WAPENDWA KARIBUNI KATIKA BLOGU YENU MPYA YA TANZANIASASA KWA HABARI MOTOMOTO NA MATUKIO YA KILA SIKU...KWA MAWASILIANO YA MATANGAZO, HABARI KATIKA PICHA, MAONI NA USHAURI, WASILIANA NASI KUPITIA tanzaniasasa@gmail.com au simu:+255 787453855 au +255754000741, karibuni sana!!!
Wednesday, May 1, 2013
HOTUBA YA WAZIRI KAGASHEKI AKIWASILISHA MAKADIRIO YA BAJETI YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII 2013/14
HOTUBA YA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII
MHESHIMIWA BALOZI KHAMIS SUEDI KAGASHEKI (MB),
AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2013/2014
I. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wake Mhe. James Daudi Lembeli (Mb.), Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kujadili Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake kwa mwaka 2013/14.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuniwezesha kuiongoza Wizara hii yenye dhamana ya kusimamia Rasilimali za Maliasili na Malikale na kuendeleza Utalii. Nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu, nikishirikiana na viongozi wenzangu ndani ya Wizara na wadau wote wa sekta hii kuhakikisha kuwa ulinzi na matumizi endelevu ya rasilimali hizo ni kwa manufaa ya Watanzania na dunia nzima.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kuishukuru kwa dhati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa kuchambua na kujadili Taarifa ya Utekelezaji kwa mwaka 2012/13 na Mpango wa Bajeti wa Wizara yangu kwa mwaka 2013/14. Nalihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa ushauri wa Kamati umezingatiwa.
4. Mheshimiwa Spika, napenda kuungana na wenzangu kutoa pole kwako Mheshimiwa Spika na kwa waheshimiwa Wabunge kutokana na kuondokewa na aliyekuwa mbunge mwenzetu Mhe. Salim Hemed Khamis Mbunge wa Chambani - CUF. Vilevile, natoa pole kwa familia za marehemu na watanzania wote kwa ujumla kutokana na majanga mbalimbali yaliyotokea nchini. Namwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi.
5. Mheshimiwa Spika, Hotuba yangu imegawanyika katika sehemu kuu tano. Sehemu ya kwanza ni Utangulizi; Sehemu ya pili inazungumzia Utekelezaji wa Mpango wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2010 - 2015; Sehemu ya tatu ni Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi wa mwaka 2012/2013 ambao umezingatia utekelezaji wa ahadi pamoja na maelekezo yaliyotolewa Bungeni na maagizo mbalimbali ya Viongozi Wakuu wa Serikali. Sehemu hii inazungumzia pia changamoto ambazo Wizara ilikabiliana nazo katika utekelezaji. Sehemu ya nne ni Mpango wa Utekelezaji na Malengo ya Wizara kwa mwaka 2013/2014, na sehemu ya tano ni hitimisho ambapo bajeti inayoombwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa mwaka 2013/2014 inawasilishwa.
II. UTEKELEZAJI WA MPANGO WA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA MWAKA 2010-2015
6. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza Mpango wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 - 2015. Utekelezaji umezingatia maeneo yaliyoainishwa katika Ilani hiyo kama ifuatavyo:
(i) Kuwezesha jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi kunufaika na rasilimali za wanyamapori na misitu
7. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, jumuiya moja ya hifadhi ya wanyamapori ya Randilen katika wilaya ya Monduli imeidhinishwa na hivyo kufanya idadi ya Jumuiya zenye hati ya matumizi kufikia 18. Katika mwaka 2012/2013, jumuiya kumi zitapata mgawo wa jumla ya Sh.164,908,467.75, ikiwa ni sehemu ya mapato yaliyotokana na uwindaji wa kitalii katika sehemu husika. Aidha, Halmashauri za wilaya 32 zenye vitalu vya uwindaji wa kitalii zitanufaika na mgawo wa jumla ya Sh.1,162,199,512.52.
8. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhamasisha jamii kushiriki katika uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za misitu. Kupitia Mpango wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu (PFM), maeneo ya misitu yenye jumla ya ukubwa wa takribani ekari milioni 7.7 katika vijiji 2,285 kwenye wilaya 77 za mikoa 21 ya Tanzania Bara yamehifadhiwa.
9. Mheshimiwa Spika, utaratibu huo umewezesha kurejesha uoto wa asili katika maeneo ambayo awali yalikuwa yameharibika. Aidha, baadhi ya misitu imeanza kuvunwa na vijiji kuongeza mapato yao na hivyo kuweza kugharimia miradi ya maendeleo. Miongoni mwa miradi iliyotekelezwa katika Halmashauri za wilaya za Chunya na Kiteto, ni ujenzi wa vyumba vya madarasa, ofisi nne za vijiji, nyumba sita za watumishi, zahanati moja, visima viwili vya maji na ukarabati wa madarasa matatu, nyumba tano za walimu na zahanati moja.
10. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia Hifadhi za Taifa 16, Hifadhi ya Ngorongoro, Mapori ya Akiba 28, Mapori Tengefu 44 na Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMAs) 38 zimesajiliwa, kati ya hizo 18 zimeidhinishwa kutumia rasilimali za wanyamapori.
(ii) Kuweka utaratibu shirikishi wa upandaji miti, uvunaji na udhibiti wa moto katika misitu
11. Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kushirikisha wananchi kulinda na kudhibiti moto katika misitu umeendelezwa kwa kutoa elimu ya uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za Misitu na Nyuki. Mikutano 360 ya uhamasishaji ilifanyika kwa jamii zinazozunguka misitu ya hifadhi katika Kanda saba za Wakala wa Misitu. Aidha, wilaya na mikoa imeendelea kuadhimisha siku ya upandaji miti kufuatana na hali ya mvua. Kitaifa siku hii huadhimishwa tarehe 1 Aprili kila mwaka. Mwaka 2012, miti 145,156,884 ilipandwa katika mikoa 17 ya Tanzania bara. Kati ya miche ya miti iliyopandwa, asilimia 74.5 imestawi.
(iii) Kuboresha Miundombinu ndani ya Mapori ya Akiba, Hifadhi za Wanyamapori na Misitu
12. Mheshimiwa Spika, kazi ya kuimarisha miundombinu imefanyika katika maeneo mbalimbali ya hifadhi za Wanyamapori na Misitu. Ukarabati wa barabara zenye urefu wa kilomita 71 katika Mapori ya Akiba na kilomita 6,526.5 katika Hifadhi za Taifa umefanyika.
13. Mheshimiwa Spika, katika maeneo ya misitu, jitihada zimefanywa kuboresha miundombinu kwa kujenga barabara mpya zenye urefu wa jumla ya kilometa 48 na kukarabati barabara zenye urefu wa kilomita 487 katika mashamba 15 ya miti ya kupandwa.
(iv) Kuwezesha uanzishwaji wa hifadhi za nyuki
14. Mheshimiwa Spika, Wakala wa Misitu Tanzania umeandaa mwongozo wa kuandaa mipango ya usimamizi wa hifadhi za nyuki. Aidha, hifadhi mbili za ufugaji nyuki za Kang’ata hekta 1,439.16 na Kwenyunga – Magiri hekta 138.62 katika Wilaya ya Handeni ziko katika hatua za awali za kutangazwa baada ya kupata ridhaa ya wananchi katika vijiji husika na mamlaka ngazi ya Wilaya na Mkoa.
(v) Kukuza mwamko na kuendesha kampeni za kuwashawishi watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii
15. Mheshimiwa Spika, kupitia maonesho na maadhimisho mbalimbali, Wizara imeendelea kuwahamasisha watanzania watembelee vivutio vya utalii. Wakati wa maonesho hayo, Wizara huweka wanyamapori hai pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii katika banda lake ambavyo huvutia wananchi wengi na hivyo kuhamasisha utalii wa ndani.
16. Mheshimiwa Spika, punguzo la gharama (Offer) limekuwa likitolewa kwa wananchi kutembelea maeneo ya vivutio kwa gharama nafuu. Kwa mfano, katika maonesho ya Sabasaba safari za kutembelea Hifadhi ya Taifa Mikumi zilikuwa Sh.10,000 kwa mtu mzima na Sh.5,000 kwa mtoto. Kiasi hicho kilijumuisha usafiri, kiingilio na maelezo mbalimbali kutoka kwa watalaam wakati wote wa safari. Mwitikio ni mzuri kwani mwaka 2011 watalii 770 walishiriki na 790 mwaka 2012. Aidha, vikundi vya utalii wa utamaduni vya Chilunga na Mto wa Mbu vilishirikishwa katika maonesho ya Sabasaba ili kuonesha mafanikio ya utalii wa kiutamaduni.
17. Mheshimiwa Spika, Kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 51 ya uhuru, Bodi ya Utalii ilidhamini tukio la kupanda Mlima Kilimanjaro. Tukio hilo lilihusisha washiriki 38, ikiwa ni pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira (8), Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (5), Kampuni ya bia ya Serengeti (7), Wajumbe wa Mamlaka ya Utalii Zimbabwe (4) na watu wengine (14).
(vi) Kupanua wigo wa aina za Utalii kwa kuendeleza Utalii unaohusisha huduma za utamaduni, mazingira na makumbusho
18. Mheshimiwa Spika, Wizara imeanzisha utalii wa kutembea usiku katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara. Aidha, Wizara imeendelea kuhamasisha wadau mbalimbali kuhusu utalii katika maeneo ya kihistoria hususan michoro ya miambani katika wilaya ya Kondoa na magofu yaliyoko Kilwa Kisiwani na Songo Mnara. Pia, Wizara ilishiriki tamasha la Utamaduni kwa nchi za Afrika Mashariki (JAMAFEST) lililofanyika Kigali, Rwanda, tarehe 11 hadi 18 Februari 2013. Lengo la tamasha lilikuwa ni kutangaza utamaduni wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia ubunifu wa soko la bidhaa na huduma za kiutamaduni ikiwemo malikale.
19. Mheshimiwa Spika, Wizara imeandaa onesho la kudumu kwenye ubalozi wa Tanzania Washington DC Marekani. Onesho hilo linahusu vivutio vya bonde la Oldupai na nyayo za binadamu wa kale (Zamadamu) za eneo la Laetoli, Ngorongoro. Onesho hilo limewavutia watalii wa nje kutembelea maeneo ya malikale yaliyopo Tanzania.
(vii) Kuongeza msukumo wa ufugaji nyuki kwa ajili ya kuzalisha asali na nta kibiashara
20. Mheshimiwa Spika, Maonesho maalum ya asali yalifanyika sanjari na kongamano la kujadili maendeleo ya sekta ya ufugaji nyuki nchini katika uwanja vya maonesho ya biashara wa Mwalimu Nyerere (Saba saba)- Dar es salaam tarehe 4 hadi 7 Oktoba, 2012. Pia, siku ya kutundika mizinga imezinduliwa rasmi na Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 4 Machi, 2013 katika wilaya ya Manyoni. Kuzinduliwa kwa siku hiyo ambayo itakuwa inaadhimishwa kila mwaka kutaongeza hamasa na msukumo katika ufugaji nyuki kwa kuongeza idadi ya mizinga na hivyo kuongeza uzalishaji wa asali. Vilevile, Mizinga 5,000 na mavazi ya kinga 200 yamegawanywa kwenye vijiji vilivyoko kandokando ya hifadhi za Misitu katika kanda saba za Wakala wa Huduma za Misitu.
III. UTEKELEZAJI WA AHADI ZILIZOTOLEWA WAKATI WA BUNGE LA BAJETI MWAKA 2012/2013
SEKTA NDOGO YA WANYAMAPORI
(i) Utekelezaji wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori
21. Mheshimiwa Spika, maandalizi ya kutoa Amri ya Wanyamapori wa Taifa (National Game Order) na Leseni Maalumu ya Uwindaji yanaendelea. Aidha, Amri ya Matumizi ya Silaha za kiraia zilizoidhinishwa kwa uwindaji wa kitalii imeandaliwa. Vilevile, rasimu ya Kanuni za Uanzishaji wa Kikosi cha Ulinzi wa Wanyamapori na Kanuni za Matumizi ya Silaha za Kiraia zimejadiliwa na wadau na kutolewa maamuzi.
22. Mheshimiwa Spika, rasimu ya Kanuni za Uchimbaji Madini Ndani ya Mapori ya Akiba imejadiliwa na wadau wa ndani na nje na kutolewa maoni. Rasimu hii itapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kupitiwa kwa mara ya mwisho kabla ya kutangazwa.
(ii) Ulinzi wa Rasilimali ya Wanyamapori
23. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori, doria -siku 59,338 zimefanyika ndani na nje ya Mapori ya Akiba. Watuhumiwa 1,215 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali na jumla ya bunduki 85 na risasi 215 za aina mbalimbali zimekamatwa. Kesi 670 zimefunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini. Kati ya hizo, kesi 272 zimekwisha kwa washitakiwa 247 kulipa faini ya jumla ya Shilingi 175,002,420 na washitakiwa 71 kupewa adhabu ya vifungo vya jumla ya miaka 99. Aidha, kesi 398 zenye jumla ya washitakiwa 897 bado zinaendelea katika Mahakama mbalimbali nchini.
24. Mheshimiwa Spika, Wizara ilifanya operesheni za kiintelijensia katika Wilaya za Liwale na Tunduru ambazo ziliwezesha watuhumiwa 354 kukamatwa na kufunguliwa jumla ya kesi 283 ambazo zinaendelea katika mahakama za Liwale na Tunduru. Bunduki 435 za aina mbalimbali, risasi 1,129, maganda 514 ya risasi, mbao 10,332 na nyara mbalimbali zenye thamani ya Shilingi 855,013,701.20 zilikamatwa. Vilevile, Wizara inaendelea na mikakati ya kuzuia, kudhibiti, na kukabili wimbi la ujangili nchini awamu kwa awamu katika maeneo mbalimbali kwa kufanya operesheni kama hizo.
25. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama imeunda kamati ndogo inayoandaa Mpango Kazi wa kuzuia na kudhibiti ujangili. Utekelezaji wa mpango kazi huo utatumia Teknolojia ya kisasa kama vile “unmanned air vehicles (UAV)” inayobaini uwepo wa majangili katika maeneo yenye wanyamapori na kuchukua hatua zinazostahili kwa wakati.
26. Mheshimiwa Spika, Wizara inatambua mchango mkubwa wa wananchi katika mapambano dhidi ya ujangili. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wananchi wanaosaidiana na Serikali kuwafichua wahalifu na kuwaomba waendelee na moyo huo wa kizalendo. Natoa rai kwa wananchi wengine wote washiriki mapambano hayo ya kulinda maliasili zetu. Aidha, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wote kwa ujumla katika juhudi za kuhifadhi wanyamapori kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
27. Mheshimiwa Spika, Baadhi ya watu kutoka ndani na nje ya nchi wamekuwa wakifanya ujangili ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa na kuchukuliwa hatua stahiki pale wanapokamatwa. Katika kutekeleza majukumu yao, baadhi ya Wahifadhi na Maafisa Wanyamapori wamekuwa wakiuawa au kujeruhiwa na majangili. Kati ya mwaka 1997 na 2012, Wizara imepoteza watumishi 17 kutokana na kuuwawa na majangili. Aidha, kumekuwepo na matukio mengi ya wananchi kujaribu kuwazuia wahifadhi wanyamapori kutenda kazi zao.
28. Mheshimiwa Spika, yapo matukio mbalimbali ya kuingiza mifugo ndani ya Mapori ya Akiba ambayo yamekuwa yakisababisha mapambano kati ya wafugaji na wahifadhi hasa wafugaji wanapolazimisha kuchukua mifugo kwa nguvu ambayo imekamatwa kisheria kama kielelezo. Mapambano hayo yamesababisha baadhi ya askari na wananchi kuuawa au kujeruhiwa wakati wa tukio.
29. Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa wananchi kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Watumishi wanaolinda wanyamapori. Hivyo,Jamii inatakiwa kutimiza wajibu wake kwa kuunga mkono na kuwapa moyo Watumishi hawa.
(iii) Ufuatiliaji wa Wanyamapori Waliotoroshwa
30. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kufuatilia suala la utoroshaji wa wanyamapori hai uliofanyika tarehe 26 No vemba, 2010. Kutokana na uchunguzi uliofanyika hapa nchini, watu sita (6) walituhumiwa kuhusika na usafirishaji huo haramu na walikamatwa na kufikishwa katika kituo cha Polisi cha KIA na kufunguliwa kesi ya Uhujumu Uchumi Na. EC.4/2011. Maelezo ya awali ya kesi hiyo yamepangwa kutolewa tarehe 07/05/2013.
31. Mheshimiwa Spika, Mawasiliano yame-endelea kufanyika kati ya Wizara na Serikali ya Qatar ili kuruhusu Tanzania kufanya uchunguzi nchini Qatar. Awali, ilipangwa timu ya uchunguzi kutoka Tanzania kwenda Qatar tarehe 27/1/2013. Hata hivyo uchunguzi nchini Qatar haujafanyika kutokana na ushirikiano hafifu kutoka Serikali ya Qatar.
(iv) Ulinzi Dhidi ya Wanyamapori Wakali na Waharibifu
32. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya iliendesha doria - siku 3,339 kwa lengo la kulinda uhai wa watu na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu. Halmashauri za Wilaya 26 zenye matatizo hayo zilihusika na kufanikiwa kudhibiti tembo na viboko dhidi ya uharibifu wa mazao na kuwarejesha wanyama hao kwenye maeneo yao ya asili. Aidha, kunguru weusi 185,179 waliuawa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Tanga.
33. Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi za Serikali katika kulinda maisha ya watu na mali zao dhidi ya wanyamapori, bado matukio ya uharibifu wa mazao na vifo vinavyotokana na wanyamapori hao yameripotiwa. Kwa bahati mbaya, watu 30 walipoteza maisha na 9 walijeruhiwa. Jumla ya ekari 1,896.7 za mazao ziliharibiwa. Ninatumia fursa hii kutoa pole za dhati kwa wote waliofikwa na majanga hayo. Serikali imetoa kifuta machozi kwa familia za walipoteza maisha na wale waliojeruhiwa cha jumla ya Shilingi 31, 800,000. Vilevile, wananchi 776 walioharibiwa mazao wamelipwa kifuta jasho jumla ya Shilingi 93,573,750.
(v) Ushirikishaji Jamii katika Uhifadhi wa Wanyamapori
34. Mheshimiwa Spika, kufuatia mafanikio yaliyopatikana kutokana na kuanzishwa kwa WMAs, juhudi zimeendelea kwa kuwezesha wananchi kuanzisha maeneo mengine. Katika mwaka 2012/2013, Jumuiya sita za Hifadhi zimo katika hatua mbalimbali za kuidhinishwa, ambapo Jumuiya ya Randilen (Monduli) imekamilisha mchakato wa kuanzisha WMA na imetangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 21 la tarehe 1 Februari, 2013. Jumuiya ya ILUMA (Kilombero na Ulanga) ipo kwenye hatua za mwisho za kutangazwa katika gazeti la Serikali. Aidha, Jumuiya za WAGA (Iringa vijijini, Mbarali na Mufindi), UMEMARUWA (Njombe na Mbarali), MBOMAMINJIKA (Kilwa) na JUHIWANGUMWA (Rufiji) zinaendelea kukamilisha taratibu za kuidhinishwa. Pori jipya la Akiba Piti limeanzishwa katika Wilaya ya Chunya kwa kushirikisha wananchi kwa lengo la kuimarisha uhifadhi.
(vi) Miundombinu katika Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba
35. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha miundombinu, jumla ya kilomita 6,526 za barabara zilikarabatiwa katika Hifadhi za Arusha, Katavi, Kilimanjaro, Kitulo, Ziwa Manyara, Mikumi, Mkomazi, Ruaha, Rubondo Saadani, Serengeti, Tarangire na Udzungwa. Aidha, njia za watembea kwa miguu zenye jumla ya kilomita 41.6 zilikarabatiwa katika Hifadhi za Katavi (km 119) Ruaha (km 124), Mikumi (km 58) na Saadani (km 85). Kwa upande wa Mapori ya Akiba, barabara zimekarabatiwa katika Mapori ya Moyowosi/Kigosi (km. 21); Lwafi (km.30) na Maswa (km. 20). Vilevile, Kilomita 81 za mipaka zimesafishwa katika Mapori ya Akiba ya Moyowosi/Kigosi (km. 31) na Lwafi (km. 50).
(vii) Uanzishwaji wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania
36. Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha uanzishwaji wa Mamlaka, Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya 2009 inafanyiwa marekebisho ili kutenganisha majukumu ya urekebu na uratibu na yale ya usimamizi. Shughuli za usimamizi zitafanywa na Mamlaka na zile za urekebu na uratibu zitabaki Wizarani. Kwa kuzingatia hayo, mapendekezo ya marekebisho ya Sheria yameandaliwa, rasimu ya muundo wa usimamizi na majukumu ya Mamlaka (structure and functions) pia imeandaliwa. Hatua inayofuata ni kupeleka rasimu hizi kwa wadau kwa ajili ya kujadiliwa na kuridhiwa. Muswada wa kuanzisha Mamlaka unatarajiwa kuwasilishwa Bungeni mwezi Novemba, 2013.
(viii) Ukusanyaji Maduhuli
37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013 hadi mwezi Machi 2013, Wizara kupitia Idara ya Wanyamapori imekusanya Shilingi 10,761,228,343 sawa na asilimia 42.75 ya lengo la Shilingi 25,175,381,917. Mapato hayo yanatokana na uwindaji wa kitalii, utalii wa picha na biashara ya ndege na wadudu.
(ix) Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori Tanzania
38. Mheshimiwa Spika, Mfuko ulikadiria kukusanya Shilingi 12,631,413,244. Makusanyo hadi Machi 2013 yamefikia Shilingi 13,296,278,179 sawa na asilimia 105.26 ya makadirio. Fedha hizo zimeendelea kutumika kwa shughuli za kulinda wanyamapori, utafiti na mafunzo, kutoa elimu kwa umma na kukarabati miundombinu.
(x) Vyuo vya Taaluma ya Wanyamapori
39. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka kimedahili wakurufunzi 502 badala ya 550. Lengo halikuweza kufikiwa kutokana na waombaji kukosa sifa za msingi za kujiunga na Chuo pamoja na ada ya kulipia mafunzo. Aidha, katika kujenga uwezo kwa wakufunzi, Chuo kiligharimia mafunzo ya wakufunzi sita kwenye ngazi ya Shahada ya uzamili na wakufunzi tisa katika ngazi ya uzamivu.
40. Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori, Pasiansi ilifikia lengo la udahili wa wakurufunzi 324. Katika kuboresha miundombinu, ujenzi wa maabara umekamilika na imebakia kuweka samani na mfumo wa gesi. Vilevile, Kituo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii Likuyu- Sekamaganga kimedahili wakurufunzi 70.
(xi) Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania
41. Mheshimiwa Spika, Taasisi ilifanya tafiti za magonjwa ambukizi kati ya wanyamapori, binadamu na mifugo. Magonjwa hayo ni kichaa cha mbwa, homa ya bonde la ufa, kifua kikuu (TB) na homa ya vipindi katika ikolojia ya Serengeti. Matokeo ya tafiti hizo yamebainisha kuwa kifua kikuu ni tatizo. Wastani wa asilimia 2.4 ya ng’ombe 1,103 waliochunguzwa kutoka kwa wafugaji 32 walionekana kuwa na kifua kikuu. Kwa upande wa wanyamapori, ilibainika kuwa asilimia 10 ya nyumbu 101 waliochunguzwa walikuwa na maambukizi ya TB. Wizara itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu vyanzo mbalimbali vya maambukizi ya kifua kikuu. Chanzo kimojawapo ni watu kunywa maziwa yasiyochemshwa pamoja na kula nyama isiyopikwa na kuiva.
42. Mheshimiwa Spika, kuhusu kichaa cha mbwa, matokeo ya utafiti yameonyesha kuwa kuna aina moja ya kirusi cha kichaa cha mbwa (Africa 1b) ambacho huathiri mifugo, wanyamapori na binadamu. Kirusi hicho kinatokana na mbwa wa kufugwa. Matokeo ya tafiti hizo yatapelekwa kwa wadau husika ili kuwezesha hatua stahili kuchukuliwa.
43. Mheshimiwa Spika, Taasisi ilifanya sensa nne za kuidadi wanyamapori katika mifumo ikolojia ya Burigi-Biharamulo-Kimisi, Moyowosi-Kigosi, Katavi-Rukwa na sensa ya mamba kwa nchi nzima. Matokeo ya sensa hizo ni kuwa wanyama walioonekana kwa wingi katika mfumo ikolojia wa Burigi-Biharamulo-Kimisi walikuwa takriban swala 1,512 pundamilia 223; Moyowosi-Kigosi tohe 509 na nyati 277; Katavi-Rukwa nyati 18,652 na pundamilia 499. Aidha, idadi ya mamba kwa nchi nzima ilikuwa takriban 5,253.
44. Mheshimiwa Spika, Taasisi iliendelea kuchunguza tuhuma za uwepo wa sumu ya tumbaku (nikotini) katika asali ya Tanzania ambapo sampuli 24 za asali zilikusanywa kutoka vijiji 13 katika Wilaya za Same, Kongwa, Sikonge, Tabora Mjini, Uyui na Urambo. Matokeo ya uchunguzi huo yalibaini kuwepo kwa kiwango kidogo cha nikotini (chini ya 0.005 nikotini), ambacho ni cha kawaida kwa mahitaji ya mwili wa binadamu. Utafiti huu ni endelevu. Aidha, Wizara inakamilisha maandalizi ya ujenzi wa maabara ya kisasa ya utafiti wa nyuki katika eneo la Ofisi za TAWIRI, Arusha ambao utakamilika katika mwaka 2013/2014.
(xii) Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
45. Mheshimiwa Spika, hadi Machi, 2013 watalii wa kimataifa 507,984 walitembelea eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kukusanya jumla ya Shilingi 47,610,714,532. Aidha, Mamlaka imekarabati barabara zenye urefu wa jumla ya kilomita 350 ndani ya hifadhi. Vilevile, Mamlaka imenunua magari manne ya doria ili kuimarisha shughuli za ulinzi wa rasilimali za Hifadhi. Kuhusu ujenzi wa jengo la Kitega uchumi mjini Arusha, tathmini ya awali (pre-qualification) katika taratibu za kumpata mkandarasi imefanyika na ujenzi unatarajiwa kuanza kabla ya mwisho wa Mwaka 2012/2013.
46. Mheshimiwa Spika, Mamlaka imekamilisha ukarabati wa majosho manne ya mifugo (Alailelai, Embulbul, Meshili na Ndian) pamoja na kujenga bwawa la maji katika eneo la Ngairish kwa ajili ya kuimarisha afya ya mifugo. Mamlaka ilinunua madume bora ya ng’ombe 40, ya mbuzi 20, na ya kondoo 20. Aidha, majike 87 ya ng’ombe yalihamilishwa. Jumla ya mitego 2,500 ya kudhibiti mbung’o iliwekwa katika kata ya Kakesio mpakani na Pori la Akiba Maswa.
47. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ilitoa chanjo ya mifugo kama ifuatavyo: mbuzi 177,965 walichanjwa dhidi ya ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na Mbuzi 66,088 walichanjwa dhidi ya ugonjwa wa kimeta. Ng’ombe 24,087 walichanjwa dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu, ambapo ng’ombe 15,595 walichanjwa dhidi ya Ndigana kali. Vile vile magunia 3,300 ya chumvi ya mifugo yalinunuliwa na kusambazwa katika vijiji vilivyopo ndani ya Hifadhi. Aidha, hadi Machi, 2013 jumla ya Shilingi 1,050,000,000 zilitolewa kwa Baraza la Wafugaji kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya jamii.
48. Mheshimiwa Spika, Ili kuwa na uhakika wa chakula kwa jamii zinazoishi ndani ya eneo la Hifadhi, Mamlaka ilinunua jumla ya magunia 16,100 ya mahindi na kuyasambaza katika vijiji vilivyopo ndani ya Hifadhi. Aidha, magunia ya mahindi 560, Sukari kilo 11,050 na kilo 450 za siagi ziligawiwa kwa shule zote za msingi zilizoko ndani ya eneo la Hifadhi.
49. Mheshimiwa Spika, mwaka 2012/2013 Mamlaka ilichangia utekelezaji wa miradi ya ujirani mwema kama ifuatavyo:- Hifadhi Mazingira Karatu (HIMAKA) Shilingi 4,000,000; ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari ya Wasichana Slahamo Shilingi 40,000,000; ujenzi wa darasa Sekondari ya Mang’ola Shilingi 5,000,000; ujenzi wa Wodi ya Wanawake kijiji cha Kambi ya Simba Shilingi 40,000,000 na madawati 135, kabati 4 meza 12 na viti 12 vya ofisi vilinunuliwa na kukabidhiwa shule ya msingi Jema Oldonyosambu. Aidha, vikundi vinane vya ujasiliamali vilifadhiliwa jumla ya Shilingi 40,000,000. Miradi sita ya ufugaji kuku ilianzishwa na vikundi 12 vya kutengeneza sanaa kwa kutumia shanga vilifadhiliwa vifaa mbali mbali vyenye thamani ya Shilingi 10,000,000.
50. Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha ulinzi wa wanyamapori katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, doria za kawaida ziliendeshwa ambapo majangili 43 walikamatwa kwa makosa mbalimbali na jumla ya bunduki nne na risasi 11 zilikamatwa.
(xiii) Shirika la Hifadhi za Taifa, Tanzania
51. Mheshimiwa Spika, kufuatia Bunge lako tukufu kupitisha Azimio la kuanzisha Hifadhi mpya ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane, taratibu za kukamilisha zoezi hili ziko katika hatua za mwisho. Vilevile, taratibu za kurekebisha mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe kwa kuongeza eneo la Ukanda wa maji katika Ziwa Tanganyika na kupunguza eneo la makaburi, mashamba na nyumba ziko katika hatua za mwisho. Lengo la marekebisho ya mpaka huo ni kulinda rasilimali ya wanyamapori na mazingira yao pamoja na kutatua mgogoro wa ardhi baina ya hifadhi na wananchi wa vijiji vya Mtanga na Mwamgongo.
52. Mheshimiwa Spika, hadi Machi, 2013 watalii wa kimataifa 750,797 walitembelea Hifadhi za Taifa ambapo jumla ya Shilingi 105,139,608,440 zilikusanywa. Katika kuboresha miundombinu ndani ya Hifadhi za Taifa, jumla ya Kilomita 6,526.5 za barabara zilikarabatiwa katika Hifadhi za Arusha (236.7); Katavi (425); Kilimanjaro (114.5); Kitulo (75); Ziwa Manyara (160); Mikumi (549.1); Mkomazi (615); Ruaha (1,435.2); Rubondo (96); Saadan (422); Serengeti (1,577); Tarangire (746); na Udzungwa (75). Aidha, njia za watembea kwa miguu zenye jumla ya kilomita 41.6 zilikarabatiwa katika Hifadhi za Kilimanjaro (km. 30.6), Udzungwa Kilomita sita na Kitulo Kilomita tano. Vile vile, njia ya kurukia ndege katika Kiwanja cha ndege Seronera imeongezwa kutoka Kilomita 1.5 hadi Kilomita 2.2. Upanuzi huo umewezesha ndege za ukubwa wa kati kama vile aina ya Fokker kutua kwenye uwanja huo.
53. Mheshimiwa Spika, Mikataba ya ujenzi wa nyumba 12 za watumishi katika Hifadhi za Ruaha, Serengeti na Tarangire imekamilika na wakandarasi wapo kwenye maandalizi ya ujenzi utakaoanza mwezi Septemba, 2013. Katika kuimarisha ulinzi Askari wanyamapori 40 waliajiriwa, magari sita ya doria yalinunuliwa na taratibu za ununuzi wa magari 10 zimekamilika, magari hayo yatapatikana mwezi Mei 2013. Aidha, siku za doria 95,283 ziliendeshwa ndani ya Hifadhi za Taifa ambapo jumla ya majangili 2,523 walikamatwa.
SEKTA NDOGO YA MISITU NA NYUKI
(i) Sera na Kanuni
54. Mheshimiwa Spika, taratibu za kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Ufugaji nyuki ya mwaka 1998 zimeanza ambapo warsha ya kwanza ya wadau imefanyika Desemba, 2012 Dar es salaam. Warsha nyingine za wadau zitafanyika kuanzia mwezi Mei 2013 kwenye kanda saba za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania.
(ii) Vyuo vya Taaluma ya Misitu na Ufugaji Nyuki
55. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuviwezesha vyuo vya misitu na ufugaji nyuki kutekeleza majukumu yake. Katika mwaka 2012/2013, jumla ya wakurufunzi 233 wamedahiliwa kama ifuatavyo:- Chuo cha Misitu Olmotonyi – Arusha 145; Chuo cha Nyuki Tabora 57 na Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi 31. Kati ya wakurufunzi 218 waliodahiliwa, 76 ni kwa udhamini binafsi.
56. Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa soroveya na ukadiriaji wa gharama za ujenzi wa jengo la Maktaba na Maabara katika Chuo cha Viwanda vya Misitu - Moshi, taratibu za kumpata mkandarasi zinafanyika ili kazi ya ujenzi ianze. Aidha, Chuo cha Ufugaji Nyuki Tabora kimekarabati majengo mawili, mifumo ya maji machafu ya nyumba mbili za watumishi, kukamilisha ujenzi wa bwalo la chakula na utayarishaji wa ramani ya chuo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali.
(iii) Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
57. Mheshimiwa Spika, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania umeendelea kutekeleza majukumu ya kiutendaji kama ifuatavyo:-
(a) Kuendeleza Ufugaji Nyuki
58. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha ufugaji nyuki, eneo lenye ukubwa wa hekta 56,290 kwa ajili ya kuanzisha hifadhi ya nyuki limeainishwa katika Kanda ya Ziwa. Aidha, makundi ya nyuki 631 kwenye manzuki tatu zenye mizinga 882 yalitunzwa katika wilaya za Bukombe, Biharamulo na Maswa. Mafunzo kwa wafugaji nyuki 162 yalitolewa katika vijiji 23 na maeneo matatu kwa ajili ya kuanzisha hifadhi za nyuki yaliainishwa huko Geita, Biharamulo na Nyantakala. Mizinga 500 ya nyuki ilisambazwa kwa wafugaji Kanda ya Kusini (Ruangwa, Mtwara, Newala, Tunduru na Namtumbo).
59. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango wa kudhibiti mabaki ya kemikali katika asali nchini, sampuli 54 za asali zilikusanywa na kufanyiwa uchambuzi wa kemikali katika maabara nchini Ujerumani. Matokeo ya uchambuzi huo yanaonyesha kuwa asali ya Tanzania ni nzuri na inakidhi viwango vinavyokubalika katika masoko ya nje.
(b) Elimu kwa Umma na Uhamasishaji
60. Mheshimiwa Spika, uhamasishaji kuhusu elimu ya uhifadhi wa misitu na ufugaji nyuki ulifanyika kupitia vipindi 78 vya Redio, saba vya Televisheni mikutano na semina 83. Aidha, vipeperushi na machapisho mbalimbali yalisambazwa. Vilevile, Wizara ilitoa elimu kuhusu njia sahihi za kufuga nyuki kwa wafugaji 979 ikijumuisha vikundi 72 katika vijiji 67 vya wilaya za Kanda za Kaskazini na Mashariki. Vikundi 52 na mafundi seremala 52 walipatiwa mafunzo ya ufugaji nyuki katika wilaya za Njombe, Ileje, Mbozi, Chunya, Rungwe, Kilolo na Ludewa.
(c) Ushiriki wa Wadau Katika Kuendeleza Misitu
61. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuendeleza ushirikishwaji wa sekta binafsi kupanda miti kibiashara, vikundi 16 vya wakulima wa miti vimeundwa na kufanya jumla ya vikundi 37. Vikundi hivi vyenye jumla ya wanachama 2,369 vimewezeshwa kupanda miti 2,530,144 katika eneo lenye jumla ya hekta 2,277 katika Wilaya za Tukuyu, Njombe, Kilolo na Mufindi. Aidha, vikundi hivyo vimewezeshwa kutayarisha mipango ya utekelezaji wa kilimo cha miti ya matunda.
(d) Usimamizi wa Mashamba ya Miti
62. Mheshimiwa Spika, miche 12,956,354 ya miti laini ilikuzwa na kupandwa kwenye eneo la hekta 3,756, ikiwa ni asilimia 90 ya lengo la kupanda miche 14,440,000 katika mashamba 15 ya miti. Aidha, tathmini ya miti imefanyika katika mashamba 14 kwa ajili ya kupata takwimu za kuandaa mipango ya usimamizi. Vilevile, eneo la mashamba ya miti ya kupandwa lenye jumla ya hekta 3,756.04 limesafishwa na hekta 14,655.42 zilipogolewa.
63. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mipaka na kuzuia moto ndani ya misitu, barabara za kuzuia moto zenye urefu wa jumla ya kilomita 1,649.3 zimesafishwa katika mashamba ya Sao Hill (km 1,147); Matogoro (km 52); Shume (km.101); Ukaguru (km 26); Kiwira (km 27.6); Kawetire (km 94.7); Rondo (km 50); Rubya (km 25); Mtibwa (km 68) na Longuza (km 58).
(e) Usimamizi wa Misitu ya Hifadhi
64. Mheshimiwa Spika, uhakiki wa mipaka yenye jumla ya kilomita 2,563.42 umefanyika katika Kanda ya Kati (km.60.92); Kanda ya Magharibi (km.1,117.60); Kanda ya Mashariki (km.100.30); Kanda ya Ziwa (km.142.30) na Kanda ya Kaskazini (km.1,152.30). Aidha, Mipango 15 ya usimamizi wa misitu iliandaliwa pamoja na kusimika maboya 479 katika kanda za Ziwa na Kati. Vilevile, ramani nane zilichorwa na mabango 255 ya tahadhari yaliwekwa kwenye misitu ya Kanda za Magharibi na Nyanda za Juu Kusini.
65. Mheshimiwa Spika, katika kuongoa maeneo yaliyovamiwa, wavamizi wa hifadhi za misitu na mazingira asilia waliondolewa katika misitu ya Mkweni hills, Nyahua Mbuga, Uyui, Kigwa-Rubuga, Goweko, North Ugalla, Mpandaline, Mbeya Range, Kilimanjaro, Chome, Rufiji Delta, Amani, Magamba, Nilo, Mkingu, Geita, Biharamulo na Sayaka. Aidha, katika Kanda ya Magharibi, wahalifu 98 walikamatwa, kati yao 48 walitozwa faini ya Shilingi 201,920,000 na watuhumiwa 50 kesi zao zipo mahakamani. Vilevile, wavamizi 516 waliondolewa katika hifadhi za misitu zilizopo Kanda ya Kaskazini na kesi 34 zipo mahakamani.
66. Mheshimiwa Spika, siku za doria 109,522 zilifanyika ndani na nje ya maeneo ya misitu. Kutokana na doria hizo mazao mbalimbali ya misitu yaliyokamatwa yalitaifishwa na kuuzwa ambapo jumla ya Sh.1, 588, 549,727 zilikusanywa.
(f) Kuimarisha ukusanyaji wa Maduhuli
67. Mheshimiwa Spika, Wakala umewezesha Halmashauri za Wilaya 26 kufanya vikao vya Kamati za Uvunaji za Wilaya pamoja na kutayarisha mipango 10 ya uvunaji. Aidha, Mfumo wa ukusanyaji wa maduhuli umeimarishwa kwa kufanya ukaguzi na uhakiki katika maeneo mbalimbali. Hadi Machi 2013, Shilingi 33,182,997,357 zilikusanywa sawa na asilimia 56.51 ya lengo la kukusanya Shilingi 58,718,747,409
(iv) Mfuko wa Misitu Tanzania
68. Mheshimiwa Spika, hadi Machi, 2013 Mfuko ulikusanya Shilingi 2,229,097,230 ikiwa ni asilimia 63.7 ya lengo la mwaka 2012/2013 la kukusanya Shilingi 3,500,000,000. Katika mwaka 2012/2013, Mfuko unatarajia kuwezesha miradi 70 ya wadau mbalimbali wa misitu na nyuki kwa kutoa Shilingi 1,940,810,000. Miradi mipya 48 na 52 inayoendelea iliwezeshwa kwa kupewa jumla ya Shilingi 1,380,478,612. Kazi zilizotekelezwa katika miradi hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu manufaa na umuhimu wa matumizi ya nishati mbadala; ushirikishaji jamii katika uanzishwaji wa hifadhi za misitu ya jamii na hifadhi za Nyuki; upandaji miti na ufugaji nyuki. Vilevile, Mfuko uliwezesha tafiti mbalimbali kwa ajili ya kuboresha usimamizi wa misitu hapa nchini.
(v) Wakala wa Mbegu za Miti
69. Mheshimiwa Spika, Kilo 5,103 za mbegu za miti zenye thamani ya Shilingi 169,309,385 ziliuzwa nchini na kilo 297 zenye thamani ya Shilingi 40,511,100 ziliuzwa nje ya nchi. Hadi Machi 2013, Wakala iliuza miche 24,789 yenye thamani ya Shilingi 24,249,600. Vilevile, vyanzo vinne vya mbegu bora za miti ya Mkaratusi, Mkorimbia, Mfudufudu na Miembe vilianzishwa. Halikadhalika, Wakala uliendesha mafunzo ya muda mfupi kuhusu utunzaji wa miche ya miti kwa washiriki 43 kutoka mikoa ya Morogoro na Iringa.
(vi) Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania
70. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Taasisi imekamilisha ujenzi wa majengo ya utawala na maabara ya Makao Makuu katika eneo la Kingolwira Manispaa ya Morogoro na kuhamia. Aidha, Taasisi inaendelea na utafiti wa mahusiano kati ya miti ya kupandwa na udongo, kazi hii imeanzia katika mashamba ya miti Meru/Usa. Matokeo ya awali yanaonesha uwepo wa upungufu wa rutuba unaosababishwa na uondoaji wa mabaki ya miti.
71. Mheshimiwa Spika, Taasisi imefanya utafiti wa familia 98 za miti ya misindano (Pinus maximinoi) katika mkoa wa Iringa na matokeo ya awali yameonesha kuwa miche michache katika familia 16 kati ya 98 imeota na imepandwa kwenye msitu shamba wa Kihanga – Mufindi kwa uangalizi ili kuwa chanzo cha mbegu hapo baadaye. Pia, Taasisi inaendelea kushirikiana na taasisi za utafiti za Afrika Mashariki pamoja na Taasisi ya Kimataifa iitwayo Central American and Mexico Coniferous Resources-CAMCORE ya Kuhifadhi na Kuongeza Ubora wa Miti. Matokeo ya ushirikiano huo ni kuandaa mpango mkakati wa kuboresha miti ya kupandwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
72. Mheshimiwa Spika, Taasisi ikishirikiana na Wakala wa Misitu inaendelea kufanya utafiti wa uoteshaji na ukuzaji wa familia mbalimbali za Mitiki na Mikaratusi kwa lengo la kusambaza kwa wadau. Aidha, mashamba darasa manne ya miti ya kuni na mkaa yenye ukubwa wa hekta moja kila moja katika wilaya za Morogoro (Kata ya Mikese na Gwata) na Bagamoyo (Kata ya Msata na Mbwewe) yameanzishwa. Kutokana na elimu waliyoipata wakulima wameweza kuzalisha miche 28,000 ya miti ya kuni na mkaa. Taasisi inaendelea kutoa elimu ili kuwezesha wakulima kuanzisha mashamba makubwa.
73. Mheshimiwa Spika, Taasisi imehamasisha utengenezaji na utumiaji wa majiko banifu ya kuni katika vijiji vya Gwata na Lubungo, wilaya ya Morogoro na vijiji vya Kihangaiko na Kwang’andu katika Wilaya ya Bagamoyo. Jumla ya familia 50 katika vijiji hivyo zimenufaika na teknolojia hiyo.
SEKTA NDOGO YA UTALII
(i) Sera na Sheria
74. Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 ambapo rasimu ya awali ya Sera hiyo imeandaliwa. Sera mpya ya Taifa ya Utalii itakamilika mwaka 2013/2014. Vilevile, Wizara imekamilisha Kanuni za Tozo ya Maendeleo ya Utalii (GN.Na.218 ya mwaka 2012) na ukusanyaji wa Tozo la Kitandasiku (bed night levy) utakaoanza rasmi Julai, 2013 kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania.
(ii) Uendelezaji wa Utalii
75. Mheshimiwa Spika, zoezi la kupanga hoteli katika daraja limeendelea ambapo mwaka 2012/2013, zoezi hilo limefanyika katika mkoa wa Manyara. Kati ya huduma za malazi 17 zilizohusika, mbili zimetunukiwa nyota nne ambazo ni Lake Manyara Tree Lodge na Kikoti Safari Camp; 11 zimetunukiwa nyota tatu na nne zimetunukiwa nyota mbili. Sambamba na jitihada za kuboresha huduma za malazi, idadi ya watalii wanaofika nchini imeendelea kuongezeka. Takwimu zilizokusanywa zinaonesha kuwa idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kutoka 867,994 mwaka 2011 kufikia 1,077,058 mwaka 2012 sawa asilimia 24.
(iii) Ukusanyaji wa Maduhuli
76. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara ililenga kukusanya Shilingi 11,091,246,108 kutokana na Tozo ya Maendeleo ya Utalii na leseni mbalimbali za biashara ya Utalii. Hadi Machi, 2013 jumla ya Shilingi 2,696,571,256 zilikusanywa. Makusanyo hayo ni asilimia 24.3 ya makisio ya mwaka 2012/2013. Hata hivyo, ifikapo mwishoni mwa mwaka 2012/2013 huenda lengo la makusanyo halitafikiwa kutokana na kuchelewa kuanza kwa Tozo ya Maendeleo ya Utalii.
(iv) Bodi ya Utalii Tanzania
77. Mheshimiwa Spika, Mkakati wa miaka mitano wa kutangaza utalii wa Kimataifa 2012/13-2016/17 ulizinduliwa mwezi Novemba, 2012. Mkakati huo unalenga kuelekeza juhudi za utangazaji katika masoko machache zaidi yenye tija ikiwa ni pamoja na masoko yenye uwezekano mkubwa wa kukua kwa utalii ambayo ni masoko ya India, Afrika Kusini, Brazil, Urusi, China, Uturuki na Nchi za Ghuba. Aidha, Mkakati huo unazingatia mbinu za kisasa za kutangaza utalii zinazojumuisha matumizi ya TEHAMA; ziara za utangazaji utalii; misafara ya waandishi wa habari na mawakala wa utalii kutoka nje; kutumia mabalozi wa hiari (tourism goodwill ambassadors) na wawakilishi wa kutangaza utalii katika nchi mbalimbali.
78. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mkakati huo umeanza kwa kufanya mikutano mitano katika mikoa ya Dar es salaam (2), Iringa (1), Morogoro (1) na Arusha (1) ili kuutambulisha Mkakati na kuhamasisha wadau kuutumia.
79. Mheshimiwa Spika, Bodi ya Utalii kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, imeweka matangazo katika kiwanja cha “Seattle Sounders” nchini Marekani ambacho kinatumika kwa soka na mpira wa miguu wa Kimarekani. Matangazo hayo yalianza kuoneshwa Mei, 2012 na yataendelea hadi Aprili, 2013 ambao ni mwisho wa msimu.
Bodi, kwa kushirikiana na Shirikisho la vyama vya Utalii Tanzania (TCT), ilipokea mapendekezo 319 yaliyotolewa na wadau kuhusu kuunda utambulisho wa pekee (Tanzania Destination Brand). Mapendekezo hayo yalichambuliwa na kupatikana matano bora ambayo yatawasilishwa tena kwa wadau ili kupigiwa kura kwa lengo la kupata pendekezo moja litakalotumika kwa utambulisho wa nchi.
80. Mheshimiwa Spika, Bodi iliendelea kuhamasisha uanzishwaji wa miradi ya utalii wa kiutamaduni ambapo vikundi jamii vya utalii wa utamaduni vimeongezeka kutoka 41 mwaka 2012 hadi 47 mwezi Machi, 2013 kati ya 50 vinavyotarajiwa kufikiwa mwezi Juni, 2013. Mwongozo wa uanzishaji wa miradi ya utalii wa kiutamaduni upo na utaendelea kusambazwa kwa wadau ili kuhamasisha uanzishwaji wa miradi nchini.
(v) Wakala wa Chuo cha Taifa cha Utalii
81. Mheshimiwa Spika, Wakala umeendelea kutoa mafunzo katika ngazi ya Astashahada na Stashahada katika tasnia ya Ukarimu na Utalii. Katika mwaka wa masomo 2012/2013, Wakala umedahili wakurufunzi 249 tofauti na lengo la awali la kudahili wakurufunzi 315. Upungufu umetokana na waombaji wengi kukosa sifa za kujiunga. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Chuo kitaanzisha programu za awali (Foundation Courses) ili wasio na sifa za kutosha wafikie kiwango kinachotakiwa.
82. kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo, utaratibu wa kuwatembeza watalii katika jiji la Dar es Salaam umeanza. Utaratibu huo umelenga kukuza utalii wa ndani na kuongeza mapato ya Chuo. Tangu kuanza utaratibu huo mwezi Januari, 2013 hadi mwishoni mwa mwezi Machi, 2013 jumla ya watalii wa ndani 280 wametembezwa katika vivutio mbalimbali vilivyoko Jijini Dar es Salaam na Bagamoyo.
SEKTA NDOGO YA MAMBO YA KALE
(i) Sera na Sheria
83. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na marekebisho ya Sheria ya Mambo ya Kale Sura 333 ya Sheria za Tanzania kwa kuendesha mikutano mitatu ya kukusanya maoni ya wadau. Uchambuzi wa maoni ya wadau utatumika katika kuandaa mapendekezo yatakayowasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa maamuzi.
(ii) Uhifadhi na Uendelezaji wa Rasilimali za Malikale
84. Mheshimiwa Spika, ukarabati wa magofu ya kihistoria ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara umefanyika kwa asilimia 80. Aidha, Wizara imeanza taratibu za ujenzi wa kituo cha Kumbukumbu na Taarifa Amboni katika Mkoa wa Tanga. Kituo hicho kitaonyesha kumbukumbu za urithi wa utamaduni katika eneo hilo na maelezo yanayotoa historia ya chimbuko la eneo hilo. Taratibu za kukarabati nyumba ya mtumishi katika kituo cha Kaole, Bagamoyo zimeanza.
85. Mheshimiwa Spika, Wizara katika kupanua wigo wa vivutio vya urithi wa utamaduni na kuhifadhi nyayo za binadamu wa kale za Laetoli, imetangaza zabuni ili kumpata mtaalamu mshauri wa kuandaa michoro ya jengo la Makumbusho ya kuhifadhi nyayo hizo ambapo kampuni saba za ushauri zimejitokeza kuomba kufanya kazi hiyo. Kati ya kampuni zilizojitokeza, mbili ni za nje, na tano ni za hapa nchini. Kazi ya kuipata kampuni ya ushauri inatarajiwa kukamilika Juni, 2013.
86. Mheshimiwa Spika, Wizara imeboresha miundombinu katika vituo vya Isimila, Lugalo, Ujiji na Tongoni ili kuimarisha uhifadhi wa malikale. Kazi zilizofanyika ni pamoja na: ujenzi wa uzio na mfereji wa maji ya mvua kwa ajili ya kuzuia mmonyoko wa ardhi katika kituo cha Isimila; ukarabati wa Mnara wa Lugalo katika mkoa wa Iringa; kukamilisha ukarabati wa jengo la ofisi Tongoni, kukamilisha ujenzi wa jengo la Kumbukumbu na Taarifa Kituo cha Ujiji – Kigoma na kuweka vioneshwa katika Makumbusho hiyo.
(iii) Utangazaji na Ushirikishwaji wa jamii
87. Mheshimiwa Spika, Elimu ya uhifadhi shirikishi na uendelezaji wa malikale kwa jamii zinazozunguka maeneo yenye rasilimali za malikale ni endelevu. Wizara imetoa elimu ya uhifadhi wa malikale kwa wakazi wa vijiji vya Pahi, Mnenia na Kolo katika Wilaya ya Kondoa kupitia vikundi vyao vya kulinda na kuhifadhi maeneo yenye Michoro ya Miambani. Aidha, elimu imetolewa kwa wananchi wa Kilwa kuhusu uhifadhi shirikishi wa Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara na kujengewa uwezo katika kuyahifadhi na kuyakarabati. Wananchi hao wamehamasishwa kuunda na kujiunga na vikundi mbalimbali vya kijamii ili kutumia fursa zilizopo za utalii wa utamaduni kujiongezea kipato na hivyo kupunguza umasikini.
Vilevile, Wizara kwa kutumia njia ya Televisheni na Redio (TBC1, ITV na Channel 10) imeendelea kuelimisha umma juu ya Sera ya Malikale, uhifadhi endelevu wa malikale, maendeleo ya urithi wa utamaduni na Tamasha la Kumbukizi la Vita vya Majimaji na Utalii. Vipindi nane kuhusu maeneo ya wapigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika yaliyoko wilaya ya Nachingwea katika Mkoa wa Lindi vilitangazwa.
(iv) Utafiti wa Malikale
88. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Kitengo cha Hifadhi ya Mazingira ya Bahari na Maeneo Tengefu (Marine Parks and Reserves), Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Shirika la Bandari Zanzibar, Idara ya Mambo ya Kale, Makumbusho na Nyaraka- Zanzibar na Kituo cha Urithi wa Utamaduni cha Uholanzi ilifanya soroveya baharini katika eneo la Kisimani Mafia na kubaini kuwepo kwa mabaki ya meli, masalia ya vigae, na sarafu za karne ya 11 na 12. Aidha, kazi ya utambuzi na uwekaji wa kumbukumbu za urithi wa utamaduni uliomo baharini katika Kisiwa cha Mafia inaendelea.
(v) Ukusanyaji wa Maduhuli
89. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/ 2013, Wizara kupitia Idara ya Mambo ya Kale hadi kufikia Machi, 2013 imekusanya Shilingi 1,124,048,564 hivyo kuvuka lengo la kukusanya Shilingi 750,000,000. Ongezeko hili ni sawa na asilimia149.87 kutokana na kupanda kwa ada za viingilio katika maeneo ya vivutio vya utalii wa kitamaduni.
(vi) Shirika la Makumbusho ya Taifa Tanzania
90. Mheshimiwa Spika, Shirika limeendelea kutekeleza majukumu yake ya kisheria ya kutafiti, kuhifadhi, kutunza, na kuelimisha umma kuhusu Urithi wa Taifa. Kwa mwaka 2012/2013, tamasha la Kumbukizi ya Vita vya Majimaji na Utalii limefanyika katika mkoa wa Ruvuma tarehe 25 hadi 27 Februari, 2013 na kujumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Morogoro, Iringa, Njombe, Ruvuma, Simiyu, Kilimanjaro, Mbeya na Pwani. Katika kuhifadhi urithi wa Taifa, Shirika limeendelea na ujenzi wa uzio katika Makumbusho ya Taifa ya Majimaji, Songea katika mkoa wa Ruvuma.
91. Mheshimiwa Spika, katika kutoa elimu kwa umma, Shirika limeandaa na kusambaza vipeperushi 10,000 katika shule, taasisi, hoteli za kitalii na wadau wengine. Aidha, jamii wakiwemo watoto na wanafunzi wamehamasishwa kutembelea Makumbusho kupitia vipindi vya televisheni vinavyoendeshwa na Shirika la Makumbusho ya Taifa kwa kushirikisha wataalamu wa makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, TBC1 na wadau mbalimbali.
URATIBU, UTAWALA NA MAENDELEO YA RASILIMALI WATU
92. Mheshimiwa Spika, Mpango Mkakati wa Wizara 2010-2013 umefanyiwa mapitio na kuandaa Mkakati mpya kwa kipindi cha Julai, 2013 hadi Juni, 2016. Mkakati huo umeainisha maeneo sita ya vipaumbele ambayo ni kuhifadhi maliasili na malikale; kuendeleza na kutangaza utalii; kuboresha mifumo ya ukusanyaji maduhuli; kushirikisha wadau katika uhifadhi wa maliasili, malikale na uendelezaji utalii; kujenga uwezo wa Wizara ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi; na kudumisha ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa.
93. Mheshimiwa Spika, katika kutoa elimu kuhusu uhifadhi na uendelezaji utalii, Wizara iliandaa na kurusha vipindi vinne vya redio na 16 vya televisheni, kuweka taarifa za matukio mbalimbali ya Wizara kwenye tovuti na mitandao ya kijamii pamoja na kuchapisha na kusambaza nakala 4,000 za Jarida la Maliasili, nakala 1,500 za kalenda. Aidha, mikutano nane ya waandishi wa habari ilifanyika pamoja na kutoa taarifa 15 kwa umma. Pia, kipindi maalumu kuhusu Mafanikio ya Awamu ya Nne kiliandaliwa na kurushwa kupitia vituo vitatu vya televisheni.
94. Mheshimiwa Spika, mwaka 2012/2013, katika jitihada za kukabiliana na upungufu wa watumishi, Wizara imepewa kibali cha kuajiri watumishi 617 na taratibu za kuajiri zinaendelea katika Mamlaka husika. Wizara imepandisha vyeo watumishi 197 wa kada mbalimbali na watumishi sita wamebadilishwa cheo.
95. Mheshimiwa Spika, katika kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji, Wizara imewezesha watumishi 103 kuhudhuria mafunzo mbalimbali. Kati ya hao, watumishi 72 wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi na 31 mafunzo ya muda mrefu. Aidha, watumishi 68 wameshiriki Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara (SHIMIWI) katika Mkoa wa Morogoro. Wizara imeendelea pia kuwahudumia watumishi waliojitokeza na wanaoishi na virusi vya UKIMWI kwa kutoa fedha kwa ajili ya kununulia virutubisho na lishe bora. Vilevile, Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi ulifanyika mwezi Machi, 2013 ili kudumisha utawala bora na uwajibikaji.
CHANGAMOTO KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA
96. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Wizara ilikabiliwa na changamoto mbalimbali katika juhudi za kulinda, kuhifadhi, kuendeleza na kusimamia maliasili, malikale na uendelezaji utalii. Changamoto hizo ni uhaba wa fedha, watumishi na vitendea kazi katika kutekeleza baadhi ya programu za Wizara hasa katika Sekta za Wanyamapori, Misitu na Malikale; mwamko mdogo wa Watanzania kutembelea vivutio vya utalii; ushirikiano hafifu wa wadau katika uhifadhi wa maliasili na malikale; kubomolewa kwa majengo ya kihistoria hususan mijini; uchomaji moto misitu; kukabiliana na ujangili na ubovu wa miundombinu katika maeneo yaliyohifadhiwa na uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za maliasili na malikale.
MIKAKATI YA KUKABILI CHANGAMOTO
97. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizi, Wizara imepanga mikakati mbalimbali kupitia Mpango Mkakati wake 2013 – 2016. Mikakati hiyo ni kuendelea kuajiri watumishi wapya kulingana na ikama iliyopitishwa; kuongeza ushiriki wa wadau mbalimbali katika uhifadhi na matumizi endelevu ya maliasili, malikale na shughuli za utalii; kukuza utalii wa ndani kwa kuhamasisha jamii kutembelea vivutio vya utalii; kufanya mapitio ya Sera na Sheria; kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji maduhuli, na kuongeza bajeti ya ulinzi, uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za Maliasili na Malikale.
IV. MPANGO WA UTEKELEZAJI NA MALENGO KWA MWAKA 2013/2014
SEKTA NDOGO YA WANYAMAPORI
(i) Ulinzi, Usimamizi wa Wanyamapori na Ushirikishwaji Jamii
98. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara itaendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali za wanyamapori kwa kuendelea kufanya doria ndani na nje ya Mapori ya Akiba kwa kuendesha doria - siku 100,000. Vilevile, miundombinu, vitendea kazi na huduma zitaboreshwa kwa watumishi katika vituo 27 kwenye Mapori ya Akiba na Kanda nane za Kikosi Dhidi Ujangili. Wizara itakamilisha Kanuni ya Kikosi cha Ulinzi wa Wanyamapori na itaandaa Kanuni mpya mbili. Kanuni ya kwanza ni Usimamizi wa Maeneo ya Ushoroba, Mazalia na Mtawanyiko wa Wanyamapori na ya pili ni Kanuni za Usimamizi Wanyamapori wa Taifa. Aidha, Wizara itatoa Amri ya Maeneo ya Uwindaji wa Wenyeji.
99. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuongeza ushiriki wa wadau katika usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itakamilisha uanzishaji wa maeneo matatu ya WMAs. Maeneo hayo ni WAGA katika Wilaya za Iringa Vijijini, Mbarali na Mufindi; UMEMARUWA Wilaya za Mbarali na Njombe na ILUMA Wilayani Kilombero na Ulanga. Aidha, Wizara itaendelea kutoa gawio la asilimia 25 ya fedha zitokanazo na uwindaji wa kitalii kwa Halmashauri za Wilaya 42 na WMAs 16 ili kuziongezea uwezo wa kusimamia rasilimali za wanyamapori.
100. Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali za wanyamapori na kuboresha uwezo wa kukusanya maduhuli, Wizara itakamilisha uanzishwaji wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania ifikapo Novemba 2013.
101. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kutekeleza mikataba na makubaliano ya Kikanda na Kimataifa ya RAMSAR, AEWA, CMS, Lusaka Agreement Task Force na CITES. Wizara pia itaendelea kushiriki katika maonesho mbalimbali ndani na nje ili kujiimarisha katika masuala ya uhifadhi endelevu wa wanyamapori nchini na kuboresha ushirikiano katika masuala ya uhifadhi wa rasilimali ya wanyamapori.
(ii) Vyuo vya Taaluma ya Wanyamapori
102. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2013/2014, vyuo vinatarajia kudahili wakurufunzi 1,020 ambapo Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka kinatarajia kudahili wakurufunzi 496 pamoja na kugharimia mafunzo kwa wakufunzi watano kwenye ngazi ya Uzamili na tisa katika mafunzo ya Uzamivu. Vilevile, Chuo kimepanga kuendelea kuimarisha miundombinu ya maji chuoni na kujenga madarasa mawili pamoja na kumalizia mapitio ya Mpango Mkakati (Strategic Plan) wake ikiwa ni pamoja na kuandaa Mpango wa Biashara (Business Plan). Chuo cha Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi kinatarajia kudahili wakurufunzi 324 na kukamilisha ujenzi wa maabara kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo. Aidha, Kituo cha Mafunzo ya Usimamizi wa Maliasili kwa Jamii cha Likuyu- Sekamaganga kinatarajia kudahili wakurufunzi 200.
(iii) Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania
103. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2013/2014, Shirika litajenga nyumba 29 katika hifadhi tisa za Arusha, Katavi, Kilimanjaro, Mikumi, Mkomazi, Ruaha, Rubondo, Serengeti na Udzungwa na barabara mpya zenye urefu wa jumla ya Kilomita 115. Aidha, ukarabati utafanyika katika barabara zenye jumla ya kilomita 6,526; viwanja 12 vya ndege na Kilomita 41.6 za njia za kutembea kwa miguu katika hifadhi za Ruaha na Kilimanjaro. Ili kuboresha huduma katika hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, Shirika litajenga mahema kwa ajili ya kulia chakula, vivuli vya kupumzikia na kuboresha malango ya kuingilia. Vilevile, Shirika litanunua magari 43, ndege mbili za doria na excavator, low loader, low bowser, roller compactor, dumper truck, tractor, water bowser kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
(iv) Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
104. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2013/2014, Mamlaka itajenga jengo moja la familia sita za wafanyakazi pamoja na kuweka uzio kuzunguka nyumba za wafanyakazi eneo la Kamyn, jengo la mapokezi uwanja wa ndege Ndutu, jiko kwenye kambi ya kulala wageni ya Simba A pamoja na nyumba moja ya askari eneo la Lositete. Aidha, Mamlaka itaendelea na ujenzi wa jengo la kitega uchumi (kwa ubia) lenye ghorofa 10 mjini Arusha.
105. Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2013/2014, maeneo ya kihistoria na urithi wa kitamaduni ambayo yamo kwenye eneo la hifadhi ya Ngorongoro, yatasimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kuhakikisha uwepo wa uwiano wa viwango vya maeneo ambayo yametangazwa kuwa Urithi wa Dunia. Maeneo hayo ni pamoja na Oldupai, Laetoli, Ziwa Ndutu pamoja na maeneo mengine ya urithi wa utamaduni yaliyopo Ngorongoro. Hata hivyo, maeneo hayo yataendelea kusimamiwa kwa kutumia Sera na Sheria ya Mambo ya Kale.
106. Mheshimiwa Spika, Mamlaka imepanga kununua mitambo miwili (grader na excavator) ya kutengeneza barabara, magari mawili kwa ajili ya kuimarisha doria, basi moja kwa ajili ya utalii wa ndani, gari moja kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa, basi moja la wafanyakazi na gari moja kwa ajili ya kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli kwenye lango la Naabi. Aidha, Mamlaka itaendelea kusaidia miradi ya maendeleo ya jamii kwa kujenga jengo kwa ajili ya kuhifadhi na kuchakata asali Endulen, kuendeleza mradi wa wenyeji waliohamishiwa Jema Oldonyosambu, kuchangia gharama za matibabu kwa ajili ya wenyeji Hospitali ya Endulen, pamoja na ujenzi wa majosho na kuboresha mifugo Ngairish.
(v) Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori
107. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Taasisi itaendeleza utafiti wa wanyamapori nchini pamoja na kuidadi wanyamapori katika maeneo mbalimbali ya nchi na kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa kuhifadhi Tembo na Faru. Aidha, Taasisi kupitia Kituo cha Utafiti wa Wanyamapori Njiro itaendelea na ujenzi wa maabara ya utafiti wa nyuki. Vilevile, kituo kitaendelea na utafiti wa mahusiano kati ya nyuki na mimea, maadui wa nyuki aina ya varroa destructor na kukamilisha maandalizi ya Mpango Mkakati wa Utafiti wa Ufugaji Nyuki Tanzania (Beekeeping Research Master Plan).
SEKTA NDOGO YA MISITU NA NYUKI
(i) Sera, Sheria na Kanuni
108. Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki, Wizara itakamilisha mapitio ya Sera ya Misitu ya mwaka 1998 na Sera ya Taifa ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998 na kuzisambaza kwa wadau.
109. Mheshimiwa Spika, Wizara inatarajia kufanya mapitio ya kanzi ya misitu na nyuki nchini (NAFOBEDA) na kuendesha mafunzo ya matumizi ya kanzi hiyo kwa maafisa misitu na nyuki 120 kutoka mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa na Morogoro. Aidha, Wizara itafanya tathmini ya Asasi zinazojihusisha na uhifadhi wa misitu na ufugaji nyuki hapa nchini ili kurahisisha uratibu katika usimamizi wa rasilimali hizo. Vilevile, kuwezesha uanzishwaji wa misitu 15 ya hifadhi za vijiji katika mikoa ya Morogoro, Tanga na Ruvuma, pamoja na hifadhi tano za nyuki za vijiji katika mikoa ya Rukwa, Kigoma na Tabora.
(ii) Vyuo vya Taaluma ya Misitu na Ufugaji Nyuki
110. Mheshimiwa Spika, Vyuo vya Misitu na Ufugaji nyuki vinatarajia kudahili jumla ya wakurufunzi 296 katika mwaka 2013/2014 kama ifuatavyo: Chuo cha Ufugaji Nyuki Tabora 63; Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi 30 na Chuo cha Misitu Olmotonyi 203. Vilevile, Wizara itaendelea kuwezesha Vyuo vya Misitu na Ufugaji Nyuki kutekeleza majukumu yake. Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi kitaanza ujenzi wa maktaba. Chuo cha Ufugaji Nyuki Tabora kitakarabati nyumba mbili za walimu; kuweka samani katika ofisi za walimu, kufunga mtandao wa mawasiliano na kuweka samani na majiko katika bwalo la chakula.
(iii) Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
111. Mheshimiwa Spika, mwaka 2013/2014 Wakala utaelekeza juhudi katika utekelezaji wa sheria, kuimarisha mipaka ya misitu, ukarabati wa maeneo yaliyoharibika na vyanzo vya maji, uendelezaji mashamba ya miti na ufugaji nyuki na usimamizi wa rasilimali ya misitu na nyuki.
(a) Utekelezaji wa Sheria
112. Mheshimiwa Spika, Ili kudhibiti biashara na uvunaji haramu wa mazao ya misitu na nyuki, jumla ya siku za doria 20,700 zitaendeshwa katika maeneo ya nchi kavu na majini (baharini). Vilevile, katika kudhibiti viwango na ubora wa mazao ya misitu na nyuki Wakala utakusanya sampuli 60 za asali kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa ajili ya uchambuzi wa kimaabara. Aidha, mafunzo kuhusu ubora wa mazao ya nyuki yatatolewa kwa vikundi/ vyama 150 vya wafuga nyuki. Wavamizi wa hifadhi za misitu na hifadhi za mazingira asilia wataondolewa kwenye hifadhi za Biharamulo, Geita, Nyantakara na Minziro.
113. Mheshimiwa Spika, ili kuondoa migongano ya kiutendaji na kuongeza ufanisi, Wizara itafanya mapitio ya Tamko la Uanzishwaji wa Wakala wa Misitu (Establishment Order No. 269 of 2011) ili kuihuisha na Sheria ya Misitu sura 323 na Sheria ya nyuki sura 224 ya sheria za Tanzania na nyaraka mbalimbali za kitaalamu katika usimamizi wa misitu ya hifadhi, hifadhi za nyuki, manzuki na mashamba ya miti.
(b) Kuimarisha Mipaka ya Misitu
114. Mheshimiwa Spika, Wakala utafanya soroveya, kufungua na kusafisha mipaka ya misitu yenye urefu wa kilomita 2,714. Aidha, maboya 200 na mabango 530 yatatengenezwa na kusimikwa kwenye mipaka ya misitu hiyo ili kutoa tahadhari kwa jamii juu ya hifadhi za misitu. Vilevile, mgawanyo wa viunga (compartmentation) utafanywa kwenye mashamba sita ya miti ya Sao Hill, Kawetire, Wino, Rubare, Buhindi na Rubya.
(c) Ukarabati wa maeneo yaliyoharibika
115. Mheshimiwa Spika, Wakala utakarabati vyanzo vya maji kwa kuondoa mimea isiyofaa kwenye eneo la ukubwa wa hekta 889 katika shamba la miti Sao Hill; kupanda miti hekta 772 kwenye maeneo yaliyoharibiwa ndani ya misitu ya hifadhi; kuongoa hekta 300 za maeneo ya misitu yaliyoharibiwa katika wilaya 12 pamoja na maeneo ya Delta ya Rufiji kwenye mikoko.
(d) Uendelezaji Mashamba ya Miti na
Ufugaji Nyuki
116. Mheshimiwa Spika, kazi zifuatazo zitafanyika katika mashamba 15 ya miti: kupanda miche 16,296,000 ya miti kwenye maeneo yenye jumla ya hekta 8,648; kupogolea miti kwenye eneo lenye ukubwa wa hekta 5,314.83; kukagua na kusimamia uvunaji wa miti yenye mita za ujazo 833,955 katika maeneo ya uvunaji ya ukubwa wa hekta 2,133; na kuongeza maeneo mapya yenye jumla ya hekta 43,000.
117. Mheshimiwa Spika, manzuki 40 zenye makundi ya nyuki 6,000 zitaanzishwa na kuendelezwa katika Kanda saba za Wakala; mizinga 10,000 ya nyuki itasambazwa katika Misitu ya hifadhi ya Sayaka (1000), Kinzi na Lowasi (2000) wilaya ya Njombe; Nkasi (2000) wilaya ya Nkasi; Patamela (1000), Lupa (1000) na Mbiwe (1000) wilaya ya Chunya na Hifadhi Asilia ya Kilombero (2000) wilaya ya Kilolo. Mafunzo ya shughuli za ufugaji nyuki kwa jamii zinazoishi kandokando ya misitu ya hifadhi ya New Dabaga, Iringa na Kalambo river, Rukwa yatatolewa.
(e) Ushirikishwaji Jamii katika Usimamizi
wa Rasilimali za Misitu na Nyuki
118. Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza dhana ya usimamizi shirikishi wa misitu, Wakala utafanya Tathimini ya rasilimali za misitu Kanda ya Magharibi ili kuandaa mipango ya usimamizi na mikataba ya makubaliano kwenye msitu mmoja utakaoteuliwa; kutoa mafunzo kwa Kamati nne za misitu za vijiji kuhusu mwongozo wa usimamizi wa misitu wa pamoja katika wilaya za Bagamoyo, Kisarawe, Kilosa na Kilombero, na kuhamasisha shughuli mbadala za kuongeza kipato kwa jamii kwenye vijiji saba vinavyozunguka hifadhi za mazingira asilia na hifadhi za misitu Kanda ya Kaskazini. Aidha, mapitio ya mipango miwili ya usimamizi yatafanyika na kutengeneza mipango mingine minane kwenye hifadhi za misitu na hifadhi za nyuki.
(f) Kuboresha Miundombinu katika
Hifadhi za Misitu.
119. Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa watumishi wanafanya kazi katika mazingira mazuri, Wakala unatarajia kujenga nyumba 10 za watumishi na ofisi tatu katika kanda saba za Wakala; kukarabati majengo 149; kutengeneza barabara zenye urefu wa kilomita 35 na kukarabati barabara zenye urefu wa kilomita 4,249.
(iv) Mfuko wa Misitu Tanzania
120. Mheshimiwa Spika, Mfuko unakadiria kukusanya jumla ya Shilingi 4,561,000,000 kutokana na vyanzo vyake. Mfuko utatoa ruzuku ya Shilingi 1,776,511,831 kwa ajili ya miradi 161 ya wadau mbalimbali wa misitu na ufugaji nyuki, kati ya miradi hiyo 69 itakuwa mipya. Wadau watakaonufaika na mpango huu ni pamoja na watu binafsi, vikundi vya jamii, Asasi za kijamii, Taasisi mbalimbali na Halmashauri za Wilaya.
(v) Wakala wa Mbegu za Miti
121. Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa upatikanaji wa mbegu bora za miti unakuwa endelevu Wakala utakusanya mbegu za miti kilo 12,500; na kukuza na kuuza miche 60,000 ya aina mbali mbali za miti. Aidha, Wakala utaanzisha vyanzo viwili vya mbegu bora za miti ya Mkaratusi na Mtiki. Vilevile, vyanzo vitano vya mbegu za miti ya kienyeji aina ya Mvule, Mkongo, Mtakowima, Mwiluti, Mninga, na Mpingo vitatambuliwa na kusajiliwa. Wakala pia utaendelea kutunza vyanzo 31 vya mbegu za miti ya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mfudufudu, Msindano, Mkangazi, Mtiki, Mwerezi, Mvule, Mninga, Mti kivuli, na Mwarobaini. Aidha, Wakala utaendesha mafunzo ya muda mfupi kuhusu kuanzisha bustani na kutunza miche ya miti kwa wadau mbalimbali humu nchini.
(vi) Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania
122. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Taasisi ya Utafiti itaendelea kuboresha mazingira na miundombinu ya utafiti kwa kuweka samani, vitendea kazi, vifaa vya utafiti na kujenga uwezo wa rasilimaliwatu. Aidha, Taasisi itaendeleza tafiti kuhusu uoteshaji wa miti asili iliyo katika hatari ya kutoweka (Mfano- Mloliondo) kwa kutumia biotekinolojia na kuboresha Mitiki kwa kutumia teknolojia ya “tissue culture”. Tafiti nyingine zitakazofanyika ni kuhusu mahusiano ya watu na misitu kufuatia mabadiliko ya mifumo ya usimamizi wa misitu nchini pamoja na vifanihisabati (Mathematical Models) za ukadiriaji wa hewa ukaa katika aina mbalimbali za misitu ya asili.
SEKTA NDOGO YA UTALII
(i) Sera na Sheria
123. Mheshimiwa spika, katika kukuza na kuendeleza utalii nchini Wizara itaendelea kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 kwa kujumuisha maoni ya wadau wa sekta. Vilevile, Wizara itaendelea kuhamasisha wakala wa biashara ya utalii kuhusu Kanuni zinazosimamia maendeleo ya utalii nchini.
(ii) Uendelezaji Utalii
124. Mheshimiwa spika, katika kuimarisha usimamizi na kuwa na mipango mizuri ya sekta ya utalii, Wizara itaendelea kufanya ukaguzi wa biashara za utalii na kutoa elimu juu ya uendeshaji wa biashara katika Kanda ya Ziwa, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Pwani, Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Magharibi. Pia, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kukusanya takwimu na kufanya soroveya zitakazohusu watalii wanaondoka nchini na wakala wa biashara za utalii.
(iii) Bodi ya Utalii Tanzania
125. Mheshimiwa Spika, Bodi itaendelea kushiriki kwenye maonesho sita ya ndani ambayo ni Sabasaba, Nanenane, Karibu Travel and Tourism Fair, Siku ya Utalii Duniani, Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar na Tamasha la Sauti za Busara ili kuutangaza utalii wa ndani. Aidha, Bodi itashiriki maonesho ya utalii ya kimataifa na misafara ya utangazaji utalii itakayofanyika Uholanzi, Hispania, Ujerumani, Uturuki, Uingereza, Australia, China, Urusi, Afrika ya Kusini, India, Brazil, Nchi za Ghuba na Italia.
126. Aidha, Wizara itaendelea kutumia mitandao ya kijamii kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii. Mikakati mingine itahusisha kuandaa Tamasha la Utalii wa Utamaduni kwa kushirikiana na Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo litakalokuwa likifanyika kila mwaka; kuandaa safari mbili za kupanda Mlima Kilimanjaro; kutangaza utalii kupitia michezo; kuendesha onesho jipya la Kimataifa la Utalii (Swahili International Tourism Exhibition). Wizara itafungua ofisi za uwakilishi kwa ajili ya kutangaza utalii nchini India na Ujerumani na kuendelea kuimarisha ofisi ya uwakilishi iliyoko nchini Marekani (the BradFord Group) pamoja na kuteua mabalozi wa hiari watatu nchini Marekani.
(iv) Wakala wa Chuo cha Taifa cha Utalii
127. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Chuo kitadahili wakurufunzi 312. Kati ya hao, wakurufunzi 240 katika fani ya ukarimu na 72 katika fani ya utalii. Vilevile, wakurufunzi hao 216 watakuwa katika ngazi ya Astashahada na 96 katika ngazi ya Stashahada. Aidha, Chuo kitaendelea na ukarabati wa hosteli mbili katika Kampasi ya Temeke na kuendelea kutekeleza mpango wake wa biashara ambapo kutokana na mpango huo mapato ya Chuo yanatarajiwa kuongezeka kutoka Shilingi 1,317,817,600 mwaka 2012/2013 hadi Shilingi 1,874,892,000 kwa mwaka 2013/2014.
SEKTA NDOGO YA MAMBO YA KALE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment