VIFO vya ajali ya
mlipuko wa kitu kinasadikiwa kuwa ni mlipuko wa bomu vimeongezeka baada ya
mtoto mdogo mwenye umri wa miaka 7 aliyetajwa kwa jina la Tija James kufariki
dunia usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya Seliani alipokuwa amelazwa.
Aidha majeruhi wengine watoto wadogo wawili ndugu Fatuma
Jumanne (10) na Sharifa Jumanne (9), usiku wa kuamkia jana walipelekwa Nairobi
nchini Kenya kwa ajili ya matibabu baada ya hali zao kuwa mbaya na kushindikana
kutibika katika hospitali za hapa nchini.
Akizungumza katika hospitali ya Mtakatifu Elizabeth jana
jijini hapa mara baada ya kutembelea majeruhi hospitalini hapo, Makamu wa Rais
Dkt. Mohamed Bilal alisema hali za majeruhi zinaendelea vizuri ijapokuwa bado
kuna majeruhi wawili ambao hali zao bado ni mbaya kufuatia kuumia vibaya maeneo
mbalimbali ya miili yao.
Bilal alilaani kitendo cha kurushwa kwa kitu hicho
kinachosadikiwa kuwa ni bomu na kuwaahidi wakazi wa Arusha kuwa Serikali
imesikitishwa na tukio hilo na imeagiza uchunguzi wa kina wa kuwabaini wahusika
wa tukio hilo ufanywe haraka na kwa makini.
“ Hili ni tukio la kusikitisha sana na sisi kama Serikali
tumesikitishwa na hali hii ambayo inapoteza amani ya nchi, nchi yetu inasifika
kwa historia nzuri ya kuwa na amani kote duniani lakini vitendo kama hivi
vinatutia doa,”alisema Bilal.
Aliwataka wakazi wa Arusha kuendelea na shughuli zao za kila
siku za kuwaingizia kipato bila kutishiwa na mtu yoyote na kwamba Serikali
haitasita kuwachukulia hatua kali wote waliohusika bila kujali itikadi zao.
No comments:
Post a Comment