Monday, August 12, 2013

TAHARUKI MSIBA WA BILIONEA MSUYA: NDUGU NA MAJIRANI WAZIMIA, WAPEWA HUDUMA YA KWANZA

BABA WA MAREHEMU MZEE ELISARIA AKIAGA MWILI WA MWANAE JANA
Na MWANDISHI WETU,  ARUSHA

ZOEZI la kuaga mwili wa marehemu, mfanyabiashara wa madini ya
Tanzanite Erasto Msuya (43), jana nusura liingie dosari baada ya
baadhi ya waombolezaji kupoteza fahamu na kuacha taharuki kubwa
miongoni mwao.

Miongoni mwa waliopoteza fahamu na kulazimika kupewa huduma  ya kwanza  kupitia gari la wagonjwa la kampuni ya ulinzi ya KK Security ya jijini
Arusha ni pamoja na mdogo wa marehemu aliyetajwa kwa jina la Atu Msuya  ambae anaelezwa kuwa karibu na marehemu wakati wa uhai wake.

Wengine waliozimia na kupatiwa huduma ya kwanza ni wanawake watatu  ambao majina yao hayakuweza kupatikana mara moja lakini hata hivyo  baada ya kuwekezwa hewa ya oxygen walizinduka.

MKE WA MAREHEMU MIRIAM MSUYA AKIMBUSU MAREHEMU
Kwa mujibu wa  kaka wa Marehemu Israel Msuya, mwili wa mfanyabiashara  huyo Erasto Msuya (43), aliyeuawa kwa kupigwa risasi zaidi ya kumi na  watu wasiojulikana unatarajiwa kuzikwa leo alasiri nyumbani kwa wazazi  wake Kairo, Mirerani wilayani Simanjiro,Manyara.

Maombolezo na mazishi ya mfanyabiashara huyo aliyekuwa akimiliki mali  kadhaa kipindi cha uhai wake yalipangwa kugharimu zaidi ya shilingi  milioni 100, huku jeneza na gari maalum ya kubeba mwili yakiagizwa  kutoka jijini Nairobi, Kenya.

Gharama ya jeneza pamoja kukodisha gari ilikadiriwa kuwa shilingi  milioni nane huku kiasi kinachosalia kikipangwa kugharamia vyakula na  vinywaji tangu siku ya kwanza ya msiba hadi mazishi ya leo.

Msuya anayemiliki hoteli ya kitalii ya SG Resort jijini Arusha pamoja  na mali kadhaa yakiwemo nyumba za kuishi, biashara na magari ya  kifahari ikiwemo aina Range Rover New Model iliyotengenezwa mwaka huu  wa 2013, alipigwa risasi eneo la Mjohoroni, katikati ya Uwanja wa
ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro na mji wa Bomang’ombe.

Katika uhai wake, Msuya alikuwa akijihusisha na uchimbaji na biashara  ya madini ya Tanzanite akimiliki migodi katika vitalu ‘B’ na ‘D’ huko  Mirerani.

Licha ya kuacha gumzo, kifo cha mfanyabiashara huyo kimezua  sintofahamu miongoni mwa wafanyabiashara wenzake, huku wengi wakihoji  sababu za kuuawa kwa kumiminiwa risasi nyingi kiasi hicho ambapo  baadhi wanahusisha tukio hilo na visasi vya kibiashara na uhasama miongoni mwa wafanyabiashara hao.MKE WA MAREHEMU, MIRIAM MSUYA AKILIA KWA UCHUNGU


MKE WA MAREHEMU MIRIAM MSUYA PAMOJA NA MWANAE PEKEE WA KIUME WAKIANGALIA MWILI WA MAREHEMU KWA UCHUNGU

MKE WA MAREHEMU MIRIAM AKIUCHUNGUZA KWA UCHUNGU MWILI WA MUMEWE

DADA WA MAREHEMU AKILIA KWA UCHUNGU NA BAADAE KUPOTEZA FAHAMU
DADA WA MAREHEMU

No comments: