Sunday, July 21, 2013

Shule ya D’Alzon iliyoungua yaomba msaada



Na Mwandishi Wetu, Tanzaniasasa

UONGOZI wa shule ya sekondari ya wasichana ya D’Alizon inayomilikiwa na shirika la watawa wa kanisa katoliki la Assumption wamewaomba wasamaria wema  kuwasaidia kujenga upya bweni la shule hiyo lenye vyumba nane lililoteketea kwa moto wiki moja iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi shuleni hapo, Meneja wa shule hiyo Sista Leah Kavugho alisema ujenzi wa bweni hilo umekadiriwa kugharimu milioni 350 na hadi sasa wamefanikiwa kupata shilingi milioni 2.3 kutoka kwa wasamaria wema.

“ Pia tumefanikiwa kupata msaada wa mifuko 150 ya saruji na lori nne za mchanga kutoka kwa diwani wa kata ya Mlangarini, Mathias Manga na msaada wa magodoro 13 kutoka katika kampuni ya Tanform pamoja na mashirka mbalimbali ya masista jimbo kuu katoliki Arusha,”alisema. 

Kivugho ambaye pia ndie mkuu wa Shirika la Assumption Tanzania alisema kwa sasa uongozi wa shule umelazimika kuomba msaada wa malazi kwa wanafunzi wake 118 wa vidato vya kwanza hadi tatu katika shule ya  watoto yatima ya St.Judy watakapotumia kwa muda wiki saba kuanzia jana shule hiyo ilipofunguliwa baada ya kufungwa kwa muda wa wiki moja kutokana na tukio hilo la moto.

Alisema mbali ya msaada huo wa kulaza wanafunzi wa shule hiyo, pia St. Jude kupitia kwa mmiliki wake, Gamma Sisiac imetoa  msaada wa shuka 300 kwa ajili ya wanafunzi 32  wa kidato cha nne ambao watakaolala kwenye jengo la bwalo la chakula wakati juhudi za kupata ufumbuzi wa kudumu wa ujenzi wa bweni shuleni hapo ukiendelea.

“ Pia St Jude imetoa msaada wa usafiri wa kuwachukua na kuwarejesha shuleni wanafunzi wote waliopata hifadhi kwenye mabweni yao ambapo watawachukua kwa magari yao asubuhi kuwaleta shuleni na jioni watawafuata kutoka shuleni kuwapelekea,”alisema.

Ujenzi wa bweni lililoteketea uligharimu zaidi ya milioni 250 huku thamani ya vifaa na mali za wanafunzi zilizotekezwa kwa moto huo unaosadikiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme ikikadiriwa kuwa zaidi ya milioni 59

Mkuu wa shule hiyo Sista Irene Mekuta alisema janga hilo siyo tu limewaathiri walimu na wanafunzi kwa kupoteza mali zikiwemo madaftari, Vitabu, nguo, masanduku, viatu na fedha taslimu, bali pia imewaletea madhara makubwa ya kisaikolojia ndio maana uongozi ulifikia uamuzi wa kuwapa likizo ya wiki moja kuwasahaulisha na mazingira ya tukio.

Aliwashukuru wananchi wanaoishi maeneo jirani kwa msaada wao uliosadia kuokoa baadhi ya vitu na kuomba wasamaria wema na wote wenye mapenzi mema kujitokeza kusaidia shule hiyo kwa njia yoyote ikiwemo michango ya fedha.

Shule hiyo tayari imetuma maombi ya misaada mbalimbali kwa Taasisi, Mashirika na watu binafsi ikiwemo TANAPA, TRA, AtoZ, Spanish Tiles, Chuo Kikuuu cha Nelson Mandela, Makampuni ya simu za kiganjani na benki zote zenye matawi Jijini Arusha.

No comments: