Wabunge wa CHADEMA wakiwa wamepozi viwanja vya mahakama kuu mkoa wa Arusha wakisubiri wabunge wanne kufikishwa mahakamani hapo |
Wabunge wa CHADEMA John Wenje na Muhonga Ruhanywa wakiwa viwanja vya mahakama kuu |
Mbunge Selasini wa Rombo na wabunge wengine wakiwa viwanja vya mahakama Kuu jijini Arusha |
Wabunge wa CHADEMA Mahakamani |
Na Mwandishi wetu, Tanzaniasasa
SAKATA la mlipuko wa bomu jijini Arusha limechukua sura mpya
baada ya Jeshi la Polisi jijini hapa kutangaza kumtafuta Mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha
mjini Godbless Lema wakituhumiwa kufanya mkutano bila kuwa na kibali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa Kamishana
wa Polisi operesheni na mafunzo, Paul Chagonja alisema viongozi hao wa chadema
wanatafutwa kwa kuwa walifanya kusanyiko kinyume cha sheria, pasipokuwa na kibali cha Polisi.
Kamishna Chagonja alisema awali katika mkutano na viongozi wa
Chadema uliofanyika katika ofisi za Polisi jijini Arusha , walikubaliana wafike
uwanjani hapo kwa ajili ya kuwatawanya wafuasi wa chama hicho waliokuwa wamekusanyika
katika uwanja wa Soweto kwa ajili ya taratibu za kuaga miili ya marehemu.
“Tulikubaliana waende pale uwanjani kutawanya wafuasi wao
lakini badala ya kufanya kama tulivyokua
tumekubaliana wakaanza kufanya mkutano, huku wakiwatuhumu Polisi kuwa polisi
ndio walihusika na shambulio la bomu lililotokea jumamosi”alisema
Chagonja alisema kuwa baada ya askari kuvumilia matusi hayo,
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha aliwafuata viongozi wa Chadema na kuwaeleza
kuwa hawajaruhusiwa kufanya mkutano katika eneo hilo na kuwataka waondoke
katika eneo hilo la Soweto jambo ambalo walilikaidi na Polisi wakaamua
kuwatawanya kwa mabomu ya machozi.
Alisema jeshi hilo linashikilia pikipiki 106,baiskeli 16 na
gari 6 ikiwemo ya Mwenyekiti wa Chadema Mbowe ambapo vyote vilikamatwa baada ya
madereva wa vyombo hivyo vya usafiri kuvitekeleza uwanjani hapo.
Alitoa wito kwa wakazi wa Arusha kutoa taarifa zozote za watu
waliohusika na mlipuko wa bomu katika uwanja wa Soweto sanjari na kuwataka
kutokaa katika makundi katika kipindi hiki
ambacho jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa mlipuko huo.
WABUNGE KUFIKISHWA
MAHAKAMANI
Katika hatua nyingine jeshi la Polisi mkoa wa Arusha
likiongozwa na Kamishna wa operesheni na mafunzo Paul Chagonja jana liliwaachia
kimyakimya watuhumiwa iliyowakamata kwa madai ya kukusanyika katika uwanja wa
Soweto kinyume cha sheria bila kuwafikisha mahakamani kama ilivyotangaza hapo
awali.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari Kamishna Chagonja
aliwatangazia waandishi wa habari kuwa wabunge na wafuasi hao wangefikishwa
mahakamani saa 6.00 mchana lakini taarifa iliyotolewa baadae zilisema kuwa
wataachiwa wakiwa polisi bila kufikishwa mahakamani.
Umati mkubwa wa wafuasi wa chadema na wabunge wa chama hicho
walikuwa wamekusanyika katika viwanja vya mahakama kwa lengo la kuwadhamini
watuhumiwa hao waliokamatwa lakini hali ilibadilika baada ya taarifa ya kuwa
watuhumiwa hao watadhaminiwa kituo cha polisi na hivyo kulazimika kuondoka
mahakamani hapo kuelekea polisi.
Baada ya kufika Polisi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas aliwaeleza waandishi wa
habari kuwa wabunge wa CHADEMA waliokuwa
wamekatwa ambao ni Mbunge wa Mbulu Mustafa Akoonay, Mnadhimu mkuu wa kambi ya
upinzani bungeni Tundu Lissu, Joyce Munkya (viti maalum), na Makamu Mwenyekiti
wa Chama hicho na mbunge wa Mpanda Said
Arfi walikuwa wamejidhamini na kuondoka kituoni hapo.
Alisema kuwa watuhumiwa wengine 63 ambao ni wafuasi na
wanachama wa CHADEMA walikuwa wamedhaminiwa na ndugu zao na kuruhusiwa kuondoka kituoni hapo.
KAULI YA MBUNGE TUNDU
LISSU
Akizungumza baada ya kuachiliwa kwa dhamana Mnadhimu wa kambi
ya upinzani bungeni Tundu Lissu alisema jeshi la Polisi limeshindwa kuwafikisha
mahakamani kutokana na maelezo ya msingi waliyotoa Polisi.
Lissu ambae pia ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema awali
viongozi wa CHADEMA walifanya mazungumzo na viongozi wa Jeshi la Polisi kuhusu
kufika uwanjani hapo kutawanya umati wa watu uliokuwa umekusanyika lakini jeshi
hilo liliwashambulia kabla hawajawaeleza wananchi hao lengo lao la kufika
uwanjani hapo.
Alisema wanashangazwa na jeshi la Polisi kulazimika kutumia
nguvu za ziada badala ya kutoa wito kwa kutumia vipaza sauti kuwataka kuondoka
eneo hilo kama sheria inavyowataka.
“Polisi hawakutumia taratibu kama sheria zinavyosema,
walipaswa kutumia vipaza sauti kutueleza tuondoke eneo lile lakini hata hivyo
sisi tulishakubaliana na kabla hatujamaliza mkutano wa kuwatawanya wananchi
wakaanza kutushambulia kwa mabomu,”alisema na kuongeza:
“Tumetakiwa kurudi tena polisi Julai 22, mwaka huu ila mimi
ninavyojua ukiniambia kuhusu kurudi hiyo ‘imeishatoka, hakuna kesi tena hapo’,
tumelazwa sero wanawake na wanaume, tumechangia choo kimoja hiyo inatosha
kabisa,”alisema.
NDUGU WA MAJERUHI
Wakati huo huo Ndugu wa majeruhi wa mlipuko wa bomu katika
uwanja wa Soweto waliolazwa katika hospitali ya Seliani mkoani hapa
wamelalamika kutishiwa na kutaka kutekwa na watu wa usalama pamoja na askari wa
jeshi la Polisi.
Akizungumza na waandishi wa
habari katika viwanja vya mahakama kuu jijini hapa, mmoja wa ndugu hao
ambae ni pacha na majeruhi Peter Mshanga
aliyelazwa katika hospitali ya Seliani aliyejitambulisha kwa jina la Paul
Mshanga alisema ndugu yake huyo ametishiwa na watu wa usalama kwa madai ya
kutaka kumhamisha hospitali hapo.
Alisema askari wa upelelezi walidai kutaka kumhamishia katika
hospitali nyingine kwa madai ya kuwa hali yake ni mbaya jambo ambalo sio kweli
kwani hali yake ni nzuri kwa mujibu wa madaktari hospitali hapo.
“ Sisi tuna wasiwasi sana na usalama wa ndugu yetu, wanataka
kumhamishia hospitali nyingi kwa madai eti hali yake ni mbaya, kwani maofisa hao wa upelelezi wamekuwa
hawabanduki hospitalini hapo baada ya
yeye kuhama kwani hali yangu ni nzuri,”alisema Paul ambae ni pacha wa Peter.
KAULI YA MNYIKA
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika viwanja vya
mahakama kuu jijini hapa Katibu Mwenezi wa CHADEMA John Mnyika alivitaka vyombo
vya usalama nchini kuacha vitisho dhidi ya majeruhi wa mlipuko huo na kwamba
vitendo wanavyofanyiwa majeruhi hao ni hatua ya vyombo vya usalama kutaka kupoteza
ushahidi dhidi ya tukio hilo
“ Hata Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari alipata
taarifa ya kuwepo kwa maofisa usalama katika hospitali ya Seliani waliokuwa
wakizungukia majeruhi huku wakiwa wameshikilia vifaa vya hospitali na kuwatia
hofu majeruhi hao, “alisema.
Alisema mbunge huyo baada ya kuwaona watu hao alipiga kelele
za kutaka msaada wa kuwakamata na wagonjwa waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo
walitoka katika wodi zao na watu hao kutokomea kusikojulikana.
Akitangaza ratiba ya mazishi Mnyika alisema kufuatia jeshi la
Polisi kuzuia mkusanyiko wa watu katika viwanja jijini Arusha, chama hicho
kimeamua kutoa heshima za mwisho za kuaga mwili wa marehemu Judith Moshi
aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Kata ya Sokoni one katika kanisa ambapo ibada
itafanyika.
Mnyika alisema kanisa ambalo ibada hiyo ya mazishi itafanyika
na makaburi ambayo marehemu huyo atazikwa vitatangazwa hapo baadae baada ya
taratibu zaidi kuendelea kufanyika ambapo anatarajiwa kuzikwa jijini Arusha.
No comments:
Post a Comment