
pamoja na kutakiwa kufungua akaunti bali walilipwa kwa fedha taslimu.
Hivyo, tunataka kujua juu ya yafuatayo;
i. Ni lini wananchi hawa watalipwa kiasi halisi kulingana na ardhi na mali zao?
ii. Ni kwanini wananchi hawa walilipwa fedha taslimu na sio
kwa njia ya hundi kama ulivyo utaratibu wa malipo wa serikali?
5.3.4 SERIKALI NA MADENI YA SHIRIKA LA UMEME TANZANIA (TANESCO)
Mheshimiwa Spika kambi rasmi ya upinzani bungeni, inaishangaa
serikaLi hii ya CCM kwa kukosa dira ya kuongoza nchi hii, hali hii
inatokana na serikali yenyewe kuwa sehemu ya kudhoofisha Shirika lake
yenyewe huku ikitaka kuwaaminisha watanzania kwamba inashughulikia
matatizo ya kupatatikana kwa umeme nchini.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa matatizo yanayokwamisha shirika la
umeme Tanzania kujiendesha ni pamoja na madeni ambayo yamekuwa sugu
kutoka kwa makampuni mbalimbali, watu binafsi , mashirika , katika hali
ya kushangaza idara za serikali zikiwemo pia Wizara za Serikali ambayo
inajinadi kuweka mpango wa kumaliza tatizo la umeme wakati ikishindwa
kulipia hata bili zake za umeme.
Taasisi za serikali ambazo zinaonekana kuwa ni wadaiwa sugu hadi kufikia
mwazi Januari 2013 ni pamoja na Zanzibar State Fuel inayo daiwa kiasi
cha shilingi 46,136,823,543/=, Jeshi la wananchi wa Tanzania (TPDF)
linadaiwa shilingi 13,839,849,487/=, Jeshi la Polisi linalodaiwa
shilingi 8,994,752,654/= Wizara ya maji inadaiwa shilingi
4,997,245,027/= DAWASA inadaiwa shilingi 4,114,828,175/= na Jeshi la
MAGEREZA linalodaiwa shilingi 3,530,850,068/= pamoja na mifano hii
michache wadai wengine ni pamoja na Regional Water Engineers, Muhimbili
Medical Centre, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Hospitali za serikali,
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Radio Tanzania.
Kwa mjibu wa taarifa rasmi za TANESCO zilizopo ni kuwa shirika linadai jumla ya Tsh 83,773,824,632/= hadi mwezi januari 2013 kutoka kwa wadaiwa ambao ni wizara na taasisi za Serikali hii ya CCM .
Kambi rasmi ya upinzani bungeni, inaitaka serikali kueleza sababu
za kulihujumu shirika la umeme Tanzania kwa kutolipa bili za umeme,
lakini pia ikumbukwe kuwa kila mwaka bunge hili Tukufu linapitisha
bajeti kwa Wizara husika zenye vifungu vya matumizi mengine (0C) ambayo
hutumika kufanyia shughuli nyingine zikiwemo kulipia bill za umeme na
gharama za wizara husika , tunataka wakati wa majumuisho serikali itoe
maelezo kwanini imeshindwa kulipa hadi sasa, fedha hizo zinafanya kazi
gani na lini serikali italilipa shirika la umeme Tanzania ili kuepukana
na matatizo ambayo serikali inayasababisha yenyewe.
6.0 MADINI
Mheshimiwa Spika, sekta ya madini ni miongoni mwa sekta ambazo,
kama serikali ikiamua kutumia vizuri rasilimali hii ni miongoni mwa
rasilimali ambazo kama zikitumika kwa masilahi ya Taifa zinaweza kulitoa
taifa katika lindi hili la umasikini. Hata hivyo inaonekana kuwa bado
sekta hii kama ilivyo kilio cha watanzania walio wengi na wenye mapenzi
mema na taifa hili bado haijaweza kuchangia pato la Taifa kwa kiwango
kinachotakiwa.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali hazina ya
madini iliyothibitika hadi sasa ni pamoja na Dhahabu tani 222, Nikel
tani milioni 209, shaba tani milioni13.65, chuma tani milioni 103,
Almasi tani milioni 50.9, Limestone tani milioni 313, magadi soda tani
milioni109, chuma tani milioni 103, jasi tani milioni 3, phosipahate
tani milioni 577, na makaa ya mawe tani milioni 911. Lakini pamoja na
kuwepo kwa hazina hii mchango wa sekta hii katika uchumi wa Taifa na
maendeleo ya jamii haukidhi matarajio ya wananchi. Aidha miongoni mwa
vitu vinavyofanya sekta hii kutochangia vyema ukuaji wa uchumi ni pamoja
na misamaha katika ulipaji wa kodi ya madini. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaishangaa serikali hii ya CCM kwa kushindwa kufuta misamaha
inayotoa kwa makampuni ya uchimbaji wa madini hapa nchini licha ya
kwamba jambo hili limekuwa linapigiwa kelele na wadau walio wengi. Kama
taifa tunajiuliza na kutaka majibu toka kwa serikali ni nini nia hasa
siri ya serikali katika kuendelea kutoa misamaha hii ya kodi.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa ripoti ya kodi katika madini iliyotolewa na shirika la International Centre for Tax and Development (ICTD)
iliyotolewa mwezi April 2013 inaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa
nchi ambazo zinapata pato dogo la mapato ya ndani yanayotokana na madini
kwa wastani wa 1:1.3 ikilinganishwa na nchi ya Botswana ambayo
inawastani wa 1.32:1 ikifuatiwa na nchi ya Chile. Aidha ripoti hiyo
inaonesha kuwa Tanzania ingeweza kufikia kiwango cha nchi ya Chile kama
ingekuwa na viwango vya kutoza kodi kama nchi ya Chile kwa sekta ya
madini na kuchangia kukua kwa pato la Taifa endapo ongezeko ya kodi ya
thamani, kodi ya kusafirisha na kodi ya mapato zinazotokana na madini
zingechangia kupanda kwa pato la Taifa (GDP).
