Na Mwandishi Wetu, Arusha
WAKATI Mmiliki wa mgodi uliodaiwa kutobozana na mgodi wa Tanzanite One, Joseph
Mwakipasile ‘Chusa’ akishikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano kuhusu mauaji
ya mfanyakazi wa Kampuni ya Tanzanite One, Willy Mushi, wizara ya Nishati na
Madini imefunga migodi minne ya wachimbaji wadogo inayopakana na mgodi wa
kampuni hiyo kupisha uchunguzi.
Kamanda wa polisi mkoa wa
Manyara, Akili Mpwapwa aliwaambia waandishi wa habari eneo la Mirerani jana
kuwa jeshi hilo linamshikilia Mwakalinga
katika kituo cha polisi Mirerani kwa mahojiano baada ya kutajwa na wafanyakazi
wa Tanzanite One kuwa mhusika wa mauaji ya mwezao.
Marehemu Mushi aliyeacha mjane na
watoto wanne aliuawa kwa kupigwa risasi mbili kifuani Saa 6:00 usiku wa kuamkia
Julai 20, mwaka huu alipokuwa zamu ya usiku na mfanyakazi mwenzake, Kennedy Msambaji.
“Polisi tunamshikilia Chusa kwa
mahojiano baa ya kutajwa kuhusika na tukio la mauaji ya Willy Mushin a
tunawaomba wote wenye taarifa za kuhusika kwake na mauaji haya kujitokeza
kusadia polisi kukamilisha upelelezi ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake,”
alisema Kamanda Mpwapwa.
Kwa upande wake, Kamishina wa
madini Kanda ya Kaskazini, Benjamin Mchwampaka alitangaza kuyafunga migodi mine
ya wachimbaji wadogo kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi wa tukio la
mauaji.
Akizungumza mbele ya mamia ya
wafanyakazi Tanzanite One ambao tangu juzi wamekusanyika katika eneo maalum la
mikutano ya kampuni hiyo karibu na bwalo lao la chakula, Kamishina Mchwapaka
alitaja miongoni mwa migodi iliyofungwa kuanzia jana kuwa ni ya Joseph
Mwakalinga ‘Chusa’ anayeshikiliwa na polisi kwa mahojiano kuhusu mauaji hayo.
Wachimbaji wadogo Abdurahakim
Mulla, Jackson Simon na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Maningoo ambao
migodi yao yapo kitalu “D” pia wamejikuta migodi yao ikifungwa kutokana na
uamuzi huo wa serikali kwa sababu inapakana na mgodi wa mwekezaji.
“Timu maalum ya wachunguzi kutoka
Wizara ya Nishati na Madini inatarajiwa kuwasili Mirerani kati ya leo na kesho
tayari kuanza uchunguzi wa tukio hilo na kubaini migodi yote ya wachimbaji
wadogo waliovamia mgodi wa Tanzanite One,” alisema Kamishina Mchwampaka.
Alisema baada ya uchunguzi huo,
serikali itaendesha oparesheni maalum kuwaondoa wachimbaji wote waliovamia eneo
la mgodi wa Tanzanite One huku akiwataka wote waliovamia eneo la mwekezaji
kuondoka wenyewe kwa hiari kabla ya oparesheni.
Hata hivyo, Kamishina huyo
alisema mipaka ya migodi eneo la Mirerani ina utata mkubwa, hasa chini ya ardhi
kutokana naugwaji uliofanyika miaka ya tisini kutozingatia mahitaji halisi na
sheria kwa wachimbaji kugawiwa maeneo madogo yasiyolingana na taratibu za
uchumbaji madini ya vito.
Kuhusu usalama kipindi hiki cha
mpito cha uchungzi na hali tete ya mahusiano kati ya wachimbaji wadogo na
mwekezaji wa Tanzanite One, Kamishina Mchwampaka aliutaka uongozi wa kampuni
hiyo kuchukua tahadhari wakati wafanyakazi wake wanaingia chini ya ardhi
mgodini ili kuepuka madhara zaidi wakati serikali inaendelea na taratibu
zingine za kisheria.
Mwenyekiti wa chama cha
wafanyakazi migodini (TAMICO), Raphael Ombade alisema wafanyakazi wamekubaliana kusitisha mgomo wao
uliodumu kwa siku tatu na kuahidi kurejea kazini kuanzia leo baada ya serikali
kusikia kilio chao na kuchukua hatua kuhusu mauaji ya mfanyakzi mwezao.
Aidha uchunguzi wa mwili wa
marehemu Mushi uliofanywa jana na madakatari na jeshi la polisi kwa
kushirikiana ndugu ulibainisha kuwa kifo cha marehemu kilitokana na kupigwa
risasi mbili kifuani ambazo zilipatikana mwilini mwake.
No comments:
Post a Comment