Sunday, August 11, 2013

POLISI ARUSHA WADAIWA KUINGIZWA KWENYE MFUKO WA TAJIRI WA KIBO PALACE HOTELI ILI KUSAIDIA KUDHULUMU HAKI ZA WAFANYAKAZI WAKE


Na MWANDISHI WETU, ARUSHA.

UONGOZI wa hoteli ya kitalii ya Kibo Palace ya jijini hapa umeingia  katika kashfa nzito baada ya kudaiwa kuwatumia vibaya askari polisi wa kituo cha polisi wilaya ya Arusha kuwakamata na kuwatishia wafanyakazi wanne wa hoteli hiyo waliodaiwa kuiba Shilingi 74,000 na kufukuzwa
kazi.

Askari hao wanadaiwa kuwatishia wafanyakazi hao waliodaiwa kuiba bili  za chakula na vinywaji ili waweze kuacha kudai mafao yao wanayoidai hoteli hiyo kwa madai ya kufukuzwa kazi kinyume cha taratibu na kulazimika kufikisha madai yao idara ya kazi na baadae tume ya  usuluhishi.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa kwa niaba ya wenzake mmoja wa wafanyakazi hao Adelaida Pancras alisema kitendo cha wao kufukuzwa kazi kwa madai ya kuiba bili za chakula si kweli kwa kile alichodai kuwa utaratibu wa hoteli hiyo wahudumu hawaruhusiwi kuandikia wageni bili  na anayefanya hivyo ni mhasibu na kisha wao wanapewa na kumpelekea mteja.

Alisema kama uongozi huo wa hoteli una watuhumu wao kufanya wizi huo bila kumuhusisha mhasibu anaeandaa bili itakua ni uonevu kwa kua oda ya chakula au vinywaji inaanzia tangu jikoni kupitia kwa mhasibu  na ndipo iwafikie wao  na kuwapelekea wageni.

Adelaida alisema anashangaa uongozi huo kuwafukuza kazi wao huku ikiwaacha wezi waliohusika kufanya wizi huo ambao ni kiongozi wa idara ya uhudumu Isack Mbise na  Julieth ambae ni mhasibu na alikiri yeye kuandika bili hiyo.

Alisema wafanyakazi wanaoonekana kuhusika na kufukuzwa kwao ni pamoja na Sinori na afisa utumishi msaidizi aliyemtaja kwa jina la Asenga na kwamba inaonekana mpango huo ni maazimio ya muda mrefu yaliyowekwa ya kuwatafutia sababu za kuwafukuza kazi.

Akizungumzia suala la kutishiwa na makachero wa idara ya upelelezi wa polisi wilaya ya Arusha, Adelaida alisema baada ya wao kuona uongozi wa hoteli unataka kuwadhulumu haki yao walilazimika kwenda kushtaki idara ya kazi na uongozi ulipoitwa ulikataa kuwalipa mafao yao ndipo
wakapewa barua ya kwenda idara ya usuluhisi.

“Tulipokuwa idara ya usuluhisi, baada ya kuzungumza na uongozi kushindwa kupatia suluhu madai yetu tulipewa tarehe ya kurudi tena ndipo tulipotoka nje ya kukuta askari wakiwa na gari na kutuamuru
kupanda hadi polisi ambapo tuliwekwa sero na kesho yake walituchukua maelezo yetu kuhusu upotevu wa fedha hizo na kutuachia kwa dhamana,”alisema.

Alisema baada ya kuachiwa waliamriwa kuripoti polisi kila jumatatu ya wiki na walipohoji kwanini suala lao halifikishwi mahakamani ili waweze kupata haki yao makachero hao waliwajibu kwa ukali kuwa ‘ kazi hiyo haiwahusu’ jambo ambalo wameona ni uongozi wa hoteli hiyo kutumia fedha na madaraka kwa polisi ili waache kufuatilia suala lao idara ya kazi.

Alisema kitendo cha uongozi huo wa hoteli kuchukua uamuzi wa kuwafukuza kazi ilikua ni maamuzi yao ya mwisho pasipo kuwachukulia hatua nyingine  na kuhoji iweje uongozi huo uwapelekee gari la  polisi
kwenda kuwakamata nje ya ofisi za idara ya kazi mara baada ya kufikisha malalamiko yao idarani hapo .

Adelaida alisema jeshi hilo la  polisi kushindwa kuwafikisha mahakamani tangu ilipowakamata Julai mwaka huu, wameshindwa kutafuta kazi katika maeneo mengine waliyopata kazi ikiwemo nje ya mkoa wa Arusha kama Mwanza na kwingineko kwa kuhofia kuruka dhamana walizowekewa.

Akijibu tuhuma za kulitumia jeshi la Polisi vibaya, Mkuu wa idara ya utumishi hotelini hapo Rodgers Mbaga alisema si kweli kwa kuwa aliwafukuza kazi baada ya kukaa vikao vya uongozi wa hoteli na
kujiridhisha kufanyika kwa wizi huo na  waliopoona wafanyakazi hao wameamua kuchukua maamuzi ya kuwashitaki katika idara ya kazi ndipo walioamua kulifikisha suala hilo Polisi.

Pia alisema suala la kuchelewa kwa kesi yao kwenda mahakamani alisema inategemea upelelezi unaoendelea kufanywa na Polisi lakini wao wako tayari kumtumia mwanasheria wao wa kampuni kusimamia kesi hiyo.

Akizungumzia utaratibu wa bili za mauzo ya vyakula na vinywaji kuandikwa na mhasibu alikiri kuwepo kwa suala hilo na kudai kuwa wafanyakazi wamekuwa wakitumia mtindo wa kuibia hoteli kwa kuandika bili hizo kwa mkono na kisha kuwapelekea wageni bila kufanya mawasiliano na wahasibu.

Kwa upande wake Mkurugenzi  wa hoteli hiyo, Vincent Laswai alikiri kufukuzwa kwa wafanyakazi hao na kudai kuwa uongozi wake umekuwa ukifuatilia taratibu za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha
polisi.

“ Ni kweli tumewafukuza na baadhi ya wenzao walioshiriki kwenye wizi huo tunaendelea kufanya nao kazi, tumewafikisha polisi baada ya wao kutufikisha idara ya kazi na tutaendelea na kesi hadi haki
itakapopatikana,”alisema na kuongeza:

“Hivi kweli ndugu mwandishi unafikiri mtu akuibie mali yako halafu umsamehe tu hivi hivi tu?, kuhusu kuwatumia vibaya polisi si kweli hayo ni maneno tu ambayo wanaweza kusema kwa sababu mimi ni tajiri na hapa pia sheria bado inaturuhusu kufanya hivyo,”alisema.

Akizungumzia tuhuma dhidi ya Polisi wake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Liberatus Sabas alidai kutofahamu uwepo wa kesi hiyo na kuahidi kuifuatilia ili kuona ni kikwazo gani ambacho kimechelewesha suala hilo kutofikishwa mahakamani.

Wafanyakazi hao walioachishwa kazi machi 28 mwaka huu ni pamoja na Adelaida Pancras, Edward Pallangyo, Monica Simon na Emanuel Salema ambao wamekuwa wakiripoti katika kituo cha polisi cha Arusha kila wakati na kuhoji ni lini kesi yao itafikishwa mahakamani bila mafanikio yoyote huku wakishindwa kutafuta kazi mahali pengine kuhofia dhamana na kukosa barua  ya walikotoka kufanya kazi.

No comments: