Na Rashid
Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Mapambano dhidi ya uzuiaji wa dawa za
kulevya nchini yanazidi kupamba moto baada ya jeshi la
Polisi Mkoani hapa kukamata gari lililokuwa na magunia sita ya bangi. Tukio
hilo lilitokea mwishoni mwa mwezi wa April muda wa saa 6:00 Mchana wilayani
Longido.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Sabas alisema tukio hilo
lilifanikiwa baada ya askari wa jeshi hilo kupata taarifa kutoka kwa raia wema
juu ya kuwepo kwa tukio la kusafirisha madawa hayo toka Longido Mjini kuelekea
Namanga.
Alisema askari walipopata taarifa
hiyo walianza kulifualia gari hilo aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili
T. 526 BWX na mara baada ya dereva wa gari hilo kugundua anafuatiliwa aliamua
kulitelekeza na kisha kukimbia.
“Mara baada ya askari kulifikia gari
hilo walilipekua na kukuta gunia sita za dawa za kulevya aina ya bangi zikiwa
nyuma ya siti ya gari na mpaka hivi sasa mmiliki wa gari hilo bado hajajulikana
na tunafanya juhudi za kumtafuta”. Alisema Kamanda Sabas.
Kamanda
Sabas aliwashukuru baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Arusha kutokana na
ushirikiano mzuri juu ya utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa jeshi
hilo hali ambayo inasaidia kuzuia vitendo vya uhalifu na kukamatwa kwa wahalifu
wa matukio mbalimbali.
Aliwasihi wakazi wa mkoa wa Arusha na mikoa ya
jirani kuendelea kushirikiana na jeshi hilo katika kupeana taarifa za uhalifu
na wahalifu ili kuweza kuzidi kuimarisha hali ya amani na utulivu nchini.
No comments:
Post a Comment