Na Mwandishi wetu, Tanzaniasasa,
MGOGORO Mkubwa umeibuka
kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro na uongozi wa mamlaka ya mji mdogo
Mirerani wilayani humo baada ya mamlaka hiyo kutangaza msimamo mgumu wa kuzuia
watendaji wa Halmashauri hiyo kukusanya mapato ndani ya mji huo na badala yake
wao ndio watafanyakazi hiyo.
Adha wajumbe wa mamlaka
hiyo wameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kuwataka radhi wajumbe hao
kwa madai ya kuwakashifu kwa kuwaita ‘bado watoto wadogo’ kupitia barua
waliomuandikia mtendaji mkuu wa mamlaka hiyo baada ya wao kuitaka Halmashauri
hiyo kusitisha zoezi la kukusanya mapato ndani ya mji wao.
Uamuzi huo mgumu
ulifikiwa jana katika kikao cha wajumbe wanaounda baraza la mamlaka ya mji
mdogo wa Mirerani chini ya mwenyekiti wake Albert Siloli ambao kwa pamoja walimtaka
Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo ya mji mdogo kuiandikia barua Halmashauri kuhusu uamuzi huo
walioufikia.
Wajumbe hao
walikubaliana kuanza zoezi la kukusanya mapato hayo leo (Julai mosi, 2013), ambapo
watatawanyika katika maeneo mbalimbali ya mji huo mdogo wa mirerani na fedha watakazozikusanya
wataziweka benki kwa ajili ya
utekelezaji wa shughuli za maendeleo zinazohusu mji huo.
Hata hivyo akizungumzia
suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro
Brigedia Jenerali Francis Kayombo alikiri kuwepo kwa mgogoro huo lakini alisema
bado Halmashauri ya Wilaya ndio yenye mamlaka ya kukusanya mapato katika eneo
hilo kufuatia kuwa na watendaji wa kuweza kusimamia mapato hayo.
“ Mgogoro huu naufahamu
lakini hii mamlaka bado ni ndogo sana na haina watumishi wa kutosha, haina mwekahazina ambae atakuwa
na jukumu la kusimamia mapato watakayokusanya lakini zaidi watazihifadhi wapi hizo
fedha wapi?, naomba unisubiri mpaka nirudi kutoka safarini nitawapatia taarifa
nzuri zaidi,”alisema.
Afisa mtendaji mkuu wa
Mamlaka hiyo ya mji mdogo Mirerani, Nelson Msangi alisema mji huo wenye wakazi
zaidi ya elfu54 unatakiwa kupokea ruzuku ya milioni 30 kwa mwaka kutoka
Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro lakini wamekuwa hawapati fedha hizo na
kushindwa kulipa madeni inayodaiwa.
Vyanzo vya mapato hayo ni
pamoja na ushuru wa stendi ya mabasi mirerani, machinjio, soko, mnada, hoteli,
saluni, nyumba za kulala wageni, kodi ya mabango, leseni za vileo na leseni za
biashara ambavyo kwa kipindi cha miaka minne toka 2008 eneo hilo lilipopewa
hadhi ya mamlaka ya mji mdogo bado halmashauri hiyo ndio imekuwa ikikusanya.
Wakati huo huo Diwani wa kata ya Mirerani na mjumbe wa baraza hilo Justine Nyari amesema endapo Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro itaifuta mamlaka hiyo atakuwa tayari kujiuzulu wadhifa wake wa udiwani kwa kile alichodaiwa itakuwa ni kuihujumu mamlaka hiyo.
Gari la kubeba uchafu ililokabidhiwa mamlaka ya mji mdogo Mirerani, hata hivyo gari hilo ni bovu |
Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani Albert Siloli akifungua kikao hicho cha baraza la mamlaka ya mji mdogo Mirerani |
Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya mji mdogo Mirerani Nelson Msangi akisoma moja ya barua zilizotoka Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro |
Diwani wa kata ya Mirerani Justine Nyari akichangia hoja ya kuizuia Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro kuendelea kukusanya mapato katika mamlaka ya mji mdogo Mirerani leo |
mmoja wa wajumbe wa baraza la mamlaka ya mji mdogo Mirerani akichangia hoja katika kikao hicho |
No comments:
Post a Comment