Thursday, March 14, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA KWA UMOJA WA WANAFUNZI WALIOFUKUZWA VYUO NA VIKUU NCHINI UTANGULIZI 14.03.013

Awali ya yote tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema na fadhia ambaye amekuwa ni tumaini la maisha yetu.

Ndugu waandishi wa habari, Mbele yenu ni umoja wa wanafunzi tuliofukuzwa vyuo vikuu nchini. Umoja huu unaitwa UUEST na unahusisha vyuo vikuu vifuatavyo; Chuo kikuu cha Dar es Salaam “UDSM”, Chuo kikuu cha Dodoma “UDOM” na Chuo kikuu cha Mhimbili “MUHAS”,Chuo kikuu cha MWALIMU NYERERE MEMORIAL, MUCCOBS, IFM na STJN. Umoja huu ulianzishwa rasmi tarehe 26/01/2013 baada ya maazimio ya wanafunzi waliofukuzwa kutoka vyuo husika kukubaliana kutengeneza umoja tajwa hapo juu.

Historia ya nchi yetu inaonyesha kuwa timua timua ndani ya vyuo vikuu nchini ilianza miaka ya 1990 [1992] lakini miaka ya 2008 hadi sasa suala hili limezidi kuwa kubwa ndani ya taifa letu,watawala wa vyuo vikuu nchini ambao ni maprofesa na baadhi ya viongozi waliopo serikalini wanalichukulia suala hili la kikatili kama mila na desturi na ni haki yao kimsingi kufukuza wanafunzi wa vyuo vikuu wenye mawazo mbadala, wenye uwezo wa kuhoji mambo, kukosoa uovu uliopo na unaoendelea kutendeka ndani ya vyuo vyetu na ndani ya taifa letu na wenye uwezo wa kutoa ushauri pale inapobidi kwa maslahi ya taifa lao. Ndugu waandishi wahabari, Kimsingi timua timua vyuoni ni janga la kitaifa ndani ya vyuo vikuu nchini na hakika tukilifumbia macho tunalizika taifa letu huku macho yetu yanashuhudia kwa sababu tunaidadi kubwa ya wanafunzi tuliofukuzwa vyuoni bila makosa kama takwimu hapo chini zinavyojionyesha na hatukustahili adhabu tulizopewa, pia tunatambua kunamikakati ya wazi iliyowekwa na baadhi ya viongozi waliopo serikalini wakishirikiana na watawala wa vyuo vikuu kuvizika vyuo vikuu visiwe visima vya fikra huru “think tank of our nation” na hii ni kwa sababu ya mfumo mbovu wa kuwapata watawala wa vyuo vikuu, mfumo huu wa kuteuana unawafanya watawala wa vyuo vikuu kutokuwa huru na kuwaabudu waliowateua, kutumika kisiasa, kukosa utashi wa maamuzi na kushinikizwa kufanya maamuzi ambayo hayaendani na utashi wa taaluma zao. Hii inapelekea vyuo vikuu kutokuwa huru na kuenenda kinyume na Tamko la Ulimwengu la tarehe 29th April, 1990 linalohusu uhuru wa kitaaluma (Academic Freedom) ambalo sisi kama taifa tuliridhia kulisaini hapa Dar Es Salaam ,Tanzania. Tamko hili linasema wazi kuwa ni lazima Vyuo vijiendeshe kwa uhuru kamili bila kuingiliwa na serikali .

Ndugu waandishi wa Habari, baada ya juhudi tulizozifanyandani ya mfumo na nje ya mfumo bila mafanikio na baada ya kupata taarifa mbaya juu yetu ambazo watawala wa vyuo vikuu walizipeleka ndani ya mfumo na nje ya mfumo kwa lengo la kutuchafua, tukaona tunahaja ya sisi wanafunzi tuliofukuzwa vyuo vikuu nchini kutafutana na kuungana kwa ajili ya kupeana taarifa rasmi za ndani ya mfumo na nje ya mfumo na pia tuamue hatima ya maisha yetu kwa kuwa na sauti moja, kupeana matumaini, kufikiri pamoja, kupanga na kufanya juhudi za pamoja ilikuhakikisha kila mmoja wetu anatimiza ndoto zake kielimu kwa namna yoyote ile.

TAKWIMU ZA WANAFUNZI TULIOFUKUZWA VYUONI MWAKA WA MASOMO 2011/2012 Kuanzia mwaka 2011 mpaka sasa, ni zaidi ya wanafunzi 145 wamefukuzwa ndani ya vyuo vyetu nchini. Tukimaanisha UDSM, UDOM, MUHAS, MWALIMU NYERERE MEMORIAL, MUCCOBS, IFM, STJN, na MZUMBE. Sababu zilizofanya wanafunzi hawa kufunzwa vyuoni ni kama ifuatavyo; Kudai mafunzo kwa vitendo,vifaa vya kujifunzia na mazingira bora ya kijifunzia Kudai kurejeshwa kwa serikali ya wanafunzi iliyofutwa na watawala wa vyuo Kudai mikopo ambayo inawasaidia kulipa ada zao na kujikimu maisha wakiwa vyuoni Kimsingi kupoteza ndoto za wanafunzi zaidi ya 145 ambao kiuhalisia wamesomeshwa na kodi za watanzania kwa sababu tu ya kudai haki zao za msingi ndani ya taifa lao ni kitendo kisichokuwa na dira njema kwa taifa.

Kwa sasa tuna msiba wa taifa katika sekta ya elimu, wanafunzi wengi waliofeli kidato cha nne ni watoto wa masikini waliosoma shule za kata, watoto hao hao wanaojitahidi kusoma na kufika vyuoni, wananyimwa mikopo, wananyimwa mafunzo kwa vitendo na wanaposimama kudai haki zao ili wamudu maisha ya kitaaluma vyuoni wanafukuzwa kikatili na kusingiziwa vitu wasivyovitenda. Uhalisia ni kwamba Taifa hili linatengeneza Tabaka la walionacho waendelee kuwaburuta tabaka la wasionacho.

NJIA TULIZOTUMIA KUTAFUTA SULUHU

Mara baada ya kufukuzwa vyuo vikuu nchini, tuliamua kuchukua hatua mbali mbali za kidiplomasia ili kuhakikisha suala letu linapatiwa ufumbuzi. Zifuatazo ni hatua tulizozifanya ndani ya taifa letu;

Tulifanya hatua za ndani ya vyuo vyetu ikiwemo kukata rufaa kwa maamuzi yaliyofanyika zidi yetu, kuomba mabaraza ya vyuo vyetu yapitie upya maamuzi yaliyofanyika kwa kuwaeleza ukweli halisi kinyume na taarifa potofu walizozitoa mbele ya vyombo vya habari bila mafanikio yoyote.

Tuliamua kwenda kwa waziri wa elimu Mh. Shukuru Kawambwa na kutuma taarifa sahihi kinyume na taarifa potofu zilizotolewa na watawala wa vyuo vyetu bila mafanikio yoyote.

Tuliamua kutuma taarifa sahihi kwa waziri mkuu wa nchi, Mh. Peter Kayanza Pinda na kumueleza ukweli halisi kinyume na taarifa potofu zilizotolewa na watawala wa vyuo vyetu, bila mafanikio yoyote.

Tarehe 27/07/2012 tuliamua kutuma waraka wa wanafunzi tuliofukuzwa vyuo vikuu nchini Bungeni kupitia kwa waziri kivuli wa Elimu Mh. Suzan. Lymo ili Bunge nalo lituhukumu kwa uhalisia wa taarifa tuliyoipeleka, Mh.mbunge aliwasilisha taarifa yetu wakati anasoma taarifa yake lakini tarehe 14/08/2012, waziri wa Elimu Mh. Shukuru Kawambwa aliipuuza hoja hii inayohusu mustakabali wa maisha yetu kielimu ndani ya taifa letu. 5. Tuliamua kwenda kamati ya bunge ya huduma za jamii na kuwapelekea taarifa rasmi juu ya matatizoyetu kinyume na taarifa za watawala wa vyuo vikuu bila mafanikio yoyote

6. Tuliamua kuwafuata viongozi mbali mbali ndani ya taifa letu ambao tulihisi watatusaidia kwa namna moja au nyigine, tulichoambulia ni taarifa mbaya zidi yetu ambazo zimepangwa na watawala wa vyuo vikuu wakishirikiana na baadhi ya viongozi serikalini.Ndugu waandishi wa habari; baadhi ya taarifa hizi ni kama zifuatazo ambazo tulizitoa kwa kiongozi nyeti ndani ya taifa hili.

Hatuta soma ndani ya nchi hii mpaka uongozi uliopo madarakani uondoke hivyo tusubiri miaka mitatu minne,

Tuliopo mahakamani tunajisumbua hatuwezi kupata haki katika mahakama,

Hatutadahiliwa chuo chochote nchini.

7. Tuliamua kupeleka taarifa katika asasi mbali mbali zisizo za kiserikali, LHRC, TLS, FORDIA, TAMWA, TAWLA, nk. Ili kuwaambia taarifa za ukweli na kuwaomba msaada wao wanaoweza kutupatia kutokana na tatizo letu. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwani baadhi yetu tulipata msaada wa kisheria toka LHRC na TLS.

8.Tuliamua kwenda katika asasi za kidini, tulituma taarifa sahihi kwa viongozi wetu wa kidini ili kupata msaada wao wa kiroho na kuliombea suala letu, pia wao kama viongozi wa dini kuingilia kati juu ya uonezi uliofanyika lakini mpaka leo bado suala letu halijapata ufumbuzi.

SABABU ZA KUUNDA UMOJA HUU
Tunafahamu kuwa ndani ya taifa letu tuna mihimili mikuu mitatu, Serikali, Bunge na Mahakama, mpaka sasa Serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halijawa suluhu ya matatizo yetu na hii ni kwa sababu ya taarifa potofu zilizotolewa na watawala wa vyuo vikuu nchini, na kupelekea kuchafua taswira zetu na kupoteza utu wetu mbele ya jamii. Ndugu waandishi wa habari; Tumechukua hatua stahiki mbali mbali kama ilivyoelezwa hapo juu bila mafanikio yoyote, na tukizingatia matamko ya watawala wa vyuo vikuu kuwa haturuhusiwi kudahiliwa vyuo vyovyote vya umma ndani ya Taifa letu kiuhalisia nisawa na kuwa tumehukumiwa adhabu ya kifo ndani ya Taifa letu na sisi tunaamini hatustahili adhabu hii.

kwa sababu watawala wa vyuo vikuu wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kututenganisha na jamii zetu, familia zetu, ndugu na jamaa, viongozi wetu wa kidini na kisiasa kwa taarifa za uongo kupitia vyombo vya habari tumeona suluhu ya maisha yetu ni kuungana, muungano huu umeundwa kwa sababu zifuatazo;

1.Hatua zote tajwa hapo juu tulizozichukua ndani ya Taifa letu zimeshindikana.

2.Wote tulikuwa tuna tatizo la aina moja la kufukuzwa vyuo vikuu kwa sababu ya uzalendo wetu wa kutetea haki zetu na haki za wavujajasho ndani ya taifa letu
3.Tumeungana kwa sababu nafsi nyingi za wanafunzi tuliofuzwa vyuoni zinakufa, kwa sababu ya kukosa matumaini ya maisha, kukosa msaada kutoka katika familia na jamii tunayotoka, hali hii ilitokana na taarifa potofu zilizotolewa na watawala wa vyuo vikuu wakishirikiana na serikali kupitia vyombo vya habari, kutusingizia kuwa ni vinara wa vurugu, tumepiga wajawazito, tumebaka, tumetengeneza mabomu, tunatumiwa na vyama vya siasa na kashfa mbali mbali ambazo jamii kwa ujumla wake walijengeka kuwa sisi ni watu hatari na hatufai hatimaye kututenga katika mapito yetu.
Kiujumla hizi ndizo sababu zilizotufanya tuungane.

AZIMIO LETU

Tunaiomba serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunamuomba raisi Jakaya Mrisho Kikwete alichukulie jambo hili kwa uzito unaostahili huku akiangalia mustakabali wetu na wa taifa letu. Lakini umefika wakati wetu wa kuwaambia ukweli kwamba tumenyanyaswa, tumepuuzwa,tumebezwa, tumetukanwa , tumeteswa na tumeonewa kwa mda mrefu mpaka hivi sasa kana kwamba sisi ni watumwa kwenye nchi hii.

HITIMISHO

Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini tutambue kwamba sisi ni sehemu ya wanajamii ya kitanzania. Hivyo kwa nafasi yetu tuna haki na ni wajibu wetu kukemea,kurekebisha,kuhoji na kushauri pale tunapoona mambo yanaenda ndivyo sivyo.Vyuo vikuu vimepoteza dira, macho yetu yanashuhudia. Taifa letu limekuwa shamba la bibi, tunashuhudia hayo na bado tupo kimya, vyuo vyetu vinazimwa visiwe visima vya fikra huru. Maadili ya viongozi ndani ya taifa letu yamepotea. Bunge linashindwa kulitendea haki taifa hili kwa sababu ya mvutano wa kiitikadi wasomi tunashindwa kunyosha vidole vyetu kukemea uovu, Tunashindwa kusimama kulisaidia taifa letu, kwa sababu ya mabomu, risasi,virungu tunayopigwa tukisimama kutetea muafaka mwema wa taifa letu, vijana wa taifa hili tufumbue macho. Ikumbukwe kuwa Mwl J.K.Nyerere aliwahi kufika chuo kikuu cha Dar es Salaam wanafunzi walipogoma, alienda akawasikiliza akayapima na akatambua kuwa wanafunzi wanahoja za msingi akaamua aanze kujipunguzia mshahara wake mwenyewe kwanza. Huyu ni mfano kiongozi wa kuigwa ambaye anahitajika ndani ya taifa letu. Suluhu ya matatizo vyuo vikuu nchini sio timua timua, sio vitisho na Mabavu, sio nguvu ya vyombo vya dola, sio mabomu, sio risasi za moto, sio virungu ila ni busara kama aliyoitumia hayati Mwl. J. K . Nyerere kuenda kusikilizana na kupata muafaka sahihi.
MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA 13/03/2013.

RAI YANGU KWA WATANZANIA.

MIMI KAMA MSEMAJI MKUU WA UMOJA HUU "UUEST".

HII NI TAARIFA SAHIHI KUTOKA KWETU. CHOMBO CHOCHOTE CHA HABARI, MTU YOYOTE YULE ATAYEPOTOSHA UKWELI HUU MFAHAMU ANALENGO LAKE BINAFSI AU AMENUNULIWA.

LAKINI PIA NACHUKUA FURSA HII KUWAOMBA WATANZANIA WOTE YANI VIONGOZI WEMA WALIOKO SERIKALINI, VIONGOZI WEMA WA KIDINI, WABUNGE WOTE BILA KUJALI ITIKADI ZA VYAMA VYETU, ASASI ZOTE ZOTE ZA KISERIKALI NA ZISIZO ZA KISERIKALI, NA WADAU MBALI MBALI AMBAO WANATAMBUA KUWA TULIPOFIKA KAMA TAIFA NI PABAYA NA NI HATARI KWA AMANI YA NCHI HII. WATUUNGE MKONO KWA NAMNA MOJA AU NYINGINE ILI KUHAKIKISHA NDOTO ZA VIJANA ZA KIELIMU ZILIZOPOTEZWA ZINAPATIKANA KWA NJIA YOYOTE ILE. HIVYO KUANZAIA SASA TUNAKUJA KWENU WATANZANIA.

KWA WALE WOTE WALIOPOST KUWA TUMEOMBA MSAMAHA HAMJUI MLITENDALO, MJUE KUWA NI UDHALIMU TU TUMETENDEWA NDANI YA TAIFA LETU . MKIKUA KIFIKRA MTAYAACHA HAYO, HATUNA UGONVI NA NYIE ILA MTAMBUE KUWA TAIFA LETU LINALIA NA TUNAHITAJI NGUVU YA PAMOJA ILI KULIKOMBOA TAIFA BILA KUJALI ITIKADI ZETU ZA KIDINI, KIVYAMA, MAKABILA YETU. ILA KWA PAMOJA TUBEBE ITIKADI YA UTANZANIA, HAKIKA TUTAFIKA.

WANAFUNZI WA VYUO VIKUU LISAIDIENI TAIFA.

MWISHO KABISA NI WAJIBU WA RAISI JAKAYA KIKWETE KULITENDEA HAKI TAIFA HILI. MOYO WAKE UTAMBUE KUWA VYUO VIKUU NI INJINI YA NCHI YOYOTE ILE DUNIANI, NI VISIMA VYA FIKRA HURU NA HUU NI UKWELI AMBAO UTASIMAMA MILELE.KUVIZIMA VYUO VIKUU NI KULIZIKA TAIFA, KITU AMBACHO NAAMINI RAISI WETU HANA LENGO HILO. TUTAITAMBUA DHAMIRA YA RAISI WETU JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA VITENDO NA SI VINGINEVYO.

MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA.

No comments: