MWANAFUNZI wa mwaka wa pili katika chuo cha
uhasibu kilichopo Njiro jijini Arusha,Henry Koga anayekadiriwa kuwa na
umri kati ya miaka (25 hadi 30) ameuawa kinyama kwa kuchinjwa na kisu shingoni
na kundi la watu wasiofahamika wakati wakitoka kwenye kumbi za starehe na
wenzake.
Kufuatia tukio hilo ,kundi la wanafunzi walileta
vurugu kubwa na kukataa kutii amri ya mkuu wa mkoa wa Arusha,Magesa Mulongo ya
kuwataka warudi darasani wakati hatua zaidi za kisheria zikichukuliwa huku wakimzomea,hali
iliyosababisha polisi kuingiliaka kali na kuwafyatulia mabomu zaidi ya 50 na
baadhi yao kujeruhiwa.
Tukio la kuuawa kwa mwanafunzi huyo limetokea
majira ya saa 4 usiku wa kuamkia leo ambapo marehemu huyo akiwa na
wenzake walivamiwa na kundi la wahuni wapatao wanne katika eneo la CDA ,umbali
mchache kutoka eneo la chuo hicho na kumchoma kisu shingoni .
Hata hivyo jitihada za wenzake kutaka kuokoa maisha
yake kwa kumkimbiza hospitalini, zilishindikana kwani alifariki dunia muda
mfupi baada ya tukio hilo kutokana na kuvuja damu nyingi.
Aidha wanafunzi hao walijikusanya asubuhi yake na
kuanza kuandamana kushinikiza uongozi wa chuo hicho kutoa tamko juu ya
vitendo vya uhalifu vinavyojirudia mara kwa mara katika chuo hicho bila
kuchukuliwa hatua zozote na kufanya maisha ya wanachuo hao kuwa hatarini.
Wanafunzi hao walisikika wakilalamikia hali ya
ukimya wa viongozi kushindwa kudhibiti matukio ya uhalifu kwani mwishoni mwa
mwaka jana mwanafunzi mwingine aliuawa na vibaka kwa kuchomwa na kisu pia wanafunzi
hao waliwahi kuvamiwa chuoni wakiwa wamelala na kuporwa vitu mbalimbali
ikiwemo laptop simu na fedha.
Wakati vurugu za wanafunzi zikiendelea alifika mkuu
wa mkoa wa Arusha ,Magesa Mulongo na kuwasihi waache vurugu na wakubali
kumsikiliza hata hivyo wanafunzi hao zaidi ya 500 walianza kumzomea huku baadhi
yao wakionekana kurushia mawe
Mkuu wa mkoa alilazimika kuondoka eneo hilo ,hatua
iliyowalazimu askari wa kutuliza ghasia kufyatua mabomu ya machozi kwa lengo la
kuwatawanya na kujikuta baadhi yao wakijeruhiwa vibaya .
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Arusha ,Ibrahimu
Kilongo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa wanafunzi
zaidi ya 7 wanashikiliwa katika vurugu hizo huku uchunguzi wa tukio hilo bado
unaendelea .
Mkuu wa mkoa Magessa Mulongo pamoja na timu yake wakiingia katika eneo la shule ambapo aliambulia zomea zomea ,kurushiwa mawe,lugha za kejeli kutoka kwa wanafunzi hao kwa kile wanachodai kuwa serikali imekuwa siyo sikivu kutatua matatizo yao ya mara kwa mara ikiwepo kuibiwa vitu mbalimbali |
ASKARI WA FFU WAKIWA TAYARI KUDHIBITI VURUGU CHUONI HAPO |
UMATI WA WANAFUNZI WA CHUO CHA UHASIBU NJIRO IAA WAKIMSIKILIZA MKUU WA MKOA MAGESA MULONGO KABLA YA KUANZISHA VURUGU WAKIPINGA MWANAFUNZI MWENZAO KUUAWA |
No comments:
Post a Comment