Wednesday, April 3, 2013

LOLIONDO KUMEKUCHA.


LOLIONDO KUMEKUCHA.

Wizara ya Maliasili na Utalii imefafanua kuwa tamko alilolitoa Waziri, Balozi Khamis Kagasheki kuhusu kupunguza eneo la pori tengefu la Loliondo halitakubalika na kuwa tamko hilo lililotolewa, limetolewa na mamlaka ya kisheria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na msemaji wa Wizara hiyo, George Matiko, ni kuwa tamko hilo limetolewa kutokana na maoni yaliyotolewa na baadhi ya watu kupitia vyombo mbalimbali vya habari, kuwa uamuzi alioufanya kuhusu pori tengefu la Loliondo, si sahihi kwa kuwa hautafuata sheria wala matokeo ya utafiti.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Waziri Kagasheki alifuata sheria alipotoa tamko kuhusu kupunguza eneo la pori tengefu la Loliondo, kutoka kilometa za mraba 4,000 hadi 1,500 na kuliacha eneo kilometa za mraba 2,500 litumiwe na wananchi.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Waziri alifanya hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, na kuwa sheria hiyo, inampa Waziri mwenye dhamana, uwezo wa kupitia upya, mapori tengefu na kufanya marekebisho mbalimbali muhimu kwa manufaa ya wananchi bila kuathiri uhifadhi.

Pia, taarifa hiyo imeeleza kuwa, waziri alifanya uamuzi huo kwa kuzingatia taarifa mbalimbali za utafiti na uchunguzi, ambazo ziliwahi kufanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) kwa kuzingatia mapendekezo ya tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza mgogoro uliokuwepo.

Hivi karibuni, baadhi ya wananchi na viongozi Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro walipinga uamuzi wa Serikali wa kuwapa sehemu ya pori tengefu la Loliondo wakidai sehemu iliyomilikiwa na Serikali ndiyo yenye huduma muhimu.Taarifa ya Wizara/Serikali aliyoitoa Waziri Balozi Kagasheki ni hii ifuatayo:

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis Kagasheki akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari juu ya msimamo wa serikali juu ya mgogoro wa muda mrefu kwenye Pori Tengefu la Loliondo, leo jijini Dar es Salaam.

 SERIKALI KUGAWANA NA WANANCHI ENEO LA PORI TENGEFU LOLIONDO

Wizara ya Maliasili na Utalii imekusudia kurekebisha mipaka na ukubwa wa eneo la Pori Tengefu la Loliondo kutoka kilomita za mraba 4,000 hadi 1,500 ili kumaliza migogoro ya muda mrefu inayotoka na mwingiliano wa matumizi ya ardhi katika eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis Kagasheki amesema serikali imefikia uamuzi huo kama njia bora ya kumaliza tatizo hilo kiserikali.
“Ili kutatua migogoro iliyopo, kunusuru ikolojia ya Hifadhi za Serengeti, Ngorongoro na pori Tengefu Loliondo, Serikali itameamua kutoa kilomita za mraba 2,500 kuwapa wananchi kuwa vijiji na wa kilometa za mraba 1,500 zitabaki serikalini na kuendelea kuwa na hadhi ya Pori Tengefu kwa ajili ya kulinda mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi wa hifadhi na Taifa,’’ anasema Mhe. Kagasheki.

Mhe.Waziri aliongeza kuwa Serikali itawawezesha wananchi kuanzisha Jumuiya la Hifadhi ya Wanyamapori katika ardhi ya kijiji, na mipango ya matumizi Bora ya Ardhi ya vijiji katika eneo la Loliondo utaandaliwa na kuambatana na huduma za mifugo ndani ya vijiji.

Mhe. Kagasheki aliongeza kuwa Pori Tengefu la Loliondo ni eneo la serikali kisheria lakini baadhi ya vijiji wamelichukua na kulifanya kuwa lao na wengine wameingia mikataba na makampuni binafsi yanayofanya shughuli za uwindaji na utalii wa picha bila kufuata taratibu.

 “Serikali imeona tatizo la ardhi kwa wanavijiji waliopo kwenye Pori Tengefu la Loliondo ndio maana limeamua kugawa eneo la ardhi kwao. Hata hivyo, nasisitiza sehemu ya vyanzo vya maji, mazalia ya wanyamapori na mapito ya wanyama katu serikali haitakubari kuwapa wananchi,” anasema Mhe. Kagasheki. 

Mhe. Waziri anasema utekelezaji wa uamuzi huo unaanza mara moja kwa kushirikiana na Aidhana Wizara ya Mifugo itakayoandaa na ukubwa wa eneo la malisho lililopo katika kijiji pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kuona uhalali wa Kampuni zinazomiliki ardhi katika eneo lililohifadhiwa kwa madai kuwa wameuziwa na serikali za vijiji.

Aidha, Mhe. Kagasheki alisema, Serikali iko tayari kuangalia upya eneo kubwa lililotolewa kwa Ottello Business Corporation ili kuona jinsi linavyoweza kupunguzwa ili wananchi wapate maeneo ya kufanyia shughuli zao na si kumfukuza mwekezaji huyo.

No comments: