Thursday, April 4, 2013

Tanzania kuunda kamati baina ya dini kuhakiki sheria za kuchinja

Wakiristo wa Tanzania wamezuiliwa kwa muda kuchinja wanayama kwa ajili ya matumizi hadi serikali iteue kamati baina ya dini kutafuta ufumbuzi wa suala hili la uchinjaji kati ya Waislamu na Wakristo.


Agizo hilo limetolewa baada ya miezi zaidi ya mitatu ya wasiwasi na mapigano katika mikoa ya Geita na Mwanza kuhusu uchinjaji wa wanyama.
"Kwa kawaida Waislamu [ndio ambao huchinja wanyama] katika nchi hii, lakini tuna mzozo huu na nimeunda kamati ya viongozi wa dini kutafuta suluhisho la kudumu," Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwaambia waandishi wa habari Jumamosi (tarehe 16 Februari) baada ya mkutano na viongozi wa Kiislamu na Kikristo katika mkoa wa Mwanza. "Kwa hiyo, [wakati] kamati hii itakapokuwa ikifanya kazi kwa juhudi kupata suluhisho la kudumu, Waislamu wataendelea kufanya kazi hii kwa ajili yetu sisi sote."
Kutoafikiana kulifikia kilele huko Buseresere tarehe 11 Februari wakati vijana wa Kiislamu walipopambana na kikundi cha Wakristo ambao walichinja ng'ombe na mbuzi wawili kwa ajili ya kuuza katika soko la ndani. Mapambano hayo yalisababisha mchungaji Mathayo Machila kukatwa kichwa, na kujeruhi wengine kadhaa na mali muhimu kuharibiwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Geita Paul Kasabago alisema watu watatu wamekamatwa kuhusiana na tukio, akiwemo Mchungaji Pastor Isaya Rutta, ambaye alichinja mifugo katika viwanja vya kanisa. Watu wengine wawili wanaoshikiliwa ni wa upande wa kanisa la Rutta. Kasabago alisema watashitakiwa kwa kukiuka sheria za afya, wakiwachochea wananchi na kusababisha kifo cha Machila.
Polisi bado haijamkamata yeyote anayetuhumiwa kufanya vurugu dhidi ya Machila.
"Sheria inasema kwamba mnyama yeyote anayechinjwa aidhinishwe na mganga wa mifugo mwenye sifa [ili kuhakikisha] anafaa kuliwa na binadamu," Kasabago aliiambia Sabahi. "Kinyume na hivyo, unahatarisha afya za walaji."
Rais Jakaya Kikwete alilaani vurugu, akisema vita vya kidini sio maslahi mazuri ya Tanzania. "Tumeishi kwa zaidi ya miaka 50 bila ya kuwa na ugomvi unaohusiana na imani zetu kama Waislamu na Wakristo," alisema huko Dodoma.
"Ni ujinga kugombana kwa ajili ya haki ya kuchinja," alisema.
Kikwete alimtuma Waziri wa Mambo ya Ndani Emmanuel Nchimbi huko Buseresere kusuluhisha jamii zenye mgogoro kuhusu haki ya kuchinja wanyama.
Nchimbi aliiambia Sabahi kwamba hali sasa imedhibitiwa, kwa kuwa mazungumzo yanaelekea katika "mwelekeo mzuri". Aliomba kwamba wale wanaohusika na vurugu watakabiliwa na adhabu za kisheria.

Utoaji kazi za machinjioni waibua maswali ya kidini

Nchini Tanzania machinjio yanamilikiwa na halmashauri za miji. Kwa miaka 50, ilikuwa ni desturi kwa machinjio kuwa na wafanyakazi wa Kiislamu, kufuatia miongozo ya Kiislamu. Hatimaye nyama huuzwa katika mabucha kwa ajili ya uuzaji wa rejereja.
Juvenary Mwaikambo, mwenye umri wa miaka 46, ambaye huuza nguruwe katika Banana Bar huko Dar es Salaam, alisema anajua machinjio mawili maalumu ya nguruwe ambayo Waislamu hawatachinja, lakini watu wachache sana wanayatumia.
"Ninajua ni kinyume cha sheria kuchinja nguruwe nyumbani, lakini ni ghali sana kuchinjia machinjioni," Mwaikambo aliiambia Sabahi. "Wanatoza shilingi 5,000 (Dola 3.10) kwa ajili ya kuchinja na mganga wa mifugo anapaswa kuidhinisha nyama kwa kuigonga muhuri. Kama [mganga wa mifugo] asema haifai kwa matumizi ya binadamu, inatakiwa kufukiwa … kuna kero nyingi katika machinjio."
Aran Mashimba, mwenye umri wa miaka 48, mkazi wa Buseresere, alisema suluhisho la mgogoro huo ni kuwa na machinjio tofauti kwa ajili ya kuwahudumia wakazi wa imani zote.
"Sio tu kwa ajili ya kuwaridhisha waumini wa Kiislamu, ni zaidi ya hilo," Mashimba aliiambia Sabahi. "Uchinjaji wa nyama ni tasnia kubwa ambayo inazalisha ajira. Kufanyika na Waislamu tu ni kutunyima [Wakristo] fursa za ajira."
Sheikh Suleiman Mtindi wa Mwanza, ambaye alishiriki katika mkutano wa pamoja uliofanyika Jumapili pamoja na Pinda, pia alipendekeza kutenganisha machinjio. Pinda alilikataa wazo hilo, hata hivyo, alisema litasababisha mgawanyo mkubwa.

No comments: