Na Mwandishi wetu, TANZANIASASA
VIONGOZI waandamizi wa chama cha demokrasia na
maendeleo (CHADEMA) akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe jana walinusurika
kufa baada ya kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu kulipuka kutokea chini ya
Jukwaa alilokuwa akihutubia katika uwanja wa Soweto muda mfupi baada ya
kumaliza kumnadi mgombea udiwani wa kata ya Kaloleni Emanuel Lewi Kessy jijini
hapa.
Mbali ya hilo pia kumekuwepo na madai ya watu watatu
kufariki dunia na wengine zaidi ya 15 kujeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao
ikiwemo miguuni na kichwani ikiwemo
watoto wawili waliodaiwa kuvunjia miguu.
Tanzaniasasa ilishuhudia majeruhi hao wakiingizwa
na kutolewa katika hospitali ya Mount Meru mara baada ya kutokea kwa tukio hilo
lililotokea saa 11.40 muda mfupi baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA Mbowe kumaliza
kuhutubia wananchi wa kata hiyo na kumuombea kura mgombea huyo.
Katika hospitali ya Mount Meru umati mkubwa wa wafuasi
wa CHADEMA ulifurika muda mfupi baada ya kutokea kwa tukio hilo ambao wengi wao
walionekana kushinikiza wauguzi wachache waliokuwepo hospitalini hapo kuwapatia
majeruhi huduma ya kwanza kufuatia kujeruhiwa vibaya katika maeneo mbalimbali
ya miili yao.
Zoezi zima la kushinikiza wauguzi hao kuwapatia
huduma majeruhi hao liligeuka baada ya baadhi ya wauguzi kujificha wakiogopa
umati huo wa wafuasi wa wachadema na hivyo majeruhi kukosa huduma ya kwanza.
Hali hiyo iliwalazimu wafuasi wa CHADEMA kubeba
majeruhi hao waliokuwa wakivuja damu katika miili yao kwa kutumia magari
binafsi na kuwahamishia hospitali mbalimbali ikiwemo hospitali ya rufaa ya Kanis
la Kiinjili la Kilutheri ya Seliani ya jijini hapa.
Mmoja wa wafuasi wa chadema aliyejitambulisha kwa
jina la Martin Lucas alidai wakiwa katika uwanja wa Soweto huku mkutano
ukiendelea kwa amani na utulivu na mwenyekiti wa Chadema alipomaliza kuhutubia
na kushuka jukwaani akielekea kupanda gari lake tayari kuondoka, ghafla mlipuko
mkubwa ulitokea katika jukwaa alilokuwa akihutubia.
“ Ndugu mwandishi hii ni hujuma kabisa, Mkutano
ulifanyika kwa amani na utulivu wa kutosha ghafla tukashangaa watu wanaanguka
chini huku moshi mkubwa ukipaa juu, sisi
tulikuwa pembeni ya mti tukafikiri Mwenyekiti wetu amepigwa bomu lakini haikuwa
hivyo, yeye alishapanda gari na kuanza safari, watu wengi wameumia sana ndugu yangu,”alisema
mfuasi huyo Robert Kinabo.
Mbali ya Mwenyekiti huyo wa CHADEMA kunusurika kwa
bomu katika mlipuko huo mwingine ni pamoja na Mbunge wa Arusha mjini Godbless
Lema ambae kwa kipindi chote cha kampeni za Chadema alikuwepo jijini Arusha
akiwanadi wagombea wa udiwani wa chama hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas alithibitisha kutokea kwa tukio hilo pamoja na vifo vya watu wawili na kusema kuwa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi zaidi ili kubaini watu zaidi waliathirika katika tukio hilo.
Wafuasi wa CHADEMA wakimbeba majeruhi wa tukio la kupigwa bomu katika uwanja wa Soweto leo kutoka hospitali ya Mountmeru baada ya kukosa huduma |
Wafuasi wa Chadema wakiwa wamembeba mtoto mdogo aliyejeruhiwa katika tukio hilo kumtoa katika hospitali ya Mount Meru na kumwamishia hospitali zingine za binafsi baada ya kukosa huduma |
Wauguzi wachache katika hospitali ya Mkoa wa Arusha Mount Meru wakiwapatia huduma ya kwanza majeruhi , kulia ni mmoja wa majeruhi mtoto mdogo akipewa oxygen |
Wafuasi wa chadema wakiwa wamejazana ndani ya hospitali ya Mount Meru wakishinikiza majeruhi kupatiwa huduma |
Majeruhi mama mwenye mtoto mdogo wakitoka ndani ya hospitali ya Mount Meru wakisubiri kupakiwa kwenye magari kuhamishiwa hospitali zingine binafsi baada ya kukosa huduma |
Gari lenye bendera za chadema likiondoka kwa kasi kutoka hospitali ya Mount Meru baada ya kupakia majeruhi waliokosa huduma na kuwawahisha hospitali binafsi |
Majeruhi |
Majeruhi akiwa amelazwa katika korido huku akisubiri huduma zaidi |
Wafuasi wa Chadema wakiwa wametanda nje ya hospitali ya Mount meru |
Majeruhi akisubiri huduma katika hospitali ya Mkoa wa Arusha Mount meru |
No comments:
Post a Comment