Mheshimiwa Spika, Swala la mrahaba limeonekana kutopatiwa jawabu
halisi kwani kiwango cha asilimia 4% kinachotozwa kwa sasa baada ya
kufanyika marekebisho bado ni kidogo. Pamoja na kwamba kamati ya Jaji
Mark Bomani kupendekeza kuwa tozo la mrahaba lizingatie ukokotoaji kwa
kigezo cha gross value badala ya net back value pendelezo hilo
halitekelezwi kwa ukamilifu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
serikali kuboresha mazingira ya utoaji wa mrahaba pamoja na kodi,
ikizingatiwa kuwa baadhi ya makampuni hayafuati sheria ya mpya ya madini
ya mwaka 2010 inayotaja kiwango kipya cha mrahaba (Royalty), na
kuchukua hatua nyingine za ziada kwa kuzingatia mapendekezo tuliyotoa
2011 na 2012 hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali ieleze kwanza ni makampuni gani ambayo hayajaanza kutumia
sheria hii mpya, pili ni hatua gani imechukuliwa dhidi ya suala hili
lakini pia viwango vya kodi na mrahaba vinavyotozwa vilingane na viwango
vinavyotozwa katika nchi nyingine kama Botswana.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mchango wa sekta ya madini katika
maendeleo na huduma za jamii (Corporate social responsibility); Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kuwa sekta ya madini inayo kazi ya
kuhakikisha maendeleo na huduma za jamii. Katika kufanikisha adhima hii
ripoti ya Jaji Mark Bomani ilipendekeza miongoni mwa mambo mengine ni
pamoja na wawekezaji kutoa huduma za jamii ili kuimarisha uhusiano na
jamii zinazozunguka migodi, wawekezaji washiriki katika mashauriano ya
mashauri ili wajue vipaumbele na mirahaba inayokwenda halmashauri
itumike katika kuboresha huduma za jamii.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mapendekezo hayo lakini hali ya
halmashauri ambako makampuni ya uchimbaji wa madini yanakopatikana bado
ni wilaya maskini sana. Halmashauri za Kahama, Geita, Tarime hazifanani
na thamani ya madini yanayopatikana katika maeneo yao. Pamoja na hayo
kuna mkanganyiko katika sheria ya Local Authority Finance Act dhidi ya
mikataba na kusababisha halmashauri kukosa haki zake. Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka serikali kueleza hatua zaidi za makusudi
ambazo inachukua kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo na watanzania kwa
ujumla wananufaika na rasilimali za nchi hii kwa maeneo hayo ikiwa ni
pamoja na kushughulikia mkanganyiko huo wa kisheria.
Mheshimiwa Spika, naomba kunukuu tulichokisema mwaka 2011/2012 kuhusiana na ujanja wa makampuni makubwa ya madini “Mheshimiwa
Naibu Spika, Ili kuongeza kiwango cha mapato ikiwemo ya kodi kutokana
na uchimbaji wa madini; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kutekeleza mikakati ya kupenya kuta za umiliki na mitaji (capital and
ownership structures) zilizojengwa kwa muda mrefu na makampuni ya
kimataifa kwa kutumia mianya ya udhaifu wa kisheria na ushawishi wa
kifisadi uliosababisha mikataba mibovu katika sekta ya madini nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kueleza bayana hatua ambazo imechukua kufuatia Ripoti ya Tume/Kamati
mbalimbali ambazo ziliundwa na Serikali kwa nyakati mbalimbali kwa
kutumia fedha nyingi za walipa kodi lakini mapendekezo yake bado
hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake. Mathalani ripoti za karibuni za
Kamati ya Masha na ile ya Bomani (2008) zilieleza bayana namna ambavyo
makampuni makubwa ya madini yamekuwa yakitumia sehemu kubwa ya uwekazaji
wao kama mkopo (debt financing). Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua
kwamba makampuni hayo yamekuwa yakitumia mianya hiyo ya kisheria na
kimikataba kuwezesha wamiliki na wanahisa kupata faida mapema kuliko
kuweka mtaji kwa kuwa riba ya mikopo huondolewa katika kukokotoa kodi.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali iwaeleze Watanzania ni trilioni
ngapi za mapato tumezikosa kati ya mwaka 1995 mpaka 2010 katika kipindi
cha miaka 15 ya kuachia mianya ya upotevu wa mapato kwa kuruhusu
asilimia kubwa ya mikopo kuwa mitaji. Aidha, ni hatua gani zimechukuliwa
kwa waliohusika kuliingiza Taifa katika mikataba mibovu iliyoruhusu
makampuni hayo kujitangazia hasara kila mwaka huku yakipata faida
kubwa”.
Mheshimiwa Spika, matatizo ya wachimbaji wadogowadogo wa madini,
kimekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa taifa hili. Kwa mujibu wa
mapendekezo ya kamati ya Jaji Bomani kuhusu namna ya kuboresha mazingira
ya wachimbaji wadogowadogo wa madini, kamati ilishauri muda wa leseni
kuongezwa kufikia miaka 10 ili kuwawezesha wachimbaji hao waweze kupata
mikopo kutoka taasisi za fedha. Wachimbaji kusaidiwa mbinu kwa ajili ya
kupata mtaji wa kufanya shughuli za uchimbaji, kuchangia katika mfuko wa
wachimabji wadogowadogo, kuwekwa kwa utaratibu wa kisheria kwa ajili ya
kuwakatia bima wafanyakazi wao na kuanzisha taasisi za fedha kwa ajili
ya mikopo kupitia SACCOS zao.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya kamati ya kudumu ya
bunge ya Nishati na Madini kuhusu utekelezaji wa majukumu ya wizara ya
Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012 pamoja na makadirio ya
mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013, kamati ilithibitisha
matatizo ya wachimbaji wadogowadogo kuwa ni pamoja bajeti ndogo
inayotengwa kwa wachimbaji, elimu kutotolewa kwa wachimbaji, uhaba wa
maeneo ya uchimbaji kwa vile maeneo yao yamechukuliwa na wawekezaji
wakubwa, ukosefu wa masoko ya kuuzia bishaa zao na kodi kubwa, Kambi
Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kueleza hatua ilizofanya
katika kutekeleza mpango mkakati wake hususan katika matatizo yafuatayo;
(a) Serikali imeongeza kiasi gani cha fedha kwenye bajeti ya
wachimbaji wadogowadogo, ni utaratibu gani umewekwa ili fedha hizo
ziwafikie walengwa?
(b) Kuna mkakati gani wa kuhakikisha wachimbaji hao wanapata
mafunzo ya uchimbaji na masuala yanayolenga kuongeza thamani ya madini
yao?
(c) Maeneo gani na kanda zipi ambapo wachimbaji hawa
wametengewa maeneo kutokana na maeneo yao kuchukuliwa na wawekezaji
wakubwa?
(d) Serikali imeweka mfumo gani katika kuhakikisha mchango wa uchimbaji mdogo unajulikana kwenye pato la Taifa?
(e) Ili kuongeza thamani ya madini, kuna mkakati gani wa wa
kuhakikisha kazi hii inafanyika hapa nchini na kuongeza siyo tu thamani
bali ajira kwa watanzania?
(f) Hatua gani zimefanywa na serikali kuhakikisha soko na
bei ya madini inakuwa imara na mikakati gani imewekwa ili kuhakikisha
umeme unapatikana katika maeneo ya wachimbaji wadogowadogo?
Mheshimiwa Spika, sasa ni takriban miaka sita toka kuwasilishwa
kwa ripoti ya Mheshimiwa Jaji Mark Bomani kwa Rais. Baada ya
kuwasilishwa pia hapa Bungeni na Kamati husika na Bunge likaijadili na
mapendekezo yake yakawa ni maazimio ya Bunge. Lakini hadi sasa maazimio
ya Bunge bado hayatekelezwa kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, Katika mapendekezo ya tume ya Jaji Bomani
ambayo pia yaliridhiwa na Bunge lako tukufu na kupitishwa kama Azimio la
Bunge ni pamoja na kufutwa misamaha ya kodi, kwa badiliko alilotoa
Waziri wa Fedha la kufuta utekelezaji wa GN 99 kuanzia Julai 2009 kwa
makampuni. Marekebisho haya yanahusu kampuni za madini zilizoingia
mkataba na Serikali kuanzia July 2009. Kwa nini ufutaji wa misamaha hii
usiyaguse makampuni yaliyokuwepo kabla ya kamati ya Jaji Bomani
haijaanza kazi?
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba msamaha ambao unaendelea
kutolewa hadi sasa kwa makampuni hayo ya mafuta unaukosesha mfuko wa
barabara mabilioni ya fedha na huko makampuni hayo ndiyo yanaharibu kwa
kiasi kikubwa barabara zetu. Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe Waziri
alieleze Bunge ni kwanini maazimio ya Bunge hadi leo hii
hayajatekelezwa kikamilifu?
Aidha, Mheshimiwa Spika, mapendekezo mengine ya kamati ya Mheshimiwa Jaji Bomani yalikuwa ni:
1. Serikali kumiliki hisa ndogo kama kwa kampuni ya Williamson
Diamonds Limited ambapo Serikali ina hisa 25%, hali ambayo si sawa kwa
umiliki wa kigeni. Upo umuhimu wa ushiriki wa kutosha wa watanzania
katika umiliki wa hisa za kampuni za uchimbaji mkubwa.
2. Shughuli zote za uchimbaji wa vito, na Kampuni za uchimbaji wa
kati wa madini mengine, zimilikiwe ama kwa 100% au kwa kiasi
kisichopungua 50% na wananchi wa Tanzania.
3. Shughuli zote za wachimbaji wadogo zimilikiwe na kuendeshwa na watanzania tu.
Mheshimiwa Spika, ni matarajio ya Kambi Rasmi ya Upinzani,
Serikali itawaeleza watanzania utekelezwaji wa maazimio hayo ya Kamati
ya Mhe.Jaji Bomani ambayo yaliridhiwa na Bunge yametekelezwa kwa
kiwango.
Mheshimiwa Spika, Utaratibu unaotumika katika kuingia mikataba ya
uchimbaji wa madini umewekwa wazi katika Sheria ya Madini ya mwaka
2010. Sehemu ya 23 ya Sheria hiyo inaelezea kuhusu kuanzishwa kwa bodi
itakayojulikana kama Bodi ya Ushauri ya Sekta ya Madini. Bodi hii
inamshauri Waziri anayesimamia madini kuhusu masuala ambayo yako chini
ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ambayo yanatakiwa kufikishwa kwenye
Bodi.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati na Madini imeonyesha udhaifu
wa kumnyima hata Mkuguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhakikia
mikataba ambayo Serikali imefunga na wachimbaji ili
“kubainisha
taratibu ambazo zinafuatwa na Wizara katika kutekeleza matakwa ya sheria
hii kwa vile mikataba hii ya Uchimbaji ni ya watu binafsi na ni siri
kwa watu wengine wasiokuwa sehemu ya mikataba hiyo. Kutokana na usiri
huo, sikupewa haki ya kuipitia mikataba hiyo na hivyo kuzuia wigo wa
ukaguzi wangu”[4].
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaliomba Bunge katika
mjadala huu utakaoendelea kupitisha azimio mahususi kuilazimisha Wizara
kuwajibika kwa kuendelea na utekelezaji wa mikataba yote ambayo, kwa
njia moja au nyingine imekiuka sheria na pia imekiuka maazimio na
ushauri unaotolewa na Bunge. Kwa njia hii tutakuwa tumetimiza wajibu
wetu wa Kikatiba wa Kuisimamia na kuishauri Serikali.
Mheshimiwa spika, mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa
bado ni mdogo mno ukilinganisha na jinsi nchi yetu ilivyojaliwa
rasilimali hii na uchimbaji unaoendelea sehemu mbalimbali katika nchi
yetu. Kwa ujumla madini tuliyojaliwa hayawafaidishi watanzania kwa
kiwango kilichotegemewa zaidi ya kuwaingiza kwenye matatizo ya uchafuzi
wa kimazingira ugumu wa maisha.
6.1 STAMICO
Mheshimiwa Spika, Shirika la Madini (STAMICO) linaimarishwa upya
na serikali baada ya kuondolewa kutoka kwenye orodha ya mashirika ya
umma yanayotakiwa kufutwa mwezi Machi, 2009. Hivyo lilipewa majukumu
makuu manne, ambayo ni:
a. Kuwekeza katika utafutaji,uendelezaji na uchimbaji wa madini
b. Kusimamia hisa za serikali katika migodi
c. Kuratibu uendelezaji wa wachimbaji wadogo nchini, na
d. Kutoa huduma za kibiashara katika sekta ya madini, huduma hizo ni
uchorongaji wa miamba, utafutaji wa madini na utoaji ushauri katika
masuala ya madini.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya shirika liyowasilishwa kwenye kamati
ya madini na nishati, inaeleza kuwa Bodi ilimaliza muda wake mwezi
Juni, 2012. Hivyo basi shirika hilo halina bodi hai. Kwa mujibu wa
taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti ameongelea kitendo cha Mwenyekiti wa Bodi
kuingilia moja kwa moja utendaji wa shirika hilo kiasi kwamba, shirika
limekuwa likimlipa posho ya mafuta Mwenyekiti huyo sawa na lita 100 za
mafuta kila wiki, asilimia 40 ya posho ya mafuta kama fedha za
matengenezo kila wiki na shilingi 500,000/= kwa mwezi kama fedha za
mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, msuguano huu wa kiutendaji kati ya mkurugenzi
mtendaji na Mwenyekiti wa bodi kwa kiasi kikubwa inadumaza utendaji wa
shirika. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kuwachukuliwa hatua za kinidhamu Wenyeviti wenye tabia kama hii kwani
malipo hayo ni aina nyingine ya matumizi mabaya ya raslimali za umma
ambayo yanapaswa kudhibitiwa.
Mheshimiwa Spika, STAMICO ndiyo yenye dhamana ya uendelezaji wa
Mgodi wa Buhemba, kwani tangu mwezi Julai, 2011 shirika lilipewa leseni
ya utafutaji wa madini juu ya eneo la mgodi wa zamani wa dhahabu wa
Buhemba, mkoani Mara kwa kumiliki asilimia 40 za mgodi huo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ukweli kwamba mgodi huu wa Buhemba
ndio uliokuwa ukimilikiwa na kampuni ya MEREMETA kampuni ambayo mbali ya
kuiingiza nchi kwenye kashfa bali pia iliwaacha wananchi/ wachimbaji
wadogo wa eneo la Buhemba wakiwa na malalamiko ya kutokulipwa fidia kwa
kutwaliwa maeneo yao. Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuelewa je
STAMICO inamkakati gani wa kwanza kuchukua mali zilizokuwa zinamilikiwa
na MEREMETA? Na pili madai ya wananchi wanayalipa vipi kwa pamoja na
mbia wake?
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ushauri ulipotolewa na Mkaguzi
kuhusu ushiriki wa Sekta ya Umma na Sekta binafsi kugubikwa na mapungufu
makubwa ambapo faida inakuwa kwenye upande wa pili zaidi na Serikali.
Mfano ni ubia wa SONGAS Ltd, IPTL ltd, Kiwira Coal Mines (TANPOWER LTD),
TICTS na kadhalika. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
iwahakikishie watanzania ni kwa kiwango gani ubia huo wa STAMICO na MANJARO RESOURCES Pty Ltd kutoka Australia utakuwa na tija kwa taifa?
6.2 WAKALA WA UKAGUZI WA MADINI-TMAA
Mheshimiwa Spika, wizara ya nishati na madini 08 desemba, 2011 ilitoa taarifa kwa umma kuhusu maendeleo ya sekta ya madini.
Mrabaha uliolipwa na migodi mikubwa ya dhahabu katika kipindi hicho cha
kuanzia mwaka 1998 hadi 2010 ilikuwa ni Shilingi Bilioni 341.57, wakati
hadi kufikia mwaka 2010 kulikuwa na Watanzania 6,129 walioajiriwa rasmi
kwenye migodi mikubwa 6 ya dhahabu. PAYE wanayolipwa ya kati ya asilimia
14 mpaka 30 kutegemea kiwango cha malipo.
Mheshimiwa Spika, ili kufanya ulinganisho ulio sahihi wa kama
kweli mchango wa sekta ya madini kwenye kodi unatokana na mrahaba au
kodi ya PAYE wanayolipa waajiriwa hao 6,129 ilitakiwa tuambiwe ni kiasi
gani, kwani kuna uwezekano mkubwa PAYE inazidi kwa mbali fedha
inayoingia itokanayo na mrahaba.
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA)
ndiye mwenye dhamana katika kudhibiti uzalishaji wa madini na ukusanyaji
maduhuli yatokanayo na mrahaba kwa kampuni za uchimbaji madini. Hata
hivyo, TMAA haina udhibiti wowote katika uzalishaji na uthamanishaji wa
madini kwa wachimbaji wadogo na wa kati ambao wameachwa kueleza wenyewe
kiasi cha madini wanachozalisha.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ukweli huo, ni kwa vipi Wizara
inataka kuliaminisha Bunge kuwa takwimu za madini hasa dhahabu
zilizozalishwa hapa nchini kuwa ni sahihi?
Mheshimiwa Spika, mapungufu haya kwa kiasi kikubwa yanatokana na
ukweli kwamba “control mechanism” kwa wachimbaji wadogo wakati wa kutoa
leseni umegubikwa na matumizi mabaya na udanganyifu ambapo watu wachache
wamehodhi maeneo mengi na kuajiri wachimbaji wadogo na kinachopatikana
kutokana na machimbo hayo Serikali inanyimwa taarifa. Pia kushindikana
kwa udhibiti ni viwanja vidogo vya ndege vilivyotapakaa hapa nchini
ambavyo TMAA haina udhibiti navyo.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa hiyo ni kwamba Serikali imechukua hatua zingine za kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini ni pamoja na:
1. Kutenga maeneo maalum ya wachimbaji wadogo;
2. TANSORT kuhamishia rasmi shughuli zake hapa nchini kutoka Uingereza mwezi Agosti, 2010;
3. Upigaji marufuku wa usafirishaji nje ya nchi madini ghafi ya
Tanzanite yenye ukubwa unaoanzia gramu moja na kuendelea mwezi Aprili,
2010;
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
ilieleze Bunge tangu kitengo hicho cha kuchambua almasi kirudishwe hapa
nchini toka Uingereza ni kiasi gani cha fedha kimepatikana kutokana na
kazi zake hizo?
Mheshimiwa Spika, yamekuwepo madai ya wachimbaji wadogo wadogo
ambao ndiyo wazawa kunyimwa leseni katika maeneo yao ya uchimbaji na
maenea yao kugawiwa kwa wanaojiita wawekezaji na wao wakihamishwa
hamishwa pasipo kupatiwa maeneo mbadala.
Mheshimiwa Spika, Kuna matatizo mengi ya wachimbaji wadogo wadogo
katika maeneo ya Kalalani Tanga, Mgusu, Nyarugusu, Mtakuja Geita, Winza
Mtakanini Mpwapwa, Simangulu Chamwino, North Mara, Rwamgasa,
Kasema,Kilindi Nyamongo na kadhalika. Hivi karibu ni wachimbaji wapatao
400 wa kijiji cha Nkongilangi wanaochimba eneo la Machimbo ya
Sekenke-Iramba Magharibi, ambao toka mwaka 1982 wamekuwa wakiomba leseni
lakini hawapatiwi majibu ya maombi yao. Mwaka 2007 waliomba tena na
kuambiwa leseni imetolewa kwa kampuni ya WASEKE, kwa mshangao mkubwa
mwaka 2011 alikuja mtu anayedai kuwa ndiye mmiliki wa eneo hilo la
uchimbaji mdogo la kijiji cha Nkongilangi aitwaye “JOHN BINA”. Na hapo
ndipo matatizo na unyanyasaji ulipoanzia na kusababisha uporaji na vifo
kutokea
[5].
Mheshimiwa Spika, katika mazingira kama hayo, wachimbaji wadogo
wapatao 3000 kwa ushirika wao wilayani Maswa baada ya kulipia ada ya
maombi yao imechukua takriban miezi minne baadae wakajibiwa kuwa eneo
hilo tayari lilikuwa na mmiliki toka mwaka 2002. Lakini baada ya
kuangalia coordinates zilizosemwa kwenye barua na zile zilizoko kwenye
ramani, ni kwamba leseni PL 4233/2007 ambayo mmiliki wake ni SAVANNAH
EXPL. Ltd iliyotolewa tarehe 02/05.2007 na eneo lake liko Luguru na
Luguru ni kijiji kilicho ndani ya wilaya ya Bariadi na sio Maswa. Huu ni
mkakati unaotumiwa na watendaji Idara ya Madini kwa kushirikiana na
wenye dhamana katika Serikali kuwanyima haki wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kuwaeleza wachimbaji fedha zilizotengwa kiasi cha shilingi bilioni moja
kama kianzio cha Mfuko wa kuendeleza Wachimbaji wadogo nchini, kama
hotuba ya Waziri Mkuu Mhe. Mazengo Pinda alivyosema Bungeni wakati
akiwasilisha mapitio na makadirio ya matumizi ya fedha yake na Ofisi ya
Bunge kwa mwaka 2010/2011 zilipewa wachimbaji wadogo wa wapi?
Mheshimiwa Spika, aidha, kwa mujibu wa maneno ya Mhe Naibu Waziri
Madini wakati akijibu swali tarehe 22 April 2013 alisema “SERIKALI
inatarajia kukamilisha taratibu za Mfuko rasmi wa kuwaendeleza
wachimbaji wadogo wa madini, ili kuwawezesha kupata mikopo, ikiwa ni
pamoja na kuwapatia mikopo ya vifaa vya kuchimbia kwa kanda zote nane
zinazochimba madini nchini”.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza mfuko huo
ambao umekwisha tengewa fedha na hapa Naibu Waziri anasema inatarajia
kukamilisha taratibu rasmi za mfuko huo, hii maana yake nini? Na mfuko
huo utaendeleza wachimbaji gani wakati ambapo maeneo mengi wana
malalamiko ya leseni na wanafukuzwa ovyo kama mifano ambayo tumeitoa
hapo juu.
Mheshimiwa Spika, Kwa wale walio na maeneo ya kuchimba madini
wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kuwa na
mtaji mdogo unaowafanya washindwe kupata zana bora kwa ajili ya
uchimbaji. Aidha, watoto wa walalahoi wamekuwa wakiajiriwa katika migodi
mbalimbali nchini mbali ya kuwa na sheria inayopinga ajira kwa watoto
hususan katika maeneo ya migodini.
Mheshimiwa spika, Kitendo cha serikali kupandisha kodi mara kawa
mara kwa wachimbaji au wawekezaji wadogo wadogo ni kufanya wawekezaji
wadogo wasimudu kushiriki kikamilifu katika kuwekeza ndani ya sekta ya
Madini wakati serikali inajigamba kuwasaidia wawekezaji hao huku
serikali ikipandisha kodi kutoka 80,000/= hadi 1,000,000/= kwa
wachimbaji hao.
Mheshimiwa spika, Jambo hili ambalo pia lililalamikiwa na wabunge
wengi limeonekana limetafsiriwa kuwa ni mkakati wa makusudi wa
kuwafukuza wawekezaji wadogo wadogo katika sekta hii na kutoa mianya kwa
wawekezaji wenye pesa zao kuendelea kuwekeza katika sekta hii ya
madini. Kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka serikali kieleze kwa
kina ni kwa jinsi kani itawasaidia wachimbaji wadogo kama gharama za
uendeshaji wa migodi hiyo zinapanda bila kuzingatia hali halisi ya
wachimbaji hao. Hii ni hatari sana kwani tunafanya wazawa washindwe
kunufaika na sekta hii moja kwa moja.
Mheshmiwa spika, Katika kuboresha sekta hii ya madini kamati ilishauri mambo yafuatayo yafanyike:
Ø Serikali kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kushiriki katika shughuli za kutoa huduma(supply)mbalimbali migodini
Ø Sheria ya ajira kwa watoto isimamiwe ipasavyo
Ø Migodi mikongwe ilipe kodi(corporate tax)
Ø Kuwepo kwa soko la pamoja la madini
Ø Kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika kila kanda na kusimamia vizuri zoezi la ugawaji wa leseni
Ø Serikali iwasaidie wachimbaji wadogo iliwaweze kapata mikopo ya
kuwawezesha kuanzisha viwanda vidogo vitakavyowasaidia kuongeza thamani
ya madini yao
Ø Serikali kukomesha biashara haramu ya madini
Hata hivyo serikali haijayafanyia kazi kwa ukamilifu mapendekezo hayo ya
kamati katika mwaka wa fedha 2012/2013 na bado sekta hii inakumbwa na
hali ileile na kuifanya iendelee kutokuwa na mchango mkubwa katika
uchumi wa nchi.
Mheshimiwa spika, Taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa fedha za
serikali ulioishia 30 Juni, 2012 inaonesha kuwa Wizara ya Nishati na
Madini imeliingizia taifa hasara ya zaidi ya shilingi 20,000,000,000
katika sekta ya madini. Hasara hiyo kama ilivyooneshwa kwenye taarifa ya
CAG ilisababishwa na malimbikizo ya maduhuli ambayo hayakuonyeshwa
Sh.1,645,582,899.Taarifa za fedha zilizowasilishwa na Wizara
hazikuonyesha malimbikizo ya maduhuli yenye jumla ya Sh. 1,645,582,899/-
kama ilivyotakiwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
Mheshimiwa spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inashangaa ni
kwa sababu gani hasa bado sheria ya zamani inaendelea kutumika wakati
tayari sheria ya mwaka 2010 imeshaanza kufanya kazi. Aidha Kambi Rasmi
ya Upinzani bungeni inaitaka Wizara ieleze kwanini hali hiyo imejitokeza
na hatua gani inachukua dhidi ya watendaji waliohusika katika kulipatia
hasara hiyo?
Kambi Rasmi ya Upinzani pia inaitaka serikali kutumia sheria mpya
ya kukusanya mrahaba katika kampuni za madini na hivyo makampuni yote
yaliyolipa mrahaba huo kwa kutumia sheria ya zamani yalipe sehemu
iliyobakia kwa mujibu wa sheria mpya.
Pamoja na hayo tunaitaka serikali ilitaarifu bunge lako tukufu kuhusu
malimbikizo ya maduhuli ambayo hayakuoneshwa kwenye taarifa za mahesabu
ya wizara hii, tunataka tujue serikali inampango gani na fedha hizi
ambazo ni zaidi ya 1,000,000,000/=.
Mheshimiwa spika, mambo mengine yanayo sababisha hasara katika
sekta ya madini ni pamoja na kutokuwa na udhibiti wa mapato ya
wachimbaji wadogo wa madini na kutokuwa na udhibiti katika viwanja vya
ndege. Udhibiti mdogo katika sekta hii ya madini kumesababisha kupotea
kwa mapato mengi ambayo nchi ingeyapata kutokana na madini
yanayosafirisha bila kulipa kodi na biashara haramu ya madini
inayoendelea nchini.
Mheshimiwa Spika, Pia kwa mujibu wa taarifa ya CAG hukuna
ushirikianao kati ya wizara na TRA na hivyo kodi nyingi zinashindwa
kukusanywa kutokana na TRA kukosa taarifa sahihi juu ya vyanzo vya
mapato vya wizara hiyo.
Mheshimiwa spika, utekelezaji wa ahadi nyingine za Waziri wa
Nishati na Madini katika bajeti ya 2012/2013; Waziri wa Nishati na
Madini katika majumuisho yake aliahidi Bunge kuwa kuna madini ya
VANADIUN na PGE yanayopatikana katika madini ya Copper na Nickel. Hilo
atalifanyia kazi suala la wawekezaji wanaochukua leseni ya Copper na
Nickel kwani kuna upatikanaji wa madini ya VANADIUM na PGE ambayo
inasemekana kuwa yanathamani kubwa kuliko Copper na Nickel. Hivyo Kambi
Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kueleza juu ya utekelezaji
wa suala hili kama waziri alivyoahidi bungeni wakati wa kuhitimisha
hotuba ya bajeti ya wizara yake ya mwaka wa fedha 2012/2013
Mheshimiwa spika, katika suala la mkopo wa billion 8.9 kwa
wachimbaji wadogo kwamba ni kwa vipi wachimbaji wadogo wangepewa mikopo
hiyo wakati kwa wakati huo leseni nyingi na maeneo yote wamepewa
wawekezaji wakubwa, Mh. Waziri aliliambia bunge kuwa lesini hizo
zinaisha muda wake, na zikiisha muda wake wawekezaji wakubwa wanaacha
nusu ya eneo walilokuwa wanamiliki na hivyo maeneo haya wanapewa
wachimbaji wadogo wadogo.
Mheshimiwa spika, katika suala hilohilo la wachimbaji wadogo
wadogo ilijitokeza pia hoja kutoka kwa wabunge, waliomuuliza Waziri wa
Nishati na Madini jinsi gani mkopo wa billion 8.9 uliopangwa
kuwanufaisha wachimbaji wadogo wadogo nchini utagawiwa kwa wachimbaji
husika. Waziri alijibu wanatakiwa waunde vyama vyao kila mkoa na wawe na
chama chao kitaifa ambako ndiko mkopo huu utaelekezwa.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali itupe takwimu
sahihi mpaka sasa tathmini ikoje juu ya leseni za wawekezaji wakubwa
kuisha muda wake na wawekezaji wadogo kupewa maeneo husika na je mkopo
wa billion 8.9 umewanufaisha wachimbaji wadogo wadogo wangapi mpaka
sasa? Na Kama wachimbaji wadogo hawajanufaika na mkopo huu serikali
itueleze fedha hizi zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwa
ajili ya kazi hii zimefanyiwa nini?
Mheshimiwa spika, kuhusu madeni ambayo wawekezaji katika sekta ya
madini wanadaiwa na serikali, Naibu Waziri Wa Nishati na Madini wakati
wa mjadala wa bageti ya mwaka 2012/2013 alipokuwa anajibu hoja ya madeni
ambayo wawekezaji katika sekta ya madini walikuwa wanadaiwa tangu mwaka
1997 hadi mwaka 2005 aliliahidi bunge kwamba kampuni ya BARRICK ambayo
ndiyo kampuni pekee iliyokuwa inakataa kulipa deni lake atalifanyia kazi
swala hilo na kuhakikisha wanalipa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka
serikali ieleze kama madeni yote yamelipwa kwa kuzingatia sheria mpya ya
madini ambayo pamoja na mambo mengine inataka mirahaba kulipwa kwa
asilimia nne [4%] kabla ya makato ya makato ya Kodi. Na kama kuna
makampuni hayataki kutii sheria hii mpya ya madini kwa nini serikali
isiyafutie leseni ya kufanya kazi za uchimbaji wa madini nchini ? Kwa
sababu nchi haiwezi ikavumilia wawekezaji ambao hawatii sheria za nchi.
Mheshimiwa spika, Pia Naibu Waziri alikiri mbele ya bunge lako
tukufu kuwa mgodi wa BUZWAGI haujalipa kodi ya kampuni yaani (Corporate
tax), na kuahidi kuwa mgodi wowote mpya utaoanza kuanzia wakati huo
serikali itaanza kuwa na share ya 15% kama hisa za kubeba (free carried
interest).
Tunaitaka serikali ilieleze bunge lako tukufu na umma wa watanzania kwa
ujumla wake kama mgodi huo umelipa kodi hiyo na serikali imejipangaje
kumiliki hisa kwenye migodi inayotegemewa kuanzishwa na hii ambayo
imeanzishwa kwa ajili ya kuwa na udhibiti wakati kwa kuzingatia
masharti ya sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inatoa haki hiyo ya
Serikali kuwa na hisa.
6.3 UCHIMBAJI MADINI AINA YA URANI
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa swala la uchimbaji na utafutaji wa
madini ya aina yeyote lipo chini ya wizara ya nishati na madini , na kwa
kuwa swala la uchimbaji wa madini ya aina ya urani kama taifa
tunahitaji kuwa na angalizo kubwa ikiwa ni pamoja na kutochimba madini
hayo ya aina ya urani kutokana na uhatari wake kwa maisha ya binadamu,
na kwa kuwa kambi rasmi ya upinzani kwa mara kadhaa ndani ya bunge hili
imekuwa ikitoa maoni yenye nia njema na maisha ya watanzania na viumbe
vingine na kwa kuwa tatizo la serikali kutokubali kufanya maamuzi ya
kubadili mtazamo wa kutegemea uchumi wa urani na kujikita katika uchumi
wa rasilimali mbadala ambazo taifa letu limebarikiwa kuwa nazo.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la mbarang’andu katika wilaya ya
Namtumbo ambapo kampuni ya Game Frontiers iliyojipatia kitalu hicho kwa
ajili ya uwindaji kwa mujibu wa sheria imeamua kufanya biashara ya
kuruhusu utafiti wa uchimbaji madini aina ya urani kinyume na taratibu
za uendesahji wa vitalu vya uwindaji.
Mheshimiwa Spika, katika bunge hili mnamo Tar 28/07/2012
zilitolewa taarifa hapa ndani ya bunge hili kwa vielelezo kutoka kwa
msemaji wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kuhusu maswala ya ardhi Mhe.
Halima Mdee juu ya kampuni ya Game Frontiers kukodisha kitalu chake cha
uwindaji kwa ajili ya utafutaji wa madini ya urani katika eneo la
mbarang’andu katika wilaya ya Namtumbo.
Mheshimiwa Spika, lakini pia msemaji wa kambi rasmi ya upinzani
alitaka kupata ufafanuzi kwa Waziri juu ya maagizo yaliyotolewa na Naibu
Spika wakati wa majumuisho ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, maagizo husika yalitaka Wizara ya Nishati na Madini, wakati wa
kupitisha makadirio ya mapato na matumizi itoe maelezo juu ya mkataba
ulioingiwa tarehe 23 Machi, 2007 kati ya Uranium Resources PLC na
Western Metals Limited na Game Frontiers of Tanzania Limited. Mkataba
ambao, pamoja na mambo mengine una ihalalishia Game Frontiers Limited
kupata malipo toka kwa makampuni yanayofanya utafiti katika kitalu cha
uwindaji katika kijiji cha Mbarang‘andu.
Mheshimiwa Spika, majibu ya waziri yalikua kama ifuatavyo nanukuu …..“Mheshimiwa
Spika, lingine lililoulizwa na Kambi ya Upinzani hasa Mheshimiwa Mdee,
huu mkataba wa siri, kweli tumeufuatilia mkataba wa siri, ule wa
uchimbaji wa uranium”…. Kuonesha waziri alikiri mbele ya bunge na kuahidi kulitafutia ufumbuzi swala hilo, na kuwa ataleta taarifa kwa mtoa hoja.
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine tena kambi rasmi ya upinzani
bungeni inataka kujua ni vipi wizara ya nishati na madini imeshughulikia
swala la kampuni ya uwindaji ya Game Frontiers kukodisha kitalu chake
cha uwindaji kwa ajili ya utafutaji wa madini ya urani katika eneo la
Mbarang’andu wialayani Namtumbo, lakini pia serikali iwaambie watanzania
kwa hatua ilizochukua za kuchimba urani ni vipi itaweza kuwalinda dhidi
ya madhara ya uchimbaji wa madini hayo?
6.4 MGODI WA KIWIRA
Mheshimiwa Spika, kati ya kashfa ambazo ziliikumba serikali ya
awamu ya tatu ya Rais Mkapa ilikuwa ni pamoja na kubinafsishwa kwa mgodi
huu wa Kiwira
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu za bunge lako tukufu,
bunge lilipitisha maazimio yake juu ya taarifa ya kamati ya Nishati na
Madini kuhusu ubinafisishaji wa mgodi wa kiwira kufuatia mapendekezo
yaliyokuwa yameelekezwa serikalini kwa ajili ya hatua stahiki, miongoni
mwa maazimio ya bunge ambayo hayakufanyiwa kazi na serikali yalikuwa ni
pamoja na;
i. Urejeshwaji wa vifaa na mali ambavyo vimeibiwa au kuhamishwa kutoka kwenye miundombinu ya mgodi wa kiwira
ii. Bilioni 17 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ukarabati wa
miundomninu ya mgodi, serikali ilitakiwa kufanya ukaguzi wa matumizi ya
fedha hizo kupitia kwa Mthibiti na Mkaguzi wa Hesabu za serikali ili
kujua matumizi halisi na halali ya fedha za umma
iii. Serikali kufuatilia uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU wa shilingi
milioni 50 zilizotolewa kutoka mfuko wa Consolidated Holdings
Corporation
iv. Kuwalipa wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira mafao yao na stahiki zao kwa wafanyakazi ambao CAG alithibitisha kuwa hawakulipwa
v. Serikali kukamilisha haraka zoezi la kukabidhiana mgodi huo
vi. Serikali kueleza kigezo kilichotumika kuwalipa viongozi waandamizi
kiasi cha shilingi milioni 80 wakati wafanya kazi wa kati walilipwa
kati ya shiligi milioni 8 na wafanya kazi wa chini wakilipwa shilingi
milioni moja na nusu.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo halijafanyiwa kazi lilikuwa ni
hili la malipo yaliyolipwa mara mbili, kwa mjibu wa hansard za bunge ,
maoni ya wabunge yalikuwa ni … “niligusie hili la dola milioni nne na
laki nane na sitini na tano ambazo ni sawa na bilioni tano na laki sita,
serikali imekiri…imefanya double payment jambo ambalo ni kosa la jinai,
… mwenzangu anadai tuachane nayo, haiwezekani” lakini katika hali ya
kustaajabisha hadi hivi leo haijulikanai hatima ya fedha hizo
zilizolipwa mara mbili. Ni maoni ya kambi rasmi ya upinzani kuwa
serikali ihakikishe maoni yote yanafanyiwa kazi , fedha za walipa kodi
haziwezi kupotea hivihivi kwa wajanja wachache.
Kambi rasmi ya Upinzani, inataka maelezo ya kina kuhusiana na mambo yafuatayo;
i. Fedha za mwaka jana zilitengwa Bilioni 40 na zilitumika
Bilioni 28 kulipa fidia, je fedha hizo alilipwa nani na zilikuwa ni kwa
ajili gani?
ii. Mwaka huu tumetenga tena bilioni 20 je, ni kwa ajili ya
kuendelea kufidia ufisadi huu ? au ni kwa ajili ya kazi gani?
7.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Maoni yetu juu ya mapitio ya utekelezaji wa
Bajeti kwa mwaka 2012/2013 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka
wa fedha 2013/2014 yanaonyesha kwamba chanzo cha hali tuliyonayo hivi
sasa ni cha muda mrefu. Bunge la tisa likiongozwa na Spika Samuel Sitta
halikuweza kukamilisha kurekebisha hali hiyo, ikiwemo kukwepa
kukamilisha kwa wakati maazimio ya Bunge ya mwaka 2010. Bunge la kumi,
likiongozwa na Spika Anna Makinda katika kipindi chake cha kwanza cha
miaka miwili na nusu, halijaweza kukamilisha utekelezaji wa maazimio ya
mwaka 2008 na maazimio yake ya mwaka 2011 na 2012. Bunge hili, bado
linalo nafasi ya kurekebisha hali hii kuanzia sasa katika kipindi chake
cha miaka miwili na nusu iliyobaki.
Mheshimiwa Spika, mwalimu nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE ukurasa wa pili (2) aya ya 4 kinasema nanukuu
“Makosa yetu mengine hutokana na woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa
japo tunajua kuwa kakosa,au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo
tunajua kuwa hana makosa. Na msingi wa woga pia ni unafsi. Pengine
twaweza kuwa hatuna cheo cochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine
huwa hatuna wala tama yoyote ya kupata cheo Fulani. Lakini woga unaweza
kutokana na tamaa ya kila bindamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi
wote tunayo tama hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza
ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio
wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa
kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha,
wasije wakatuchukia. Huu ni unafsi mbaya sana. Ni kweli kwamba
demokrasia haiwezi kudumu ikiwa wachache hawatakubali matakwa ya wengi,
lakini matakwa ya wengi hujulikana katika majadiliano au mazungumzo ya
wazi wazi.
Mheshimiwa Spika, lakini pia katika ukurasa wa tatu (3) aya ya pili anasema nanukuu “Kadhalika,
matakwa ya wachache hujulikana katika majadiliano na na mazungumzo.
Bila wale wachache kusema wazi wazi matakwa yao, majadiliano hayana
maana. Wakati mwingine, hata baada ya majadiliano, wachache japo
wamekubali kutii uamuzi wa wengi wanaweza kuendelea kuamini kwamba
mawazo yao ni sawa, na ya walio wengi yamepotoka. Demokrasia inawapa
haki, na ukweli unawapa wajibu wa kuendeleza mawazo yao mpaka wengi
waone kuwa ni ya kweli.Bila hivyo maendeleo katika mawazo hayawezekani,
kwani mara nyingi wazo zuri hutokana na mtu mmoja tu. Mwanzo laweza
likapigwa, pengine kwa nguvu kabisa,na walio wengi, lakini hatimaye
wengi hulikubali. Huu ndio msingi wa maendeleo katika mawazo ya
binadamu”.
Mheshimiwa Spika, Katika sekta za Nishati na Madini, kama ilivyo
katika sekta nyingi nchini; tumefika hapa tulipo kwa sababu ya udhaifu
wa Serikali inayoongozwa na Rais Kikwete, uzembe wa Bunge na ulegelege
wa CCM. Kambi Rasmi ya upinzani inayoongozwa na CHADEMA inataka kama
taifa; TUBADILIKE, TUWAJIBIKE, TUJISAHIHISHE.
Mheshimiwa Spika, Naomba kuwasilisha.
John John Mnyika(Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-
Wizara ya Nishati na Madini
22.05.2013