Monday, June 17, 2013

BREAKING NEWS, MTOTO MWINGINE WA MIAKA 7 AFARIKI KATIKA AJALI YA BOMU SOWETO, NI BAADA YA KUPATA MAJERAHA MAKUBWA KICHWANI


VIFO vya  ajali ya mlipuko wa kitu kinasadikiwa kuwa ni mlipuko wa bomu vimeongezeka baada ya mtoto mdogo mwenye umri wa miaka 7 aliyetajwa kwa jina la Tija James kufariki dunia usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya Seliani alipokuwa amelazwa.

Aidha majeruhi wengine watoto wadogo wawili ndugu Fatuma Jumanne (10) na Sharifa Jumanne (9), usiku wa kuamkia jana walipelekwa Nairobi nchini Kenya kwa ajili ya matibabu baada ya hali zao kuwa mbaya na kushindikana kutibika katika hospitali za hapa nchini.

Akizungumza katika hospitali ya Mtakatifu Elizabeth jana jijini hapa mara baada ya kutembelea majeruhi hospitalini hapo, Makamu wa Rais Dkt. Mohamed Bilal alisema hali za majeruhi zinaendelea vizuri ijapokuwa bado kuna majeruhi wawili ambao hali zao bado ni mbaya kufuatia kuumia vibaya maeneo mbalimbali ya miili yao.

Bilal alilaani kitendo cha kurushwa kwa kitu hicho kinachosadikiwa kuwa ni bomu na kuwaahidi wakazi wa Arusha kuwa Serikali imesikitishwa na tukio hilo na imeagiza uchunguzi wa kina wa kuwabaini wahusika wa tukio hilo ufanywe haraka na kwa makini.
“ Hili ni tukio la kusikitisha sana na sisi kama Serikali tumesikitishwa na hali hii ambayo inapoteza amani ya nchi, nchi yetu inasifika kwa historia nzuri ya kuwa na amani kote duniani lakini vitendo kama hivi vinatutia doa,”alisema Bilal.

Aliwataka wakazi wa Arusha kuendelea na shughuli zao za kila siku za kuwaingizia kipato bila kutishiwa na mtu yoyote na kwamba Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali wote waliohusika bila kujali itikadi zao.




No comments: