Thursday, July 25, 2013

MWANAMKE ALIYEDAIWA KUPANGA MAUAJI YA MTOTO NA MUMEWE AFIKISHWA MAHAKAMANI BAADA YA MAKACHERO WA POLISI KUMKAMATA MUUAJI BUKOBA, MWINGINE ATOROKA

Na Mwandishi Wetu, TANZANIASASA
Janeth Jackson anaedaiwa kupanga njama za kumuua mume wake ili arithi mali
MWANAMKE anayedaiwa kupanga njama za kumuua mumewe wa ndoa na mtoto wa
mumewe, jana amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya Arumeru, iliopo
Sekei, akiwa na mtuhumiwa mwingine wa mauaji hayo.

Watuhumiwa hao ni Janeth Jackson (32),mkazi wa Moshono jijini Arusha
na Novatus Elias, walifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha /Arumeru, Devotha Kamuzora na
kusomewa makosa mawili ya kula njama ya kutaka kumwua Simon Jackson
ambaye ndiye mume wa Janeth.


Mwendesha Mashitaka wa Serikali,Edna Kasala alidai mahakamani hapo
kuwa, washitakiwa wote wawili, walitenda kosa la pili ya kula njama na
kutaka mumuua Desderi Sabas, ambaye ni mtoto wa nje wa mume huyo
anayeishi Bukoba mkoani Kagera.

Washitakiwa  wote hawakutakiwa kujibu lolote mahakamani hapo, kwa
sababu Mahakama hiyo kisheria haina mamlaka ya kusikiliza kesi za
mauaji.


Mwendesha Mashitaka huyo wa serikali iliiomba mahakama kuwanyima
dhamana, watuhumiwa kwa sababu watuhumiwa wengine wawili katika kesi
hiyo bado wanatafutwa na hivyo kuwapa dhamana, kunaweza kuharibu
upelelezi ambao bado haujakamilika na washitakiwa hao wakatokomea
kusikojulikana.


Alisema kutokana na uzito wa tuhuma hizo, maombi hayo ya kuwanyima
dhamana watuhumiwa yameambatana na hati ya kiapo ya Mkuu wa Upelelezi
wa Makosa ya Jinai mkoani Arusha, akisisitiza kutowapa dhamana, licha
ya makosa hayo kuwa na dhamana.


“Mheshimiwa tunafahamu kwamba dhamana ni haki ya kikatiba ya kila
mtu,lakini kutokanana mazingira ya kesi hii kuwa magumu tunaomba
dhamana isitolewe, ili kuwatafuta watuhumiwa wengine wa kesi hii, na
hawa wasikimbie pia,’alisema MwendaMashitaka huyo.

Kwa upande wake,Wakili wa Utetezi,Fidelis Peter alipinga maombi hayo
na kutaka mahakama itoe dhamana kwa washtakiwa, kwa sababu ni haki yao
ya kikatiba na kuwa hilo lilikuwa kosa lao la kwanza.

Alitoa sababu nyingine ya kupinga maombi ya upande wa mashitaka kwamba
sababu kuwa watuhumiwa wanaweza kuvuruga upepelezi akiachiwa, kuwa si
za msingi kwa ni watu wanaoaminika katika jamii.

“Mheshimiwa sababu za kuwanyima dhamana watuhumiwa hazina uzito wowote
pia mshitakiwa wa kwanza(Janeth) ana mtoto wa miezi sita na tangu
akamatwe alhamisi iliyopita hajamwona wala kumnyonyesha mwanaye  hivyo
anastahili kupewa dhamana,”alisema Wakili Peter.


Hata hivyo,baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili. Hakimu
Kamuzora alikubaliana na maombi ya upande wa mashitaka na kuamuru
watuhumiwa warejeshwe ndani, hadi Agosti 5,mwaka huu,kesi hiyo
itakapotajwa tena.

“Kutokana na uzito wa kesi hii, nakubaliana na hati ya kiapo ya Mkuu
wa Upelelezi ya kutowapa dhamana hadi hapo itakapobidi kufanya hivyo,
hivyo naomba mshitakiwa awe chini ya ulinzi,”alisema kamuora.

Katika kesi hiyo iliyovuta hisia watu wengi jijini hapa,inadaiwa kuwa
Janeth alitaka kumwua mumewe ambaye ni mfanyabiashara ya madini
Ya tanzanite na mwanaye wa kiume ili arithi mali na utajiri alionao
mfanyabiashara huyo.

Akiwa amejifunika uso muda wote alipokuwa mahakamani, Janeth
alionekana kuwa na mawazo mengi na macho mekundu kwa sababu ya kulia
baada ya njama hizo kugonga mwamba

Hata hivyo nje ya Mahakama hiyo, habari za uhakika zilizopatikana
kutoka ndani ya familia hiyo, zimedai mshitakiwa huyo ana watoto
wawili ambao, mmoja ana miaka mitatu na mdogo ana miezi tisa na siyo
sita kama alivyodai Wakili wa utetezi.

TAARIFA YA AWALI YA POLISI

JESHI la Polisi jijini hapa limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja kati ya wawili waliyedaiwa kuagizwa na Janeth Jackson kufanya mauaji ya mume wake ambae ni Mfanyabiashara wa madini jijini hapa Jackson Kaijage pamoja na mtoto wake wa kiume aliyezaa na mfanyabiashara huyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa jiji la Arusha, Liberatus Sabas, mtuhumiwa huyo Novatus Elias Mrisha(35) alikamatwa na makachero wa jeshi hilo katika mji wa Bukoba Mkoani Kagera akiwa katika hatua za mwisho za kutekeleza mauaji hayo huku
mtuhumiwa mwingine akitoroka.

Kamanda Sabas alisema kuwa baada ya jeshi hilo la polisi kupata taarifa ya uwepo wa mpango wa mauaji hayo, Julai 17 mwaka huu jeshi hilo lilituma makachero wake Bukoba kufuatilia wauaji hao na kuwanasa.

Alisema makachero hao walifika Julai 18 mwaka huu na ilipotimu saa 4.00 usiku wauaji wakiwa katika harakati za mwisho za kutekeleza mauaji kwa mtoto huyo wa kiume wa Jackson anayeishi mjini humo walifanikiwa kumnasa mtuhumiwa mmoja aliyetajwa kwa jina la Novatus Elias Mrisha (35).

“ Julai 18 mwaka huu saa 4.00 usiku kikosi cha askari waliotumwa kutoka Arusha kwa kushirikiana na askari Polisi Mkoani Kagera waliweza kumkamata mtuhumiwa mmojawapo kati ya watuhumiwa wawili waliokuwa wamekwenda Bukoba kutekeleza mpango wa mauaji ambapo mtuhumiwa Novatus mkazi wa moshono alikamatwa na mtuhumiwa mwingine alifanikiwa kutoroka,”alisema Sabas.

Kamanda Sabas alisema kuwa mpango huo wa mauaji ulipangwa kufanyika  katika miji ya Bukoba kwa wauaji kumuua mtoto wa mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 12 pamoja na ndugu zake kadhaa na baadae kumalizia mpango huo wa mauaji kwa kumuua mume wake Jackson Kaijage
maarufu kwa jina la ‘Jackson Manjuruu’ jijini Arusha.

Kamanda Sabas alisema baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa na kuhojiwa alikiri kuhusishwa katika mpango huo wa mauaji na kumtaja mke wa mfanyabiashara huyo kuwa ndiye aliyewatuma kwenda kutekeleza mpango huo.

“Mke wa mfanyabiashara huyo aitwaye Janeth Jackson (32), mkazi wa Moshono amekamatwa na anaendelea kuhojiwa, watuhumiwa wote hao wawili watafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika,”alisema Kamanda Sabas.

Kwa mujibu wa taarifa za awali zilidai kuwa Janeth Jackson alipanga kumuua mumewe huyo kwa lengo la kurithi mali walizokuwa nazo ikiwa ni pamoja na kuwaua mtoto wake na ndugu zake wa karibu .

Wakati huo huo, Kamanda Sabas alisema kwa jeshi hilo limekamata dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilo 50 zilizokuwa zikisafirishwa na gari aina ya Nissan Mingroad namba za usajili
T904 BSJ kutokea eneo la Unga limited kuingia katikati ya mji.

Sabas alisema kuwa jeshi hilo lilipata taarifa ya kubebwa mirungi ndani ya gari hilo na kuweka mtego ili kuwanasa watuhumiwa lakini hata hivyo walifanikiwa kukamata dawa hizo pekee kufuatia watuhumiwa waliokuwa wakiendesha gari hilo kulitelekeza gari na kukimbia kusikojulikana.

Wednesday, July 24, 2013

ALIYEFANYA MAUAJI YA MCHIMBAJI TANZANITE ONE AKAMATWA, SERIKALI YAFUNGA MIGODI MINNE KUPISHA UCHUNGUZI




Na Mwandishi Wetu, Arusha

WAKATI Mmiliki wa mgodi uliodaiwa kutobozana na mgodi wa Tanzanite One,  Joseph Mwakipasile ‘Chusa’ akishikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano kuhusu mauaji ya mfanyakazi wa Kampuni ya Tanzanite One, Willy Mushi, wizara ya Nishati na Madini imefunga migodi minne ya wachimbaji wadogo inayopakana na mgodi wa kampuni hiyo kupisha uchunguzi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa aliwaambia waandishi wa habari eneo la Mirerani jana kuwa jeshi hilo linamshikilia  Mwakalinga katika kituo cha polisi Mirerani kwa mahojiano baada ya kutajwa na wafanyakazi wa Tanzanite One kuwa mhusika wa mauaji ya mwezao.

Marehemu Mushi aliyeacha mjane na watoto wanne aliuawa kwa kupigwa risasi mbili kifuani Saa 6:00 usiku wa kuamkia Julai 20, mwaka huu alipokuwa zamu ya usiku na mfanyakazi mwenzake, Kennedy Msambaji.

“Polisi tunamshikilia Chusa kwa mahojiano baa ya kutajwa kuhusika na tukio la mauaji ya Willy Mushin a tunawaomba wote wenye taarifa za kuhusika kwake na mauaji haya kujitokeza kusadia polisi kukamilisha upelelezi ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake,” alisema Kamanda Mpwapwa.

Kwa upande wake, Kamishina wa madini Kanda ya Kaskazini, Benjamin Mchwampaka alitangaza kuyafunga migodi mine ya wachimbaji wadogo kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi wa tukio la mauaji.

Akizungumza mbele ya mamia ya wafanyakazi Tanzanite One ambao tangu juzi wamekusanyika katika eneo maalum la mikutano ya kampuni hiyo karibu na bwalo lao la chakula, Kamishina Mchwapaka alitaja miongoni mwa migodi iliyofungwa kuanzia jana kuwa ni ya Joseph Mwakalinga ‘Chusa’ anayeshikiliwa na polisi kwa mahojiano kuhusu mauaji hayo.

Wachimbaji wadogo Abdurahakim Mulla, Jackson Simon na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Maningoo ambao migodi yao yapo kitalu “D” pia wamejikuta migodi yao ikifungwa kutokana na uamuzi huo wa serikali kwa sababu inapakana na mgodi wa mwekezaji.

“Timu maalum ya wachunguzi kutoka Wizara ya Nishati na Madini inatarajiwa kuwasili Mirerani kati ya leo na kesho tayari kuanza uchunguzi wa tukio hilo na kubaini migodi yote ya wachimbaji wadogo waliovamia mgodi wa Tanzanite One,” alisema Kamishina Mchwampaka.

Alisema baada ya uchunguzi huo, serikali itaendesha oparesheni maalum kuwaondoa wachimbaji wote waliovamia eneo la mgodi wa Tanzanite One huku akiwataka wote waliovamia eneo la mwekezaji kuondoka wenyewe kwa hiari kabla ya oparesheni.

Hata hivyo, Kamishina huyo alisema mipaka ya migodi eneo la Mirerani ina utata mkubwa, hasa chini ya ardhi kutokana naugwaji uliofanyika miaka ya tisini kutozingatia mahitaji halisi na sheria kwa wachimbaji kugawiwa maeneo madogo yasiyolingana na taratibu za uchumbaji madini ya vito.

Kuhusu usalama kipindi hiki cha mpito cha uchungzi na hali tete ya mahusiano kati ya wachimbaji wadogo na mwekezaji wa Tanzanite One, Kamishina Mchwampaka aliutaka uongozi wa kampuni hiyo kuchukua tahadhari wakati wafanyakazi wake wanaingia chini ya ardhi mgodini ili kuepuka madhara zaidi wakati serikali inaendelea na taratibu zingine za kisheria.

Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi migodini (TAMICO), Raphael Ombade alisema  wafanyakazi wamekubaliana kusitisha mgomo wao uliodumu kwa siku tatu na kuahidi kurejea kazini kuanzia leo baada ya serikali kusikia kilio chao na kuchukua hatua kuhusu mauaji ya mfanyakzi mwezao.

Aidha uchunguzi wa mwili wa marehemu Mushi uliofanywa jana na madakatari na jeshi la polisi kwa kushirikiana ndugu ulibainisha kuwa kifo cha marehemu kilitokana na kupigwa risasi mbili kifuani ambazo zilipatikana mwilini mwake.

Monday, July 22, 2013

WILAYA YA HAI YAINGIA USHIRIKIANO WA MAENDELEO NA SWEDEN

Meya wa manispaa ya Arvidsjaur,Jerry Johqnsson(Katikati) akifafanua jambo baada ya kumalizika itifika ya kusaini makubaliano na hamashauri ya wilaya ya Hai,anayeshuhudia ni mwenyekiti wa halmashauri Clement Kwayu

Viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai na wale wa Manispaa ya Arvidsjaur katika kusainiana makubaliano ya ushirikiano

Watendaji wa Manispaa ya Arvidsjaur na halmashauri ya wilaya ya Hai wakibadilishana mkataba wa ushirikiano

Mratibu wa mipango ya maendeleo ambaye pia ni diwani katika manispaa ya Arvidsjaur,Stina Johansson(tatu Kulia) akiwa na ujumbe wa viongozi kutoka wilayani Hai-kutoka kulia,Novats Makunga(Mkuu wa wilaya),Clement Kwayu(Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya),Melkizedeck Humbe(Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri) na Ester Mbatiani ambaye ni afisa mipango mkuu wa Halmashauri
Na Richard Mwangulube,Hai


Halmashauri ya wilaya ya Hai,imeingia mkataba wa miaka minne wa ushirikiano na Manispaa ya Arvidsjaur  nchini  Sweden  unaolenga katika maeneo ya kiuchumi na kijamii ukiwemo wa teknolojia ya kisasa ya udhibiti wa takataka kiuchumi kwa kuziwezesha kutengezwa upya bidhaa kwa ajili ya matumizi.

Mkataba huo ulitiwa saini  wakati wa ziara ya ujumbe wa viongozi  wa wilaya ya  Hai uliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya Hiyo, Novatus Makunga hivi karibuni katika  makao Makuu ya Manispaa hiyo nchini Sweden.

Wajumbe wengine Katika ziara hiyo ya siku tano ambao ndiyo waliosaini mkataba huo ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri  ya Wilaya ya Hai Clement Kwayu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Melkizedeck Humbe pamoja na Afisa Mipango   wa Halmashauri Ester Mbatian.

Kufuatia  mkataba huo, Halmashauri ya Wilaya ya Hai itapaswa  kuandaa na kuwasilisha katika Manispaa ya Arvidsjaur  miradi mbalimbali inayolenga katika Nyanja za biashara na  viwanda vidogo na vya kati.

Maeneo mengine ya shirikiano huo ni pamoja na  elimu na utoaji wa taarifa, uboreshaji   na usimamizi  wa mazingira endelevu pamoja na miradi inayolenga   masuala ya  ajira  kwa vijana.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Hai mwishoni mwa wiki,Makunga  amesema kadhalika ushirikiano ho unalenga  katika kuimarisha  shughuli  mbalimbali zinazohusiana na masuala ya sekta ya utalii na utawala bora kuanzia ngazi ya chini kabisa.

“Kwa kushirikiana na wenzetu tunaandaa mkakati wa kuimarisha mafunzo kwa  jamii katika masuala ya uchumi na  shughuli za maendeleo ya Kijamii na lengo kubwa zaidi ni kwa kundi la vijana”. Amefafanua Makunga.

Ameeleza kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Sweden[SIDA] ushirikiano huo pia   utatoa fursa kwa Manispaa ya Arvidsjaur kushirikiana na wilaya ya Hai katika ujenga uwezo kwa halmashauri juu ya namna ya kupata taarifa mbalmbali za maendeleo  na kiuchumi kutoka maeneo ya vijijini nakuzifanyia kazi.

Amesema pia ushirikiano huo umelenga katika kuhakikisha halmashauri ya Hai inaingia katika mfumo wa kisasa wa namna ya kusimamia  ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za maendeleo, kuboresha mawasiliano na wadau mbalimbali  ikiwemo kupitia kituo cha halmashauri hiyo cha redio  Boma FM.

Amesemasa Manispaa  hiyo ya Sweden  itasaidia  katika ujenzi,uboreshaji na uendelezaji wa  kituo cha  mafunzo kwa ajili ya  maendeleo ya jamii katika wilayani Hai pamoja na kusaidia  katika kuboresha huduma za afya.

Masuala mengine yatakayotekelezwa  kutokana na mahusiano hayo  ni pamoja na Manispaa ya Arvidsjaur kusaidia katika teknolojia ya urudufishaji wa taka ambapo unawezesha taka ngumu na taka maji kuweza kutumika tena.

Makunga amesema kuwa suala la udhibiti wa takataka ni changamoto kubwa katika mji wa Hai ambao hauna dampo huku kukabiliwa na ongezeko la kasi la watu wanaopenda kuweka makazi ya kuishi na kuendesha shughuli zao za kazi Arusha,Moshi,Siha na Simanjiro.

“Kwa wenzetu taka ni rasilimali, inachambuliwa kuanzia ngazi ya familia na kupelekwa eneo la kutupa taka, kwa kupangwa kuangalia na aina, na hutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali vikiwemo vikombe, vijiko, sahani na umeme pamoja na mafuta ya kulainishia vyuma kutumika upya,”amefafanua.

Ametaja mengine ambayo yatatiliwa mkazo kutokana na ushirikiano huo ni pamoja na  Manispaa hiyo kusaidia katika kukuza uchumi na kuimarisha miundo mbinu ya kiuchumi.

Makunga ameeleza kuwa manispaa hiyo ambayo inamiliki uwanja wa ndege wa kimataifa imeonyesha kuvutiwa kusaidia uimarishaji wa  uwanja wa kimataifa wa Kilimanjaro(KIA)  uliopo wilayani Hai kwa kuongeza  shughuli za  biashara za Anga pamoja na kuboresha miundo mbinu katika Uwanja huo.

Ujumbe huo uliweza kupata taarifa juu ya shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Manispaa hiyo zikiwemo za kuchumi, kijamii pamoja na usimamizi bora  wa ukusanyaji na matumizi ya Mapato.

Kwa mujibu wa nchi ya Sweden, Mamlaka zote  za Serikali za Mitaa zinajulikana kama Manispaa zinaongozwa kwa sheria ya bunge la nchi hiyo ambapo hivi sasa kuna Manispaa zipatazo 260 nchini Sweden
 
Manispaa hizi zinawajib wa kusimamia  masuala ya  elimu kuanzia ngazi ya chekechea hadi Sekondari pamoja na kujenga na kusimamia vituo vya malezi ya  wazee na wasiojiweza.

Kadhalika manispaa hizi zinawajibu wa  kusimamia vituo vya zimamoto na uokoaji,kusimamia ujenzi  na uendeshaji  wa viwanja vya ndege,kusaidia walemavu pamoja na kuunganisha wajiri na waajiriwa

Pia Makunga ameeleza kuwa Manispaa hizi zinajukumu la kusimamia vituo vya  elimu ya ujasirimali kwa vijana na masuala ya Utalii ambapo  Sweden kila siku hupokea watalii zaidiya 500,000 wanaotembelea vivutio mbalimbali katika Manispaa hizo kutoka nchi za ulaya.

Sunday, July 21, 2013

UFUGAJI BORA NYUMBANI KWA MKURUGENZI WA TANZANIASASA BLOG





MORANI ANUSURIKA KUCHAPWA MBOKO 7O, NI BAADA YA KUKIRI KUWACHAFUA WAZEE WA KIMILA 'MALAIGWANAN' KWENYE MITANDAO YA KIJAMII


Na Mwandishi Wetu, Tanzaniasasa
ARUSHA

KIJANA mmoja wa jamii ya kimasai Lomayani Mitewasi juzi alinusurika  kupewa adhabu ya kuchapwa viboko 70 aliyokuwa apewe na viongozi wa jamii  hiyo baada ya kutuhumiwa kusambaza taarifa  ya uongo kwenye  mitandao ya kijamii.

Adhabu nyingine aliyokuwa apewe kijana huyo ambaye ni mkazi wa kata ya Elerai  ni pamoja na kulipa ng’ombe dume  kwa kosa la kukiuka mila za kimasai kwa kutoa taarifa za uongo

Mwenyekiti wa MAA akizungumza katika kikao hicho
Kufuatia hali hiyo Mitewasi alilazimika kusimama mbele ya wazee hao wa kimila(Malaigwanani) ikwa ni pamoja na kukiri kuwa taarifa hizo ni za uongo na kwamba amekiuka mila za jamii hiyo kwa kuandika taarifa za ungo katika mitandao ya kijamii

“Wazee wangu naomba mnisamehe nilighafilika ninakiri  kuandika habari za uongo katika mitandao hiyo mimi binafsi sikijui kimasi huwa nina sikia neo mojamoja tuu japo nilikuwepo kwenye mkutano uliopita sikujua hata mlizungumza nini kwa kuwa mlikuwa mnazungumza kilugha”

Kwa mujibu wa kijana huyo mbele ya malaigwanani alisema kuwa aliandika kuwa malaigwanani wagawanyika katika makundi mawili moja linatetea CCM na Lingine CHADEMA jambo ambalo ni uongo

Pia aliandika Naibu waziri wa Ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Goodluck Ole Medeye amewatumia malaigwanani kuvuruga uchaguzi mdogo wa Arusha

Mitewasi pia aliandika kuwa kikao hicho kililenga kubagua wakazi wa Arusha kwa tofauti za makabila yao, alilazimika kufuta kauli yake hiyo na kuomba radhi mbele ya Malaigwanan hao kwa kile alichodai alighafilika

Awali akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana, Katibu wa Baraza la MAA, Amani Lukumay alisema kuwa wazee hao wamesikitishwa sana na taarifa hizo za uongo  ambazo zilisambazwa katika mitandao ya kijamii ambayo ina lengo la kuvuruga amani ya jiji la Arusha lakini pia kuwagawanya wazee hao

Lukumay alisema kuwa lengo la kukutana kwa wazee hao wiki iliyopita ililikuwa na lengo la kuzungumzia amani ya katika mkoa wa Arusha na kwamba hakuna kitu kingine lichozngumzwa katika kikao hicho

“Onyo hili halilengi chama chochote cha siasa, bali tunavionya vyama vyote vinavyofanya shughuli za kisiasa Arusha kwa sababu Malaigwanan hatufungamani na itikadi za vyama kwani miongoni mwetu wamo wanachama wa vyama tofauti vya kisiasa,” alisema Amani.

Katibu huyo alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya Malaigwanan hao waliokutana kwenye kikao cha Julai 12, mwaka huu katika eneo lao maalum ya ibada za jadi lililoko ndani ya   Chuo cha Ufundi Arusha(ATC), kudaiwa kutoa kauli zenye muelekeo wa kisiasa unaolenga kukinufaisha CCM dhidi ya Chadema.

Wakati huo huo wazee hao waliwataka waandishi wa habari kuzingatia maadili ya kazi yao kutokana na baadhi ya magazeti kuandika taarifa za uongo juu ya kikao cha mila.

waliwataka walioandika taarifa hizo kukanusha ili kuuhabarisha umma ukweli wa kilichozungumzwa na kuitoa  doa jamii hiyo dhidi ya jamii zingine kama ilivyoripotiwa katika vyombo hivyo.

MASABURI ATETEA ULAJI WA WABUNGE, MADIWANI, YAITAKA TUME YA KATIBA KUONDOA UKOMO WA WAO KUONGOZA



 Na Mwandishi Wetu, Tanzaniasasa
JUMUUIYA ya Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (ALAT), imepinga kipengele kinachotaka kuwepo kwa ukomo wa nafasi za uongozi wa kuchaguliwa na wananchi ikiwemo ubunge na udiwani.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi katika ukumbi wa ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Arusha, Mwenyekiti wa ALAT Didas Masaburi alisema jumuiya hiyo inapinga sura hiyo kwa kile alichodai kufanya hivyo ni kuwanyima haki wananchi wanaotaka kiongozi husika kuendelea kuwaongoza.

Alisema kabla ya kuwasilisha maoni yao kwenye tume hiyo walifanya mazungumzo na wananchi kupitia madiwani katika kata wanazowakilisha ambao wengi wao walitoa maoni wakitaka kutokuwepo kwa kipengele cha ukomo wa uongozi na badala yake wananchi waachiwe wenyewe kuamua kama wanamuhitaji kiongozi husika au la.

“ ALAT tuliwasilisha tume maoni 13 yaliyoelezwa kwa undani matakwa ya wananchi katika katiba mpya lakini cha kushangazwa tume imeweka maoni yake yenyewe na kutupilia mbali maoni yetu, hata hivyo bado hatujachelewa tutapeleka tena kwa mara nyingine maoni haya kupitia marekebisho ya rasimu hii ya awali,”alisema Masaburi.

Alisema maoni mengine waliyoyawasilisha katika tume hiyo ni pamoja na kutaka katiba iweke sura itakayobainisha namna ambavyo madaraka yatapelekwa kwa wananchi, kutamka katika katiba mpya uwepo wa Serikali za mitaa chini ya mfumo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nyingine ni pamoja na kutamka kazi na majukumu ya Serikali za Mitaa, uwezo wa kujiamulia mambo yao tofauti na hivi sasa kila kiongozi katika wizara amekuwa akiamua anavyopendelea yeye, namna mawasiliano yatakuwa baina ya Serikali kuu na Serikali za mitaa.

“ Pia tumependekeza kuwepo kwa kipengele kitachoonyesha namna viongozi wa Serikali za mitaa watakavyopatikana ili kuweka uwajibikaji wa viongozi hao ikiwemo kuchaguliwa na wananchi moja kwa moja katika eneo husika, benki kuu pia tunataka iwepo tu ya jamhuri isiwe kama ilivyo hivi sasa pamoja na idara ya uhamiaji kuingizwa katika eneo la Jamhuri,”alisema.

Masaburi alisema endapo Serikali za mitaa hazitaingizwa kwenye Katiba mpya tabaka la wenye nacho na wasiokuwa nacho litakuwa kubwa na matokeo yake ni ongezeko kubwa la watanzania masikini.

Alitoa wito kwa madiwani kote nchini kutumia nafasi ya kupitia rasimu mpya kuwaelimisha wananchi katika maeneo yao umuhimu wa uwepo wa sura inayoelezea serikali za mitaa.

Alisema Serikali za mitaa ndio ambazo zimekuwa mtetezi mkubwa wa wananchi katika suala la maendeleo kufuatia wao kusimamia fedha ambazo zimekuwa zikipatikana kupitia kodi inayokusanywa na Serikali kuu.

Masaburi alisema katika kikao walichofanya hivi karibuni jijini Arusha cha kupitia rasimu hiyo mpya ya Katiba wamekubaliana kabla ya Agosti 31 mwaka huu kuwasilisha maoni yao waliyoyawasilisha hapo awali katika tume hiyo.

JIJI LA ARUSHA KUNUNUA GREDA KUDHIBITI BARABARA KOROFI



Na Mwandishi Wetu, Tanzaniasasa 

HALMASHAURI ya Jiji la Arusha inakusudia kununua magreda na vifaa mbalimbali vya ujenzi wa barabara ili kujijengea uwezo wa kujenga na kuhudumia barabara zake kwa wakati na gharama nafuu.

Akizungumza katika mahojiano maalum ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita, Meya wa Jiji la Arusha, Mstahiki Gaudance Lyimo alisema kwa kuanzia, halmashauri itanunua magreda mawili na rola mbili ifikapo Agosti mwaka huu.

“Fedha kwa ajili ya ununuzi wa Magreda haya mawili na rola tayari tumepata. Tunaendelea kufanya majadiliano na wahusika ili tuweze kupata zana na vifaa vingine kwa njia ya mkopo nafuu ili Jiji liwe na uwezo kamili wa kujenga na kuhudumia barabara zake,” alisema Mstahiki Lyimo.

Katika mpango huo wa kuboresha miundombinu ya barabara, Jiji la Arusha pia linakusudia kuanzisha ujenzi wa barabara za mawe ambazo licha ya kuwa imara lakini pia ujenzi wake hutoa fursa ya ajira kwa vijana wengi watakaohusika katika ukusanyaji na urandazaji wa mawe hayo.

“Wenzetu wa Jiji la Mwanza na Kigali nchini Rwanda tayari wamefanikiwa kujenga barabara za mawe, kwanini sisi tushindwe,” alisema na kuhoji Meya Lyimo.

Alisema mpango huo ukitelezwa kwa mafanikio, kata zote 19 za Jiji la Arusha aidha zitakuwa na barabara za lami au za mawe na hivyo kurahisisha mawasiliano na kuwaondolea adha wananchi wa barabara kutopitika nyakati za masika.