Wednesday, May 14, 2014

MACHIFU 120 WAKUTANA ARUSHA KESHO, NI KWENYE TAMASHA LA UTAMADUNI LA 'MTU KWAO'

Chifu wa Kasulu Kigoma, Isambe Gilbert Isambe


Chifu wa Kasulu mkoani Kigoma Isambe G. Isambe wa kwanza kushoto, Chifu wa Old Moshi, Gerald Madara katikati na Mkurugenzi wa Utamaduni Training Janeth Jonas kulia wakizungumza na waandishi wa habari jana

Chifu wa Kasulu mkoani Kigoma Isambe G. Isambe wa kwanza kushoto, Chifu wa Old Moshi, Gerald Madara

Chifu wa Kasulu, Kigoma Isambe G Isambe akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo kuhusu tamasha la utamaduni linaloanza kesho jijini Arusha, kulia ni Mkurugenzi wa Utamaduni Training Ltd


Na Seif Mangwangi, Arusha

TAMASHA kubwa la utamaduni linalokutanisha zaidi ya machifu 120 wa kabila mbalimbali nchini, linaanza leo katika uwanja wa mpira wa miguu wa Shekh Amri Abeid jijini hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana  jijini hapa, Mkurugenzi  wa kampuni ya  Utamaduni Training, Janeth Jonas alisema tamasha hilo linafanyika kwa mara ya kwanza nchini likiwa na lengo la kuenzi utamaduni wa Mtanzania kwa vizazi vilivyopo.

Chifu wa Kasulu Kigoma Isambe G Isambe akiwa katika vazi la kitamaduni la jamii yake
Alisema katika tamasha hilo la siku tano linalotambulika kwa jina la ‘MTU KWAO’, washiriki zaidi ya 10,000 wanatarajiwa kushiriki ambapo shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwemo kuonyesha mavazi, ngoma za asili za makabila hayo na elimu ya tamaduni zao.
Janeth alisema wasanii mbalimbali watakuwepo kutumbuiza katika tamasha hilo ikiwemo Mrisho Mpoto, Jambo Squard, Dogo Janja, Wema Sepetu, Roma Mkatoliki,Weusi na  Daniel Sekuo kutokana nchini Kenya.

“Mbali ya wasanii hawa pia kutakuwa na ngoma za asili kwa kila kabila ikiwemo ngoma ya Mtingo kutoka Moshi, Hadzabe, Maasai, Datoga n.k, lakini pia kutakuwa na tamaduni mbalimbali zitakazoonyeshwa,”alisema.

Alisema siku ya mwisho ya kilele cha Tamasha hilo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Pascal Mabiti ambae pia ni Chifu katika jamii yake anatarajiwa kuwa mgeni rasmi ambapo shughuli mbalimbali pia zitafanyika.

Kwa upande wake chifu kutoka wilaya ya Kasulu,  Mkoa wa Kigoma, Isambe Isambi alisema Tamasha hilo linafanyika ikiwa ni kukumbusha watanzania utamaduni wao ambapo miongoni mwa shughuli zitakazofanyika ni pamoja na kutoa elimu ya tamaduni ambazo zinaweza kuendelea kuenziwa na kuondoa ambazo zimepitwa na wakati.


No comments: