Na Mwandishi Wetu, Tanzaniasasa
JUMUUIYA ya Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (ALAT),
imepinga kipengele kinachotaka kuwepo kwa ukomo wa nafasi za uongozi wa
kuchaguliwa na wananchi ikiwemo ubunge na udiwani.
Akizungumza na waandishi wa habari
juzi katika ukumbi wa ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Arusha, Mwenyekiti wa
ALAT Didas Masaburi alisema jumuiya hiyo inapinga sura hiyo kwa kile alichodai
kufanya hivyo ni kuwanyima haki wananchi wanaotaka kiongozi husika kuendelea
kuwaongoza.
Alisema kabla ya kuwasilisha maoni
yao kwenye tume hiyo walifanya mazungumzo na wananchi kupitia madiwani katika
kata wanazowakilisha ambao wengi wao walitoa maoni wakitaka kutokuwepo kwa
kipengele cha ukomo wa uongozi na badala yake wananchi waachiwe wenyewe kuamua
kama wanamuhitaji kiongozi husika au la.
“ ALAT tuliwasilisha tume maoni 13
yaliyoelezwa kwa undani matakwa ya wananchi katika katiba mpya lakini cha
kushangazwa tume imeweka maoni yake yenyewe na kutupilia mbali maoni yetu, hata
hivyo bado hatujachelewa tutapeleka tena kwa mara nyingine maoni haya kupitia
marekebisho ya rasimu hii ya awali,”alisema Masaburi.
Alisema maoni mengine
waliyoyawasilisha katika tume hiyo ni pamoja na kutaka katiba iweke sura
itakayobainisha namna ambavyo madaraka yatapelekwa kwa wananchi, kutamka katika
katiba mpya uwepo wa Serikali za mitaa chini ya mfumo wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Nyingine ni pamoja na kutamka kazi
na majukumu ya Serikali za Mitaa, uwezo wa kujiamulia mambo yao tofauti na hivi
sasa kila kiongozi katika wizara amekuwa akiamua anavyopendelea yeye, namna
mawasiliano yatakuwa baina ya Serikali kuu na Serikali za mitaa.
“ Pia tumependekeza kuwepo kwa
kipengele kitachoonyesha namna viongozi wa Serikali za mitaa watakavyopatikana
ili kuweka uwajibikaji wa viongozi hao ikiwemo kuchaguliwa na wananchi moja kwa
moja katika eneo husika, benki kuu pia tunataka iwepo tu ya jamhuri isiwe kama
ilivyo hivi sasa pamoja na idara ya uhamiaji kuingizwa katika eneo la
Jamhuri,”alisema.
Masaburi alisema endapo Serikali za
mitaa hazitaingizwa kwenye Katiba mpya tabaka la wenye nacho na wasiokuwa nacho
litakuwa kubwa na matokeo yake ni ongezeko kubwa la watanzania masikini.
Alitoa wito kwa madiwani kote
nchini kutumia nafasi ya kupitia rasimu mpya kuwaelimisha wananchi katika maeneo
yao umuhimu wa uwepo wa sura inayoelezea serikali za mitaa.
Alisema Serikali za mitaa ndio
ambazo zimekuwa mtetezi mkubwa wa wananchi katika suala la maendeleo kufuatia
wao kusimamia fedha ambazo zimekuwa zikipatikana kupitia kodi inayokusanywa na
Serikali kuu.
Masaburi alisema katika kikao
walichofanya hivi karibuni jijini Arusha cha kupitia rasimu hiyo mpya ya Katiba
wamekubaliana kabla ya Agosti 31 mwaka huu kuwasilisha maoni yao
waliyoyawasilisha hapo awali katika tume hiyo.
No comments:
Post a Comment