Wednesday, April 3, 2013

TAMKO LA WAZIRI KAGASHEKI KUHUSU ENEO LA PORI TENGEFU LA LOLIONDO



 

 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII TAARIFA KWA UMMA UFAFANUZI KUHUSU TAMKO LA WAZIRI KAGASHEKI KUHUSU ENEO LA PORI TENGEFU LA LOLIONDO TAMKO HALITABADILIKA

Wizara ya Maliasili na Utalii imefafanua kuwa tamko alilolitoa Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Khamis Kagasheki mbele ya waandishi wa habari tarehe 26 Machi 2013 kuhusu kupunguza eneo la Pori Tengefu la Loliondo halitabadilika na kuwa alilitoa kutokana na mamlaka ya kisheria aliyo nayo.Ufafanuzi huu umetolewa kutokana na maoni ya baadhi ya watu waliyoyatoa kwa njia ya mtandao na kwenye vyombo vingine vya habari kuwa uamuzi uliofanyika kuhusu Pori Tengefu la Loliondo si sahihi kwa kuwa haukufuata sheria wala matokeo ya utafiti. Maoni hayo si sahihi. TAMKO NI KWA MUJIBU WA SHERIA Ukweli ni kuwa Waziri Kagasheki alifuata sheria alipotoa tamko kuhusu kupunguza eneo la Pori Tangefu la Loliondo kutoka kilomita za mraba 4,000 hadi 1,500 na kuliacha eneo la kilomita za mraba 2,500 litumiwe na wananchi. Alifanya hivyo kwa kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009, Sehemu ya 16 Vifungu Na. 4, 5 na 6. Sheria hiyo inampatia Waziri mwenye dhamana uwezo wa kupitia upya mapori tengefu na kufanya marekebisho mbalimbali muhimu kwa manufaa ya wananchi bila kuathiri uhifadhi.Aidha, Waziri alifanya uamuzi huo kwa kuzingatia taarifa mbalimbali za utafiti na uchunguzi ambazo ziliwahi kufanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI). Pia alizingatia mapendekezo ya tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza mgogoro uliokuwapo.Mojawapo ya tume hizo ni Tume ya Waziri Mkuu ya mwaka 2010 ambayo ilijumuisha wajumbe kutoka wizara 9, Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro. Pamoja na mambo mengine Tume hiyo ya Waziri Mkuu ilipendekeza kuwa kuna umuhimu wa kupunguza eneo la Pori Tengefu la Loliondo bila kuathiri mapito ya wanyamapori, na vyanzo vya maji.Vilevile, kwa muda mrefu viongozi wa Wizara wamekuwa wakikutana na wananchi na viongozi wa Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro kujua kero zilizopo ili zitatuliwe. Mikutano hiyo imemwezesha Waziri Kagasheki kufanya uamuzi alioufanya wa kuligawa eneo hilo la Pori Tengefu la Loliondo.UMUHIMU WA PORI TENGEFU LA LOLIONDOWizara inasisitiza kuwa eneo la kilomita za mraba 1,500 litaendelea kuwa Pori Tengefu na kumilikiwa na Wizara kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 kwa sababu zifuatazo:

Ni sehemu ya mazalia ya wanyamapori;
Ni sehemu ya mapito ya wanyamapori;
Ni vyanzo vya maji.
Kwa ajili hiyo eneo hilo litaendelea kuwa chini ya Wizara, kwa kuwa linachangia kwa kiwango kikubwa kuimarisha mfumo-ekolojia wa Serengeti.

MASLAHI YA WANANCHI YANAZINGATIWA
Wizara imesisitiza pia kuwa ardhi iliyobaki baada ya kuondoa eneo la Pori Tengefu la Loliondo itasimamiwa na vijiji kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya Mwaka 1999. Vilevile Wananchi watawezeshwa ili waanzishe Eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) katika ardhi hiyo kwa manufaa yao.Tanzania inajali uhifadhi lakini pia inajali maslahi ya wananchi, ndiyo maana asilimia 25 ya eneo la nchi hii limehifadhiwa bila kuwepo migogoro. Hakuna migogoro kati ya wananchi na Serikali, kwa kuwa wananchi wanatambua umuhimu wa uhifadhi kwao na kwa vizazi vijavyo. Ndiyo maana wananchi wanachangia kwa kiwango kikubwa katika kufanikisha uhifadhi.Pale ambapo kunajitokeza mgogoro kuhusu uhifadhi Serikali na wadau husika hujadili na kufikia mwafaka. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Loliondo, ndiyo maana kilomita za mraba 2,500 zimemegwa na kukabidhiwa wananchi.

WANAHARAKATI WANACHOCHEA MGOGORO

Tatizo la Lolindo, tofauti na maeneo mengine ya hifadhi, ni kuwa mgogoro uliopo unachochewa na wanaharakati na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), mengi yakiwa yanatoka nje ya nchi. Hata hivyo, ajenda yao ya siri imeshagundulika na haitaifanya Serikali kufanya uamuzi kinyume cha sheria za nchi na maslahi ya wananchi.Wananchi wa Loliondo wametakiwa kupuuza mbinu za wanaharakati ambazo hazina maslahi kwao, wala kwa uhifadhi na taifa kwa ujumla.
[MWISHO]
George Matiko
MSEMAJI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Simu +255 784468047 1 Aprili 2013

No comments: