Monday, June 10, 2013

DC LONGIDO, ARUMERU WATUNISHIANA MISULI KWENYE MBIO ZA MWENGE, NI BAADA YA DC WA ARUMERU KUBEZA UTENDAJI WA DC WA LONGIDO

Ngombe

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Munasa nyerembe akimkabidhi mwenye wa uhuru Mkuu wa wilaya ya Longido, James Millya kulia mara baada ya Mkuu wa wilaya ya Arumeru kudaiwa kumtolea maneno ya kashfa mkuu huyo wa wilaya ya Longido kwa madai kuwa hajui thamani ya miradi inayozinduliwa wilayani humo


Na Mwandishi Wetu, Tanzaniasasa
WAKUU wa wilaya za Longido James Ole Millya na Arumeru Nyirembe Munasa leo wametunishiana misuli mbele ya mkimbiza mwenge kitaifa Juma Ali Simai katika makabidhiano ya mwenge wa Uhuru.

Hatua hiyo imefuatia maneno ya vijembe yaliyotolewa na mkuu wa wilaya ya Arumeru wakati akiwakabidhi viongozi wa mbio za mwenge huo pamoja na wakimbizaji kitaifa na kimkoa ili kuanza mbio zake wilayani Longido.

Mwenge wa uhuru uliwasili jana katika wilaya ya Longido Mkoani Arusha baada ya kumaliza mbio zake katika wilaya Arumeru na kufungua na kuweka mawe ya msingi miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi
bilioni 1.4.

Katika hali isiyo ya kawaida mkuu wa wilaya ya Arumeru alitamka maneno yaliyoonekana kumuudhi mkuu wa wilaya ya Longido kwa maelezo kuwa alikua na nia ya kumponda yeye na kujisafishia ili kupata alama zaidi.

Kama ada wakuu wa wilaya na Mkoa hutupiana vijembe katika makabidhiano ikiwa njia mojawapo ya kunakishi mbio hizo na wananchi na viongozi wa wilaya husika huonekana kufurahishwa na hali hiyo lakini hali ilikuwa kinyume kwa wilaya ya Arumeru na Longido katika kukabidhiana mwenge huo.

Mkuu wa wilaya ya Arumeru alianza kutoa maneno yake ya kashfa kwa Mkuu wa wilaya ya Longido kwa kusema hawawezi kushindana na wale wa wilaya ya Arumeru na kisha kusema miradi yao haina ubora kulingana na thamani ya fedha zilizotolewa.

Munasa wakati akiendelea kuwatambulisha na kuwakabidhi wakimbiza mwenge hao na waandishi huku akichomekea utani kwa kusema
‘’Angalia Mkuu wa wilaya wakimbiza mwenge hao walipokuwa kwangu walikuwa na afya
njema sana na wamenenepa na huko kwako kuna mifugo mbalimbali hivyo nataka uiendeleza afya yao’’

Akiendelea kukabidhi viongozi hao Munasa alimtupia kijembe kingine Ole Millya kwa kusema ‘’Arumeru ina halmashauri mbili lakini wilaya ya Longido ina Halmashauri moja lakini ina washinda’’

Millya ambaye ni wa jamii ya kifugaji ya kimasai alitupiwa kombora lingine la utani pale alipoambiwa kuwa ‘’Arumeru wamefanikiwa katika mpango wa ardhi kwa kupima vijiji kadhaa lakini Longido hali hiyo
hakuna na ndio maana kuna migogoro mingi ya ardhi na ndiyo sababu wananchi wake wanaingilia ardhi ya wananchi wa Arumeru na yeye kama mkuu wao wa wilaya ameshindwa kuzuia’’Arumeru Hoyeee.

Munase alimpa kijembe cha haja Ole Millya kwa kumweleza kuwa miradi yote ya Arumeru imefanyiwa tathimini kwa kujua thamani yake lakini Longido hilo haliko na sijui kama wanajua maana ya thamani ya miradi yao.

Wakati vijembe hivyo vikielekezwa kwa Millya Mkuu huyo wa Longido wakati wote alikuwa kimya na kuonyesha wazi kukerwa na kauli hizo huku akionyesha mikono juu kuonyesha kusikitishwa kabisa na mipasho hiyo.

 Baada ya kukabidhiwa mwenge wa uhuru na  wakimbiza mwenge wa uhuru ngazi ya Mkoa na Taifa na waandishi wa habari ndipo ilipofika zamu ya Ole Millya kusema yaliyomsibu kwa kuanza kwa kusema kuwa hakufurahishwa na kauli za Mkuu wa wilaya ya Arumeru.

Millya alienda mbali zaidi na kusema kuwa yeye hafanyi kazi kwa kujisifu na alisikitishwa na kauli hizo kutolewa na mkuu wa wilaya hiyo na kusema mambo ya wilaya zingine wakati hajui uhalisia wa miradi
ya wilaya ya Longido.

‘’Mimi nimesikitishwa sana na kauli za Mkuu wa wilaya ya Arumeru na zimeniudhi sana na sikutarajia kusikia zikitamkwa na kiongozi kama yeye sasa nasema mimi sijisifu nataka tuende wenyewe eneo la tukio kwa kukagua mradi mmoja baada ya mwingine’’alisema Millya

Baada ya mtifuano huo ndipo ilipofika zamu ya Mkuu wa mbio za mwenge mwaka 2013 Juma Ally Simai aliposema kuwa yaliyosemwa na Mkuu wa wilaya ya Arumeru yalikuwa  ni utani.

Simai aliongeza kuwa kauli hizo ni za utani lakini hazikupaswa kusemwa mahali pale kwakua nyingine zina ukweli hivyo zilipaswa kutafutiwa sehemu sahihi kwaajili ya kuzungumziwa.

“mheshimiwa mkuu wa wilaya naomba usichukie yale maneno mimi naona yalikua ni ya utani lakini hupaswi kuchukia ingawa utani mwingine unaudhi maana mengine yana ukweli na yalipaswa kutafutiwa sehemu sahihi ya kusemewa”alisema Kongozi huyo Simai aliamua kusema hivyo mara baada ya kuona hali ya hewa ilikuwa imechafuka kwa Mkuu wa wilaya ya Longido kupandisha jazba na kuamua
kumshambulia moja kwa moja Mkuu wa wilaya ya Arumeru kwa kauli zake .

‘’Mkuu wa wilaya Longido naomba ukuchukulie kuwa kauli zilizokuwa zikisemwa na Mkuu wa wilaya ya Arumeru ulikuwa ni utani na usione kuwa  kama amekudharau katika kazi zako kwani naamini kuwa kauli hizo ni kama vibwagizo vya mbio za mwenge tu na sio vinginevyo’’alisema Simai

Wakati huo huo Mkuu wa wilaya ya Longido Mkoani Arusha James Ole Millya katika taarifa yake kwa kiongozi wa mbio za mwenge alisema kuwa shirika lisilo la kiserikali la Pastoral Women’s Council {PWC} lina malengo ya kuinua wanawake wa kifugaji kiuchumi,kisiasa na kijamii na hata kupata haki stahili na vikundi 116 ndani ya Tarafa ya Ketumbeine vimepewa mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 78.

Millya alisema katika tarafa hiyo yenye vijiji 5 vya Orkejuloongishu,Gilay Lumbwa,Meirugoi na Noondoto kwa kila kikundi kimepewa shilingi milioni 2 zitakazotumika kufanyia shughuli zao za kiuchumi na kurudisha na riba ya nafuu ya shilingi 200,000.

 Alisema jumla ya miradi 9 itazinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi katika wilaya ya Longido ikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 374.5

No comments: