Sunday, July 21, 2013

MASABURI ATETEA ULAJI WA WABUNGE, MADIWANI, YAITAKA TUME YA KATIBA KUONDOA UKOMO WA WAO KUONGOZA Na Mwandishi Wetu, Tanzaniasasa
JUMUUIYA ya Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (ALAT), imepinga kipengele kinachotaka kuwepo kwa ukomo wa nafasi za uongozi wa kuchaguliwa na wananchi ikiwemo ubunge na udiwani.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi katika ukumbi wa ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Arusha, Mwenyekiti wa ALAT Didas Masaburi alisema jumuiya hiyo inapinga sura hiyo kwa kile alichodai kufanya hivyo ni kuwanyima haki wananchi wanaotaka kiongozi husika kuendelea kuwaongoza.

Alisema kabla ya kuwasilisha maoni yao kwenye tume hiyo walifanya mazungumzo na wananchi kupitia madiwani katika kata wanazowakilisha ambao wengi wao walitoa maoni wakitaka kutokuwepo kwa kipengele cha ukomo wa uongozi na badala yake wananchi waachiwe wenyewe kuamua kama wanamuhitaji kiongozi husika au la.

“ ALAT tuliwasilisha tume maoni 13 yaliyoelezwa kwa undani matakwa ya wananchi katika katiba mpya lakini cha kushangazwa tume imeweka maoni yake yenyewe na kutupilia mbali maoni yetu, hata hivyo bado hatujachelewa tutapeleka tena kwa mara nyingine maoni haya kupitia marekebisho ya rasimu hii ya awali,”alisema Masaburi.

Alisema maoni mengine waliyoyawasilisha katika tume hiyo ni pamoja na kutaka katiba iweke sura itakayobainisha namna ambavyo madaraka yatapelekwa kwa wananchi, kutamka katika katiba mpya uwepo wa Serikali za mitaa chini ya mfumo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nyingine ni pamoja na kutamka kazi na majukumu ya Serikali za Mitaa, uwezo wa kujiamulia mambo yao tofauti na hivi sasa kila kiongozi katika wizara amekuwa akiamua anavyopendelea yeye, namna mawasiliano yatakuwa baina ya Serikali kuu na Serikali za mitaa.

“ Pia tumependekeza kuwepo kwa kipengele kitachoonyesha namna viongozi wa Serikali za mitaa watakavyopatikana ili kuweka uwajibikaji wa viongozi hao ikiwemo kuchaguliwa na wananchi moja kwa moja katika eneo husika, benki kuu pia tunataka iwepo tu ya jamhuri isiwe kama ilivyo hivi sasa pamoja na idara ya uhamiaji kuingizwa katika eneo la Jamhuri,”alisema.

Masaburi alisema endapo Serikali za mitaa hazitaingizwa kwenye Katiba mpya tabaka la wenye nacho na wasiokuwa nacho litakuwa kubwa na matokeo yake ni ongezeko kubwa la watanzania masikini.

Alitoa wito kwa madiwani kote nchini kutumia nafasi ya kupitia rasimu mpya kuwaelimisha wananchi katika maeneo yao umuhimu wa uwepo wa sura inayoelezea serikali za mitaa.

Alisema Serikali za mitaa ndio ambazo zimekuwa mtetezi mkubwa wa wananchi katika suala la maendeleo kufuatia wao kusimamia fedha ambazo zimekuwa zikipatikana kupitia kodi inayokusanywa na Serikali kuu.

Masaburi alisema katika kikao walichofanya hivi karibuni jijini Arusha cha kupitia rasimu hiyo mpya ya Katiba wamekubaliana kabla ya Agosti 31 mwaka huu kuwasilisha maoni yao waliyoyawasilisha hapo awali katika tume hiyo.

No comments: